Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia. Kwanza niwapongeze sana Wenyeviti wa Kamati na Wajumbe kwa taarifa nzuri, pia ninaipongeza Ofisi ya CAG kwa taarifa ambayo ametupa Wabunge kuweza kuona mapungufu.
Mheshimiwa Spika, ningependa nianze kwa upande wa Halmashauri. Jana nilimsikia rafiki yangu Boniphace Getere alizungumza kwa uchungu sana kuhusiana na madudu yaliyofanyika kwenye Halmashauri yake, hili ni somo zuri sana la kujifunza. Sisi Wabunge wote humu ndani tunamheshimu sana Mheshimiwa Boniphace Getere kwa sababu ya information, ni mtu ambaye anajua vitu kabla ya wengine hamjajua. Hebu fikiria mtu tunaemheshimu kama hivi Halmashauri yake kuongoza kuwa na Hati Chafu. Hili ni suala ambalo tunahitaji pia Serikali itusikilize.
Mheshimiwa Spika, siyo kwamba Mheshimiwa Boniphace Getere hajawahi kuona haya matatizo kabla, ameyaona hata kabla ya Mkaguzi lakini sasa ni nani anachukua hatua ambapo Mheshimiwa Boniphace anapoona yale matatizo akiyapeleka kwa wahusika yanachukuliwa kama majungu.
Mheshimiwa Spika, sasa najiuliza mara mbili mbili, hivi ni kweli Wabunge kwenye Halmashauri zetu tunasubiri mpaka Mkaguzi wa Hesabu za Serikali atutangaze kwenye vitabu kwamba Halmashauri yako ina Hati Chafu? Hapana hii ni aibu. Ni lazima tuone namna! Nilikuwa najaribu kujiuliza kaguzi kama tatu nikiwa hapa Bungeni, madudu mengi sana yanaonekana yako Halmashauri, ni kweli tunajadili humu na tunasema, sasa najiuliza tulitengeneza Sheria kwamba Mheshimiwa Rais anakabidhiwa ripoti ya CAG halafu inasema ipelekwe Bungeni sasa kujadiliwa kwenye Bunge la Wananchi, nasi tunakuja tunaongea, lakini mwakani yale yale yamezaa na kuzaa! hii siyo sawa nafikiria nasi tubadilike ni lazima na sisi tuone namna ya kuishauri Serikali au tuone namna kama ni Sheria tulitunga Sheria mbaya basi tubadilishe, hakuna maana ya kuja kujadili wizi kila mwaka, wizi wakati hakuna hatua zinazochukuliwa.
Mheshimiwa Spika, najaribu kuchukua mfano mmoja, utanisamehe maana wewe ni Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Law School. Ni kama pale Law School watoto wanavyolalamika kila mwaka, wanalalamika wanafunzi 600 wanafaulu 26 na sisi hatuchukui hatua, sasa najiuliza wakalie wapi? Kwa sababu tatizo ni walimu au tatizo ni wanafunzi? Maana kila mwaka Law School wakimaliza Mia Sita wanafaulu wanafunzi 20 au wanafunzi 30 na hakuna hatua tunachukua kama Bunge. Sasa ndiyo kama huku, kama chuo hakifaulishi tatizo ni Walimu wa Chuo au tatizo ni Wanafunzi? Sasa tunaambiwa kila siku na CAG matatizo yako Halmashauri na Bunge tunawalalamikia Viongozi wetu huku kuna wezi, huku kuna nini lakini matatizo yanajirudia yaleyale na hatuchukui hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili suala ningeomba sana Wabunge tuone aibu na ingependeza zaidi, maana wananchi wetu wanajua na ikitokea Halmashauri yako imepata hati chafu wa kwanza kuwa mchafu ni Mbunge kwa sababu wewe ndiyo wamekuchagua uwe mle, uwasaidie kuwasemea, uwasaidie kusema huyu ni mbovu, sasa unanioneshaje mimi kama Mheshimiwa Musukuma ni mchafu na sina uwezo wa kukagua hesabu, sina uwezo wa kusimamia miradi mpaka inakuja kusemwa na CAG? Nilikuwa nashauri sana kama wenzetu huko nyuma walikosea kutunga sheria, hili Bunge ni la kisasa tubadilishe sheria ili tutengeneze adhabu humu ndani. Nami naunga mkono maneno ya ndugu yangu Mheshimiwa Kunambi, mengine hatuungani lakini hili nakuunga mkono.
