Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Ripoti ya CAG, lakini na ripoti za Kamati hizi. Kwanza nakupongeza sana kwa uamuzi uliochukua kutoa siku zote hizi tuweze kujadili ripoti na haya mambo ya Kamati. Nakupongeza kwa sababu hii inaonesha ni jinsi gani ambavyo umenuia kulisaidia Taifa na kumsaidia Mheshimiwa Rais. Naamini tutakapokuwa tunafunga tutakuwa tumetoka na maazimio makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa sana kwenye kutafuta fedha za Taifa hili, lakini ukiisoma Ripoti ya CAG, narudia lugha moja kwamba, ukiwa huna akili huwezi kupata shida, ila ukiwa na akili timamu hii Ripoti ya CAG unaweza ukachukua maamuzi magumu sana. Ukisoma Ripoti ya CAG anazungumzia mtiririko wa matumizi mabovu ya fedha kwenye Taifa letu kwa muda wa miaka mitatu mfululizo. Kwa mwaka 2018/2019 CAG anasema matumizi mabovu yalikuwa ni bilioni 14. Mwaka 2019/2020, CAG anasema matumizi mabovu yalifika bilioni 380. Mwaka 2020/2021, CAG anasema matumizi mabovu yamefika bilioni 1.14, maana yake kila siku fedha za Serikali zinapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Joe Biden, Rais wa Marekani alizungumza alisema: “Corruption is a cancer, a cancer that eats away at a citizen’s faith in democracy, diminishes the instinct for innovation and creativity.”

Mheshimiwa Spika, Rais Rodrigo wa Ufilipino anasema: “Where there is no corruption, there will be no poverty.”

Mheshimiwa Spika, sasa hapa nataka kuzungumzia nini? Nataka kuzungumzia shirika moja tu la umma kwa mfano, Wakala wa Huduma za Manunuzi Serikalini (GPSA). CAG anamtaja GPSA kama ni mtu ambaye hadi dakika hii amechukua zaidi ya bilioni 10 na hajaleta magari ndani ya miaka mitatu, ndani ya miaka miwili. Utajiuliza huyu GPSA ni Wakala wa Serikali, nakupa mfano mmoja tu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wanamdai GPSA zaidi ya magari 500 na fedha amelipwa kwa muda wa miaka miwili, lakini hajaleta magari hadi leo. Ukimuuliza GPSA anasema kulikuwa na Covid. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa namuuliza GPSA Bandari ya Dar-es-Salaam ni lini ilisimama kutoa huduma wakati wa COVID? Soko la Kariakoo lilisimama wakati wa COVID, lakini GPSA alisimama kutoa huduma wakati wa COVID, Serikali inamdai magari. Achana na hapo, Wizara ya Afya wamempelekea GPSA ombi la kuwanunulia magari ya bilioni 17. GPSA kawaletea quotation ya magari 487 kwamba, kwenye hizo bilioni 17 nitanunua magari 487. Wizara ya Afya wakajiongeza wakasema sisi hatununui kupitia wewe, wameenda UNICEF, wameenda kupata magari 663.

Mheshimiwa Spika, sasa unajiuliza UNICEF sio shirika letu la ndani ambalo tunafanya nalo kazi, ila tuna Wakala ambaye ni GPSA ameweka difference ya magari 100 ndani ya Wizara ya Afya, yeye angenunua angenunua magari 400, lakini UNICEF ameweza kununua magari 663 kwa fedha zilezile bilioni 17. Sasa najiuliza Serikali yetu, wataalam wetu wana lengo gani na wana nia gani na Serikali yetu?

