Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia taarifa za Kamati zetu tatu, PAC, LAAC pamoja na PIC. Kwanza nianze kwa kuzipongeza sana Kamati hizi tatu kwa kazi kubwa ambazo wamefanya kuhakikisha kwamba wanapata ripoti iliyo salama na wametuletea hapa leo.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayofanya ya kutafuta fedha, ingawa yapo mambo ambayo yameelezwa kwenye taarifa za Kamati ambayo si mazuri kwa nchi juu ya ubadhirifu wa fedha za Serikali.

Mheshimiwa Spika, katika ripoti hii nitajikita maeneo matatu. Jambo la kwanza ni eneo la Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Pia nitachangia uendeshwaji wa Kiwanja cha Ndege Kilimanjaro (KIA) na la tatu kama muda utakuwa bado unaruhusu nitazungumza kidogo Wakala wa Mabasi Yaendayo kwa Haraka (DART).

Mheshimiwa Spika, CAG amefanya ukaguzi wa ufanisi katika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Kuna mambo yamebainika ambayo yanahitaji kupelekewa miongozo ya namna ya uendeshaji wa mifumo ya upatikanaji wa wanafunzi ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa.

Mheshimiwa Spika, jana tumezungumza sana hapa juu ya hoja ambayo ililetwa na Mheshimiwa Ezra juu ya wanafunzi ambao hawajapata mikopo. Katika ukaguzi huu wa ufanisi uliolenga kuangalia ufanisi wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wetu. Vilevile ukaguzi huu ulilenga kuangalia ufanisi wa namna zinavyoshughulikiwa rufaa pale ambapo wanafunzi wanapokuwa wamekata rufaa juu ya upatikanaji wa mikopo yao.

Mheshimiwa Spika, yapo mambo machache ambayo yamebainika. Kwenye taarifa ile alifanya ukaguzi wa miaka mitano, lakini kuna mwaka 2018/2019 mwaka ule ulikuwa na shida kubwa. Ilibainika kwamba wanafunzi 6,182 walipewa mikopo zaidi ya kiwango walichotakiwa kupewa chenye thamani ya 5,670,000,000, kiwango hiki kama wangepewa wanafunzi wengine ambao hawakupata mikopo tungepata wanafunzi wengine 2,835. Tungegawa katika halmashauri zetu 184, kila halmashauri wanafunzi 15 wangenufaika na fedha hizi ambazo walipewa wanafunzi zaidi ya kile walichokuwa wanahitaji.

Mheshimiwa Spika, nikisema hivi naamanisha nini hapa? Namaanisha kwamba mwanafunzi amekubaliwa kupewa kiasi fulani cha mkopo, lakini katika reality wakati anapokuja kupewa mkopo ule anapewa zaidi ya kile kiwango alichokubaliwa, inapelekea wanafunzi wengine kukosa mikopo na huu ulikuwa ni mwaka mmoja wa 2018/2019. Ukiangalia katika miaka yote mitano aliyofanya ukaguzi wa ufanisi CAG 13,000,000,000 zilizidishwa kwa wanafunzi ambao walikuwa wanapewa zaidi ya mikopo husika.

Mheshimiwa Spika, wanafunzi 2,852 walipewa mikopo chini ya kile kiwango walichokuwa wamekubaliwa pale awali. Hii inaamanisha nini? Maana yake mwanafunzi amekubaliwa atapewa asilimia kadhaa, lakini mwisho wa siku anakuja kupewa chini ya kile kiwango ambacho alitakiwa kupewa. Tunamfanya mwanafunzi asimalize masomo yake au tunamfanya mwanafunzi kuhangaika na masomo yake. Nini kilifanyika hapa? Zaidi ya 1,147,000,000 wanafunzi hawakupewa stahiki waliokuwa wanatakiwa kupewa.

Mheshimiwa Spika, wanafunzi 756 walipewa mikopo bila kuwa na sifa za kupewa mikopo, yaani hawana sifa ya kupewa mikopo lakini wakapewa, thamani yake 2,255,000,000. Hapa napo tungepata wanafunzi wengi ambao wangeweza kunufaika na mikopo hii hata pale Mbeya Jiji nao wangepata kupitia fedha ambazo kuna wanafunzi walipewa ambao walikuwa hawahitajiki kupewa mkopo.