Mheshimiwa Spika, labda tufike wakati hizi nafasi za Wakurugenzi zitangazwe. Ukiuliza Wabunge humu kila mtu ana presha na Mkurugenzi! Mbunge pale yupo yupo tu kama mpita njia, yale mambo mabovu anajua sasa hivi mko kwenye Bunge anapitisha fastafasta na anakualika leo kesho ngoma inatembea, ninaomba sana kama tulifanya makosa huko nyuma ni vizuri tukarekebisha maana sote ni Wabunge, tunatoka kwenye Majimbo kwa hiyo, siyo vizuri na siyo sahihi kusemwa humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ninadhani hata kwenye Ofisi ya CAG inatakiwa tuseme vizuri, kuna vitu najaribu kuona hapa sijui kama nitatumia lugha ya kuudhi kwamba muda mwingine hizi hati safi na hati chafu hazipatikani hivi hivi, kuna sehemu ambapo ni pachafu pamepewa hati safi, sitaki kutaja ni wapi. Sasa najiuliza, wenzetu hawa wanapokuja kukagua pengine huwa kuna mazungumzo ili itengenezwe hati safi na hati chafu au ni vitu gani? Kwa hiyo, nishauri na wao watu wa CAG wanyooke kama wanavyotaka sisi tunyooke kwenye ripoti ili ripoti zao ziwe na msimamo mzuri. (Makofi)
Mheshimwa Spika, kwa mfano, kwenye Halmashauri tunapata wageni kwa mfano Mawaziri mnapokuja. Na hili Mawaziri mtusikilize mtuelewe, mnapokuja kwenye Halmashauri zetu punguzeni mwendokasi kwa sababu haya mambo tunayajadili humu mnayasikia na kila siku tunawauliza maswali, lakini Waziri unakuja dakika kumi unapelekwa kwenye majengo huna muda wa kusikiliza, sasa unajiuliza yaani Waziri unakwenda kupima performance ya Halmashauri kwa kukagua tu jengo au darasa lililopakwa rangi vizuri? Hapana kaeni ndani mtusikilize tunazungumza nini, sikilizeni Madiwani, kuna sehemu Madiwani hawana nafasi hata ya kuwashauri Wakurugenzi.
Mheshimiwa Spika, Mimi najiuliza sijui muundo wetu sijui ulikuwaje kwa sababu hebu jiulize, huwa namuona Mheshimiwa Waziri Mkuu akienda mahala anakaa anaanza kutaja Tarehe Fulani, wiki fulani, document fulani huwa anatoa wapi hizo document? Kwa sababu nanyi ni Mawaziri, mbona huwa hampati huo muda wa kuwaambia hivyo wale mnaoweza kuwawajibisha? Lakini tunaona Mheshimiwa Waziri Mkuu anapoenda akifika pale anaeleza yale, anasindikizwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama hili nalo ni tatizo lingine tukitaka kukomesha haya mambo. Kwa sababu Kamati zetu za Ulinzi na Usalama, Mkuu wa Wilaya uwezo ni mdogo wa Kwenda kukagua, ili akakague anahitaji mafuta ya Mkurugenzi, hivi vitu hawezi kuvikemea hata kidogo, kwa sababu mtu amekuwekea mafuta, ukute amekuandalia na lunch, haya mambo utafanya kwa design gani? unakuwa kama mtumwa! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unajisikiaje Mheshimiwa Waziri Mkuu ukifika pale unakosoa? Niliona kajengo Milioni 20, mimi naweza kukajenga kwa Milioni Moja na Laki Tano na Kamati ya Ulinzi ipo, unawaambie eeh… na jana walienda ku-reck njia ya Waziri Mkuu anapoenda pale, sasa najiuliza kwa nini tusifukuze wote wale? Kwa sababu kuna vitu vingine kwenye muundo wa Serikali vilitengenezwa kwamba hili litafatiliwa na mtu fulani, lakini wenzetu hawatimizi majukumu yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ningeomba sana suala la Halmashauri linahitaji muda, Wabunge tupewe heshima tunapoleta matatizo yetu kwa Mawaziri, Mawaziri chukulieni serious, sisi siyo wapiga majungu! Mnachukua maneno yetu mnayapeleka kule ndani yanageuka kwamba huyu ni mwongeaji! Hapana, mwisho wake mtatukatisha tamaa na sisi tuwe watazamaji ili mkija, nakaa nyuma, ukiuliza maswali na mimi nashangaa. Hivyo, ni vizuri zaidi tuone wivu na Ubunge wetu siyo vizuri kuanza kukosoana humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni suala la asilimia Kumi, kama tuna mahala tulikosea muundo wake ni hapa. Hizi ni hela unamchukua mtu wa Maendeleo ya Jamii, unamkabidhi Halmashauri kama ya Geita ambayo kwa mwaka inatoa asilimia Kumi Shilingi Bilioni Moja, halafu anakwambia miaka mitatu sijakusanya. Hivi tuna watu wangapi waliosoma mambo ya uhasibu, mambo ya fedha? Kila siku benki zikitangaza kazi watoto wanaomba mpaka Elfu Tano, Elfu Kumi, kwa nini tusiwe na Kitengo cha Benki kwenye Halmashauri ambapo zinao uwezo? Kama hatuwezi kuna Mbunge mmoja jana alisema, tukubaliane na mabenki, tupunguze tu masharti kwenye kitengo cha vijana walemavu na akina mama, lakini fedha ziwe benki, watu ambao wana uwezo wa kuzikusanya hizo hela. Unakuta Halmashauri inadai karibia Bilioni Kumi na Sheria inakutaka utoe, sasa tunachukua hela tunaenda kuzigawa ambazo hazina return siyo vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilitaka nizungumze kuhusu DART, nimesoma kwenye DART yale mambo ya mwendokasi, huwa najiuliza mara mbilimbili kwamba, DART tunamiliki miundombinu, kuna mwingine anaendesha magari, hata mwaka mmoja kila siku ana-declare matatizo, lakini Serikali inachukua ela inarundika kutengeneza mabarabara, tuliutumia mfumo mzuri kweli kwamba, Serikali inatumia mabilioni ya pesa kutengeneza barabara kwa ajili ya kumtengenezea mtu mmoja apitishe magari ambayo tena hayafanyi vizuri! Sasa najiuliza tuna Mkurugenzi, tuna nani, tuna makoloko kwenye idara ambayo haizalishi! Ni vizuri tukawa tunatengeneza miradi ambayo inazalisha
Mheshimiwa Spika, nilikuwa namsikiliza Ndugu yangu Mheshimiwa Kunambi hapa anasema hotel nyota tano sijui nini, lakini kama kuna vitu wasomi mnatuangusha, Mimi ni Daktari wa heshima ni hapo, kutengeneza vitu ambavyo havina return. Mimi ninakaa Dodoma hapa huwa naumia sana nikipita pale nikiona ile hotel najiuliza kwamba, wasomi walikaa na ku-discuss kutengeneza ile hotel wanaita mmh! (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, wakati hapa Dodoma kuna maeneo ya heka kumi na yeye ndiye aliyekuwa anauza viwanja! Hii hotel ilikuwa nzuri na ya mfano ya kutengeneza Jiji, ingekuwa sehemu yenye heka tano, hivi vitu unatengeneza soko halafu unajisifu, tuambiwe return hizi ni hela za wananchi…
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, taarifa!
SPIKA: Mheshimiwa Musukuma, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kunambi.
