Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba nimshukuru sana Mungu, ameniwezesha kupitia wananchi wa Jimbo la Ukonga kuingia kwenye jengo hili na naomba nitoe mchango wangu. Naomba Waheshimiwa Mawaziri wanisikilize vizuri kwa sababu Wabunge hawa wa CCM hawatawasaidia sana kwenye utendaji wa kazi, kwa hiyo, ni muhimu sana. Wanasifia yote, halafu wanalalamika mwanzo mwisho, kwa hiyo mimi utaratibu huo siupendi. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kaulimbiu ya Serikali hii ni Hapa Kazi Tu maana yake inaonesha hawa watu walikuwa wazembe muda wote tangu mwaka 1961. Wazembe tu ndio maana nasema wamezinduka sasa, eti hapa kazi. Kwa hiyo, mnapokuwa mnapendekeza kauli hizi ni muhimu mkachunguza kama zina mwitikio chanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Serikali inatumbua majipu, maana yake kuna wagonjwa wengi na ugonjwa huu umesababishwa na wenyewe CCM. Halafu Serikali ya CCM waoga sana. Ndio maana kuna polisi huku, wamezunguka jengo la Bunge, wanajaza askari humu ndani watu waogope kutoa hoja, maana yake ni waoga kweli kweli. Wangekuwa sio waoga wangetulia tushughulikiane kwa hoja na kwa vyovyote itakavyokuwa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine waongo, Serikali hii inawaambia watu utawala bora, tena utawala wa kisheria, lakini ukiangalia kauli hii na yote yametajwa kwenye mapendekezo, mmetaja, nilikuwa nasoma hapa.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mmesema utawala bora, mimi naenda kwenye hoja. Hamjasoma vizuri, utawala bora. Naamini kikwazo cha maendeleo ya Tanzania ni CCM wenyewe.
Kwa hiyo, tukipanga mipango tukajadiliana, siku CCM ikitoka madarakani, nchi hii itapata maendeleo makubwa sana. Kwa hiyo, nawaambia Watanzania wajipange kuiondoa CCM madarakani ili wapate maendeleo kwa sababu shida ni CCM, mipango hakuna shida, rasilimali zipo, wataalam wapo, ardhi ipo, kila kitu kipo, shida ni hao wenyewe tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo yangu mawili ya msingi. Moja ni elimu. Nashangaa sana Waziri, kaka yangu Simbachawene wakati anachangia, akawa anakataa tusiseme elimu ya bure haipo. Jambo la kawaida kabisa, kwamba unalipa ada ya shilingi 20,000/= kwa shule za kutwa na shilingi 70,000/= shule za boarding, gharama zingine wazazi wanaingia halafu unasema eti elimu hii ni ya bure, lugha ya kawaida ya Kiswahili tu. Wekeni lugha hii ili msiwachanganye wananchi, elimu ni ya kuchangia, Watanzania wajue na wajue majukumu yao, wafanye kazi ya kusomesha watoto wao, kwamba Serikali ilichofanya imepunguza gharama, very simple ili watu waelewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mnapowaambia watu elimu ni bure, akienda pale anadaiwa mahindi, apeleke maharage, halafu michango mbalimbali, wanaambiwa walipie mlinzi, semeni ili jambo lieleweke vizuri, kwani siyo dhambi. Hapa hakuna elimu ya bure, ni elimu ya kuchangia na Watanzania wajue. Kwa hiyo, nadhani ni muhimu sana hili jambo likawekwa wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika hizi shule, kwa mfano, nina madai hapa ya waraka uliotolewa ili wale walimu, wanasema Waraka kwa Watumishi wa Serikali Namba 3 wa mwaka 2014 kuhusu mishahara na posho ya madaraka kwa viongozi wa elimu. Hawa ni wakuu wa shule za sekondari na msingi na vyuo. Maana yake mpaka leo hawa watu wanadai, wametengewa tu shilingi 250,000/-, kwa hiyo maana yake hawa hawawezi kuwa na moyo wa kuendeleza elimu vizuri kama wenyewe wana madai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani Mkuu wa Chuo analalamika, Mwalimu Mkuu analalamika, na wazazi wanalalamika, wanafunzi wanalalamika, kwa hiyo mkitaka