Mheshimiwa Spika, nini sasa hapa tafsiri yake? Tafsiri yake katika Bodi yetu ya Mikopo bado kuna shida ya mfumo unaotumika katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu. Kama mwanafunzi alitakiwa kupewa 1,000,000 anapewa 1,200,000 tafsiri yake ufanisi wa ule mfumo siyo salama. Hapa umefanyika ukaguzi wa ufanisi. Sasa ukifanyika ukaguzi wa hesabu itakuwa tatizo zaidi.

Mheshimiwa Spika, nashauri sasa kama inawezekana tufanye ukaguzi wa kina juu ya mfumo unaotumika wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Ukisoma ripoti ya CAG inakupa indication kwamba mfumo siyo salama kwa kutoa mikopo kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile katika ukaguzi huu uangalie hizi 5,670,000,000 za 2018/2019 walipopewa wale wanafunzi zaidi hao wanafunzi walikuwepo kule site au kuna watu walikuwa wanawapa halafu baadaye wanakwenda kuzichukua? Hizo ndio indication za hii. Je, hao wanafunzi waliopewa mkopo wakati hawana sifa hao waliowapa bado wako ofisini? Kwa hiyo ukifanyika ukaguzi wa kina utayabaini haya mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende eneo la pili, eneo la uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro unaoendeshwa na Kampuni ya KADCO, hapa bado kuna shida. Kampuni ya KADCO iliingia mkataba na Serikali mwaka 1998 ili kuendesha Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro kwa miaka 25. Wakasainishana mkataba, ule mkataba Serikali ikawa na hisa asilimia 24 na kampuni ikawa na hisa asilimia 76. Katika kuendesha ule uwanja inaonekana ufanisi haukuwa mzuri. Serikali 2009 kupitia Baraza la Mawaziri wakakubaliana kununua hisa zote za KADCO kwa asilimia 100. Mwaka 2010 Serikali ilinunua hisa zote za KADCO kwa asilimia 100. TAA ililipa fedha milioni 5.3 fedha za Kimarekani sawa na milioni karibu 12.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2010 baada ya Serikali kununua zile hisa nini kiliendelea? Uendeshwaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro umeendelea kuendeshwa kama private entity. Wameendelea kuwa na mkataba wa concession agreement. Sasa unajiuliza maswali ya kutosha. Swali la kwanza, kama Serikali imenunua hisa zote asilimia 10,0 maana yake Serikali 100% ndio mmiliki wa kiwanja. Kwa tafsiri ya kawaida uendeshwaji wa kiwanja ulitakiwa kuwa chini ya Serikali kupitia TAA. Sasa hii concession agreement iliyopo wanaoendelea kutumia mpaka leo mpaka kesho na jana ni kati ya mkataba wa Serikali na watumishi wa KADCO walioko Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro au ni kati ya KADCO kama private entity na Serikali? Kama ni hili la pili nini maana ya kununua hisa kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama Baraza la Mawaziri lilishauri kiwanja kile kiendeshwe na TAA kwa nini hakikuendeshwa mpaka leo? Kwanza cha ajabu zaidi hata fedha wanazokusanya KADCO mpaka leo tunaweza kusema wanazitumia fedha mbichi, kwa nini? Kwa sababu hazipiti Mfuko Mkuu wa Serikali, yaani wao wanakusanya kesho wanapanga matumizi, wanatumia. Wana kipengele kidogo tu wanalipa dividend Serikalini kwa TR hapo tu. Mwaka 2021wame-declare kulipa 350,000,000.

