Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. JAPHET N. HASUNGA - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, naomba kuchukua nafasi hii kutoa ufafanuzi wa hoja chache ambazo Waheshimiwa Wabunge wamechangia katika taarifa ambayo tuliwasilisha hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa na kwa moyo wa dhati, naomba kukushukuru wewe mwenyewe kwa kutoa muda wa kutosha kwa upande wa Bunge kuweza kuchambua taarifa ya CAG kwa undani. Pili, naomba kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita Mama yetu mpendwa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyoendelea kutafuta fedha na rasilimali mbalimbali ili ziweze kusaidia katika kuleta maendeleo ya nchi yetu, nampongeza sana. Tatu, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote ambao kwa namna mbalimbali wamechangia katika hoja hii ambayo tumeiwasilisha. Wabunge takribani 82 wamechangia, michango yao imesaidia sana kuboresha maazimio ambayo kwa kweli tutayaleta hapa Bungeni sasa.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kuwashukuru Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa namna mbalimbali walivyochangia hizi hoja na fafanuzi mbalimbali ambazo wamezitoa. Kwa kweli tunawapongeza sana, wametoa ufafanuzi, wamenirahisishia ili niende moja kwa moja katika kusoma maazimio.

Mheshimiwa Spika, jukumu la kuisimamia Serikali ni jukumu la kikatiba, kwa mujibu wa Katiba yetu ukisoma ibara ya 63(2) ndio inayoelekeza Bunge hili kama chombo mahususi cha kuisimamia Serikali. Sambamba na hilo tunazo sheria, lakini tunazo kanuni zinazotuongoza katika kutekeleza majukumu yetu. Kamati yetu ya Hesabu za Serikali inazungumzwa pia katika Kanuni za Bunge ambapo katika Nyongeza ya Nane imeeleza mambo tunayotakiwa kuzingatia katika utekelezaji wa majukumu.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme hili ili Waheshimiwa Mawaziri watuelewe. Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge mambo tunayoyaleta ndani ya Bunge ni maeneo ambayo yana matumizi mabaya ya fedha za umma. Kwa hiyo, yapo mambo mazuri ambayo yamefanywa kwa mujibu wa kanuni hatuyaleti hapa. Tunaelewa mambo mengi yanaendelea, lakini tunaleta yale yenye viasharia vya matumizi mabaya, hayo ndiyo tunayaleta humu Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinachotuongoza katika kutekeleza majukumu yetu, tunaangalia Sheria za Fedha. Sheria ya Fedha ya mwaka ya mwaka 2001, marekebisho ya mwaka 2004 mpaka marekebisho ya mwaka 2020, inatuongoza kwa namna ambavyo fedha za umma na mali zinavyotakiwa kusimamiwa katika kila eneo na huo ndio msingi wa kuchambua hoja zetu humu ndani. Pia kanuni inatuelekeza, sisi Kamati ya PAC tunajadili mambo ambayo yamebainishwa katika ripoti ya CAG. Kwa hiyo, kama hayajabainishwa hatuwezi kuyajadili humu ndani, hivyo, tunayajadili haya, zipo Sheria za Manunuzi na sheria nyingine ambazo tunaendelea kuzizungumzia.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme kwa kifupi sana, wengi wamechangia utekelezaji wa maagizo ya Kamati, maazimio ya Bunge na hoja za CAG. Katika maeneo mengi bado utekelezaji wake ni hafifu na wajumbe wamechangia, nawapongeza sana wameliona kabisa na ndio uhalisia uliopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna maeneo yenye udhaifu katika usimamizi wa fedha za umma. Sheria zipo, taratibu zipo, miongozo ipo, lakini watu wanakiuka kwa malengo yao na kwa nia zao. Nadhani hili halikubaliki.

