Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukushukuru wewe na kulishukuru Bunge lako Tukufu kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Lakini zaidi nimshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini ninamshukuru Rais wetu; hapa Bungeni mmetupitishia trilioni 1.1 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za afya, lakini yeye kwa kutumia mbinu nyingine tumepata nje ya bajeti zaidi ya bilioni 891.5. Siyo kazi rahisi; una trilioni 1.1 halafu nje ya bajeti inapatikana fedha karibia na hizo zilizopo kwenye bajeti.
Mheshimiwa Spika, hizi fedha zimepunguza rufaa za nje kwa zaidi ya asilimia 97. Tulikuwa na hospitali mbili tu za mikoa ambazo mpaka mwezi Februari zilizokuwa na CT scan, lakini sasa hospitali zote za mkoa zitakuwa na CT scan. Leo kwa mwezi Oktoba na Novemba tunakwenda kugawa X-ray machines 174 kwa nchi nzima kwa Wabunge wote na hakuna wilaya ambayo haitaguswa. Hii ni kazi kubwa sana ambayo Rais wetu ameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unakumbuka Mheshimiwa Rais alikwenda pale Muhimbili akapewa ripoti kwamba kuna watoto zaidi ya 500 ambao wana ulimi mkubwa wanaosubiri kwenda nje kutibiwa India. Rais wetu aliagiza pale na vifaa vililetwa na sasa watoto wote wametibiwa ndani ya nchi, hawajaenda nje, na wapo kwenye familia zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende sasa kwenye hoja. Kulikuwa na hoja nyingi lakini naomba niende kwenye tatu. Hoja ya kwanza ni bima kutorejesha gharama za matibabu. Kwa mwaka 2021/2022 kwenye halmashauri zote madai yalikuwa bilioni 29.6 na sasa zimerejeshwa bilioni 26.6, kwa maana kuna asilimia nane ndiyo bado hazijarejeshwa kutokana na sababu mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, sisi tumekwenda mbali zaidi na tumekwenda kwenye maeneo mbalimbali tumeangalia tatizo hili. Nitolee mfano sehemu moja ya Mkoa wa Kigoma. Tulikwenda tukawakuta kwenye bima tu peke yake walikuwa wanapata milioni 70 kwa mwezi, lakini tulipokaa kwa kushirikiana na Wabunge, Serikali ya Mkoa na watumishi wa hospitali husika, walifanya mabadiliko na sasa ukienda Hospitali ya Mkoa wa Kigoma wanapata zaidi ya milioni 200 kwa mwezi kupitia bima.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hatukuwa tunapoteza tu pesa kwenye eneo la marejesho lakini kulikuwa na pesa ambazo hazikuwa zinadaiwa nyingi sana kwenye eneo letu. Hilo eneo tumeshaliboresha. Na kuna makubaliano yanaendelea na TAMISEMI na Bima kuhusu pesa hizi ili waweze kupelekewa vifaa na vitu vingine ambavyo vitatiokea kule upande wa bima.
Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ni kuisimamia MSD kupeleka vifaa kulingana na mahitaji. Moja, kuna hatua mbalimbali zilipendekezwa, hatua zote ambazo zilipendekezwa kwa ajili ya kuchukuliwa kutokana na matatizo yaliyokuwepo kwenye mfumo wa dawa zimeshachukuliwa.
Mheshimiwa Spika, vilevile, baada ya kuchukua hatua hizo tukaenda mbali zaidi tukasema kwamba kuna mambo yaliyokuwa yanasababishwa na masuala ya manunuzi, ucheleweshaji ulikuwa unasababishwa na manunuzi. Tulichokifanya pale tumeweka mikataba ya muda mrefu ili kuondoa hayo mambo ambayo yanachelewesha upatikanaji wa dawa kutokana na sheria za manunuzi kuchukua muda mrefu kila hitaji linapotokea.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na tatizo la halmashauri zetu kupeleka fedha MSD lakini dawa hazipelekwi kule kwenye halamshauri zetu. Tulichokifanya hapa, kwa fedha ambazo tayari halmashauri wanazo, kama MSD hana dawa hizo, ndani ya saa 24 atoe OS ili halmashauri waweze kwenda kununua dawa sehemu nyingine badala ya kuchukua fedha na kuzipeleka MSD na wanashindwa kupeleka dawa sehemu husika.
Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo, tunakwenda kushirikiana na kamati zetu za ulinzi na usalama kwenda kufika zaidi, tushirikiane pamoja kwenye kufanya kazi kwenye medicine audit na kutengeneza mfumo ambao tutaona dawa inapotokea MSD mpaka inaposhuka halmashauri na jinsi dawa zinavyotumika. Mfumo uweze kuonekana upande wa TAMISEMI na upande wa Afya, tuhakikishe kunakuwepo na control kubwa ya dawa na vifaatiba.
Mheshimiwa Spika, eneo la tatu ni eneo la uteketezaji wa dawa. Moja; kwa nini kumekuwepo na dawa nyingi zilizoteketezwa. Tumeona kwamba kulikuwepo na mabadiliko makubwa ya tiba, hasa kwenye eneo la Ugonjwa wa UKIMWI, maana kwenye eneo hilo mwaka 2018 na 2021 kumekuwepo na mabadiliko makubwa sana kwenye eneo la tiba. Lakini wakati mabadiliko yanafanyika kuna dawa tayari zilikuwa zimepelekwa kwenye site. Hizo dawa hazikutumika kwa sababu ya hayo mabadiliko na ni dawa zenye thamani ya bilioni 16.
Mheshimiwa Spika, wakati huohuo kumekuwa na mabadiliko ya teknolojia ambayo nayo yamesababisha vitendanishi aina mbalimbali vyenye thamani ya bilioni sita kuharibika. Na fedha hizi ni zile za wadau, na mara nyingi wanapeleka pesa lakini wakati huohuo wanakuja na mambo kama haya. Hilo tumekwenda nalo kulishughulikia.
Mheshimiwa Spika, sasa ni kwamba vitu hivi vyote vitafanyika kupitia Mfuko wa MSD, siyo kufanyika tena direct kwenda kwenye mikoa yetu ili tuweze kufanya reconciliation na kuondoa hili ambalo limeonekana hapa.
Mheshimiwa Spika, kwenye mfumo wetu wa dawa wa manunuzi ya kawaida…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Sekunde 30, malizia.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwenye mfumo wetu wa kawaida kumekuwa na asilimia nane kweli ya upotevu wa dawa kama hiyo. Tumeshashughulikia maeneo yaliyokuwa na shida, kama alivyosema Waziri wa TAMISEMI, kuna mabadiliko makubwa sana yamefanyika, wakuu wa idara na mambo mengine. Wakati huohuo tunataka, ndiyo maana tunasema tunakwenda kukaa na kamati za ulinzi na usalama, tumekwenda Nzega tumekuta ndani ya hospitali duka la dawa linauza dawa bei ghali kuliko maduka yaliyozunguka hospitali. Lakini ni mkakati uliotengenezwa palepale ndani.
Mheshimiwa Spika, maana yake nini; tukishirikiana kwa pamoja, dawa hazitaharibika kwa sababu watu sasa wanakwenda kununua dawa nje ya hospitali badala ya ndani na zinabaki zinaharibika. Hayo yote tumeshayafanya.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)