Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza jioni ya leo. Katika hoja tatu kubwa zilizowasilishwa jioni ya leo. Hoja ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Hoja ya Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na ile Kamati ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Spika, katika fursa hii niliyopata mimi mjadala wangu utajikita katika taasisi kubwa mbili. Leo nitajadili Fungu Namba 28 – Jeshi la Polisi na Fungu Namba 93 – Jeshi Uhamiaji. Katika ripoti ya CAG na ripoti iliyowasilishwa leo na Kamati ya PAC kuna mambo muhimu ambayo yamezungumzwa; na mimi katika uchambuzi wangu nitaanza na Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Jeshi la Polisi, katika ripoti ya CAG na ripoti ya Kamati imeonesha ndani ya Jeshi la Polisi kuna mfuko ambao ulianzishwa na Jeshi la Polisi unaoitwa Reward and Fine Fund ambao kwa jina lingine unaitwa Tuzo na Tozo. Mfuko huu ulianzishwa kwa nia njema. Nia ya Serikali au Jeshi la Polisi ilikuwa ni kwa ajili ya ustawi wa Polisi ili kuwawekea mazingira mazuri, ikiwemo ujenzi wa nyumba zao na miradi mbalimbali. Lakini uanzishaji wa mfuko huu ulikuwa na sheria yake, na sheria ile ilitungwa; na kulingana kufuatana na taratibu na mahitaji ya sheria ya fedha na kufuatana na kuanzishwa kwa mfuko huu miaka 10 ilitakiwa kwanza ipate idhini, kwa maana kanuni zitungwe na Waziri mwenye mfuko husika.
Mheshimiwa Spika, lakini cha ajabu mpaka hivi ninavyoongea ni zaidi ya miaka kumi na CAG amebaini kwamba mfuko huo umekuwa ukipokea ela na unafanya matumizi lakini Waziri hajawai kutunga kanuni zinazoelekeza namna fedha zitumike. Tafsiri yake ni kwamba mfuko umekuwa ukijiendesha kienyeji.
Mheshimiwa Spika, nataka kusema, kwamba fedha zimekuwa zikikusanywa na chanzo kikubwa cha fedha kwenye mfuko huu ni huduma ambazo wamekuwa wanazitoa kwenye ulinzi wa taasisi za fedha, migodi na sehemu nyingine. Mfuko huo una fedha nyingi na Jeshi la Polisi linaweza kukusanya bilioni 10 hadi bilioni 15 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, lakini fedha hizi hazina mwongozo wa kanuni uliotungwa na Waziri, hakuna Mhasibu wa kusimamia mfuko huu na haujawahi kukaguliwa tangu uanzishwe na CAG, na, hakuna hesabu zilishawahi kufanywa kwenye mfuko huu. Bahati mbaya huu mfuko kuna ukiukaji mkubwa sana. Kwa mfano mkataba unaingia na taasisi ya fedha, let us say wanaingia mkataba wa milioni 80 kwa mwezi; sasa mchezo unaofanyika ni kwamba, wale Askari wanaopangiwa kwenda kufanya majukumu wanalipwa posho kutokana na hizo fedha, na baadaye Jeshi la Polisi likihitaji malipo wanakata kulingana na ile fedha waliolipa kwanza wale Polisi waliotoa huduma.
Mheshimiwa Spika, maana yake ni kwamba kunafanyika matumizi ya fedha mbichi. Yaani ina maana wanafanya invoice discounting wanachukua ela yao mapema. Hapa pana-create mwanya, fedha zinaweza zikachukuliwa nyingi. Kama Jeshi la Polisi lilitakiwa kukusanya milioni 80 unaweza ukakuta mwisho wa siku invoice wanayo peleka ni milioni 20, milioni 80 zimechukuliwa zikiwa mbichi.
Mheshimiwa Spika, mimi sipingi askari wetu wanapofanya kazi ya kulinda malindo haya kupewa risk allowance, lakini risk allowance lazima iwe na utaratibu wake kwa miongozo ya Sheria ya Fedha. Huwezi ukachukua tu huko benki unakolinda kwamba wanakulipa huko huko. Benki au migodi imeingia mkataba na Jeshi la Polisi, kwa hiyo ilibidi fedha zote ziingie kwanza kwenye mfuko halafu Jeshi la Polisi lifanye arrangement ya kuwalipa askari kule kule na si kule wanapofanya kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jambo hilo limeendelea na haijulikani sasa utaratibu upi wanafanya ili kufanya reconcialiation ya fedha hizo. Hivyo, Kamati iliona na CAG aliona kupitia mazingira haya kunaweza kukawa na upotevu wa fedha nyingi kwa sababu control yake ni ngumu.
