Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nami nafasi ili kuchangia hoja iliyoko mezani. Kwanza kabisa nami naomba nitoe pongezi kubwa sana kwa Kamati zote ambazo zimewasilisha ripoti zao ili tuweze kuzijadili, kwa sababu wamewasilisha ripoti ambazo kwa kweli wamewasilisha vizuri sana nasi tumeweza kuzitambua na tunaweza kuzichangia vizuri. Moja kwa moja nami nianze na Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Spika, tathmini ya ufanisi wa mfuko huo unaonyesha kwamba kuna vikundi 155 havikurejesha mikopo ya Bilioni 47 iliyotolewa katika vikundi mwaka 2019. Pia umebaini kwamba kuna mamlaka 83 za Serikali za Mitaa hazikuweza kuchangia jumla ya Shilingi Bilioni 6.26 katika vyanzo vyao vya mapato. Hili jambo siyo dogo, kumekuwa na hoja nyingi sana katika utoaji wa hii mikopo, Bunge letu lilitunga sheria ya utoaji wa ile asilimia 10, asilimia Nne kwa akina mama, asilimia Nne kwa vijana na asilimia Mbili kwa watu wenye ulemavu, sasa ni kwa nini sheria hii haitekelezeki? Kwa nini Halmashauri zinakuwa hazitekelezi hizi sheria, siku zote tumekuwa tukizungumzia hili jambo katika hili Bunge. Tumekuwa tukiuliza maswali tunaona yanajibiwa lakini bado tatizo linaendelea, zikija hoja bado tunaona hoja zile zinajirudia mara kwa mara. Kuna baadhi ya Halmashauri hoja zimejirudia miaka saba, kumi, au miaka mitatu ni kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Halmashauri zingine tunaona kwamba zinatoa fedha hewa katika vikundi, Halmashauri nyinginezo zinatoa fedha chini ya kiwango ya mikopo na Halmashauri nyinginezo zinabadilisha matumizi ya hizi fedha. Ipo haja Serikali sasa ipendekeze adhabu kwa Halmashauri ambazo hazitekelezi hii sheria ambayo tumeitunga wenyewe hapa Bungeni, kwa sababu imekuwa kila siku tunaongea lakini hakuna adhabu yoyote inayotolewa pengine ikitolewa leo adhabu hizi fedha zitaweza kutekelezeka na kila Halmashauri itatendewa haki, na wananchi wetu inapotolewa hii mikopo maana yake sisi tunapigania kwamba Serikali ilikuwa inayo nia njema kabisa kuhakikisha kwamba wanawake, vijana na watu wenye ulemavu waweze kukopeshwa ili ilete tija.

Mheshimiwa Spika, naomba nami niungane na watu wa Kamati kwamba sasa ipo haja kuwepo na akaunti maalum ya hizi fedha za kutoa na kukusanya. Itakukwa rahisi sasa kui-monitor ili iweze kuleta manufaa zaidi. Pia kuwepo na mpango mahsusi wa wanufaika kupatiwa elimu, kwa sababu bila elimu tumeona kwamba vikundi vingi sana vinapewa hii fedha lakini hawana elimu hata ya kuweza kufanya biashara ambazo wanapatiwa.

Mheshimiwa Spika, tumeona sasa hivi, tunavyo Vyuo vya VETA, tunavyo Vyuo vya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri zetu na Mikoa yetu, ni kwanini sasa elimu isitolewe katika hivi vyuo vya VETA? Tumeona vijana wengi sana wanamaliza vyuo vya VETA bado hawana mkakati wowote hata wakisaidiwa kupewa hii mikopo ya vijana, mpaka vijana muda mwingine wanajishughulisha kwenye bodaboda hata wengine hawakupenda kukopa hizi bodaboda lakini kutokana na pesa ndogo sana ambayo vijana wanakopeshwa na akina mama. Unakuta kikundi kimoja kinapatiwa labda mkopo wa Shilingi Milioni Mbili akina mama 20 au vijana 10 wanapatiwa mkopo wa Milioni Tatu, matokeo yake wanaona bora tukinunua bodaboda tuizungushe ili iweze kutusaidia. Bado kungekuwa na mkakati, vijana wanaomaliza vyuo vya VETA, wamesoma wapatiwe mashine badala ya kupatiwa fedha, wanaweza wakapatiwa hata mashine ya kufyatua tofali, wakapatiwa mchanga, simenti na baadae Halmshauri iweze kuchukua ijengee labda shule na hospiatali. Utaona hawa vijana watakuwa na uhakika wa kulipa ule mkopo kuliko ilivyo sasa hivi vijana wanapatiwa fedha hawana elimu au utaalam wowote wa kuendesha hizi fedha na matokeo yake zinashindwa kurudishwa kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, unakuta kwamba sasa hivi vijana wamesomea mambo ya uvuvi, wamehitimu masomo ya mifugo na kilimo, hizi fedha bado baadhi ya Halmashauri tunapata fedha nyingi sana kwa ajili ya kilimo au uvuvi au mifugo. Kwa nini vijana wasipatiwe elimu ya ufugaji wa samaki, wakajengewa bwawa, wakanunuliwa samaki, wakapatiwa vyakula halafu baadae wakianza kurudisha tena kuna masoko mengi wakapatiwa hata hayo masoko, Kwa hiyo Halmashauri zinakuwa na uhakika kwamba hizi fedha ni lazima zitarudi kwa sababu ni revolving fund ambazo mtu akirudisha, vijana wengine wanakopa au akinamama wanakopa na watu wenye ulemavu pia.

