Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, natumia fursa hii kukushukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuweza kuchangia taarifa ambazo zipo mbele yetu. Kwanza niwapongeze sana Wenyeviti wote wa Kamati hizo tatu ambazo tunazijadili leo, lakini niipongeze sana Serikali kwa juhudi kubwa ambayo inafanywa ya kuwekeza kwenye taasisi mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, tuna jumla ya takribani mashirika na taasisi 237 na kati ya hizo 10 zimewekeza nje ya nchi yetu ya Tanzania. Kwa mwaka 2020/2021, Serikali imekwishawekeza mtaji wa thamani ya shilingi trilioni 67 na point. Kwa kweli ni juhudi kubwa sana na Serikali inafanya kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uwekezaji huo ambao ni zaidi ya asilimia 63.8 toka ilipoanza kuwekeza mwaka 2016/2017, ilikuwa kama trilioni 49 na kidogo, lakini mpaka 2020/2021 tumefikia trilioni 67, kwa kweli ni uwekezaji mkubwa ambao Serikali inaufanya.
Mheshimiwa Spika, sisi kama Kamati ya Uwekezaji Mitaji ya Umma kwa kweli tumeshuhudia kwa macho kuona ni jinsi gani Serikali yetu ya Tanzania chini ya Mama Samia Suluhu Hassan inawekeza.
Mheshimiwa Spika, mbali na kuwekeza bado kuna changamoto. Changamoto kubwa ambazo tumeziona ni pamoja na kutokuwa na Bodi za Wakurugenzi kwa wakati kwa baadhi ya Taasisi za Serikali na Mashirika ya Umma. Kusipokuwepo na hizi Bodi za Wakurugenzi, usimamizi wa fedha ambayo Serikali imewekeza unakuwa na mashaka. Kuna taasisi zaidi ya miaka miwili haina Bodi ya Wakurugenzi.
Kwa mujibu wa Sheria kama Bodi ya Wakurugenzi haipo. Katibu Mkuu wa Wizara husika anawajibika kusimamia ile Taasisi, naye ana muda wake wa kusimamia ile taasisi si zaidi ya miezi kumi na mbili, lakini unakuta Katibu Mkuu bado anasimamia hiyo taasisi zaidi ya miaka miwili, ufanisi unakua mdogo, ufanisi unakuwa na mashaka.
Mheshimiwa Spika, tunakumbuka mwezi Machi, 2022 wakati Mheshimiwa Rais anapokea ripoti ya CAG alitamka akasema yeye masuala mazima ya uteuzi ya hizi bodi yakifika mezani kwake hachukui muda kuyasaini na kazi zikaendelea. Hivyo basi, tuwaombe Wizara na Taasisi ambazo zinasuasua au kuna delay fulani ya kuteua hizi Bodi za Wakurugenzi, basi ziweze kufanya hivyo ili taasisi na fedha hiyo ambayo ni ya Watanzania imewekezwa iweze kuwa na tija. Kuna taasisi zingine ambazo zinachelewa sana kupata vibali vya ajira, unakuta ina watumishi wachache, unakuta kuna watumishi wa muda, lakini unaweza ukakuta tena kuna watumishi ambao wanakaimu zaidi ya miaka sita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mtu anapokaimu kwenye position moja zaidi ya miaka sita, mitano hata ile confidence ya kufanya kazi anakuwa hana. Anakuwa hana maamuzi kamili ya kuweza kufikia maamuzi ili taasisi iweze kusonga mbele. Nashauri mamlaka husika waweze kufuatilia kujua kwamba ni taasisi ngapi ambazo zina matatizo au changamoto hizo. Tunamshukuru sana na kumpongeza sana TR, amekuwa akifanya kazi kubwa sana kuhakikisha kwamba anasimamia haya Mashirika ya Umma yanafanya kazi zake kwa ufanisi, lakini kuna mambo mengine ambayo kama Serikali, kama Wizara, kama Taasisi husika ni lazima waweze kufuatilia.
