Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Tarime Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hoja, lakini pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwamba, sasahivi fedha nyingi sana zinaenda katika Halmashauri katika miradi mbalimbali. Takriban kila Mbunge hapa ana jambo la kusimama na kusema juu ya Mheshimiwa Rais na juu ya Serikali ya Awamu ya Sita, tunamshukuru sana kwa hatua hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais alitoa muelekezo kwa wewe Mheshimiwa Spika na Wabunge ambao mlisaidia kusema; wananchi wa Tarime Vijijini wanashukuru sana kwamba, ile fedha ya CSR imetoka na miradi sasa inaendelea; hali ya kisiasa itakuwa tulivu jimboni.
Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Rais ametoa fedha ambazo kwa sasa vijana wa darasa la saba wakimaliza mitihani yao mwakani wataingia form one kwa kuwa madarasa yamejengwa na kazi inaenda mchakamchaka sana.
Mheshimiwa Spika, nampongeza CAG kwa kazi ambayo anaifanya. Ametoa taarifa ambayo kila Mbunge akisoma baadhi ya mambo ambayo yapo kwenye majimbo yetu tunayaona kwenye ripoti hii. Tunamshukuru na tunaomba aendelee hivyo.
Mheshimiwa Spika, lakini ziko changamoto nyingi sana. Na ukitaka kusaidia Watanzania wakati ukiwa umekalia hicho Kiti kwa muda ambao Mungu atakupa na sisi kukujalia kuendelea kukaa hapo ni kuangalia namna ambayo tutapitia mfumo wa Serikali za Mitaa Tanzania. Mfumo huu umeanza tangu mwaka 61, ukashindwa 71, ukawa resumed mwaka 82, tukaanza operation mwaka 84; ni miaka 38 mpaka sasa tunao mfumo huu. Kunakuwa na changes ndogondogo sana.
Mheshimiwa Spika, mazungumzo yote humu Wabunge wakisimama tunazungumza fedha ambazo zikienda kwenye majimbo yetu zitaondoa kero za Watanzania ambao wametuchagua sisi kuja kukaa kuzungumza. Tunazungumza hoja ambazo kila Mbunge angetamani fedha zinazotajwa hapa, haya mabilioni yanayotajwa kwa namna mbalimbali kwamba, yamepotea tungetamani yaende yakaondoe changamoto za barabara, maji, afya, shule, mikopo watu wawasomeshe Watanzania wapate elimu na huduma bora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili jambo ni muhimu sana kwa sababu tunazungumza hapa fedha nyingi katika halmashauri. Tuchukue mfano rahisi, tulipata fedha za Uviko zikaja kwenye majimbo. Mheshimiwa Rais akatoa maelekezo, Wakuu wa Mikoa na Ma-DC wakafanye special operation, yale madarasa yakajengwa ndani ya muda mfupi yakakamilika. Malalamiko ni machache, lakini fedha hizi za Serikali, za wananchi kule, hili ni shamba la bibi, ndiyo fedha ambazo zimeibwa sana na zimeliwa. Miradi mingi katika maeneo haya haijakamilika, na hoja nyingi ukisoma zinajirudia.
Mheshimiwa Spika, CAG miaka miwili mpaka mitatu nyuma alisema hoja ile ile. Sasa kama kuna mtu yupo mahali alipewa hoja mwaka uliopita, mwaka wa kwanza, mwaka wa pili na mwaka huu imejirudia, mwakani ataleta story hiyo hiyo, kwa nini watu hawa wasiwajibishwe? Kwa nini wasichukuliwe hatua? Hawa ni watumishi, CAG na watu wake, wanalipwa posho, wanatumia muda, akili na damu, wanasafiri wanaumia, hawa wakienda wakaleta ripoti tunatarajia mabadiliko.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia michango ya Wabunge humu ndani, watu wanaumia sana, kwamba tunazungumza kwamba kwenye majimbo yetu kuna changamoto, tuna shida na watu wetu, lakini tunaambiwa fedha zimekusanywa, zimepotea. Ripoti hii imetoa tathmini ya ukaguzi wa fedha. Tungetaka tupate ripoti nyingine sambamba na hii ambayo inaonesha, watumishi ambao wamekula fedha za Umma ni akina nani; na wapo wapi; wanafanya nini kwa sasa? Lazima watuoneshe.
Mheshimiwa Spika, CAG ameonesha fedha ambazo zimepotea, tupate ripoti ya wale ambao wamehusika. Yaani haiwezekani watu hapa watoe mishipa kujadili fedha imepotea, halafu kuna mtu anakula kiyoyozi tu, au mwingine amehamishwa kutoka point A kwenda point B. Hii haikubaliki.
