Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nami naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa hii nafasi. Kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya. Sisi watu wa Manyoni tunamshukuru sana kwa fedha ambazo ameleta nyingi sana za miradi.
Mheshimiwa Spika, mimi leo nitachangia maeneo makubwa mawili. Eneo la kwanza nitachangia kuhusu Mfuko wetu wa Bima ya Afya ya Taifa, na nitajikita zaidi kwenye suala la matumizi ya TEHAMA. Eneo la pili nitachangia kuhusu mfumo wa ujenzi wa viwanja vya ndege ambao kwa sasahivi kuna mkanganyiko kati ya TANROADS na Wakala wa Usimamizi wa Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Mheshimiwa Spika, naomba nianze na suala la bima ya afya. Sasahivi tunaenda kwenye mchakato ambapo tunataka kuja na bima ya afya kwa wote. Naomba nikiri kwamba nimepitia taarifa ya CAG na tumefanya uchambuzi kwenye kamati yetu ta PIC. Sidhani kama Shirika la Bima ya Afya ya Taifa ambalo hili shirika tunalo sasahivi lina uwezo wa kuistahimili kubeba watu takribani milioni 61.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi Shirika la Bima ya Afya linahudumia wanufaika takribani milioni 4.6. Kati ya hawa milioni 4.6 milioni 1.2 ni wale wanaochangia. Tunategemea kama tutakuja na Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, hili shirika litahudumia watu zaidi ya 60,000,000.
Mheshimiwa Spika, nikwambie tu kwamba shirika letu linamatatizo makubwa sana na nitaomba niyaseme.
Mheshimiwa Spika, nimepitia taarifa ya CAG, lakini tulipitia taarifa ya TR. Vile vile tulifanya uchambuzi kwenye kamati yetu. Shirika hili lina matatizo makubwa matatu. Kwanza, tulitegemea hili shirika liweze kujikita zaidi kwenye matumizi ya TEHAMA. Shirika linatumia kwa kiwango kidogo sana TEHAMA, hususan maeneo ya vijijini. Lingine, kuna udanganyifu mkubwa sana kwenye utoaji wa ile huduma, hususani kwenye matumizi ya kadi. Nitatolea mfano baadae. Jambo la tatu, tulitegemea shirika lingejikita zaidi katika kukusanya madeni, hata hivyo Shirika halijaweza kukusanya madeni. Kuna madeni mengi sana ya zaidi shilingi bilioni 10 yapo nje, na tunategemea hili shirika lijikite kweye uwekezaji; litaweza kuwekeza vipi kama halina capacity ya kukusanya madeni?
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, hoja yangu ni kwamba, tunategemea mbali ya kwamba hili shirika lengo lake ni kusajili wanachama na kutoa huduma, lakini linahitaji kujikita katika kuwekeza. Uchambuzi wetu tulioufanya kwenye Kamati ya PIC, tuliona kwamba kama itaenda na trend hii nadhani uwezo wake wa kuwekeza utakuwa mdogo sana.
