Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kupata nafasi hii ya kuwa mchangiaji wa kwanza kwa mchana huu. Nitachangia kwenye taarifa ya Kamati ya LAAC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naishukuru kwanza Serikali yetu chini ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo imeendelea kutuongoza vizuri na kuwapelekea wananchi wetu huduma mbalimbali ikiwa ni za kiuchumi, za kijamii na kadhalika. Hivi ninavyozungumza, jimboni kwangu tulikuwa tunakabiliwa sana na tatizo la chakula, lakini leo hii kuna chakula cha bei nafuu ambacho kinashushwa kupitia NFRA. Naishukuru Serikali, na kipekee namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, nilimlilia sana na hata kuomba kuongezewa kwa sababu ya hali ilivyo. Kwa hiyo, Serikali inafanya kazi nzuri kiuchumi, kijamii na pia kuwahudumia wananchi pale panapokuwa na majanga.

Mheshimiwa mwenyekiti, shughuli zote hizi, wasimamizi wakuu ni Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo nazizungumzia leo kwenye taarifa hii ya LAAC. Sote ni mashahidi kwamba miradi mingi inatekelezwa na mamlaka hizi. Nikitoa tu mfano kwenye Jimbo langu la Mwanga, Halmashauri ya Mwanga inasimamia vizuri ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, kazi inakwenda vizuri; Halmashauri imesimamia vizuri ujenzi wa Vituo vya Afya, na sasa wanamalizia Kitua cha Afya cha tatu cha kimkakati, shule na kadhalika. Kwa hiyo, kwa kweli wanafanya kazi nzuri, nawapongeza Halmashauri yangu ya Mwanga, Viongozi wote pamoja na Baraza la Madiwani kwa kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi hizi wanazoendelea kuzifanya sasa, ili waendelee kuzimudu vizuri, yapo mambo ambayo Serikali pia inahitaji kuendelea kuyafanya kwenye Halmashauri zetu. La kwanza hasa ni kuwajengea uwezo kwenye eneo la Bajeti. Halmashauri yangu ya Mwanga kwa hesabu hizi tulizozizungumzia za mwaka 2021, ilipokea 33% tu ya bajeti iliyotengwa. Sasa hili ni tatizo kubwa sana kutegemea utekelezaji wa miradi kwa asilimia kubwa kwa kiwango cha bajeti ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ipo changamoto pia ya watumishi. Nikitolea mfano hapo hapo kwenye Malmashauri yangu ya Mwanga, mahitaji ya jumla ya watumishi ni 3,117 lakini halisi tulionao ni 1,861, kuna upungufu wa 1,256, upungufu huu ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye sekta mbili nyeti sensitive; Afya mahitaji ni watumishi 786, lakini halisi ni 336 tu, kuna upungufu wa 400. Ukija kwenye elimu; elimu msingi mahitaji ni 1,274, lakini actual tulionao ni 674, na upungufu ni 450. Ukija kwenye elimu ya sekondari, mahitaji ni 683, halisi ni 583, kwa hiyo kuna upungufu wa
100. Kwa hiyo, pamoja na yote hayo tunayozungumza, lakini ni vema tukawajengea uwezo wa kibajeti, pia suala la watumishi na kuwajengea uwezo katika mifumo ambayo inafanya kazi kule, hasa mifumo hii ya kielektroniki ambapo imeonekana wazi kwamba ziko halmashauri nyingi ambazo zina upungufu wa watu wenye uwezo wa ku-manage mifumo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kutupitisha juzi kwenye mfumo huu wa TAUSI, sisi tumeuelewa kidogo, lakini tungependa kuuelewa zaidi. Sasa kama wenzetu kule hawatajengewa uwezo wa kutosha ambao ndio watumiaji wakuu wa mfumo huu, kutakuwa kuna tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo linahitaji kujengewa uwezo ni juu masuala ya mikataba na manunuzi. Sasa pamoja na mafanikio haya na haya yote ambayo nimeomba kwamba wawezeshwe, bado katika mchakato wa kazi hii tuliyoifanya kwenye Kamati, yako mambo ambayo bado wangeweza kuyatimiza lakini hawajayatimiza, nami nitazungumzia maeneo kama manne tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza, zipo kesi nyingi sana Mahakamani zinazoendelea na zilizokwisha. Kuna ambazo halmashauri zetu zinashtakiwa na kuna ambazo halmashauri zetu zinashtaki. Nikizungumzia zile ambazo tunashtakiwa, ziko ambazo nyingi tumeshindwa, lakini tukumbuke kwamba halmashauri haipelekwi Mahakamani kabla haijapewa notice ya siku 90.