Mheshimiwa Spika, CAG alielekezwa kwenda kufanya ukaguzi maalumu kwenye mfuko huu ambao umekaa zaidi ya miaka kumi haujafunga hata hesabu zake. Mpaka sasa hivi kuna kigugumizi na ushirikiano wanaopata ni mdogo. Sasa nashindwa kuelewa ni kwa nini CAG hapewi ushirikiano wa kufanya hii special audit ili sasa umma ujue na sisi Wabunge kwa niaba ya wananchi tujue, fedha hizo zilizokusanywa kwenye mfuko huo ni kiasi gani, matumizi yake yalikuwa yapi na kwa nini kanuni ya kuongoza na kuguide namna ya matumizi ya mfuko huo hazijatungwa mpaka leo? Sipati majibu ya mambo haya na mabo yanaendelea.
Mheshimiwa Spika, Mfuko huu ni mfuko ambao una fedha nyingi, na umesikia mara nyingi hata Mheshimiwa Waziri akiwa anajibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge, wakiomba kituo cha Polisi anawaambia tutaenda kuchukua kwenye tozo na tuzo. Lakini hiyo, tozo na tuzo haina control yoyote, ni kama kichaka fulani hivi. Sasa hatuwezi katika nchi hii, na hizo fedha hazipitishwi wala haziidhinishwi na Bunge, zinaishia huko. IGP anamwandikia Pay Master General; anataka bilioni 10, zinakuja kwa IGP zinaenda kwenye matumizi moja kwa moja, hakuna utaratibu wa namna hiyo. Hivyo, kuna ukiukwaji wa Sheria ya Fedha maana hakuna control yoyote wala hesabu zinazowekwa.
Mheshimiwa Spika, sasa niombe nishauri mambo yafuatayo; mfuko huu una fedha nyingi, pamoja na kutumika hadi anapoondoka CAG zipo fedha kwenye akaunti yao huko BOT, bilioni 35 karibia na milioni 300 na kidogo, na bado wanaendelea kukusanya. Niombe, kama tuna nia njema na tunataka kuweka transparency kwenye matumizi ya fedha za umma, niombe mambo yafuatayo: -
i. Wa-suspend matumizi kwenye mfuko huu mpaka kanuni ziundwe na Waziri mwenye dhamana.
ii. Serikali ijikite kwenda kumpa CAG ushirikiano afanye audit ili tujue kuna nini na fedha hii imetumikaje kwenye mfuko huu.
iii. Tuombe wakaandae hesabu, inakuwaje mfuko ambao hauna mhasibu upo tu na billions of money zipo tu zinachukuliwa kiholela. Waende pale wakatuandalie hesabu na sisi tuweze kujua ni jambo gani linaendelea kwenye mfuko huu wa tozo na tuzo.
Mheshimiwa Spika, Kuna njia rahisi, tuwasaidie Serikali, tunahangaika tunashida na vituo vya polisi nchi nzima. Tengenezeni arrangemet kwani kile chanzo kina fedha ambazo ni stable and sustainable, nendeni kwenye financial institution mkaombe mortgage mjenge kwa wakati mmoja Vituo vya Polisi nchi nzima. Halafu, kwa kuwa ile fedha kwa kuwa source iliyo stable mtaenda kulipa huo mkopo na tutakuwa na Vituo vya Polisi nchi nzima bila upendeleo na kila mtu ataona manufaa ya mfuko huu, kuliko wakati huu ambapo IGP akiwa huru ataona sasa hivi nina interest na sehemu gani ngoja nikajenge majengo hapa. Akiondoka IGP huyo ana-abandon majengo yale anakuja IGP mwingine anaanzisha uelekeo wake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hatuna direction kwenye mfuko huu. Kama nchi tutafakari kwa pamoja, twende tukafanye jambo la muhimu kwenye mfuko huu, ili uletwe. Na kwa kuanzia mwaka wa fedha ujao tupitishe hapa makadirio ya mapato na matumizi ya mfuko huu ndani ya Bunge hili na hapo ndipo tutakuwa tumefanya kazi. Tumekosea sana tumevunja Sheria ya Fedha, hatujali tunaenda tu.
Mheshimiwa Spika, niombe sana, Serikali ipo hapa, hili jambo mkiendelea ni bomu kubwa sana, kuna ubadhirifu mkubwa upo hidden kwenye huu mfuko. Mkiuacha bila Kwenda kuufanyia hatua za haraka bomu litakuja kulipuka, tusije tukalaumiane.
Mheshimiwa Spika, hilo nimemaliza. Nadhani watakuwa wamenielewa juu ya mfuko huu wa tozo na tuzo. Niwaombe kabisa tena mambo mengine ya kuja kutuambia tutakwenda tutaenda kuchukua; m-suspend huo mfuko mpaka mfuate taratibu zote zinazo wahitaji kama Serikali ili kusiwe na mkanganyiko. Hiyo nimemaliza naomba niende kwenye fungu lingine la uhamiaji Fungu Namba 93.
Mheshimiwa Spika, hii ni taasisi nyingine iliyo ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Mambo ya kusikitisha kabisa, nitatoa literature moja juu ya kilichotokea pale Uhamiaji. Alisema hapa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, kuna habari ya stickers za visa. Hizi stickers za visa ni kichaka ambacho kinagharimu Taifa letu hasara kubwa. Wale Maafisa wa Uhamiaji ulikuwa ni mradi wao wa kujitengenezea mabilioni.
Mheshimiwa Spika, walikuwa na mambo mawili; mwaka 2019 CAG alienda pale kufanya special audit tena ilikuwa ya interval ndogo ya miezi sita, kuanzia Januari mpaka Juni, 2019, kukagua namna ya utoaji wa stickers za visa kwa wageni wanaokuja ndani ya nchi. Alikutana na maajabu makubwa sana. Alikuta kwanza kuna visa zaidi ya 33,500 zilizotolewa ni fake. Yaani wale Maafisa Uhamiaji walienda kujitengenezea hizo stickers, wakagawa, wakachukua hela, wakaweka mfukoni zaidi ya Shilingi 3,800,000,000/=, maisha yakaendelea business as usual.
Mheshimiwa Spika, walipoendelea kukagua wakakuta zaidi ya visa 21,705; zilipokelewa fedha zikaingizwa kwenye database ya Uhamiaji, baadaye wale Maafisa wakaenda kufuta zile taarifa zote kwenye database, wakachukua zaidi ya Shilingi 2,516,000,000/= wakagawana wafanyakazi 40, maisha yakendelea, business as usual. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kilichokuja kutokea sasa, Maafisa saba wakapelekwa Mahakami wakafunguliwa kesi ya Uhujumi Uchumi kwenye Mahakama Kuu Moshi. Wakakaa pale gerezani miaka miwili, baadae DPP akafanya nolle prosequi kwamba sina nia ya kuendelelea na kesi hii. Wakarudi kazini, wakaendelea kupiga maisha. Tuki-audit mwakani tutakuta wametupiga tena Shilingi bilioni sita, business as usual. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lazima kama Taifa tutafakari. Watu 40 wamekula vituo vya afya sita peke yao, na wamerudishwa kazini, wameingia kwenye payroll na maisha yanaendelea. Sisi tunakuja kupiga kelele hapa, tutawasadiaje Watanzania masikini tuliowaacha huko Vijijini, waliotutuma ndani ya Bunge hili? Watu wachache wananufaika na fedha za Umma.