Mheshimiwa Spika, kwa uamuzi uliouchukua kwamba sasa Bunge liisimamie Serikali, hapa maazimio, nataka niwahahkikishie Waheshimiwa Wabunge, nilisoma maazimio hapa, lakini sasa yanayokuja yatawezesha Bunge kuwa ni chombo kinachosimamia Serikali. Maazimio haya yamezingatia yale waliyoyasema ili Bunge kiwe chombo mahususi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye maeneo, yapo maeneo ya mifumo na Serikali kila siku hapa wanasema wanaenda kutengeneza mfumo mwingine. Nataka niliambie Bunge hili kuwa, eneo la mifumo ya TEHAMA linatumia fedha nyingi sana za umma na mifumo hiyo mingine wanatumia fedha nyingi halafu wanaiacha, wanakwenda tena kwenye mfumo mwingine. Ni eneo ambalo lazima litazamwe kwa mapana na marefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni eneo la manunuzi. Eneo la manunuzi ya vifaa na mali linatumia fedha nyingi na ni eneo ambalo ubadhirifu mwingi umekuwa ukitokea. Kwa hiyo hili eneo lazima liimarishwe. Kuna eneo la usimamizi wa mikataba, lakini yapo maeneo ya usimamizi wa ndani. Nataka niwaambie, bila kuwa na mfumo thabiti au mfumo madhubuti wa usimamizi wa ndani (internal controls), hizi hela zitaendelea kupigwa. Tuiombe Serikali waimarishe hiyo mifumo, itasaidia kupunguza ubadhirifu, rushwa na itasaidia kuhakikisha uzembe unapungua.

SPIKA: Mwenyekliti tuongoze vizuri hapo, umesema uiombe Serikali, ndio umeshaanza maazimio au ni jambo lingine? Maana sasa Wabunge tutakuwa hatuelewi hapa wakati tutakapokuwa tunahojiwa, kwenye hilo unalolisema azimio la Bunge ni nini? Yaani kama bado uko kwenye maelezo ya awali, sawa. Tuongoze vizuri, maana hatutaki kufika mahali tukawa hatujui Bunge linaamua nini?

MHE. JAPHET N. HASUNGA - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, bado sijaanza maazimio. Kwa hiyo ni uchangiaji tu.

SPIKA: Kwa hiyo sasa unaleta maombi kwa Serikali?

MHE. JAPHET N HASUNGA, MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

Mheshimiwa Spika, labda katika maeneo machache nataka nitoe ufafanuzi kwa dakika chache. Kuna baadhi ya Waheshimiwa akiwemo Mheshimiwa Mpina alizungumzia suala la Deni la Taifa ambalo halikuonekana kwenye taarifa hiyo. Nataka niliambie Bunge lako kwamba, Kamati ilichambua Deni la Taifa, tuliangalia vigezo vyote na tuliangalie taarifa iliyopo, hakukubainika dosari zozote katika hilo, ndio maana kwenye ripoti hatujalileta. Vinavyokuja humu ni vile ambavyo vinaonekana ni madhaifu ya muda mrefu na ambayo yanaendelea kujirudia. Tulipoona hakuna hoja hatujaleta na ndio maana taasisi nyingi hatukuleta humu kwa sababu hatukubaini mapungufu kwenye hayo maeneo.

Mheshimiwa Spika, lipo eneo la KADCO, eneo hili nashukuru jinsi ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamelichambua na michango ya wajumbe imekuwa mizuri sana. Suala la Kamati lilikuwa kwamba kama wawekezaji, waliwekeza shilingi ngapi? Hapa ndiyo tulitaka Serikali watuambie, hawa wawekezaji waliokuja wakati huo wakaunda hiyo KADCO waliwekeza shilingi ngapi? Mpaka wakalipwa hiyo millioni 5.3, walilipwa kwa uwekezaji upi? Hilo ni suala la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili, tunataka kujua baada ya Serikali kuchukua mwaka 2010 mpaka leo KADCO imetekeleza mambo gani na fedha hizo za umma zimesimamiwaje? Bado hatujapata majibu ya hayo yote. Yapo mambo ya TPA na mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda naomba niende kwenye uchambuzi na mapendekezo ya maazimio moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo ya Kamati yametolewa kwa kuzingatia matokeo ya uchambuzi wa Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, mahojiano na Maafisa Masuuli pamoja na majadiliano na michango ya Waheshimiwa Wabunge iliyotolewa kuanzia tulipoanza kujadili tarehe 2-5 Novemba, 2022.