mambo yaende sawa, nilimsikia Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini amesema, yeye hataenda kwenye mpango wa tatu wa REA, mpaka makando kando ya mpango wa kwanza…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri hii kauli ikifanyika itasaidia sana. Miradi yote ambayo Wabunge wanataja hapa, barabara ambazo zilipangwa, kama ile ya kutoka Kitunda kwenda Msongora, tangu wakati Mheshimiwa Magufuli akiwa Waziri awamu ya kwanza, awamu ya pili mpaka leo Rais, ni wimbo. Mvua ikinyesha watu hawawezi kwenda mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda hivyo katika miradi mbalimbali ya maji kule Chanika, Msongora, Kidole, Mgeule, ikakamilika, maana yake watu wale ukizungumza habari ya maendeleo na uchumi wa kati watakuelewa. Kwa hiyo, mambo haya ni muhimu sana mkayakamilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya msingi sana ambayo mambo haya hamjayafanyia kazi na nimwombe Mheshimiwa Waziri anisaidie. Kwa mfano, kwenye upande wa elimu, Mawaziri, kila mtu anaibuka na jambo lake katika nchi hii. Tuliwahi kuwa na Mungai akaja hapa na unified science, mimi bahati nzuri ni mwalimu wa hesabu na kemia, akachanganya masomo watoto wakaogopa sana masomo ya sayansi, kwa hiyo watu wakarudi nyuma sana, Waziri akawa na mamlaka hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeenda hapa, akawepo Kawambwa, akaibuka na GPA na nampongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Ndalichako amefuta ile, namuunga mkono, turudi kwenye division. Kwenye Sheria za Baraza la Mitihani, kifungu namba 20, kinasema, The Minister may give the Council directions of a general or specific character and the Council shall give effect to every direction. Kumbe hiki kifungu ndiyo kifungu ambacho Waziri anaibuka asubuhi, anaenda anatoa maelekezo Baraza la Mitihani, wanaambiwa sasa hivi ni GPA, ni Division, hiki kifungu kiondolewe. Hata kama Waziri ana mamlaka ashauriane na wataalam wenzake, ili mambo haya yasiwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake mnawayumbisha Watanzania, watoto hawa mnawayumbsha, mara division, yaani mnachofanya nyie ni kwamba kuna golikipa yupo mlangoni pale, anachofanya ameshindwa kiutaalam, kimpira, anaamua aongeze tu ukubwa wa goli, ili ionekane kwamba wamefunga. Hiyo maana yake ni failure, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango wa elimu hapa, hatuna vile vitu vya kitaalam kwa mfano Teachers’ Profession Board, haipo, Quality Assurance Board, haipo. Kama ambavyo kuna Wanasheria wana Chama cha Wanasheria, Walimu wana chama ambacho kinaelekea kuwa chama cha kisiasa siku hizi. Sasa hawa watu lazima wawezeshwe ili waweze kusimamia, lakini ni muhimu sana mkaangalia mambo ya maslahi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi unaleta mpango wa kipato cha kati unazungumza habari ya viwanda, halafu shuleni hata matundu ya choo hamna, hivi kweli hayo ni maendeleo? Yaani uzungumze upate mainjinia wakaendeshe viwanda, matundu ya choo tu ni shida. Yaani madawati ni shida, mnazungumza vitu vikubwa, vidogo tu vimeshindikana hapa. Wewe unazungumza habari hii wakati hata choo hakipo shuleni. Sasa hivi watoto wameandikishwa katika shule hizi, kuna shule ina watoto 617, ina madarasa mawili ya darasa la kwanza. Sasa huu uchumi wa kati nataka nione miujiza, hapa kazi tu na jipu, tuone mambo yatakavyokuwa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya mwisho, utawala bora. Zamani niliwahi kumuunga mkono Mheshimiwa Nape, wakati nilipokuwa kule chama cha zamani, lakini nikagundua Mheshimiwa Nchimbi aliwahi kufuta kanuni ili Nape asigombee Uenyekiti, naona alikuwa sahihi.