Mheshimiwa Spika, vilevile ningependa kuchangia kujikita kwenye Shirika moja la Umma ambalo kwangu naona kama ni uti wa mgongo, Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (Tanzania Agricultural Development Bank). Benki hii inamalengo yake matatu, naomba niyarejee; la kwanza ni kusaidia utoshelezi wa usalama endelevu wa chakula Tanzania. Lengo la pili ni kuchagiza mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kilimo cha biashara. Lengo la tatu, ni kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi. Ni ukweli usiopingika, kilimo ndio ndio uti wa mgongo kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ambayo tumeipitisha mwaka huu Wizara ya Kilimo imetengewa zaidi ya bilioni 900 na kidogo. Ukiangalia Benki hii inawajibika moja kwa moja kwa wakulima wa Nchi yetu ya Tanzania. Ukiangalia tena mtaji ambao wanao hii Benki ya Maendeleo ya Wakulima Tanzania, bado haukidhi. Kwanza Benki yenyewe iko Stationed Dar-es -Salam, mikoani kule ambako kuna wakulima, mikoa ya pembezoni hakuna tawi lolote. Sasa nashauri kwamba, Serikali kwa sababu ilishaji-commit kuwapa mtaji hii benki na iliahidi kuwapa bilioni 700 na ikasema itakuwa inatoa bilioni 100 kila mwaka.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi tunapoongea Benki hii imekwishapewa bilioni 208 ina jumla ya mtaji bilioni 268, bado ni kidogo sana kwa majukumu ambayo benki hii inayo ya kuhakikisha kwamba kilimo cha umwagiliaji Tanzania kinakua, kuhakikisha kwamba wakulima wa kule Shinyanga, Songwe na Tanzania nzima wananufaika na hii mikopo ya benki hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukiiwezesha Benki ya Kilimo, tukawa-link na Wizara ya Kilimo ambapo Wizara ya Kilimo ina fedha ambazo zinakwenda moja kwa moja kwenye kilimo cha umwagiliaji, wana fedha ambazo zinakwenda kukopesha na kuwapa wakulima pembejeo, kuna fedha ya ufuatiliaji na usimamizi, lakini kuna fedha ya kuweza kuwapa miundombinu kama matrekta wakulima wadogo wadogo. Benki hii ikiwa linked pamoja na Wizara ya Kilimo ikasimamia zile fedha ambazo tunategemea wakulima wa Tanzania wakopeshwe waweze kutengeneza kilimo cha umwagiliaji, waweze kukopa matrekta, tunaweza tukawakomboa wakulima wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nishauri kama inawezekana, kama ni sera, sheria au kanuni ziangaliwe tuone ni kwa jinsi gani benki hii itakuwa inafanya kazi kwa karibu sana na Wiizara ya Kilimo ili kuweza kurahisisha kuwakopesha Watanzania pembejeo, matrekta na kuwawezesha kwa namna yeyote ile ili uchumi wetu uweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna Benki ambazo zinatoa mikopo kwa wakulima wa Tanzania, lakini Benki yetu ya (TADB) haijawafikia Wakulima wengi. Ukiangalia katika taarifa unaona kabisa kwamba kuna vikwazo ambavyo Serikali inaweza kukaa chini na kuvirekebisha, mfano, wakati benki inahitaji kukopa, labda imepata uhitaji mkubwa wa watu ambao wanahitaji kukopa ili waweze kufanya shughuli za kilimo, lakini kutokana na masharti ambayo yanakuwepo ni lazima Serikali ikope kwa niaba ya ile benki.
Mheshimiwa Spika, kukishindanishwa benki mbili kati ya hii Benki ya Maendeleo ya Kilimo na benki nyingine labda ya binafsi, zote zinakwenda nje ya nchi kwenda kukopa, ukiangalia masharti ya hii Benki yetu ya Maendeleo ya Kilimo ya Tanzania na masharti ya benki zingine, unakuta kwenye hii Benki ya kwetu ya Kilimo kuna vikwazo. Ni lazima mchakato ufanyike na unachukua zaidi ya miaka miwili, mitatu, lakini Benki nyingine au Taasisi nyingine ambayo haina milolongo ya vikwazo, haina milolongo ya procedures wao wanakwenda direct kama ni Ufaransa, kama ni Canada wanachukua mkopo, wanakuwa fedha na kuanza kukopesha.
Mheshimiwa Spika, ushindani wa Benki ya Kilimo na ushindani wa benki zingine, kwa kweli benki yetu inaonekana bado haina tija kukidhi soko, kukidhi ushindani ambao benki zingine unazifanya. Ningeshauri tuangalie taratibu zetu kama Serikali, kama nchi kuweza kuinusuru benki yetu hii, kuweza kuiongezea mtaji ili basi hii benki kwanza iwe na matawi mengi Tanzania, iwe na matawi mikoani isikae Dar-es -Salaam peke yake na iwe na matawi sehemu ambazo kweli wanalima. Kwa sababu Dar-es-Salaam wakulima ni wachache, sana sana wengi ni wakulima labda wa Msimbazi pale kulima mbogamboga, lakini wakulima ambao wanaitaji huu mkopo wako mikoani na vijijini.
Mheshimiwa Spika, nashauri kabisa kwamba ni vizuri tukaangalia Serikali ikatoa mtaji ambao iliahidi kila mwaka ingewapa bilioni 100, basi iwape hizo fedha na ikiwezekana iwaongezee zaidi ili Benki yetu sasa iwe na ushindani na iwe na tija na iweze ku-complete na benki zingine na Watanzania wote waweze kunufaika.
Mheshimiwa Spika, sitakuwa na mengi ya kusema kwa leo, isipokuwa nashauri tu kwamba hizo bilioni 700 ambazo Serikali iliahidi na ilisema kwamba itatoa kwa instalment kila mwaka, basi ifanye juu chini ili Benki yetu ya Maendeleo ya Wakulima iweze kupewa mtaji na wakulima waweze kunufaika na kile ambacho Serikali imewekeza kwenye taasisi.
Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa, ningependa sana kuwapongeza TANROADS kwenye sekta ya uwekezaji wa SGR, niipongeze sana Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan, Kamati yako ya PAC ilipata fursa ya kuweza kutembelea na kukagua kuangalia uwekezeaji ambao umefanywa wa SGR.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli unaingia kwenye ile treni unasema hivi kweli tupo Tanzania? Hivi kweli Tanzania tumefikia hatua hii? Ni maendeleo makubwa ambayo yamefanyika. Unafika karibu na Kilosa kule unaingia kwenye handaki, kwenye shimo, yaani daraja lipo chini mpaka unasema waoo! Kwa kweli Tanzania tumepiga hatua, nawapongeza sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya, kazi hazijasimama, hazijalala, wanachapa kazi. Kwa hiyo niwapongeze sana Serikali kwa kutoa fedha kwa kuwekeza fedha na sisi Watanzania, Wabunge kama Wawakilishi wa Watanzania tunasema kwamba fedha zetu ambazo Serikali imeweza kweli zinafanya kazi, zinaonekana kwa macho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa hii nafasi. Ahsante. (Makofi)