Mheshimiwa Spika, Bodi ya Mikopo inahangaika hawana fedha, GPSA hela anayo na ameshalipwa. Kwa hiyo, nashauri ni vema GPSA ikaangaliwa, ikaundiwa tume, ikachunguzwa. Hakiwezekani kikawa ni chombo cha kunyonya badala ya ku-regulate matumizi ya fedha ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naenda kwenye Mamlaka ya Serikali za Mitaa, nazungumzia vitu vitatu. Kuna kitu ambacho sijakisoma, hata kwenye Kamati humu sijakiona, kuna kitu kinaitwa bakaa. CAG anazungumzia bakaa kwamba halmashauri zetu nchini zilivuka na bakaa ya bilioni 30. Waheshimiwa Wabunge naomba tuelewane, mimi niko Kamati ya USEMI, halmashauri nyingi nchini zina-underestimate ukusanyaji wa mapato, zikisha- underestimate ukusanyaji wa mapato, ndani ya muda mfupi unashangaa wamevuka lengo la ukusanyaji wa mapato.

Mheshimiwa Spika, leo nazungumza, Halmashauri ya Tunduma anakotoka Mheshimiwa David Silinde, tayari robo hii wameshavuka tayari nusu ya ukusanyaji wa mapato wa bajeti waliyotuomba sisi. Maana yake ni nini? Wataenda zaidi ya asilimia 120 au 150, ile fedha inayobaki ya bakaa Wabunge jiulizeni wanaifanyia nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda halmashauri mbalimbali hapa, ukienda Halmashauri ya Kinondoni walivuka karibu na milioni 500. Ukienda kwa Mheshimiwa Cosato Chumi wamevuka karibu na bilioni moja. Ukienda Halmashauri ya Mwanza wameenda zaidi ya bilioni moja. Hawa wote wanabakiwa na bakaa hizi ambazo ukifuatilia matumizi yake ni matumizi ya chinichini, fedha za Serikali zinapigwa. Naomba sana LAAC wachunguze matumizi ya bakaa kwenye halmashauri zetu kwa sababu kimekuwa ni kichaka cha ku-underestimate ukusanyaji wa mapato, wanavuka lengo, fedha zinazobakia wanazipiga kupitia vikao na mambo ambayo hayamo kwenye bajeti na utunzaji wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kuna suala la POS. CAG anazungumzia POS anasema halmashauri 46, Mamlaka za Mitaa 46, kwa muda wa siku tatu hadi siku 400, hizi POS zilikuwa zinapotea, nyingine zinaonekana leo, kesho zinapotea kwenye mfumo hazionekani. Serikali imepoteza mapato zaidi ya bilioni 427. Sasa ni lazima tutafute mfumo bora wa jinsi gani ya kukusanya mapato kwenye halmashauri zetu, kwa sababu hizi POS zinatumika ni kichaka pia cha kuiba fedha za Serikali.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine, hili la asilimia 10. Asilimia 10 nilizungumza hapa kwa muda wa miaka mitatu yote hadi sasa tuna zaidi ya bilioni 100 za asilimia 10 ziko mitaani, lakini kwenye Taifa hili wenzetu wa Jiji la Dar-es-Salaam walijaribu kutumia DCB Bank kama sehemu ya kusambazia fedha na DCB Bank ilifanya kazi vizuri sana. Walivyogundua kwamba, inafanya vizuri sana kazi wakaiondoa kwa sababu walikuwa hawana sehemu ya upigaji, wameirudisha kwenye mfumo wa kawaida fedha zinapigwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda Burundi, Serikali ya Burundi inajua sana kusimamia hizi fedha. Wameandaa madirisha ya kibenki kwa ajili ya wanawake na vijana ili hizi fedha ziweze kusimamiwa vizuri, lakini kwenye Taifa letu wanakwepa huo mlango kwa sababu unakwepa mianya ya upigaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, CAG anasema mwaka 2020/2021 bilioni 47 hazijarejeshwa, ziko kwenye mifuko ya watu, lakini halmashauri hazijapelekwa zaidi ya bilioni sita, unakuta is a lot of money. Mheshimiwa Rais anatafuta hela ya ruzuku ya mafuta, hela zimefichwa. Mheshimiwa Rais anafuta ruzuku kwa ajili ya mbolea, hela zimepigwa. Tunamsaidiaje Mheshimiwa Rais wetu kama hizi fedha tutaendelea kuruhusu kuendelea kupigwa hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna watu walishauri hapa kwamba, watu wengine wapigwe risasi na wengine wanyongwe, lakini nasema kabla hatujalifanya hilo lazima tufanye list of shame. Lazima tutangaze list of shame of this country kwenye institutions za Serikali, kwenye Mawakala wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakupa mfano, kwenye list of shame mojawapo, kuna watu hapa wanaitwa Mamlaka ya Maji Safi ya Dar-es-Salaam. CAG anasema wamekusanya zaidi ya milioni 755 kwa kudanganya sio kusoma mita; wanafika mtu wanamwambia tupe hizo hela, zaidi ya milioni 700, hii lazima iingie kwenye list of shame.

