Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Ulyankulu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mungu jioni ya leo, kuwa nami ni miongoni mwa wanaochangia hotuba zilizopo mbele yetu kuhusu hizi Kamati zetu tatu. Tena nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa zawadi ya uhai mpaka leo nipo humu ndani ya hili bunge.
Mheshimiwa Spika, nikiwa mjumbe wa Kamati ya LAAC, ambapo umenitua hivi karibuni, ninakushukuru sana wewe kunipeleka kwenye hiyo Kamati, kiukweli ninashuruku sana.
Mheshimiwa Spika, nikiwa mjumbe wa Kamati ya LAAC ambao umenitua hivi karibuni, ninakushukuru sana wewe kunipeleka kwenye hiyo Kamati, kiukweli ninashuruku sana kwa sababu ninaenda kuifanyia kazi nchi yangu ambayo wananchi wamenituma.
Mheshimiwa Spika, kwenye kamati yetu kuna mambo mengi sana ambayo tumeyapitia, hasa hizi hoja za CAG. Ni mambo mengi sana yanasikitisha, very very sad stories hasa yanayofanyika kwenye hizi halmashauri zetu. Tumeangalia hoja nyingi ambazo kiukweli kama tutazifumbia macho, halmashauri zetu nyingi zinakwenda ku-collapse. Mbaya zaidi, wanaofanya yote haya yatokee mpaka sasa hivi wako ofisini wanakula kiyoyozi lakini bado wanatembelea V8 zetu na mafuta yetu wanatumia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwenye 10% ya mapato ya ndani. Hili ni eneo ambalo halmashauri nyingi wanatumia kama mwanya wa kupiga hela za wananchi wetu. Serikali ilitunga hii sheria ili kuweza kuyasaidia haya makundi matatu ambayo hayana uwezo wa kukopesheka katika benki zetu. Kuna kundi la wanawake ambalo ni kubwa sana, haliwezi kukopesheka na wala hawana dhamana, kuna kundi kubwa la vijana, na kundi la walemavu. Hata hivyo, halmashauri zetu zilizo nyingi, kwa masikitiko makubwa zinatumia kama mwanya wa kuweza kuyaminya haya makundi yasiweze kupata hizi fedha kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Spika, ukipiga hesabu, hizi fedha kama zitasimamiwa vizuri, Shilingi bilioni 75, ni nyingi sana ambapo zingeenda kuwasaidia akina mama na vijana wakaondokana na umasikini. Katika hali ya kusikitisha, mfano hapa tukiangalia kuna halmashauri 17. Hizi halmashauri 17 zilitoa mikopo ya Shilingi 3,260,000,000/= bila kuzingatia uwiano. Tunajua kabisa sheria inasema ni 4:4:2 lakini wao kuna kundi moja wanalipendela zaidi. Tuangalie kabisa hili kundi ambalo linapendelewa lina athari kiasi gani na ambalo halipewi lina athari kiasi gani katika maendeleo ya nchi yetu?
Mheshimiwa Spika, tukiangalia kundi la vijana; vijana sasa hivi ni wengi sana, graduates ni wengi sana, wako huko mitaani, hawana mikopo wanahangaika na bahasha kila kukicha. Bado hili kundi halipewi fungu lake kama inavyotakiwa. Kwenye ripoti ya CAG inaonesha kwamba vijana ndio hawapewi fedha kwa kiasi kikubwa kwa kigezo cha kwamba wana-misuse hizi fedha. Cha kushangaza, kwani ni lazima hawa vijana tuwape fedha? Ni ukweli kabisa kwamba ukiwapa vijana fedha, wanaweza wakazitumia ndivyo sivyo, lakini kwanini tu- stick katika aina moja tu ya mikopo?
Mheshimiwa Spika, kwenye halmashauri nyingi ukitembelea kule, hii mikopo kwa ajili ya vijana, unakuta ni boda boda tu; hivi hakuna creativity nyingine ya kuwasaidia hawa vijana zaidi ya kuendesha tu bodaboda? Tumeona kuna halmashauri moja vijana ambao wamesoma mambo ya medicine wameweza kuji-organize wakapewa mkopo wakaweza kufungua hadi kituo cha afya ambacho kimeenda kuajiri na watu wengine, lakini hawa watu wetu wa Maendeleo ya Jamii wanakosa ubunifu, wanashindwa kutoa elimu kwa watu wetu, matokeo yake vijana wetu wote wanakomalia mradi mmoja tu wa bodaboda. Kila siku ni bodaboda, mwisho wa siku zinakosa thamani huko kama vijijini, hata abiria hawapati na wanashindwa kupeleka marejesho. Matokeo yake kipengele cha kupeleka marejesho hakipo. Tunakuwa tunatoa hizi fedha, lakini mwisho wa siku hazirejeshwi.