T A A R I F A
MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa ndugu yangu Musukuma kwamba, tulikuwa tumeangalia kwenye hotel anazosema, kuna ile ya Mjini inaitwa Drop off Hotel na lengo tuliangalia viability of the project, returns on investment, tuliangalia pia muda gani utatumika. Kwa ile kulingana na andiko letu ilikuwa ni miaka sita, sasa hoja tulisema wawa-engage operator ili a-operate, lakini ndani ya miaka sita ile fedha ilikuwa inarudi Bilioni Tisa. Kwa maeneo anayosema, Mji wa Serikali tukaona lile eneo ni kubwa, tukatengeneza hotel nyingine ambayo ni ya nyota nne yenye parking kubwa sana. Kwa hiyo msingi wa hotel ya Mjini ni drop off hotel hata Dubai zipo. Ahsante. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Msukuma unapokea taarifa hiyo.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, siipokei taarifa hiyo, mwenye macho ameona na mwenye masikio amesikia, kwa sababu tutajibishana na ninamheshimu ni mdogo wangu na nimheshimiwa Mbunge lakini ni lazima tushauri vitu vyenye maendeleo.
Mheshimiwa Spika, ukichukua hiyo hotel anayoisema na vitu viwili vitatu umevisema ukiweka na soko la Ndugai nikikuuliza return yake hata na mimi nitakuwa nimeshakufa bado hata theluthi moja haijawahi kuwa na return, halafu unasema hiki tunatengeneza chanzo baada ya kumaliza ardhi, Hapana! Tutengeneze vyanzo vyenye maslahi, tushauri watu, vitu vyenye maslahi.
Mheshimiwa Spika, kuna Mjumbe jana alisema humu ndani, ukienda kwenye kila Halmashauri wote tunaandika maandiko kwa sababu hela zipo tunataka stendi, lakini stendi siyo mradi endelevu. Kuna watu wengine wameweka stendi baada ya miaka mitano au 10 haina return yoyote. Lazima tuone sehemu kama Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, kwenye Majiji sawa lakini unachukua stendi ya Bilioni 29 unaenda kuweka kwenye Halmashauri inayokusanya Laki Tatu na Hamsini kwa siku, halafu unaita mimi nimesoma, nimefanya upembuzi yakinifu, hiyo haiwezekani! Tunawaingiza chocho kwa sababu wanaolipa ni wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na wewe kwamba tunavyo vyanzo vya mapato ambavyo vitalipa yale madeni, kwa nini tusifikirie kuisaidia Serikali kama ulivyojenga kule Mlimba Vituo vya Afya na vitu vingine ambavyo moja kwa moja vitakwenda kuwasaidia wananchi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ningeomba nishauri suala lingine moja la mwisho. Nimepita pale Dar es Salaam ninajua tu hili litakuja kuamka, jana humu ndani nimesikia wamechangia. Ukiangalia mwendo kasi leo wa kutoka Mbagala stendi yake imeenda kuangukia pale kilipojengwa kitovu cha ramani nzuri sana ya mwendokasi mkubwa, watoto wa mjini tunaita Tanzanite pale. Jiulizeni jamani mtu anatoka Mbagala halafu kituo kinakuja kuangukia palepale kwenye ramani ambayo tunachukua ramani hata Kimataifa tunarusha kwamba mwendokasi, tunadondoshea kituo pale cha watu wanatoka Mbagala. Kwa hiyo, mwingiliano ule ni vizuri yaani…(Makofi/Kicheko).
Mheshimiwa Spika, kwanza hata ramani, najiuliza kwa nini tusingeondoa elimu za darasani tukatumia kama yangu ya heshima? Yaani nafikiria unajiuliza kabisa kwamba wamekosa sehemu yoyote ya kuweka kituo? Ramani ya ile Tanzanite, glass yote ile nzuri, halafu inakuja kudondoshewa pale pale giiih!, Mtu ametoka rangi tatu kule, huku inaka…jamani, jamani ndugu zangu na lenyewe tunasubiri CAG mwakani atuletee taarifa? Kwa hiyo, ninaomba sana niwashauri, tuna wivu na Ubunge na Wasomi wetu tunawapenda, ningeomba mtumie shule zenu vizuri. Ninakushukuru ahsante sana.(Makofi/Kicheko)
SPIKA: Kengele ya pili Mheshimiwa.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, ahsante sana.