Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpwapwa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi ya kuchangia katika ripoti hizi tatu za Kamati za LAAC, PIC na PAC. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuleta maendeleo katika nchi yetu. Pia nikupongeze wewe binafsi kwa kazi nzuri ambayo unaendelea kutusimamia ndani ya Bunge hili. Tatu, niwapongeze Wenyeviti wa Kamati hizi tatu pamoja na Wajumbe wote wa Kamati hizi tatu kwa ajili ya kazi njema ya kuandaa ripoti ambayo leo tunapata fursa ya kuichangia.
Mheshimiwa Spika, ukisikiliza hotuba nyingi hapa ndani, malalamiko makubwa sana yapo kwenye utendaji hafifu wa mashirika yetu ya Umma. Malalamiko haya yanakuja kwa sababu mashirika haya yanatumia mitaji ya Umma, yaani fedha za walipa kodi, lakini faida ambayo ilikuwa imetarajiwa kutoka kwenye mashirika haya, haipo. Kwa hiyo, ndiyo maana Wajumbe au Wabunge wanalalamika sana.
Mheshimiwa Spika, zipo sababu nyingi ambazo zinasababisha mashirika haya yasifanye vizuri. Wabunge wengi wameeleza, lakini nami nitaeleza. Moja, ni mashirika haya mengi kuendeshwa bila Bodi za Wakurugenzi kwa kipindi kirefu sana.
Mheshimiwa Spika, majukumu ya bodi yanajulikana. Bodi ndiyo chombo pekee kinachosimamia kutoa maamuzi, usimamiaji wa utekelezaji wa majukumu yote ya taasisi, lakini unakuta mashirika mengi kwa kipindi kirefu yanaendeshwa bila bodi.
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba nitoe mifano michache tu. Katika ripoti ya CAG ukurasa wa 62 ameorodhesha kwamba mwaka 2020/2021 kulikuwa na orodha ya mashirika 31 ambayo yalikuwa yameendeshwa bila bodi kwa kipindi kirefu sana. Mojawapo ni Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere; kimekaa bila bodi kuanza Julai, 2015 mpaka Februari, 2022. Muda huu ni wa miezi 80 ambao ni sawa na miaka sita, taasisi kama hii inakaa bila bodi.
Mheshimiwa Spika, lingine ni Shirika la Maendeleo na Utafiti wa Viwanda Tanzania, na lenyewe limekaa bila bodi kuanzia Oktoba, 2015 mpaka Februari, 2022, miezi 77 ambayo ni sawa pia na miaka sita na miezi kadhaa. Lingine ni Makumbusho ya Taifa, kuanzia Julai, 2015 mpaka Februari, 2022 sawa na miezi 38, nalo pia kwa miaka mitatu limekuwa halina bodi.
Mheshimiwa Spika, kwa vyovyote vile uendeshaji huo wa mashirika yetu hauwezi kutarajia kupata tija kwa sababu menejimenti inajiendesha bila kuwa na mtu wa kumwangalia, matokeo yake ukiangalia mashirika yetu yote Kamati ya PAC ambayo tunashughulikia mashirika na tumepitia mashirika yote ama yana mzigo wa madeni, ama yanaendeshwa kwa hasara lakini ni kwa sababu hakuna chombo madhubuti, hakuna bodi ambayo inaweza ikasimamia utekelezaji wa majukumu yao na mwisho wa siku tuweze kushuhudia tija ambayo ilikuwa imekusudiwa.