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wito wangu kwa halmashauri ni kwamba kwa kesi zile ambazo wanaona kabisa kwamba hapa mtu ali-supply kitu chake, kuna delivery note, kuna invoice na kila kitu, wanapopewa ile notice ya siku 90 watumie huo muda ku-settle hizi kesi kuliko kuacha ziende Mahakamani tushindwe halafu tuingie gharama kubwa ya kuja kulipa riba na gharama na kadhalika. Pale ambapo tumeshindwa, na kuna sababu za kukata rufaa, ni vizuri rufaa ikakatwa ndani ya muda ili tusiendelee kupoteza muda halafu tukaingia hasara kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko settlement ambazo zimefanyika nje ya Mahakama, ni vizuri halmashauri zikafuata utaratibu wa kusajili zile settlement Mahakamani ili tusije tukaingia shida wakati wa utekelezaji wa hukumu tukashindwa kupata kile ambacho tunatakiwa kupata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni masuala ya mikataba. Halmashauri zetu zinaingia kwenye mikataba mingi sana, ipo mingine mizuri na mingine mibovu; lakini upo udhaifu ambao ningependa kuuzungumzia. Udhaifu wa kwanza ni kutokufuata mikataba inavyotaka. Tumekutana na maeneo mengi sana ambapo mkataba wa ujenzi unasema kabisa kwamba kabla mkandarasi hajalipwa yale malipo ya awali (advance payment) lazima alete advance payment guarantee, lakini yapo maeneo ambako mkandarasi amelipwa bila advance payment guarantee, amefika mahali sasa ameshindwa, tunashindwa kupata zile fedha na hao wenzetu wakiulizwa huko, hawana maelezo kwamba kwa nini hamkuchukua advance payment guarantee?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sidhani kama Wanasheria wetu kule kwenye halmashauri au Maafisa Mipango au Wakurugenzi wanashindwa kusoma mikataba kwa mambo mepesi kama hayo. Kwa hiyo, hili ni eneo ambalo wanatakiwa kulikazia kuhakikisha kwamba wanafuata mikataba inavyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuna baadhi mikataba ambayo kwa kweli ni dhaifu. Yapo matukio ambayo tumekuta halmashauri tatu zimepewa dhamana moja kwa ajili ya mradi fulani, yaani mkataba unataka kwamba kabla yule mzabuni hajapewa ile tenda, basi alete dhamana. Sasa mtu anakuja ameshinda tender kwenye Halmashauri ‘A’ analeta hati, anaweka pale, labda inapigwa copy hapo, kinyume kabisa na utaratibu, anaondoka nayo, anaenda kuchukua tender ya Halmashauri ‘B’ na Halmashauri ‘C’, sasa amefika mahali ame-default kote, wanashindwa ku-recover kwa sababu hati ni ile ile moja, kila mtu anaing’ang’ania na licha ya hivyo, utakuta thamani yake ni ndogo zaidi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu katika eneo kama hili, suala la kuchukua dhamana ni suala ambalo linafanyika na mabenki au na makampuni ya insurance, ambao wakishachukua ile dhamana, wao wanaisajili ile dhamana, halafu wanatoa guarantee kwa Halmashauri ili iendelee kumpa kazi yule mzabuni ambaye amepata. Wao wana uwezo wa kuchukua hata dhamana moja kwa halmashauri tatu kwa sababu wanazitengeneza kwa uratatibu wa Pari-Passu ambao unasajiliwa, na pale kunakuwa na default, kila mtu pale anapata haki yake, kwa sababu wanaangalia thamani ya ile dhamana, thamani ya mikataba ambayo inatakiwa kutoa dhamana ile, wanaitoa kwa utaratibu wa sheria na kunakuwa hakuna matatizo. Ila halmashauri zinapochukua kienyeji, ndiyo matokeo yake unakuta hati moja imedhamini halmashauri tatu tofauti na default inatokea, wote wanashindwa ku-recover. Tumelikuta hili sana kwenye halmashauri, tunaomba lizingatiwe kwa nguvu sana, lirekebishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la kukabiliana na vitendo vya ubadhirifu, wizi, kughushi, matumizi mabaya ya madaraka na kadhalika. Hivi vitendo vinajitokeza kwa wingi kwenye halmashauri zetu, lakini imekuwa kama dini sasa