Mheshimiwa Spika, nilifanya uchambuzi wa taarifa ya CAG. Katika taarifa ya CAG, nitatoa mfano. Kuna wafanyakazi 2,495 wa sekta binafsi ambao wanatoka katika kampuni 87, hawa walisajiliwa kama wafanyakazi wa umma. Hili ni tatizo kubwa sana la mfumo wa TEHAMA. Jambo lingine, taarifa ya CAG inasema kuna wanachama 165 ambao kimsingi sheria inasema wale wategemezi wasizidi watano, lakini wanachama zaidi ya 165 walikuwa na wategemezi ambao wamezidi kiwango kile ambacho sheria imesema. Hili ni tatizo kubwa la mfuko.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kwamba kuna wategemezi 73 waliosajiliwa kama wachangiaji. Hili pia ni tatizo kubwa sana la mfumo wetu wa TEHAMA. Mbali na hiyo, taarifa ya CAG, inasema kwamba kuna wanufaika 731, ambao ni wanaume walipata huduma ya upasuaji wa kujifungua, na haya malipo yalillipwa. Naomba nirudie, taarifa ya CAG, inasema, kuna wanufaika 731, wanaume walipata huduma ya kujifungua na haya madai yakapelekwa NHIF yakalipwa. Hili ni tatizo kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kwamba, kuna wanachama 444, walipata huduma ya full blood picture zaidi ya mara moja kwa siku. Narudia tena, kuna wanachama 444, walipata huduma ya picha kamili ya damu, yaani full blood picture zaidi ya mara moja kwa siku ndani ya siku 30. Hili ni tatizo kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, kulingana na kanuni za NHIF, ni kwamba mwanachama akipewa miwani mara moja kwa mwaka, hatakiwi kupewa miwani tena. Madai yaliyopelekwa na wanachama, kuna wanachama walipata miwani zaidi ya mara moja ndani ya mwaka mmoja. Hili ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, kuna tatizo lingine kubwa. Nimepitia taarifa ya CAG. Katika taarifa ya CAG, kwanza kuna madai ambayo yalikataliwa kabisa na shirika la bima. Kwa mfano, madai kutoka Muhimbili na madai kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete zaidi ya Shilingi bilioni 3.87 yalikataliwa. Sababu ya kukataliwa ni kwamba kuna kughushi na taarifa zisizo rasmi. Ndiyo maana nimesema kama tunataka hili shirika ndiyo libebe bima ya afya kwa wote, kama tu hii asilimia nane, kwa sababu sasahivi linachukua asilimia nane ya watu wote, je, tukimpa asilimia 100, zaidi ya watu milioni sitini, hili shirika linaweza likastahimili? Kwa hiyo tuna matatizo makubwa sana
Mheshimiwa Spika, zaidi ya hiyo ni kwamba, katika mwaka wa 2019 na 2020, shirika lenyewe llilikataa zaidi ya madai ambayo yanatakribani shilingi bilioni tatu, madai ambayo wenyewe waliyakataa, kwamba haya ni madai ambayo ni batili. Kwa hiyo hii inaonesha kabisa kwamba tuna matatizo makubwa sana kwenye shirika letu.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, shirika limeshindwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 11. Tunategemea shirika liende likawekeze lakini linadai taasisi za umma zaidi ya shilingi bilioni nane na linadai taasisi za sekta binafsi zaidi ya shilingi bilioni mbili, zipo nje hawajalipa na tunategemea hili shirika lijiendeshe. Haya ni matatizo makubwa sana.
Mheshimiwa Spika, ninashauri; kwanza hili shirika tunategemea tulipe mzigo mkubwa baadaye wa kusimamia bima ya afya kwa wote, lakini tumeona halina uwezo wa kukusanya madeni na wakati huo huo mfumo wa TEHAMA bado unasumbua sana. Nashauri kwamba tulifanyie restructuring hili shirika Ili tunapokuja na hoja kwamba linahitaji kubeba bima ya afaya kwa wote liwe na uwezo wa kubeba bima ya afaya kwa wote.
Mheshimiwa Spika, la pili ni kwamba tumeona kuna matatizo makubwa sana ya TEHAMA hususan maeneo ya vijijini ambako hakuna mitandao, na kuna muda ambapo kama hakuna mtandao ndani ya masaa 24, wanatakiwa wawe wamesha-submit zile claims zao na wakishindwa ku-submit, system ina-reject. Kwa maana hiyo mimi nashauri; kwamba tunahitaji vile vile kuangalia ule mfumo wa TEHAMA, upitiwe upya na hivyo uweze kuwa na tija.
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nitachangia leo ni kuhusu mfumo wa ujenzi wa Viwanja vya Ndege.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2016 Serikali iliamua kuhamisha majukumu ya ujenzi wa viwanja vya ndege kutoka TAA (Wakala wa Kusimamia Viwanja vya Ndege) kwenda TANROADS.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilikuwa na nia njema, lakini nadhani umefika muda muafaka sasa, tumejitathmini. Sisi tumechambua ndani ya Kamati yetu, tukaona kwamba bado ni muda muafaka ambapo majukumu ya kujenga viwanja vya ndege yarudi TAA.