Mheshimiwa Spika, kwa watu wenye ulemavu kuna miradi maalum ingetengenezwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu, kwa sababu tumepitisha kwamba mlemavu mmoja mmoja anaweza akakopa ama walemavu wawili. Sasa kungekuwa na miradi maalum kwa ajili ya watu wenye ulemavu wapatiwe vifaa na pia wasaidiwe kutafuta masoko ili iweze kuwasaidia kuliko ilivyo sasa hivi tunapoteza mapato makubwa bila sababu lakini kumbe nia ya Serikali ilikuwa nzuri sana kuhakikisha kwamba tunawasaidia watu wenye ulemavu, akinamama na vijana ili ulete tija. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulifanya ziara na tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri ambae ameteuliwa sasa hivi Mheshimiwa Angellah Kairuki, alipokuwa Katibu wa Wanawake kwenye Chama chetu hiki cha Wanawake hapa Bungeni, alitutafutia ziara nyingi sana kwenda kujifunza miradi ya akina mama. Kwa mfano, tulikwenda China, Uingereza na sehemu nyingi sana, tulikuta pale China akina mama wana miradi mikubwa sana kwa sababu wanavyo viwanda vidogovidogo vya ndani, sasa ifikie sehemu hata Halmashauri zetu, badala ya kuwapatia pesa tuwapatie viwanda vidogovidogo ambavyo kila nyumba ikiwa ina viwanda tayari hata ajira kwa vijana tutatengeneza ajira nyingi sana hata wenyewe tutajiajiri kwa kutumia viwanda vidogovidogo ambavyo viko katika Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tayari Halmashauri zetu zitapata chanzo cha mapato kwa sababu watalipa kodi za Halmashauri pia tutaongeza pato katika nchi yetu na ndivyo ambavyo hata Wachina wenzetu wanafanya vitu vingi ni kwa sababu badala ya kuwapatia fedha wanawapatia viwanda vidogovidogo ambavyo viko katika nyumba zetu wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nilikuwa nataka kuchangia ni kuhusu uteketezaji wa madawa ya binadamu kwenye vituo vya afya na katika hospitali zetu. Taarifa ya CAG ya mwaka 2020/2021 inaonesha kuwepo kwa wimbi kubwa kabisa la uteketezaji wa madawa. Kitu ambacho mimi nimejifunza hapa, utaona hivi vituo vya afya na Hosipitali za Wilaya, Mkoa zimekuwa zinalipia madawa kule MSD lakini unakuta kwamba haya madawa yanacheleweshwa kuletwa kwenye hospitali zetu kwa muda mrefu kiasi kwamba sasa muda mwingine yakiletwa inakuwa muda wa matumizi umekwisha. Kwa hiyo, matokeo yake sasa madawa yanateketezwa, kunatakiwa kuwepo na fedha tena ya kuteketeza hayo madawa. Vilevile tatizo kubwa wananchi wanakwenda kutibiwa, wanaandikiwa dawa na dawa hazipo. Huo ni uzembe, tunapoteza mapato makubwa wananchi wakitegemea kwamba watapata huduma za afya lakini matokeo yake hawapatiwi huduma za afya, dawa zinateketezwa na fedha za Serikali inaliwa, matokeo yake tunaletewa hoja kubwa kwa Serikali, hakuna kinachofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilisahau kusema, tulivyokwenda China, tuliambiwa kwamba wao watu wanaoiba fedha ya Serikali adhabu yao ni kuuawa lakini sisi kwa sababu ya haki za binadamu hatuwezi kufanya kitu kama hicho, tufanye kitu kikubwa ambacho kitasababisha watu wawe na nidhamu ya matumizi ya fedha ambazo tunazipeleka kwenye Halmashauri zetu. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, mimi ninaomba uteketezaji wa hayo madawa….