Mheshimiwa Spika, pia kwenye ripoti ya CAG ukurasa wa 66 aya ya 47 na 48 ya Mwongozo wa Uhasibu (NBAA) ya mwaka 2021 zinaeleza umuhimu wa bodi, kwamba bodi lazima iidhinishe hesabu za taasisi yake. Kabla ya CAG kukagua, lazima bodi iidhinishe ndipo ikague; lakini CAG anasema, alishindwa kutoa maoni kwa mashirika Matano. Hakutoa maoni yake (opinions) kwa sababu hesabu zile zilikuwa hazijaidhinishwa.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi tunapoongea, hatuna uhakika; siyo Serikali na Umma kwa ujumla kwamba status ya mashirika haya ikoje? Maana jicho la Serikali au jicho la Umma ni CAG. Kwa hiyo, tunasubiri CAG akishakagua atoe maoni kuhusu shirika husika, lakini mpaka sasa hivi mashirika hayo matano ambayo CAG alishindwa kutoa maoni yake ni kwa sababu hayakuwa na bodi na sheria inataka hesabu zake ziidhinishwe na bodi, halafu ndipo afanye ukaguzi na atoe maoni yake.
Mheshimiwa Spika, mashirika hayo nitayataja machache. Mojawapo ni Shirika la Maendeleo na Utafiti wa Viwanda Tanzania, lingine ni Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere, na lingine ni Shirika la Utafiti wa Uvuvi. Haya mashirika CAG hajatoa maoni mpaka leo na hatujui yanaendeleaje mpaka sasa. Hilo ni eneo ambalo pia linaleta shida kwamba bila kuwa na bodi, kuna mambo mengi yanaweza kukwama kabisa.
Mheshimiwa Spika, pia kuna issue ambayo pia CAG amei-raise kwenye ripoti yake ukurasa wa 75 anasema; mashirika manne hayakukata michango ya kisheria ya kupeleka kwenye Mifuko ya Pensheni na Mfuko wa Fidia wa Wafanyakazi. Sasa hayo yote ni kwa sababu ya udhaifu wa usimamizi. Haiwezekani mashirika yakakata makato ya kisheria halafu yasipelekwe kunakotakiwa. Hasara yake ni kukosekana kwa mafao ya wafanyakazi wanaostaafu. Watapataje mafao kama haya yamekatwa, lakini hayajapelekwa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndiyo maana tunaona wazee wengi wanakufa mapema wakishastaafu, kwa sababu wanamangamanga, wanakwenda kufuatilia fedha hazipo. Kumbe taasisi hiyo waliyokuwa wanafanya kazi ilikuwa haipelekei ile michango. Kwa sababu menejimenti ilikuwa haipeleki, hakuna mtu wa kuangalia juu kuona kwamba wanapeleka au hawapeleki. Kwa hiyo, jambo hili ni muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatizo lingine au hasara nyingine ni kwamba kunakosekana na fidia kwa wafanyakazi inapohitajika. Mfanyakazi anaweza kuwa anahitaji fidia, lakini kwa sababu fedha hii haikuwepo kwenye ule mfuko, haitakuwepo, matokeo yake anapigwa danadana. Pia kushindwa kutuma hizo fedha kwenye taasisi hizi kuna hasara kubwa sana, kuna attract invoice penalty. Shirika linapigwa penalty kwa sababu halikupeleka michango kwa wakati au halikupeleka kabisa. Hii penalty inasababisha hasara na ndiyo maana tunaona mashirika mengi yanaendeshwa kwa hasara kwa sababu hizo; fedha nyingi zinalipwa kwa sababu ya penalty au adhabu, wakichelewa kupeleka kwenye mifuko ya kisheria.
Mheshimiwa Spika, jambo la kuwa na bodi tungeamua kabisa kusema kwamba ni jambo la kufa na kupona ili taasisi hizi tunazowekeza fedha nyingi za Serikali ziweze kuleta tija iliyokusudiwa ni lazima mashirika yote yaendeshwe chini ya bodi zake za Wakurugenzi.
Mheshimiwa Spika, nije kwenye kipengele cha matumizi mabaya ya fedha za Serikali; mashirika yote yameonekana yanashindwa kudhibiti matumizi yake na ndiyo maana hayafanyi vizuri, na mengi hayawezi hata kutoa gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Nichukue mfano mmoja tu wa taasisi moja eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Mheshimiwa Spika, eneo hili la Hifadhi ya Ngorongoro linamiliki ndege aina Cessna yenye namba ya usajili 5H-MPZ. Ndege hii ni ya zamani sana. Mpaka mwaka 2021 ilikuwa na umri wa miaka 47. Taasisi hii ilikuwa inatumia ndege hii kwa ajili ya doria, lakini CAG anasema katika ukurasa wa 59 Mamlaka hiyo ya Ngorongoro ilifanya matengenezo kwa gharama ya shilingi milioni 278.42, lakini plan yao ilikuwa ikishakamilika ifanye safari za saa 900, lakini cha kusikitisha sana ndege hii imefanya safari saa 18 tu.
