Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia ripoti za Kamati zetu tatu. Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na Kamati ya Hesabu za Serikali. Mimi nitajielekeza zaidi kwenye Kamati hii iliyochambua ripoti ya CAG ya Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili nimeisoma vema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwenye eneo la Mashirika ya Umma. CAG amepitia Shirika la Bandari (TPA), TTCL, TANESCO, Shirika letu la Nyumba - NHC na TRC. Nitajielekeza kwenye Shirika la TANESCO na hususan kwenye mradi mkubwa tulionao. Mradi wa Trilioni 6.5 wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, CAG anasema alivyokwenda kuangalia bwawa hili alikuta ujenzi umechelewa kuisha kwa asilimia 46.45. Bwawa hili ni la muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu, Watanzania wanahitaji bwawa hili likamilike ili tuweze kupata umeme wa uhakika. Viwanda vyetu vinahitaji bwawa hili likamilike ili viweze kufanya uzalishaji. Miradi yetu ya REA tunayoitengenza sasa inahitaji bwawa hili likamilike ili iweze kupata source ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gridi yetu ya Taifa ili iwe na umeme stable inahitaji bwawa hili likamilike ili tuweze kupata umeme wa uhakika. Vilevile, gharama zetu za umeme ziko juu, umeme wa maji ni umeme cheap kuliko umeme wowote, Watanzania wanahitaji bwawa hili likamilke ili waweze kupata umeme wa gharama nafuu. Sasa taarifa zilizopo hivi sasa, ukizingatia hii taarifa ya CAG, kwamba ujenzi umechelewa, bwawa lilitakiwa likamilike mwaka huu mwezi wa Sita, mwezi wa Sita umepita bwawa halijakamilika, hivi sasa ujenzi uko asilimia 74 na bado hujakamilika, Mkandarasi na Serikali wanabishana. Mkandarasi anaomba kuongezewa miaka mingine miwili zaidi na kwa maana hiyo kwa mujibu wa Mkandarasi, bwawa hili litakamilika mwaka 2024. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali wao wanasema kwamba wamekataa kumwongeza miaka miwili, badala yake wamemwongeza mwaka mmoja. Nataka nilipitishe Bunge hili sababu ambazo zimetolewa na Mkandarasi na mpaka wakafikia kumwongeza mwaka mmoja, pamoja na kumwongeza huo mwaka mmoja yeye bado mpango kazi ambao ameuweka Serikalini unaonesha ni miaka miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya kwanza, anaomba nyongeza ya muda na kuongezewa gharama kwa sababu watengenezaji wa mitambo walijitoa. Sababu ya pili, anaomba nyongeza ya muda na gharama kwa Watanzania kwa sababu ya taarifa za miamba. Sababu ya tatu, anaomba kuongezwa muda na ongezeko la gharama kwa sababu pale site anasema umeme haumtoshi. Sababu ya nne na ya mwisho, anaomba kuongezewa muda na gharama kwa sababu njia ya kupelekea vifaa site ni mbaya. Jambo hili halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Trilioni 6.5, kodi za Watanzania, bado inafanyika janjajanja ya kutaka tena kuongeza gharama ya mradi huu? Kuongeza gharama ya muda na gharama ya fedha? Serikali inasema sababu zilivyotolewa haikukubaliana nazo. Kama hawakukubaliana nazo nataka Waziri mwenye dhamana akija hapa atuambie, kama sababu hizi hamkukubaliana nazo kwanini mmemwongeza mwaka mmoja? Kwa nini mmekubali kumwongeza mwaka mmoja ilihali mpangokazi wake unasema anataka miaka miwili, nani mnamdanganya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali na Mkandarasi wameunda Bodi inayoitwa DAB, (Dispute Adjudication Board) kwa ajili ya kufanya suluhu ya haya. Mkataba Serikali umesema kwamba sababu hukubaliani nazo, inamaana ulitakiwa ukabidhiwe kazi mwaka huu, mkataba unasema nini kama kazi haijakabidhiwa? Kwa nini madai ya Serikali kwa Mkandarasi hapa hatuyaoni? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kushangaza mpaka sasa Mkandarasi tumeshamlipa asilimia 65.9 ya fedha. CAG anasema mradi umechelewa, Mkandarasi tumeshamlipa asilimia 65.9 ya fedha zote yaani Trilioni 4.3, lakini Serikali badala ya kulipa trilioni 4.3, wamemlipa trilioni 4.43. Wamemlipa ziada ya shilingi bilioni 113. Sababu waliyoitoa ya kulipa ziada ya shilingi bilioni 113 wanasema eti ni mabadiliko ya kubadilisha dola na shilingi.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Twaha Mpembenwe.

T A A R I F A

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba tofauti hii anayoizungumzia hapa ya fedha ya Bilioni 113 fedha za walipa kodi zilizolipwa kwa uwiano wa kawaida tu, kwa fedha tulizokuwa tumezizoea kawaida kwa kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI, Shilingi Milioni 500 inajenga kituo kimoja cha afya. Kwa hesabu za kawaida hivi ni vituo 226 vya afya ambavyo vingeweza kujengwa katika Jimbo la Handeni, Kibiti na Majimbo mengine yote hapa Tanzania.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kwagilwa unaipokea taarifa?

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo taarifa naipokea, shilingi 113,196,370,381.06 eti kwa sababu ya kubadilisha dola na shilingi, mkataba gani huo kwenye nchi ya wanasheria wasomi? Yaani unawezaje kuwa na mkataba wa hivyo? Eti kwenye malipo mkianza kulipana wewe ukianza kutafuta dola unapoteza bilioni 115. Vituo 226 vya afya! Hatuwezi Kwenda hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi wengine lazima tuwaambie tu, kazi yetu hapa ni kuwaambieni ukweli. Sisi sote tutapita lakini Tanzania itabaki. Bilioni 113 kubadilisha shilingi na dola, naongelea bilioni; hii si sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu mkubwa mpaka sasa taifa halina uhakika kama utakamilika. Kwenye hili tusitake kuumauma maneno. Kutokukamilika kwa mradi huu kunafanya wananchi wa Handeni hawatapa umeme; kutokukamilika kwa mradi huu kunafanya ndugu Waheshimiwa Wabunge kwenye majimbo yenu miradi ya REA tunayopeleka haitakuwa na source ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niseme kwa lugha fupi, kwamba hii ni hujuma. Tunanunua umeme kwa gharama kubwa sana kutoka mitambo ya kukodisha. Kwa nini hatumalizi wa kwetu? Kwa nini mtu asishawishike kuamini kwamba hii ni hujuma? we cannot go like that as a nation, hatuwezi kwenda hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa sababu leo tuko hapa kuisimamia Serikali ninamwomba Mheshimiwa Spika, aunde kamati tuchunguze hili. Haiwezekani mradi ambao ni tegemezi kwa taifa usikamilike kwa wakati, na bado panaanzishwa longolongo nyingine zitakazopelekea tulipe zaidi na tukabidhiwe mradi baadaye zaidi, na huenda hata usikamilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi mikubwa tu nchi hii ya kwanza SGR trilioni 16, huu tunaotengeneza. Mradi wa pili ni huu takriban trilioni saba why can’t we be serious on this.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa muda nawashukuru sana. (Makofi)