Huyu jamaa amekuja hapa, anaondoa hoja, unawaambia watu utawala bora, wana haki ya kupata taarifa kwa mujibu wa Ibara ya 18, Waziri anakaa chumbani, tumelalamika jana yake, kesho yake amekuja hapa akatuambia kuna utafiti wa Uingereza, yaani unawezaje Waziri kujifunza kuzuia taarifa, usijifunze demokrasia ya Uingereza, miundombinu na vitu vingine vikubwa, wewe ukajifunza kuzuia taarifa tu. Unatuambia, kuna utawala bora hapa? Yaani, unazuia Watanzania wasijue tunazungumza kitu gani humu kwenye hili Bunge. Halafu Waziri Mkuu na Mawaziri, wengine ni wataalam na wasomi, wanaunga mkono na kupiga makofi. Ndiyo maana nikawaambia Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge wa CCM hawawezi kuwasaidia sana. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo mambo kwa kweli ni muhimu mkayatafakari upya. Haiwezekani mkazuia taarifa ya kile kinachoendelea, unatuambia suala la muda wa kazi, sasa, hivi asubuhi na jioni, upi ni muda wa kazi mzuri? Kwa hiyo, asubuhi mnaonesha, jioni mnazima. Yaani jioni saa tisa na nusu, ndiyo muda sasa umekwisha, halafu asubuhi mnaonesha. Unarekodi masaa saba, halafu mna-edit mnatoa kwa saa moja, mnatoa mnayotaka wenyewe muone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar itakuwa hoja yangu ya mwisho. Mimi najua na CCM wanajua kwamba Zanzibar uchaguzi ulikwenda vizuri na Maalim Seif alishinda. Huo ndio ukweli, hata kama hamtaki. Dunia inajua, Afrika inajua, Tanzania inajua, CCM mnajua na Taifa hili mnajua na Mwenyekiti unajua. Uchaguzi wa Zanzibar ulikwisha. Kwa hiyo, mnachofanya ni magumashi na sisi kama watoto wa Tanzania hii hatuwezi kuunga mkono mambo haya. Nchi hii ni ya demokrasia kila mtu ana haki ya kuongoza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tukienda kwenye uchaguzi watu wakapiga kura, hakuna malalamiko, aliyeshinda apewe haki yake, ndiyo mpango mzuri wa maendeleo utakavyokwenda. Twende kwa amani kwa kuheshimiana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, sijaunga mkono hoja mpaka kwanza Mpango wa Maendeleo uje, ndio nitaunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)
TAARIFA
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa.
MBUNGE FULANI: Mwenyekiti, kuhusu utaratibu, kanuni ya 63, ile ile inayotumika. Mimi ninao ushahidi ya kwamba...
MBUNGE FULANI: Kanuni ya 63 ngapi?
MBUNGE FULANI: Kanuni ya 63(3)
MBUNGE FULANI: Mbunge mwingine yeyote anaweza kusimama mahali pake na kutamka kuhusu utaratibu na baada ya kuruhusiwa na Spika kudai kwamba, imetosha. Mbunge aliyezungumza kuhusiana na kwamba Maalim Seif ameshinda, amesema uongo.
WABUNGE FULANI: Kweli!
MBUNGE FULANI: Kwa mujibu, nathibitisha sasa, Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, kifungu cha 42 kutoka (i) mpaka (v) kinazungumzia Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar pekee ndiyo yenye mamlaka ya kumtangaza na kujumuisha kura za ushindi.
(Hapa baadhi ya Wabunge walimzomea Mzungumzaji)
MBUNGE FULANI: Kama Mheshimiwa Mbunge amezungumza, maelezo hayo, kama ameeleza maelezo hayo, kwamba uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa una mshindi, naomba atoe uthibitisho.
WABUNGE FULANI: Aaaa, hakuna.
MHE. MWITA M. WAITARA: Kuhusu utaratibu Mwenyekiti.
MBUNGE FULANI: Aah, atoe.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waitara, unaipokea hiyo taarifa?
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie na Kamati hii kwamba sipokei na yeye yupo humu baada ya uchaguzi wa Zanzibar, uchaguzi ulikuwa na karatasi tano, kwa nini wamehesabu moja ni halali nyingine zote nne sio halali?