kwamba likitokea tatizo, TAKUKURU; mtu anadaiwa deni, peleka TAKUKURU; mtu amekimbia na hela za POS, amekusanya amekimbia nazo, peleka TAKUKURU; Mkandarasi hajamaliza ujenzi wake, peleka TAKUKURU. Sasa tunawajazia TAKUKURU mzigo wa mambo ambayo hata uwezo wao siyo mkubwa kiasi hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi sote Waheshimiwa Wabunge, tuangalie kwenye majimbo yetu tuone Ofisi za TAKUKURU zina wafanyakazi wangapi; zina magari mangapi; zina resources kiasi gani za kukabiliana na haya mambo? Mengine ni mambo ya wizi yanayotakiwa yapelekwe Polisi yashughulikiwe na mambo mengine ni ya utakatishaji fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kuna halmashauri ambayo fedha za TANESCO za kwenda kufidia watu ambao zile waya za high tension zimepita kwake, zimekuwa diverted zikapelekwa kwenye vijiji, kutoka kule zikapigwa kwenye account za watu binafsi wakagawana, lakini mwisho wa siku unaambiwa Watendaji wa Vijiji wamepelekwa TAKUKURU, lakini wale wakubwa, huyu kahamishiwa huku na huyu kahamishiwa huku. Tunaipa mzigo TAKUKURU bure, tutailaumu wakati ambapo kwa kweli haya mambo wakati mwingine hayako ndani ya mamlaka yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachosisitiza ni kwamba tusibebeshe TAKUKURU kila mzigo. Haya mambo yaende kwenye kila taasisi kwenye vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambavyo vina mamlaka ya kisheria na uwezo wa kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo nimeliona lina-shout, yaani linaonekana kila mara, ni udhaifu unaotokana na matumizi ya force account hasa kwenye miradi ya ujenzi. Utaratibu wa ujenzi uko wazi sana, kwamba mradi wa ujenzi unaanza na msanifu (architect) anachora, halafu unakwenda kwa mkadiriaji wa ujenzi (quantity surveyor) anakadiria kwamba gharama ni kiasi gani, halafu kunakuwa na yule mjenzi; na mjenzi kuna contractor yule aneyejenga na kuna structural engineer; na kila mmoja hapa ana majukumu yake kisheria na yote ndiyo yanayopelekea kwenye kupata value for money.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo utaratibu sasa ambao tunaukuta kule, unaenda unakuta mchoraji, yaani msanifu, Tadayo; mjenzi, Tadayo; sijui consultant ni huyo huyo. Kwa hiyo, hata zile certificate ni yeye mwenyewe anangalia, anajikadiria, anasema hapa nilipwe kiasi fulani. Tukiendelea hivi, hatutapata value for money. Tutapata product ambayo ni dhaifu na tusije tukalaumu sana hawa wakurugenzi au wale watu wanaosimamia ambao wengine ni walimu, lakini hao watu walioweka utaratibu kwamba miradi ya ujenzi iende na wataalamu wa fani mbalimbali walikuwa na maana kabisa kwamba bila hivyo hatuwezi kupata value for money. Sasa hiki ndicho kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukikuta namna hiyo, utakapoenda kusoma lile bango la ujenzi, utakuta hata building permit hakuna, kwa sababu huwezi kupata building permit kama huja-involve hizi taaluma zote ambazo nimezitaja hapa. Kwa hiyo, hili jambo nadhani tunahitaji kuwa serious. Kama hatuna hao wataalam, tujaribu kutumia hata wataalam kutoka maeneo mengine ili tu kuhakikisha kwamba tunapata value for money. Hela inayokwenda kwenye halmashauri zetu kwa kweli ni kubwa, ni lazima tuitendee haki kwa kuhakikisha kwamba kazi inayifanyika inakidhi viwango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, siyo mwisho kwa umuhimu, mimi binafsi katika mchakato wa kazi yetu ya kamati, nawiwa kabisa kuishukuru sana Ofisi ya CAG kwa kazi ambayo wamefanya. Ofisi ya CAG imekuwa mwalimu, imekuwa mlezi na imekuwa na umuhimu mkubwa sana katika hizi halmashauri zetu. Watakaofuata ushauri wao, watapona, lakini ambao hawataufuata watatuletea matatizo na hatutakubali kuendelea kuwa na matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, naunga mkono hoja ya Kamati kama ilivyoletwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)