Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii nami niweze kuchangia kwenye kamati zetu hizi tatu. Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu. Pia nawashukuru Wenyeviti wa Kamati hizi pamoja na Wajumbe wake kwa kufanya kazi ambayo kwa kweli ni nzuri sana na ripoti zao zimesheheni taarifa za muhimu tupu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikupongeze wewe binafsi kwa kuona kwamba hizi Kamati tatu ni uti wa mgongo wa Taifa letu na kuzitengea muda mwingi ili Wabunge waweze kuzichambua, kushauri na kuisimamia Serikali. Kila siku umekuwa unatuambia tumuunge mkono Rais kwa maneno, lakini kwa kufanya hivi unatuambia tumuunge mkono Rais kwa vitendo kwa kuhakikisha fedha zinazokwenda kwenye halmashauri kwenye mashirika yetu, basi zifanye kazi ambayo imetakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana umesema kwamba umetenga muda mkubwa ili watu waweze kuchangia kwa ustadi, pia umeongeza dakika kwa sababu kikanuni ni dakika 15, lakini mara nyingi tumekuwa tunachangia kwa dakika10, dakika saba, hata dakika tano pia. Kwa kuona unyeti wa hili suala, umesema tuchangie dakika 15. Tunakupongeza sana kwa kutuonesha unamuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa vitendo. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza Waziri Mkuu wetu, amekuwa miongoni mwa watu wanaofuatilia fedha zilizotumika kama zimetumika inavyostahili. Tumemwona siku zote, mara zote anaenda kukagua miradi na anagundua vitu ambavyo vilitakiwa kugunduliwa labda na Wakurugenzi na taasisi zetu nyingine ambazo zipo kule, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu anafuatilia kitu kwa kitu na anaenda kugundua vitu ambavyo unaweza usiamini kama vitu hivi kavigundua Waziri Mkuu. Kwa hiyo, tunampongeza sana kwa kufuatilia value for money kuona fedha inayokwenda inafanya kazi kama ilivyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, binafsi nianze kuongelea 10%. Kwa nini naongelea 10%? Mimi kama Mbunge wa Chama cha Mapinduzi, kwenye ilani yetu tumeongea kwamba tutawawezesha wanawake, vijana na walemavu kwa kuwapa mitaji ili waweze kufanya shughuli zao, lakini nikiangalia trend, kama alivyosema jana Mheshimiwa Getere kwamba tunashauri, lakini hakuna kinachoonekana; ukiangalia trend mwaka 2016/2017 halmashauri 84 hazikufanya revolving. Watu walipewa fedha na hazikufuatiliwa ambazo ni Shilingi bilioni 5.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018 Shilingi bilioni 10 kwa halmashauri 90. Angalia kila siku inaenda inapanda, baadaye inaenda ikishuka. Mwaka 2018/2019, halmashauri 111 zenye thamani ya Shilingi bilioni 13 hazikufanya revolving wala marejesho ya Shilingi bilioni 13 hazikurudishwa. Mwaka 2019/2020 zinaenda zinaongezeka, halmashauri 130 hazikufanya revolving jumla ya Shilingi bilioni 27 zimeachwa mikononi. Kwa hiyo, kila Wabunge wakiongea, ndiyo kwanza inaenda inaongezeka, haipungui.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2020/2021 halmashauri 155 zenye thamani ya Shilingi bilioni 47 hazikurejeshwa wala hazikufanyiwa revolving, wakurugenzi wake wapo, waweka hazina wapo, Maafisa Maendeleo wapo, Serikali haijachukua hatua yoyote. Kwa hiyo, tutegemee 2021/2022 halmashauri zote zitafanya revolving, zimebakia 31 tu ndizo ambazo zilirejesha, tena siyo kwa 100%, zilirejesha kwa asilimia chache sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka kusema nini? Wabunge hapa tunachoongea, hakuna kinachochukuliwa, hakuna kinachofanyiwa kazi, matokeo yake, leo unaongea kwamba fedha zirejeshwe, kila mwaka zinaenda zinapanda mpaka zimefikia halmashauri 155. Tulitegemea zitashuka kutokana na Wabunge wanavyosema, ma-auditor wanavyokagua, Kamati zetu za LAAC zinavyokwenda kule watashusha, lakini ndiyo kwanza kama watu hawajali wala hawafuatilii.