Mheshimiwa Spika, nenda pia kwenye Shirika la Bima ambalo tuna ndege 11, lakini wanakata zaidi ya dola milioni tano wakati Rwanda wana ndege 12 wanakatwa kwa dola milioni mbili. Maana yake ni Shirika letu la Bima nalo ni kichaka cha wizi wa fedha ambazo ni fedha nyingi zinakwenda huko kwenye bima. Achana na hilo tu, Shirika la Bima la Afya limeacha dola laki tatu kwenye akaunti namba 1156119 kwenye benki iliyoko Uingereza kwa zaidi ya miaka mitano, halisemi kama hizo fedha zipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, twende kwenye Shirika la Bandari. Ukienda kwenye shirika hili napo kuna upigaji. Wana zaidi ya vifaa vya bilioni mbili ambavyo vilitakiwa vipigwe mnada kwa miaka mitatu iliyopita, wanapiga chenga, vinaibiwa, vimepotea, vifaa vya bilioni mbili, lakini wana fedha zaidi ya dola laki tatu kwenye Benki ya Deutsche akaunti iliyoko Uholanzi, hawajawahi kuzisema kwa muda wa miaka mingi zipo kule. Mheshimiwa Rais anatafuta fedha hizi kila siku. Rais hawezi kufika kila kona, Watanzania hili ni Taifa letu tunataka tuamini kwamba, hii nchi inajengwa na wenye moyo na inaliwa na wenye meno? Hatuwezi kuamini katika hilo. Hili ni Taifa letu lazima tulipiganie na hawa wataalamu wanatusikia, nawaomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nenda kwenye Bodi ya Mikopo. Bodi hii ilikopa mkopo, ambao Mheshimiwa Mkenda anahangaika nao, walikopa mkopo wa bilioni 54, wame- delay kulipa, saa hizi wanadaiwa bilioni 68. Yaani kutoka bilioni 54 waliyokopa, sasa hivi wanatakiwa walipe bilioni 68, over 100% wanadaiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nenda kwenye Mamlaka ya Elimu. Mamlaka ya Elimu ya Ufundi, Makete Jimboni kwangu, wameingia mkataba wa kujenga na Wakala wa Nyumba za Taifa, jengo la bilioni 1.5 hadi leo; mtu amelipwa, majengo hayajajengwa, ametawanyika hadi saa hizi hayupo, hii ni list of shame kwenye Taifa letu, mnataka list of shame ipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakuomba tutakavyoondoka kwenye maazimio haya, hawa watu wasione kama sisi tunapiga story, ni muda muafaka wa Bunge lako, wa Kiti chako kuonesha kwamba, tuna msuli wa kupigania Taifa letu, kuonesha kwamba, tuna uwezo wa kuwawajibisha. Kama hatuwezi kuwapiga risasi basi hata kesho tuwaone magerezani. Kama hatuwezi kuwanyonga basi kesho tuwakute magerezani kwa sababu, wote ni Watanzania wenzetu na wananufaika kwa pesa za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na Mungu akubariki sana. (Makofi)