Mheshimiwa Spika, tukiangalia pia nature ya utoaji wa hii mikopo, tunawapa for free, wanafikiria hizi fedha ni kama za TASAF. Kwa hiyo, hata kusema kama kuna mechanism ya kusaidia hizi fedha zirudi, na hizi fedha ni revolving, hakuna. Kwa hiyo, ifikie mahali sasa Wizara iweke mkazo kuhakikisha kabisa hizi fedha zinakwenda kuwa ni zenye manufaa kwa vijana, akina mama na watu wenye ulemavu. Isifikie kwamba hizi fedha ni kama za TASAF, wanapewa for free, hakuna cha kurejesha. Ni lazima uwepo mkakati wa kuhakikisha hizi fedha zinarudi ili watu wengine waweze kukopesheka. Pia hizi fedha ziende zikawafikie hadi watu wa chini kabisa huko.
Mheshimiwa Spika, taarifa inaonesha wanaopewa hasa ni vijana na akina mama wa mijini. Kwani huko vijijini kwetu akina mama hawahitaji mikopo? Wanahitaji. Kwa hiyo, naomba sana Serikali kupitia TAMISEMI, wahakikishe wanawasimamia na kutoa amri kwa hawa watu wa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha hii mikopo inakuwa ni yenye tija kwa vijana wetu, akina mama na watu wenye ulemavu, na isiwe tu inaingia kwenye mifuko ya watu.
Mheshimiwa Spika, kuna halmashauri nyingine hata kutenga, hawatengi, na pia hawasimamii urejeshaji. Hicho ndiyo kinatumika kama kichaka. Unakuta watu hawarudishi, hawatengi au wanachukua zile zilizorudi kidogo ndiyo wanaenda kutoa kwenye awamu inayofuata. Hapana, hilo halikubaliki.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu uwekezaji wa mitaji ya Umma katika miradi ya halmashauri. Ni kweli kabisa ili halmashauri zetu ziweze kuendelea ku-exist ni lazima basi ziweke miradi ya aina mbalimbali ambayo itazifanya halmashauri zetu ziweze kupata mapato mengi na ya uhakika.
Mheshimiwa Spika, sasa tunaona na ripoti inaonesha halmashauri nyingi sana zinafanya uwekezaji ambao hauna maana, unakwenda kuzitia halmashauri zetu hasara, na yote haya yanasababisha hazifanyi upembuzi yakinifu vya kutosha, hata maandiko ya miradi hawafanyi. Unakuta kila halmashauri sasa kama ilivyosema ripoti, wanafaya uwekezaji kwa kuiga. Leo hii kila halmashauri ukienda ni soko na stendi. Sasa kama kila halmashauri kutakuwa kuna soko na stendi, leo hii hata bei za nauli zimepanda kwa sababu kunakuwa kila mahali kuna stendi.
Mheshimiwa Spika, leo dereva kila akiingia stendi lazima aache tax. Sasa huyu anayeendesha biashara ya mabasi, yeye atapata nini? Kwa maana hiyo lazima wampandishie nauli huyu mtumiaji wa mwisho, ambaye ni abiria, lakini yote haya ni kwa sababu tu tuna miradi ya kuigana. Kwa nini tusiwe na miradi ambayo itakuwa ni tofauti na ambayo inakwenda kuzalisha?