Mheshimiwa Spika, nimefuatilia kwa kina hiki kitu, kinaleta ukakasi kabisa kwa sababu halmashauri 83 yenye thamani ya Shilingi bilioni saba, hazikutoa hata hiyo 10%, wakati hapa Wabunge tulipitisha sheria kwamba ni lazima on source 10% wakopeshwe vijana, walemavu na wanawake. Ukijiuliza, hizi halmashauri 83 ambazo hazikutoa hii 10% zimechukuliwa hatua gani? Kwa nini na nyingine zisiache kutoa? Kwa sababu hizi zipo, hazijatoa na hazijachukuliwa hatua. Kwa hiyo, tutegemee nyingine nyingi ambazo hazitatoa, zimevunja sheria, na hazijachukuliwa hatua yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaposema tunashauri na tunaongea hamna hatua yoyote, nadhani unatuelewa vizuri, na jana umeongea vizuri sana nadhani unatuelewa. Tunajua kabisa kwamba sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tutaenda kuomba kura na tuliahidi kwenye ilani, tunamwona Mheshimiwa Rais anavyohangaika huku na huku kutafuta pesa ili aweze kutekeleza ilani yake ya Chama cha Mapinduzi. Tunamwona kabisa anavyoshusha fedha kwenye TARURA, kwenye Halmashauri kwa asilimia 100, kwenye RUWASA, yote hiyo anatimiza ahadi walizoziahidi Chama Cha Mapinduzi wakati wa kuomba kura, lakini sisi leo hapa tunaacha tu hivi vitu, tunaviona tu viko kawaida lakini ni vitu ambavyo watanzania wana akili, wanajua na watakuja kuvihoji.

Mheshimiwa Spika, mtaji wa Shilingi bilioni 75 ulitumbukizwa mwaka 2020/2021 katika hii revolving fund. Hebu tujiulize, Shilingi bilioni 75, zingekuwa zina-revolve, leo hii tungekuwa na Shilingi bilioni karibia 300. Kwa hiyo, watu wetu wangeenda kutoa umasikini kwa kiwango kikubwa, lakini tukubali tumeshindwa kusimamia hizi fedha, zinashuka siku hadi siku. Yaani zimekuwa kama fedha ambazo hazina mwenyewe hivi, yaani watu wanazitumia tu, wanajiita vikundi vya kindugundugu wanapeana, hazirudi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nadhani hili suala sasa Mheshimiwa Waziri Angellah Kairuki ameongea vizuri sana hapa leo, nami Mheshimiwa Angellah namwamini sana, ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi. Kwa hiyo, tumwombe aanze na hili suala kwa sababu linamgusa mwananchi mmoja mmoja wa kule chini. Tunaomba aanze nalo kufanya kazi vizuri kwa ustadi mkubwa Mheshimiwa Spika, hizi fedha, nashauri zingefanyiwa vitu maalumu, mfano, kule kwetu Tabora sisi tunalima mpunga. Fedha hizi za vijana zingechukuliwa zikajengwa ghala kubwa, ikajengwa mashine ya kukobolea mpunga, vijana hawa wakakabidhiwa ghala pamoja na mashine wakafanya biashara. Moja, wangeajiri vijana wenzao; pili, wao binafsi wangejikomboa na umasikini; na tatu, ile fedha ingezunguka na wengine wangekopa, wakakopa, wakakopa, ikawa fedha ambayo inaonekana inazunguka na vijana wetu wengi wangeweza kufanikiwa, kuliko kuvipa vikundi viwili au vitatu vinaenda vinakula hela, moja kwa moja ile hela haizunguki, hatimaye tunaonekana kama Serikali tuliwadanganya watu wakati wa kampeni, lakini hatufanyi. Kumbe Serikali inafanya kwa uwezo mkubwa sana, lakini hakuna usimamizi unaojitokeza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba pesa hizi sasa zirudi kufanya vitu vya kimiradi. Kwa mfano, sisi Tabora tumelima alizeti sana, halmashauri iamue kununua mashine za kukamulia mafuta ya alizeti, ipeleke kwenye vikundi, wakamue alizeti, wakishakamua alizeti, watawaajiri wenzao, lakini mashine zote zitaendelea kukamua alizeti siku hadi siku na hela itarudi halmashauri. Vile vikundi vitakuwa vinasimamiwa.

Mheshimiwa Spika, tunaangalia kule Mtwara wenzetu wanalima korosho, naona kuna mtu ana kiwanda cha kubangua korosho, ameajiri wanawake kama 200. Hivi zile hela zote zingekusanywa zikanunulia kiwanda kidogo cha kubangua korosho, wakachukua akinamama na vijana, wakaajiri na wanawake wengine na vijana wengine, ile hela ingerudi na ingenunuliwa kiwanda kingine, kingine na kingine. Tungejikomboa katika umaskini kwa hali nzuri tu, tungelipa kodi ya Serikali kwanza, kwa sababu ukishafungua kiwanda utalipa kodi, utaajiri lakini owners wa kile kiwanda watakuwa ni wale akinamama na wale vijana wa pale Mtwara. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, alichukue hili na hizi pesa sasa ziende moja kwa moja kwenye miradi ya kuwawezesha akinamama na vijana badala ya kumkopesha mtu mmoja mmoja na kuona kama shamba la bibi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili suala tunaloongea wafuatilie, maana tumeshaongea sana lakini hakuna ufuatiliaji na nimekusomea hapa kwenye Jedwali, inapanda kila mwaka. Nimesoma chart one imeandika mchanganuo wa hati ya ukaguzi, ukiangalia paragraph 2.2.1, matumizi yasiyofaa ya akaunti ya Amana (deposit account).