Mheshimiwa Spika, tukitaka kupiga hatua; tena Mheshimiwa Rais wetu yuko China, ningeomba akope sheria za Wachina kidogo tu, siyo zote, watu wa namna hiyo kule China hawawezi ku-survive. Umefanya kosa, imethibitika, hujaonewa, unawajibishwa, anakaa mtu mwingine. Wapewe nafasi watu wenye uwezo huo. Kama mtu amekaa mahali kwa bahati mbaya, atoke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huu mjadalla wa sasa hapa, hata huko mtaani watu wanatushangaa. Tulikuwa tupewe hapa ripoti wahusika wote wakiwa korokoroni, ndiyo tunazungumza hapa. Anaitwa mmoja mmoja, anaulizwa fedha ziko wapi? Rudisha, kama umemeza, tapika fedha ili zirudi katika eneo lake. Ndiyo hoja ya msingi hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ni mjadala hapa wa maneno mengi; kwa mfano, unaposema MSD wanaidai Serikali Shilingi bilioni 250, halmashauri tumekabana mashati, mia mbili mia mbili; mia tano, mia tano; buku buku; tumepeleka fedha pale kuomba dawa. Dawa hazijaja, kumbe hawa wanaidai Serikali hawajalipwa fedha. Sasa Mbunge unasema nini kwenye jimbo lako? Yaani wananchi wametoa kodi wamelipa kutoka mazao yao na shughuli mbalimbali, fedha imepatikana, tumepeleka pale MSD, dawa hazipo. Kwa hiyo, mzigo huo siyo wa kwetu. Tunaomba hao watu walipwe fedha ili wananchi wapate dawa na huduma kama ambavyo wamechangia.
Mheshimiwa Spika, hizo fedha wamepeleka miaka miwili mpaka mitatu hawajarejesha, dawa hazipo, fedha wamechukua na maelezo hamna, na watu wapo ofisini. Mimi naona hii siyo sawa.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine nataka nizungumze, kwenye halmashauri zetu na ndiyo maana naomba tupitie huu mfumo wa Serikali za Mitaa. Halmashauri zile, Mbunge anazungumza hapa, ikitokea kuna shida kwenye jimbo, Mbunge utaulizwa, hujasemea watu wako, hufanyi kazi nzuri, lakini twende kwenye maeneo yetu, kuna maagizo ambayo Katibu Mkuu TAMISEMI anamwagiza Mkurugenzi. Mkurugenzi anaitwa Dodoma halafu anapewa maagizo, na halmashauri Madiwani wamepitisha mipango yao. Sasa wanasigana; Mkurugenzi ameambiwa lazima nitekeleze hili. Fedha nifanye re-allocation ifanye mradi fulani, na mradi huo haukupendekezwa, mradi wa Madiwani ni tofauti na ule pale. Kwa hiyo, Mkurugenzi anasimama kwamba bosi amesema lazima lazima nitekeleze; Madiwani wanasema, hiki siyo kipaumbele chetu; Mbunge anasema yuko kwake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimekusikia umesema mara kadhaa kwamba kama Bunge likiisha kwa mfano 2025, wengi hapa asilimia 60 mpaka 70 hatutakuwepo. Sababu mojawapo ni miradi kwenye halmashauri na maagizo mbalimbali. Wapo Wakurugenzi kwenye halmashauri zetu hawafanyi kazi. Anaitwa mkoani asubuhi mpaka jioni, kaenda na gari, kaenda na dereva, kapewa maagizo; maagizo hayo, Mbunge hajui, Mwenyekiti wa Halmashauri hajui. Kwa hiyo, kuna shida. Kwa hiyo tuangalie hata mfumo wetu unavyofanya kazi.
Mheshimiwa Spika, hawa wakurugenzi pia wapewe watu wenye uwezo. Zamani walikuwa wanateuliwa miongoni mwa Watumishi wa Umma. Wanafanyiwa vetting, wana uzoefu. Leo kwa mfano ukimwuliza CAG, kwenye halmashuri hizi atuambie maeneo ambayo watu wameshindwa kuandaa ripoti ni wangapi? Pale Tarime ili wafunge mahesabu walikuwa wanaenda kuazima watu Serengeti. Wataalamu hawapo. Kwa hiyo, tunazo hoja nyingi sana za kuangalia.
Mheshimwa Spika, naomba kwamba fedha ambazo zimepotea, wamezungumza, sitaki kusema kwa sababu nilikuwa kule Tanga, lakini nimefurahi kuiona kwenye ripoti hii. Haya mambo yapo, yamefanywa, na wahusika wapo, peleka ukaguzi maalumu Bandari ya Tanga, watu wawajibishwe, tupone. Ukitaka kutengeneza taswira nzuri, kama kuna mtu amepoteza fedha ya Serikali, halafu amewajibishwa, hata kizazi kingine kitajifunza. Kama kuna mtu amepoteza fedha na hakuwajibishwa kwa sababu ni mjomba, shangazi, mnafahamiana, ni ukanda, kabila moja, hili Taifa litakufa.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)