Mheshimiwa Spika, kwanini tunasema hivyo? Ukiangalia international standards zina-guide kwamba, wataalamu wengi wa kujenga viwanja vya ndege, wa kutoa guidance wapo TAA. Tunatambua kwamba kweli tuna wataalamu wetu wapo TANROADS, lakini wale wengi wamebobea kwenye ujenzi wa madaraja, barabara na mambo mengine. Kwa hiyo hii imekuwa hoja; na kuna muda ambapo wakati vile viwanja vinatengenezwa vinakuwa havina zile international standards.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi…
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Chaya kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Ulenge.
T A A R I F A
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba; si tu hilo la kupora miradi kutoka TAA kuipeleka TANROADS, lakini pia chanzo kikuu cha mapato kwa TAA ni passenger service charge, ambayo dola 40 kwa kila anayepanda ndege za kimataifa, na shilingi 10,000 kwa kila anayepanda ndege za ndani. Fedha hizi zote zinakimbizwa TRA wakati TCAA, kampuni ambayo inafanya kazi zinazolandana na TAA, wanakusanya na kufanya miradi yao ipasavyo. Kuna nini kutokuiamini TAA kufanya kazi zake ipasavyo? Hiyo ndiyo taarifa niliyotaka kumpa.
SPIKA: Hilo swali anapswa kulijibu Serikali au anapaswa kulijibu mwenyekiti wa Kamati. Maana unayempa taarifa ni yeye, atamuuliza nani swali sasa maana yeye ni mjumbe wa Kamati?
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, nimeongezea tu mchango wake in terms ya taarifa kwamba siyo hilo, kuna hili lingine pia linaibana TAA.
SPIKA: kwa maana nyingine ni kwa ajili yako na wengine. Yaani hizi hoja ni hoja zetu sisi kama Bunge. Kwa hiyo ukiuliza swali ni kwamba mwenyekiti. Kama swali alilokuwa anauliza Mheshimiwa Mpina maana yake mwenyekiti wa kamati atakapokuja kuhitimisha ataanza kujibu yale maswali. Kwa hiyo wewe umeeleweka na Mheshimiwa nadhani pia ameshakuelewa hoja yako.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa mwongozo wako.
SPIKA: Karibu sana.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa huo muongozo…
SPIKA: Mheshimiwa Chaya, subiri kidogo. Mheshimiwa Chaya unaipokea taarifa hiyo?
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA: Mheshimiwa Spika, naipokea na ninashukuru kwa ufafanuzi wako.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema kwamba nia ya Serikali ya kuhamisha ujenzi wa viwanja vya ndege kutoka TAA kupeleka TANROADS kipindi kile haikuwa nia mbaya. Hata hivyo ndhani muda muafaka umefika sasa kwamba turudishe yale majukumu kutoka TANROADS tuyarudishe TAA, na nimetoa sababu za msingi. Kwanza watu wa TAA ndiyo wana-guide zile international standards za ujenzi wa viwanja vya ndege, wana wataalamu ambao wapo TAA, wanye ubobezi kwenye masuala ya ndege na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba TANROADS tuna wabobezi wengi sana kwenye kujenga barabara na madaraja. Kwa hiyo tumeliona hili na tumelijadili katika Kamati yetu. Tunaishauri Serikali, muda muafaka umefika sasa kurudisha yale majukumu ambayo tuliyapeleka TANROADS yarudi TAA ili basi TAA iwe na majukumu kamili ya kuhakikisha, kwamba wanajenga vile viwanja vya ndege, wanasimamia viwanja vya ndege na vile vile wana-provide ile maintenance kwa ajili ya viwanja vya ndege.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, narudia tena kushukuru sana kwa nafasi uliyonipa na ninaunga mkono hoja. (Makofi!)