SPIKA: Mheshimiwa Ritta Kabati, hebu hapo kwenye mchango wa China na watu kuuawa na haki za binadamu hebu paweke vizuri.

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nimesema hivi: tulipokwenda China kuangalia miradi ya akina mama, tulipokuwa tunapewa ripoti kwamba wao China, watu wakiiba fedha ya Serikali adhabu ni kifo, lakini kwa sababu Tanzania hatuna adhabu ya kifo kwa sababu ya haki za binadamu, basi angalau tutoe kitu kikubwa kitakachowafanya hawa watu wanaoiba mali za umma, wapewe adhabu kali ambayo itawafanya hata wananchi waone kwamba sisi wananchi tunachangia pato la nchi lakini watu ambao wanafanya uhujumu wa hii fedha kweli wanapatiwa adhabu ambayo inasababisha wananchi turidhike na kile wanachokifanya. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

SPIKA: Mheshimiwa Ritta Kabati, nilikusudia kusema hivi kwa sababu unazungumzia nchi, watu kuuawa, Bunge lisielekezwe upande huo, kwa hiyo huo mchango wa China na kuua watu, hata sisi tunayo adhabu ya kifo haijafutwa, tunayo adhabu ya kifo ila siyo kwa haya unayoyazungumzia. Kwa hiyo, hii habari ya China na mfano wa wao kuwa wanaua watu naamini na wao wanafuata utaratibu kama ambavyo na sisi tunayo adhabu ya kifo. Kwa hiyo, mchango wako hapo uondoe kwenye Hansard halafu weka hoja yako ni nzuri tu, inaenda vizuri sana bila huo mfano. Ahsante sana.

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba basi Hansard iweze kutoa mambo ya kifo lakini kupoteza mali ya umma siyo nzuri.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ninataka kulizungumzia ni kuhusiana na michango ya NHIF. Kuna mapato mengi sana yanapotea. Yanapotea kwa sababu gani? Tumeona jana kuna Mheshimiwa Mbunge alizungumza kwa uchungu sana kwamba hata akinababa wanaambiwa kwamba wamejifungua iko kwenye madai yao kwamba wanaume wamejifungua na fedha ipo imekatwa NHIF. Tumeona sasa hivi wanao utaratibu mzuri sana, unatoa taarifa kwamba umetibiwa katika kituo fulani. Sasa kwa nini wasiseme kwamba wametibiwa kwa mfano, mimi labda nimetumia kadi yangu ya NHIF kwenye hospitali hata ya private, sasa niambiwe kwamba nimetumia kiasi gani? Kwa sababu tunaona kama kuna mapato mengine mtu anasingiziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mfano wa Mbunge mmoja alikwenda kutibiwa kwenye kituo cha afya, alipokwenda kutibiwa kwenye kituo cha afya, ana ulcers tu, akapewa dawa za ulcers, baadae akapigiwa simu kwamba ulikuwa umelazwa? Akasema sijalazwa lakini inaonesha kwamba amelazwa siku saba, katumia drip, wakati alikuwa ametumia dawa tu na mfano hai upo, Mbunge aliyepigiwa simu yupo. Kwa hiyo, NHIF basi ingekuwa wanafuatilia wanatuletea hizo taarifa za matibabu yetu pamoja na bills tumetibiwa kiasi gani itakuwa rahisi, hata kama sisi wenyewe Wabunge saa nyingine tunakwenda kutibiwa kwenye Mkoa mwingine basi taarifa ziletwe Bungeni kwamba Mbunge fulani katibiwa sehemu fulani na gharama zake ni kiasi hiki itakuwa rahisi hata kufanya reconciliation kwamba Bunge letu, Wabunge tumetumia kiasi hiki kuliko ilivyo sasa hivi, mtu unalimbikiziwa gharama ambazo zisizo zinakwenda kwenye Mfuko matokeo yake wanaua Mfuko bila sababu.

Mheshimiwa Spika, hivyo ninaomba Serikali yetu iangalie huu Mfuko kwa sababu ni muhimu na tunaenda sasa kupitisha Sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya lakini kama kutakuwa hakuna control yoyote ya matibabu ya watu wanavyotibiwa itakuwa haina maana yoyote kwamba nia nzuri ya Serikali inakuwa inapotoshwa. Watu wachache wasifanye watu wakaichukia Serikali yao kwa sababu ya vitu vidogo sana.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa naomba nikushukuru sana na nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anazozifanya. (Makofi)