Mheshimiwa Spika, sasa ukijiuliza, Shilingi milioni 278 zimetumika kukarabati ndege hii, lakini makusudio au matarajio waliyokuwa wametarajia kufanya safari au kuzunguka kuangalia doria kwa saa 900 inaishia kufanya doria kwa saa 18. Hasara hii ni kweli inafanyika na watu ambao wameenda shule? Je, hao watu tuliowaweka humo kufanya kazi hizo za kusimamia mamlaka yetu, wanao uwezo wa kufanya kazi kama hiyo? Ni kweli hawaoni kwamba hili lilikuwa ni kosa kubwa sana? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana hatua kali zichukuliwe kwa watu kama hao, kwa sababu hatuwezi kuendelea, hatuwezi kupata mafao, hatuwezi kupata tija kwenye mashirika kama haya kama tuna watu ambao wanaendelea kucheza na fedha za walipa kodi katika mazingira kama haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine, naomba kuzungumzia changamoto ya kupata vibali vya ajira na mfumo wa ununuzi kwa mashirika ya Umma na hasa yale yanayofanya biashara. Mashirika mengi yanapata mitaji ya Serikali ili kufanya biashara na kuleta tija na kuchangia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. Hata hivyo, kwa mazingira ya biashara ya leo, huwezi kushindana.
Mheshimiwa Spika, nashauri, tufanye biashara mashirika haya ya Umma, lakini tutumie private thinking. Maana yake ni kwamba, lazima tubadilike. Wenzetu wa private wana-enjoy flexibility ya maamuzi. Mfano, akipata bidhaa fulani kwenye soko kwamba ina-hit katika soko, wao wanafanya maamuzi overnight. Wanahitaji mtaalamu wa kutengeneza hiyo bidhaa, kesho wameshampata. Kesho kutwa wanaanza uzalishaji. Wanahitaji raw materials; kesho wameshatafuta raw materials zinapatikana, wananunua na kuanza uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, sisi tunaanza mchakato wa ajira, unachukua miezi mitatu ndiyo tumpate huyo mtaalamu kuja kutengeneza bidhaa hiyo ambayo wenzetu wameshaanza mara moja, lakini sisi hiyo kupata raw materials lazima mchakato pia uwepo wa manunuzi unaochukua zaidi ya miezi mitatu. Unaporudi, unaanza kutengeneza bidhaa, unakuta ama imeshatoka kwenye soko au lile soko limeshakuwa captured na private sector. Kwa hiyo, hatuwezi kushindana na ndiyo maana unaona pia hakuna tija kwenye mashirika yetu.
Mheshimiwa Spika, ningeshauri tukitaka kufanya bishara lazima tubadilike. Yale mashirika ambayo yanafanya biashara, tuwape uhuru wa kufanya maamuzi haraka. Tunaweza kukasimu madaraka kwenye bodi ili waweze kufanya maamuzi haraka ili wafanye biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, biashara haihitaji mchakato wa miezi mitatu na kuendelea, biashara haihitaji theories, biashara inahitaji maamuzi. Biashara ni maamuzi na biashara lazima uamue kwa sababu biashara ina- determine soko. Soko likipatikana leo, lazima upambane kulipata leo, huwezi kupambana kwa ajili ya kusubiri mchakato. (Makofi)
SPIKA: Muda wako ulishakuwa umeisha, nilikuacha kwa sababu ni wewe ni mtu wa mwisho ili umalizie mchango wako. Kwa hiyo, nakupa sekunde 30.
MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa na mengi lakini naomba basi, niunge mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)