Mheshimiwa Spika, mapendekezo hayo kwa kiasi kikubwa yatasaidia kuongeza uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma kama ambavyo Bunge linatakiwa kusimamia na kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamesisitiza katika siku hizi nne za mjadala hapa Bungeni. Mapendekezo yanayoletwa mbele ya Bunge lako Tukufu ni kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, moja, azimio kuhusu nakisi ya Ukusanyaji wa Mapato kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA kiasi cha Shilingi trilioni 2.81: -

KWA KUWA taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amebainisha kiasi cha Shilingi trilioni 2.81 cha mapato ambayo hayakukusanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwa mwaka wa fedha 2020/2021 kutokana na mapungufu mbalimbali;

KWA HIYO BASI Bunge liazimie kwamba: -

(a) Serikali ifanye mapitio ya kina ya mfumo mzima wa ukusanyaji kodi (comprehensive tax regime review) ili kuhakikisha kodi zote zinakusanywa kama ambavyo Bunge linaidhinisha na kwa mujibu wa taratibu zetu.

(b) Serikali ifanye uchunguzi na kufanya hatua stahiki kwa watumishi wote wa Mamlaka ya Mapato Tanzania waliohusika kwa kukadiria kodi chini ya kiwango, kutoshughulikia madeni ya kodi kwa wakati, kuchelewa kusajili mapingamizi ya kodi kwa wakati, kutosimamia ushuru wa forodha kwenye bidhaa za mafuta na magari pamoja na usimamizi usioridhisha wa matumizi ya mashine za kielektroniki; hali iliyosababisha ongezeko la madeni ya kodi kwa zaidi ya 95% ndani ya mwaka huo wa fedha hivyo kuikosesha Serikali mapato ya kuhudumia wananchi.

Mheshimiwa Spika, mbili, azimio kuhusu dosari katika usimamizi wa mikataba na athari zake katika matumizi ya fedha za umma: -

KWA KUWA Kamati imebainisha upungufu katika uingiaji na usimamizi wa mikataba katika taasisi mbalimbali za Serikali hali iliyosababisha hasara kwa Serikali ikiwemo shilingi bilioni 68.7 kwa TANROAD, TANESCO dolla za Kimarekani milioni 153.43 na NFRA dola za Kimarekani milioni 33.4 na TPA bilioni 137.38;

KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba: -

(a) Serikali ifanye uchunguzi kubaini iwapo riba zilizotokana na mikataba ya ujenzi wa barabara katika TANROAD zilikuwa na uhalali na ulazima wa kuwepo? Hatua stahiki zichukuliwe kwa wahusika kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi huo. (Makofi)

(b) Serikali ichukue hatua stahiki kwa watumishi wa Wizara ya Nishati, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha na Mipango na TANESCO walioshiriki katika mchakato mzima wa uingiaji, usimamizi, utekelezaji na uvunjaji wa mikataba kati ya TANESCO na Symbion. (Makofi)

(c) Serikali ichukue hatua stahiki za kisheria kwa mkandarasi aliyechelewesha kukamilisha ujenzi wa ghati ya kuegesha meli katika Bandari ya Mtwara.

Mheshimiwa Spika, tatu, azimio kuhusu hali ya ukwasi kuhusu taasisi za kimkakati za Serikali (TPDC, TANESCO na STAMICO): -

KWA KUWA Taarifa ya CAG imebainisha changamoto za mtaji katika Mashirika ya Umma ya kimkakati kama TPDC, TANESCO na STAMICO;

KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina iongeze mtaji katika mashirika ya kimkakati ya Serikali kwa kufanya marekebisho ya msingi katika madeni ya taasisi hizo ili kuyageuza kuwa mtaji (equity). Pamoja na hatua hiyo, Serikali ihakikishe kuwa mikataba inayoingiwa na TANESCO, TPDC na STAMICO inakuwa na maslahi makubwa ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, nne, azimio kuhusu Ukaguzi maalum wa REA,Uhamiaji na Hombolo:

