Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Nianze kwa kumpongeza Waziri pamoja na Naibu wake kwa hotuba nzuri yenye kuleta matumaini kwa Watanzania, lakini niwapongeze sana kwa kazi nzuri waliyokuwa wanafanya kwani haifichiki. Tumeona ujenzi na ukarabati wa hospitali zetu za rufaa lakini tumeshuhudia pia uanzishwaji wa hospitali maalum ya Benjamin Mkapa Ultra Modern Hospital iliyopo hapa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo, napenda kuikumbusha Serikali kwamba bado haijafikia lengo lililowekwa miaka 15 iliyopita ndani ya Azimio la Abuja linaloitaka Serikali kutenga asilimia 15 ya bajeti yake ya Taifa kwa ajili ya afya. Hapa ninavyoongea sasa Wizara hii imetengewa bajeti chini ya asilimia kumi ya bajeti ya Taifa. Napenda kuiomba Serikali iweze kufikiria upya suala hili na kurejea katika msimamo wa makubaliano hayo na kuwezesha Sekta hii ya Afya kufanya vizuri kwani tutakapowezesha sekta hii tutawezesha pia sekta nyingine kuweza kukua na kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoani Mwanza zipo changamoto nyingi ambazo zinaikabili sekta hii ya afya. Changamoto hizi tayari zimeshatajwa na Wabunge wenzangu lakini na mimi nitaweka msisitizo japo kwa ufupi. Kuna changamoto ya ucheleweshaji wa dawa kutoka MSD; kumekuwa na wafanyakazi wachache katika sekta hii ya afya; kumekuwa na ucheleweshwaji wa mishahara ya wafanyakazi; kumekuwa na ukosefu wa maduka ya dawa katika hospitali zetu za wilaya na lipo tatizo ambalo limekuwa likisumbua sana la ukosefu wa usafiri wa uhakika kwa wagonjwa wa wilaya zote za Mkoa wa Mwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Wilaya ya Magu ina magari manne ya wagonjwa lakini katika magari manne ni gari moja tu la kituo cha Lugehe ndilo linalofanya kazi, mengine matatu yote ni mabovu na magari haya yamekuwa yakikarabatiwa mara kwa mara bila mafanikio. Kwa kuwa pia Wilaya ya Magu haina mapato ya kutosha, magari haya yamesababisha deni la shilingi milioni 38 kwa ajili ya service zilizokuwa zinafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Ilani ya Chama changu cha Mapinduzi iliahidi kwamba, itaboresha mazingira ya wafanyakazi wa sekta mbalimbali ikiwemo sekta hii ya afya, napenda kuikumbusha Serikali kwamba ni wajibu wake sasa kutekeleza Ilani hiyo kwa kuweza kutatua changamoto hizi ili wafanyakazi waweze kufanya kazi katika mazingira yanayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Wilaya ya Sengerema nayo inahitaji ruzuku stahili. Mheshimiwa Ngeleja amesimama mara kwa mara na kuhamasisha suala hili na kuiomba sana Wizara na napenda kuungana naye katika vita hii. Hospitali ya Wilaya ya Sengerema inapata ruzuku ya vitanda 150 tu wakati hospitali hiyo ina vitanda zaidi ya 370 na inategemewa na wakazi wengi wanaoishi ndani ya Jimbo hilo la Sengerema. Ombi hili tayari lipo Wizarani na ni matumaini yetu kwamba Wizara itatupatia jibu zuri ambalo litatuletea matumaini kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimebahatika kuzunguka katika baadhi ya shule za msingi na sekondari ndani ya Mkoa wa Mwanza nikiwa na wanaharakati wanaotoa elimu ya afya ya uzazi. Kwa fursa hiyo ya muda mfupi, nimegundua kwamba ipo haja ya Serikali kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wa jinsia ya kike wanapata taulo za kujisitiri ili kupunguza changamoto kubwa ya wanafunzi hawa kutokuhudhuria masomo wakiwa kwenye siku zao. Kwa sababu tayari Serikali inatoa vitabu na madawati mashuleni, naomba suala hili pia liweze kupewa kipaumbele ili kuweza kunusuru wasichana hawa kukosa masomo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri wapo vijana wa Mwanza ambao wamejitolea kufanya utafiti na wakatengeza washable sanitary towels yaani pedi ambazo zinaweza kufuliwa na kutumiwa zaidi ya mara moja kwa muda mrefu. Naomba Serikali iwasaidie vijana hawa ili bidhaa zao ziweze kuthibitishwa na TBS na endapo zitatufaa bidhaa hizi ziweze kununuliwa na Selikali na kusambazwa katika shule mbalimbali hasa zile zilizopo vijijini. Napenda kumwomba Waziri wa Afya anipokee nitakapowaleta vijana hawa ofisini kwake kwani ni fahari kwa Tanzania kuwa na vijana wabunifu tena wenye kujituma kwa niaba ya nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, napenda kusema kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante.