Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza kabisa, ningependa kumshukuru sana Rais wetu mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Pia, yeye akiwa kama Rais wetu tunaona nia njema ambayo anayo kwa nchi yetu kwa kumpa maelekezo CAG, kwamba afanye uchambuzi wa kina, asipepese macho, aandike ripoti yenye kueleweka ili tuijenge nchi yetu. Ripoti hii ya CAG ambayo tunaiangalia leo sisi kama Wabunge tunapaswa kutimiza jukumu letu la kuisimamia na kuishauri Serikali kwa niaba ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mengi ambayo yameelezwa ndani ya Ripoti ya CAG, lakini mawili makubwa ambayo ningependa kuyaangalia; kwanza ni uwekezaji wenye tija, lakini pia kuangalia sehemu ya matumizi. Tunazungumzia Mitaji ya umma, kwangu mimi moja ya mitaji mikubwa ya umma ni nguvu kazi, ni rasilimali watu. Katika ripoti hii ya CAG, tunaona kuna watoto 53,755 ambao waliandikishwa kuanza darasa la kwanza kati ya mwaka 2018 na 2021 ambao hawakumaliza elimu ya msingi. Tunafahamu nchi yetu inawekeza fedha nyingi sana kwenye elimu ya watoto wetu, kile ambacho kinaitwa elimu bure sio bure, mlipakodi wa nchi hii analipa fedha nyingi kama capitation kwa ajili ya watoto wetu waende shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto hawa ambao wanaandikishwa darasa la kwanza hawafiki la saba, maana yake uwekezaji mkubwa ambao unafanywa na nchi hii na walipa kodi wa nchi hii unapotea bure. Ningeomba kwa unyenyekevu kabisa, Bunge na Serikali kuchukulia ripoti hii kwa umakini mkubwa. Watoto 53,755 si idadi ndogo, watoto hawa wanaondoka katika mfumo katika elimu ya msingi. Tunapozungumzia elimu ya msingi huko ndiko tunapojenga Taifa, zile manners ndogondogo, raia mwema anatakiwa ku-behave vipi, kuheshimu wakubwa na wadogo, kuheshimu mamlaka, zote zinafunza katika katika shule ya msingi na ndiyo maana inaitwa msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuta watoto hawa wanaondoka katika mfumo huu wa elimu ya msingi, maana yake sio tu tunapoteza Watoto, lakini ni suala la security ya nchi yetu. Watoto hao wako wapi? Wanafanya nini? Wamekwenda wapi? Nani ambaye anasumbuka kujua watoto hawa wapo wapi? Watoto 53,755 si watoto wachache na hili ni suala la security ya nchi yetu na ni lazima tulichukulie kwa uzito ambao unastahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia kuwekeza kwa wananchi wetu, kama ilivyo kwenye elimu tunavyowekeza kwa hawa Watoto, lakini pia Serikali imekuja na mpango maalum kabisa wa kuwezesha makundi maalum ya vijana, wanawake na walemavu. Fedha ambazo zinatengwa kwa ajili ya makundi haya, kuyakwamua katika hali ya umaskini ni fedha nyingi sana ukilinganisha na mahitaji ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua bajeti yetu ya nchi, fedha ambazo tunalipa madeni, fedha ambazo tunalipa mishahara ya watumishi wa umma, fedha kidogo ambayo inabaki kwa ajili ya maendeleo, hatuna anasa ya kupoteza hata shilingi tano. Hatuna anasa hiyo, kwa sababu tunapambana kukusanya hela ambayo inaishia kwenye mahitaji ya lazima, hatuna fedha za kufanyia anasa. Unaposikia fedha zinapotea, fedha za umma zinapotea, inaumiza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, hesabu ambazo CAG amewasilisha kati ya mwaka 2020/2021, zaidi ya bilioni 75 za mikopo zilitoka katika mwaka huu mmoja wa bajeti. Katika hizo zaidi ya bilioni 47 hazijarejeshwa. Fedha hizi ni nyingi sana, fedha hizi zinaweza zinaweza kubadilisha maisha ya watu wengi katika nchi hii, kutengeneza barabara za vumbi kuwa za changarawe kilometa za kutosha; kutengeneza lami nyepesi, kutengeneza shule za msingi, shule za sekondari, zikakarabati vyuo vya ufundi, zikapeleka hata vifaa tiba katika hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaposikia kuwa fedha hizi zimepotea na hatuoni jitihada za kweli za kuzikusanya fedha hizi, Bunge lako haliwezi kunyamaza. Ningeomba kwa namna ya kipekee, kwanza kabisa nishukuru Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kuna jitihada za wazi ambazo imezichukua kuhakikisha kwamba wanaenda kusimimamia suala zima la utoaji wa mikopo lakini pia ukusanyaji wake. Ni hatua nzuri lakini jitihada pia zifanyike, kuhakikisha kwamba zile fedha ambazo zimetoka kimichongo wahusika wanachukuliwa hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kutoa mkopo ni suala moja na suala la haki kwa makundi ambayo yanastahili kupata mkopo ni suala lingine. Wote ni mashahidi, juzi tulikuwa na mjadala mrefu sana kuhusiana na haki ya mikopo kwa wale ambao wanastahili elimu ya juu. Vijana wetu ambao wameomba mikopo na wanastahili kupata mikopo lakini hawajapata mikopo, hali si tofauti kwa mama zetu kwa vijana na walemavu katika halmashauri tunazotoka. Kuna makundi mengi ambayo yanastahili kupata mikopo hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la uwazi kwenye ugawaji wa fedha hizi, linafanya makundi mengi ambayo yanastahili kupata fedha hizi wasizipate. Matokeo yake, Wabunge na Madiwani wamekuwa wahanga wa lawama kutoka kwa makundi haya na wenyewe wanabakia kulalamika kwa sababu hata ushirikishwaji wao si mkubwa ukilinganisha na majukumu waliyonayo hasa kuwa sehemu ya majibu ya changamoto kwa wananchi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado naomba tena, nilizungumza mwaka jana, lakini nazungumza tena leo, rasilimali za halmashauri kutumika kwa uwazi, kutumika kwa haki na wale wote ambao wana haki ya kupata fedha hasa hizi za ten percent, basi wajulikane na taratibu zijulikane na wao wanufaika wapate fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni mgawanyo wa fedha za asilimia 40 kwa 60. Kwa maana fedha za matumizi mengineyo, lakini pia fedha za maendeleo. Haiyumkiniki na sijadili busara ya hawa ambao walitengeneza vigezo hivi, lakini napata shida sana kuona kwamba kuna halmashauri ambayo inapata bilioni 30, inaambiwa itenge asilimia 40 kwa ajili ya matumizi mengineyo na halmashauri nyingine ambayo inapata milioni 800 ama bilioni moja na yenyewe inaambiwa itenge asilimia 40 kwa ajili ya matumizi mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiziangalia hizi halmashauri, utakuta huyu ambaye anaingiza bilioni moja anajitahidi kulipa malimbikizo ya posho za watumishi wake, Wauguzi na Walimu, lakini utakuta huyu ambaye anapata bilioni 30 hajishughulishi na madeni ya watumishi wake. Pia, hata kupeleka fedha ambazo kisheria anapaswa kupeleka, kwa maana ya asilimia 10 hapeleki. Sasa, rai yangu kwa Serikali tujaribu ku-review mgawanyo wa fedha za matumizi mengineyo na fedha za maendeleo. Ikiwapendeza waone mgawanyo wa haki ili fedha nyingi ziende kutibu matatizo na changamoto ambazo Serikali kuu haiwezi kuzibeba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nilizungumze hapa, ni suala la matumizi ya hii akaunti ya Amana. Ripoti inaonyesha kwamba kimekuwa ni kichaka cha kufichia fedha, lakini pia kufanyia ubadhirifu. Ni rai yangu, hatua zichukuliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile matumizi ya bakaa, fedha za bakaa kwa maana ya salio ambalo halmashauri inaingia nalo katika mwaka mpya wa fedha. Sheria ya Matumizi ya Fedha za Serikali za Mitaa zinaitaka halmashauri kuripoti kwenye vikao katika robo ya kwanza, lakini haizungumzii baada ya robo ya kwanza wanaripoti wapi na chenyewe ni kichaka cha matumizi mabaya ya fedha za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni rai yangu kwa Serikali na ikipendeza Bunge lako, ripoti ya matumizi ama kuchunguza akaunti za amana kwenye halmashauri zetu, lakini pia matumizi ya fedha za bakaa, ripoti hiyo ije kwenye Bunge tuijadili, kuona uhalali na matumizi sahihi za fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia suala la uwekezaji wenye tija; halmashauri nyingi zimewekeza kwenye kile ambacho kinaitwa miradi ya kimkakati. Kwa mfano, stendi za malori na za mabasi lakini pia masoko. Pia, kuna halmashauri ambazo hazina wataalam wa kuandika maandiko, hazina utaalam huo, nyingi zimeishia kuwa wahanga wa mfumo wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kuna ajenda ya kuzisaidia halmashauri hizi, ikiwemo Kilosa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)