Mheshimiwa Spika, sasa nashauri kwamba, kwa kuwa Serikali ilinunua hisa zote asilimia 100, sasa kiwanja hiki shughuli zote za uendeshaji zirudi TAA. Kwa nini nasema hivyo? tulipohoji kwa Afisa Masuhuli kwa nini wameamua kuendeleza hizi alitujibu jibu simple sana anasema kiwanja hiki kipo kimikakati ya kibiashara. Sasa mimi tu wa la saba wa Busega kule inaniingia kweli kichwani kwamba Kiwanja cha Ndege cha Dar es Salaam hakiko kibiashara eti cha Kilimanjaro kiwe kibiashara zaidi? Kama ingekuwa ni kibiashara basi Kiwanja cha Ndege cha Dar es Salaam ndicho kiko kibiashara zaidi kuliko Kiwanja cha Kilimanjaro. Kwa hiyo, nashauri tufanye hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili tufanye special audit ili kuangalia mapato yote yaliyopatikana katika miaka 10 hii yote ambapo KADCO walikuwa wanaendesha kiwanja kile kama Serikali, ili tubaini kama fedha hizi zilitumiwa vizuri na sheria za fedha zilifuatwa. Tukifanya yale yote yatatusaidia kujua ni kwa kiwango gani tumepata hasara kule Kilimanjaro. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ambacho nataka nichangie ni Wakala wa Mabasi Yaendayo kwa Haraka (DART). Tumeona Taarifa ya Kamati imesema hawa DART walilipa 1,700,000,000 kama fidia kwa wananchi kuachia maeneo, lakini CAG anasema fedha hizi zilikuwa nyongeza ya malipo nje ya valuation report iliyokuwepo, yaani Valuation inasema lipa 5,000,000,000 wao wakalipa zaidi 1,700,000,000. Sio hivyo tu, wakalipa na posho za usumbufu 435,000,000. CAG alipoomba kibali, walipata wapi kibali cha kuongeza kulipa fidia hawana. Hivi kweli wanapata wapi ujasiri wa kulipa 1,500,000,000 nje ya valuation report? Wanajibu kirahisi tu waliambiwa na Serikali. CAG anauliza leteni hicho kibali mlichopewa na Serikali, hawana. Hivi tumefika kuendesha taasisi yetu kwa style hiyo?

Mheshimiwa Spika, hapa kuna madudu ya kutosha juu ya malipo ya 1,500,000,000. Vilevile hapa tufanye special audit kuwabaini wale wote waliolipwa 1,500,000,000 kama ilikuwa ni halali. Pia wachukuliwe hatua watumishi ambao wameisababishia hasara Serikali kwa kulipa watu bila kufuata valuation report.

Mheshimiwa Spika, fedha hizi ni fedha za Watanzania na kibaya zaidi miongozo inasema valuation ikifanyika leo baada ya miezi sita, mnaongeza interest kwa wale mliowakadiria. Baada ya miaka miwili, miongozo inasema kurudia valuation. Sasa wale muda umepita miaka 10, hawajafanya tena valuation, wanaibuka tu kulipa zaidi 1,570,000,000. Hili haliwezekani tufanye special audit DART ili tupate taarifa rasmi, fedha hizi wahusika waliolipwa na tuone tija kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo moja la kumalizia. Ukienda pale Soko la Kariakoo, nafikiri liliungua mwezi Julai mwaka jana, pale napo kuna shida. Tunawaza kwamba, baada ya kufunga mwaka wa fedha 2021 kwa maana Juni, baada ya siku 10 tu soko likaungua, documents zote zikaungua, hamna cha risiti ya mapato, hamna cha risiti ya matumizi. CAG amewapa unqualified report, lakini ni kwa nini? Hapana siyo unqualified report amewapa disclaimer report ameshindwa kutoa maoni kwa sababu hamna document yoyote inayomfanya ku-verify mapato ya 3, 500,000,000 na matumizi ya 3,500,000,000.

Mheshimiwa Spika, sasa hii kwa akili tu ya kawaida inanitafakarisha na kunifanya nione inawezekana Soko la Kariakoo liliungua baada ya documents hizi kutoonekana ofisini. Ni akili tu ya kawaida inanituma hivyo. Kwa nini baada tu ya kufunga mwaka wa fedha Juni, siku 10 tu, halafu mwisho wa siku CAG ameenda pale hamna document yoyote ameshindwa ku-verify matumizi ya 3, 500,000,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa leo nimekuja na special audit tu mwanzo mwisho. Hapa napo ifanyike special audit ya 3,500,000,000 tujue tatizo kubwa lilikuwa ni nini. Sasa sijui watapata wapi document, lakini najua kwa sababu itakuwa ni special na kwa sababu special unaweza ukawahoji watu, CAG atajua namna ya kufanya, lakini mwisho wa siku tupate mbichi na nzuri kwa hapa kwenye Soko la Kariakoo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja za Kamati. Ahsante sana. (Makofi)