Mheshimiwa Spika, nawaomba sana watu wa Serikalini, ninyi mliopewa dhamana na Mheshimiwa Rais, katusaidieni katika mambo haya. Kuwaachia watu wanakula fedha, wamerudi wako ofisini na hiyo audit ilikuwa ni trend a miezi sita, just imagine kama unge-audit ya miaka mitano, si ungekuta karibia bajeti ya Wizara nzima watu saba wamekula, business as usual na maisha yanaendelea! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili la Uhamiaji nadhani message mmeipata vizuri kitu gani nakusudia kusema. Nendeni mkafanye upya, mrudie na ule mfumo, hao watu walienda kufuta vitu kwenye database. Ule mfumo mmeuanzishaa upya, nendeni pia mkafanye reconciliation baada ya ku-abandon ule mfumo wa zamani: Je, huu mfumo mpya una-address yale matatizo? Au mme-create mfumo mpya ambao ni loophole nyingi kutupiga zaidi na zaidi! Kwa hiyo, nawaomba watu wa Serikali mkawe makini kuangalia hasara tuliyosababishwa, lakini watu hawa waliosababisha wizi wa namna hiyo kuwarudisha ndani ya Uhamiaji ina-send message mbaya kwa wale waliopo mle, kwamba, kumbe unaweza ukapiga hela! Mimi napokea mshahara wa Shilingi 800,000/=, mwenzangu kapiga Shilingi bilioni mbili kaenda kupumzika kidogo gerezani mwaka mmoja amerudi, tumeendelea na Shilingi bilioni mbili na hakuna chochote! Naye atakuwa attempted, atachukua naye Shilingi bilioni tano, naye ataenda kukaa gerezani mwaka mmoja atarudi nolle prosequi, maisha yataendeleea. Ndugu zangu, haya ni mambo ya kusikitisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna jambo kubwa ambalo pia niwaombe watu wa Serikali, nimepitia sana ripoti ya CAG katika area ya compliance kwenye Public Procurement Act. Yaani taasisi hii, ile sheria ni kama wameiweka huko kwenye kabati wanajiendeshea mambo. Nimeona Jeshi la Polisi pale, hata issues zao za procurement, 70% ya issues zote walizozifanya ni non-compliance na sheria. Wanaenda kulipa fedha wakandarasi bila hata kazi kukamilika, Auditor anaenda kukuta fedha zimelipwa na mradi haupo.
Mheshimiwa Spika, kuna Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa walinunua magari, magari yenyewe hayo yalilipiwa zaidi ya Shilingi bilioni mbili na milioni mia saba na kidogo, lakini magari yenyewe hayapo. Kwa maana hayo magari yalilipiwa hata kabla hayajawa delivered. Yaani you pay before delivery of goods. Katika bajeti hiyo, tena wame-exceed. Bajeti iliyokuwa approved na budget approving authority ilikuwa ni Shilingi milioni 388. Kwa bahati mbaya, unakuta wamefanya expenditure ya Shilingi 2,400,000,000/= bila budget approving authority.
Mheshimiwa Spika, sasa variance unayoiona hapo kwenye Shilingi 2,300,000,000/= iliyokuwa approved, variance ni kubwa sana. Sasa tuki-entertain mambo haya na tukaona hii ndiyo culture ya kuendesha mambo yetu ndani ya Serikali, tuta-create vacuum kubwa kwenye Taifa hili. Watu wataacha ku-comply, tutakuwa na hizi documents kama urembo tu na watu watakuwa hawa-comply. Kwa sababu tunaweka wenyewe sheria, badala ya kuzifuata, tunaweka kwenye makabati, tunaanza kutumia sisi wenyewe tunavyofikiria. Haiwezi kutusaidia.
Mheshimiwa Spika, nimeona pale TTCL kwenye manunuzi, yaani ni wezi. Tuombe PPRA ikafanye special audit kwenye mashirika haya ambayo tumeona. Compliance kwenye Sheria ya Manunuzi ni mbaya. Compliance siyo ile ambayo, inaishia tu kwamba tume-comply, ni compliance ambazo zina impact kwenye finance. Kwa sababu unakuta umesaini mkataba na mtu, hakuna power of attorney, kwa maana ule mkataba is null and void. Mmempa kazi, kesho na kesho kutwa asipo-perform hamwezi kumshitaki. Hakukuwa hat ana mtu aliyepewa power ya kisheria ya kusimamia mkataba wa Shirika. Shirika kubwa kama TTCL yanafanyika mambo ya ajabu kama haya. Nawaomba ndugu zangu, kuna issues nyingi sana kwenye compliance ya manunuzi. Nendeni mka-scrutinize document ya CAG muone weight ilivyo na significant impact itakayotupelekea. Kutakuwa na issue za litigation, tusipoona hapa tutashtakiwa.
Mheshimiwa Spika, kuna mkataba mmoja nimekuta pale TTCL wa Shilingi bilioni tano. Wamesaini ule mkataba na Mkandarasi alitakiwa amalize ndani ya miezi ya mitatu, ilikuwa ni kutengeneza ule mfumo wa short sms, lakini mpaka leo una zaidi ya miaka tisa hajawahi kumaliza. Nikawauliza sasa position ya mkataba kama huu ni upi? Yaani yeye alitakiwa awakabidhi kazi ndani ya miezi mitatu, lakini amechukua zaidi ya miaka mitano na mnaendelea na maisha na mnasema this is good, let us live, business as usual.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)