Mheshimiwa Spika, kule halmashauri kuna account inaitwa deposit account. Kwa mfano, hizi hela za mikopo zinaweza zikaja zikaingia kwenye deposit account. Labda zimekuja bilioni tano, wakatoa bilioni nne, wakakopesha watu, bilioni moja ikabaki, ikatulia tu. Auditor akija akauliza mbona mmetoa bilioni tatu lakini mlipewa bilioni nne? Wanajibu, tulianza kidogo kidogo lakini baadaye tutazitoa, zikishasahaulika wanazitoa, wanafanya wanavyojua wao. Nasema hivyo kwa sababu nimefanya kazi halmashauri ndani ya miaka 13, najua.

Mheshimiwa Spika, kwenye taarifa ya ukaguzi, imetokea kwamba halmashauri 11, zimeweka kwenye deposit account bilioni moja na laki mbili na zimeshindwa kutolewa kwenye deposit account na zilikuwa ni hela za kuwakopesha akinamama na hazijulikani hizo hela ziko wapi, zimepotelea ndani ya deposit account. Hii ni taarifa ya CAG ambayo ameisoma Mwenyekiti wetu wa LAAC. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaweza kujifunza kabisa, kwamba account ya deposit ni akaunti ambayo ina ushiriki mkubwa katika kupiga hela za halmashauri. For example, leo tunalipa posho za chanjo za watumishi na watu walienda kwenye semina ya chanjo. Zimebaki milioni 400 zinawekwa deposit, kesho kutwa zinabaki milioni 100 zinawekwa deposit, baada ya muda, zile hela hazionekani deposit wala hazipo. Sasa, huwa najiuliza tu, hawa watu wanaogundulika wamefanya hivi, mwisho wa siku tunafanyaje? Tunawahamisha kuwatoa ofisi moja kuwapeleka ofisi nyingine, wanachukuliwa hatua ili mwingine asifanye tena au tunawaacha tu, tunakuja kuongea hapa Bungeni wanabaki? Nasema hivi kwa sababu wangekuwa wanachukuliwa hatua vitendo hivi visingepanda mwaka hadi mwaka, vingeshuka, lakini vinapanda mwaka hadi mwaka. (Makofi)

Mheshiwa Spika, hivi kweli tumeamua kumsaidia Rais juhudi anazozifanya au tumeamua kufanya kazi, yaani tupo ili mradi tunasema Bungeni, nimeoneka leo Munde nimechangia. Kwa hiyo tunaendelea tu, ripoti ya mwaka 2022 ikija leo halmashauri 155, inakuja halmashauri 160, tunaendelea tu. Nadhani hili suala nimeliongelea kwa makusudi mazima, naamini hili suala litachukuliwa hatua. Kwa mfano, Wilaya ya Buchosa milioni 94 hazionekani, zilikuwa deposit account (akaunti ya Amana). Nimesoma kwenye taarifa ya CAG. Kwa hiyo matendo haya yamefikisha bilioni tisa kwa mwaka 2021 hela ya deposit account. Bilioni tisa inajenga vituo vingapi vya afya au inajenga madarasa mangapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana, tumeahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi, bilioni tisa zinapotea, imeandikwa kwenye ripoti ya CAG hakuna kinachoendelea na tunajua kila halmashauri unaweza kuona zimepotea shilingi ngapi za hela ya deposit account, mpaka kufikia bilioni 9.4 ambazo hazionekani zilipo na zilikuwa kwenye akaunti ya Amana. Pale kuna Mhasibu, Mkurugenzi alikuwepo hata kama amehama, waulizwe zile pesa zimekwenda wapi? Kwa sasa hakuna kinachoendelea na ndiyo maana hivi vitu vinaendelea kufanyika siku hadi siku na vitaendelea kufanyika siku hadi siku tusipokuwa makini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunajenga Taifa au tunajenga halmashauri ambazo zinapiga hela, ndiyo maana kila siku watu wakisimama wanasema, halmashauri inapiga hela. Naamini kwamba sio watumishi wote wa halmashauri wanapiga hela, wala sio Waweka Hazina na Wakurugenzi wote, lakini wapo wachache ambao wanaenda kuchafua jina zima la halmashauri. Siamini kwamba ofisi zingine za Wizara au za Taasisi za Umma hazifanyi haya yanayofanyika, naamini haya yanafanyika. Kwa sababu sisi tunatoka kwa wananchi na halmashauri zina-deal na mwananchi mmoja mmoja ambao kila siku tuko nao, ndio maana tunaziona kwa macho mengi zaidi hizi halmashauri zetu. Pia, tunapokea malalamiko mengi zaidi kutoka kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache niliyosema, nimwambe Mheshimiwa Waziri wetu yupo, tena mwanamke mzuri ambaye ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi tunamfahamu, tumekuwa naye humu kwa muda mwingi, aende sasa akalete mabadiliko ndani ya halmashauri zetu hasa kwa hizi pesa tulizoziahidi kwenye Ilani ya Uchaguzi, zitakwenda kuwainua watu kiuchumi. Ahsante. (Makofi)