Mheshimiwa Spika, leo hii tunaona kuna masoko hayazalishi chochote. Mfano Soko la Ndugai pale, ni white elephant. Tuna soko pale la Machinga Complex, ni white elephant. Sasa hivi eti imefikia, Soko la Ndugai limelazimishwa sasa daladala zote ziende zikashushe watu kule Ndugai. Hivi tuliandaa lile soko kwa ajili ya kupeleka abiria kule au wanunuzi? Yaani tunafanya fanya ilimradi ionekane kule kuna ka-movement ka watu. Are we serious? Hebu tu-plan vitu ambavyo vinakwenda kuliletea hili Taifa faida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala lingine la NHIF. Huku ndiyo kwenye majanga makubwa. NHIF ndiyo tunaiamini kama tool ya kutusaidia sisi wananchi tuweze kutibiwa pindi ambapo hatuna fedha. Jana tumeangalia tunakwenda kuleta Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ambapo NHIF ndiyo atakuwa kingi wa kuweza kutuhakikishia afya zetu zinakuwa bora, lakini NHIF imegundulika ina madudu mengi sana. Kwanza, inashindwa kurejesha fedha kwenye halmashauri zetu. Halmashauri zinatoa huduma kwenye vituo vyetu vya afya lakini yenyewe inashindwa kurejesha. Cha kusikitisha zaidi, ujazaji mbovu wa fomu unaofanywa kwenye hosipitali za Serikali.
Mheshimiwa Spika, sasa hawa watu wanafanya kazi purposely kurudisha nchi yetu nyuma au vipi? Kwa nini hawachukuliwi hatua? Wapo tu wamekaa ofisini, na mbaya zaidi tunaambiwa hapa; ukiangalia ukurasa wa nane pale unasema, yanafanyika hayo kwa sababu Serikali imeshindwa kuchukua haraka hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wanaobainika kuhusika na ubadhirifu. Serikali ndiyo chanzo cha haya. Tumeona watumishi wengi wanaofanya huu ubadhirifu Serikali ndiyo inawalinda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumehoji halmashauri nyingi. Watu wengi tunaowahoji; Maafisa Masuuli na Wahasibu, ukimwuliza anakwambia yuko pale kwa miezi miwili, mwaka mmoja au miaka miwili. Kwa maana hiyo, ni kwamba kuna kamchezo kanaendelea huko kwenye Serikali hasa TAMISEMI. Wanamhamisha mtu, wanampeleka sehemu nyingine. Huyo mtu ameshaharibu. Leo nemesema huyu mtu ni mwizi, ukimhamisha kutoka Halmashauri A, kumpeleka Halmashauri B, huo wizi atakuwa ameuacha? Kwa nini umhamishe? Kwamba mnakwenda sasa kumtoa kafara yule anayekwenda kwenye hiyo post au vipi? Kwa nini tuwalinde hao watu? Kwa nini Serikali isiwachukulie hatua?
Mheshimiwa Spika, eti hatua tunazowachukulia; tunamhamisha kutoka kituo A kumpeleka B. Tayari huyu mtu ni mwizi, ni mbadhirifu, ataendeleza kufanya yale aliyokuwa anafanya Halmashauri A. Ifikie mahali tuonee uchungu hizi fedha. Wanapiga sana hizi fedha, lakini tunawalinda. Halafu mbaya zaidi juzi tunaambiwa kwamba, timu ya TAMISEMI imekwenda halmashauri fulani kuweka kambi. Siku zote mlikuwa wapi?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mpaka madudu yafanyike ndiyo mnakwenda kuweka kambi. Kambi for what? Tunaweka kambi for what? Watu wameshapiga hela halafu tunawaangalia, tunawahamisha hamisha tu! Ifike mahali hawa watu walioiba fedha za Watanzania, fedha zinapotea, washughulikiwe. Siyo tu kuwahamisha kituo kimoja, watu wamepiga dili za mchongo sasa hivi...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Rehema Migilla, kengele ilikuwa imeshagonga, lakini naona kuna taarifa hapa. Mheshimiwa Charles Kajege.
T A A R I F A
MHE. CHARLES M. KAJEGE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa msemaji, kwamba mkakati wa TAMISEMI kuhamishana siyo kwamba ni wajinga, hapana. Ni namna ya protection. maana yake ni kwamba anayeiba kwa sababu mkimbana kule wanaona dah, sasa tufanyeje? Wanamhamishia katika halmashauri nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina mifano mingi katika jimbo langu. Watu ambao ni wezi wamehamishiwa katika maeneo mengine. Nami nasema kesho, wale wote lazima wakamatwe. Ahsante. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Rehema Migilla, unaipokea taarifa hiyo?
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa asilimia 100. Hawa watu tusiwachekee. Masuala ya kulindana tunamrudisha mama. Mama anahangaika kila kukicha, anatafuta fedha kwa ajili ya Watanzania halafu kuna watu wachache, tena Serikali eti inawalinda, wamrudishe mama nyuma, hatukubali kabisa. Tunaongea hapa, kesho tutashika shilingi! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi/Kicheko)