KWA KUWA Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, zimebainisha mambo muhimu katika kaguzi nne zilizopitiwa na kuchambuliwa na Kamati ambazo zimebainisha upungufu katika usimamizi wa fedha za umma;

KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba: -

(a) Serikali ichukue hatua za kisheria kwa Mkandarasi wa kampuni ya Derm Electric Tanzania Limited kwa udanganyifu na ubadhirifu pamoja na hatua za kisheria na kinidhamu kwa watumishi wa REA na TANESCO waliohusika kusimamia Mradi wa REA, awamu ya pili, Mkoa wa Mara, kwa kutotimiza majukumu yao ipasavyo.

(b) Serikali ichukue hatua za kisheria kwa watumishi 32 wa Idara ya Uhamiaji waliotajwa kuhusika katika mauzo ya sticker za Visa bandia katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro kwa kuzingatia uhusika wa kila mmoja na matokeo ya ukaguzi maalum.

(c) Serikali ichukue hatua za kisheria kwa watumishi wawili waliojihusisha na ubadhirifu wa fedha za ada ya wanafunzi katika Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo.

Mheshimiwa Spika, kwenye ile (b), Mheshimiwa Waziri ametoa maelezo kwamba wameifanyia kazi, lakini sisi Kamati hadi tunachambua, juzi wakati wanakuja kwenye Kamati ni watumishi 11 tu ambao walikuwa wamepelekwa Mahakamani na hao 11 nao wote wamesharejeshwa. Kwa hiyo Waziri kusema kwamba hatua zilishachukuliwa, sisi kama Kamati mpaka juzi ilikuwa bado hatua hazijachukuliwa. Labda Waziri kama atatuambia kwamba hatua zimechukuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tano, azimio kuhusu kutozingatiwa kwa Sheria ya Fedha za Umma, Sura ya 348:

KWA KUWA kupitia Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Kamati imebaini ukiukwaji wa Sheria za Fedha za Umma, Sura 348 hivyo kuchangia upotevu wa fedha za Serikali;

KWA HIYO BASI Bunge linaazimia yafuatayo: -

(a) Shirika la Masoko Kariakoo, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, afanye ukaguzi wa kiuchunguzi yaani (forensic audit) ili kubaini iwapo kuna ubadhirifu wa fedha za umma uliofanywa na kufichwa baada ya soko hilo kuungua moto. Aidha, vyombo vya dola vianze uchunguzi kwa uliokuwa uongozi wa Soko la Kariakoo ili kubaini iwapo wahusika wana jinai katika kuficha nyaraka za fedha kwa Wakaguzi.

(b) Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART). Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, aombwe kufanya ukaguzi maalum (special audit) wa malipo ya fidia ya kiasi cha bilioni moja na malipo ya fedha za usumbufu kiasi cha Shilingi milioni 434 yaliyofanyika DART ili kubaini iwapo yalifanyika kwa mujibu wa sheria.

(c) Mfuko wa Tozo na Tuzo wa Jeshi la Polisi, Fungu 28. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum (special audit) wa matumizi yote ya Mfuko wa Tozo na Tuzo wa Jeshi la Polisi tangu ulipoanzishwa na kisha kutoa taarifa yake kwa Bunge mapema iwezekanavyo. Aidha, Mlipaji Mkuu wa Serikali aandae kanuni za kusimamia uendeshaji wa Mfuko huo na malipo yote kutoka kwenye Mfuko yafanyike kwa kuzingatia kanuni zilizoandaliwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, sita, azimio kuhusu umiliki na uendeshaji wa Kampuni ya Uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KADCO):

KWA KUWA mkataba wa uendeshaji wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro kati ya Serikali na Kampuni ya KADCO (concession agreement) unakosa misingi ya kisheria tangu mwaka 2010, wakati ambapo Serikali ilinunua hisa kwa asilimia 100 za KADCO baada ya malipo ya fedha za umma dola za Marekani milioni 5.3;

KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba Serikali irejeshe shughuli zote za uendeshaji wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kama ambavyo inafanyika kwa viwanja vingine vya ndege hapa nchini kwa kuzingatia majukumu ya kisheria ya TAA na uamuzi wa Serikali uliokuwa umetolewa hapo awali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aidha, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi wa kina (comprehensive audit) wa mapato na matumizi ya KADCO kuanzia mwaka 2010 baada ya kuanza kumilikiwa kwa 100% na Serikali hadi sasa na Bunge lijulishwe ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, saba, azimio kuhusu utendaji wa kifedha wa benki za Serikali TCB na TIB:

KWA KUWA Taarifa ya CAG imebainisha kutokuwepo kwa mtaji wa kutosha wa benki ya Serikali za TIB na TCB, hivyo kukwamisha shughuli za benki husika na kuhatarisha fedha za umma zilizowekwa kwenye benki hizo;

KWA HIYO BASI Bunge linaazimia kwamba TCB na TIB zikusanywe mikopo yote ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali za dhamana zilizowekwa na wakopaji husika kwa mujibu wa sheria ili kurejesha mtaji wa benki inayohusika.

Aidha, vyombo vya dola vifanye uchunguzi wa mikopo yote chechefu iliyotolewa na TIB na TCB ili kubaini iwapo ilitolewa kwa kuzingatia taratibu za kibenki na kuchukua hatua dhidi ya watu waliohusika.

(viii) Kuhusu ubadhirifu katika upanuzi wa Bandari ya Tanga.

KWA KUWA, Kamati ilifahamishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwamba Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Tarehe 14 Juni, 2021 aliomba kufanyika kwa ukaguzi wa kiuchunguzi na kuainisha tuhuma za ubadhirifu wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka uliofanywa na Watumishi wa TPA katika utoaji wa tuzo ya zabuni ya uboreshaji wa Bandari ya Tanga kwa Kampuni ya China Harbor Engineering Company Limited (Check). Ukaguzi huo umekamilika na kubaini ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma takribani Bilioni 65.3 ambayo ni hasara kwa Serikali; Na kwa kuzingatia masharti ya Kanuni ya 81(a) ya Kanuni za Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2009, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU alipewa matokeo ya ukaguzi huo;

KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali ichukue hatua za kisheria kwa makampuni na Watumishi wote wa TPA waliotajwa katika taarifa ya ukaguzi maalum kwa kuhusika kwao katika ubadhirifu wa fedha za umma wakati wa utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa Bandari ya Tanga. (Makofi)

(ix) Kuharibika kwa dawa na kutokuwepo kwa dawa katika baadhi ya maeneo ya kutoa Huduma za Afya.

KWA KUWA, taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Bohari ya Dawa (MSD), umebaini uwepo wa dawa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 23.04 zilizokwisha muda wake zinatakiwa kuharibiwa. Pamoja na hilo ukaguzi umebaini kutokuwepo kwa dawa katika baadhi ya maeneo ya kutolea huduma za afya wakati ambapo kuna dawa zina maliza muda wake wa matumizi;

KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Bohari ya Dawa wasitoe dawa, vitendanishi au chanjo ambazo muda wake wa matumizi upo chini ya Miezi Sita ya kutumika yaani Shelf Life. Aidha, Serikali isipokee dawa, vitendanishi au chanjo za msaada ambazo pia muda wake wa matumizi upo chini ya Miezi Sita na kupelekwa MSD. Aidha MSD ipeleke dawa kwa wakati kwa wanao hitaji kwa maeneo yote ambayo wanakuwa wamepokea fedha zao. (Makofi)

(x) Mapitio na tathmini ya hesabu za Mifuko ya Hifadhi za Jamii.

KWA KUWA, uchambuzi wa taarifa ya CAG umebainisha kupungua kwa uwezo wa mifuko ya PSSSF kulipa mafao yake, pamoja na uwepo wa deni ambapo mifuko ya PSSSF na NSSF inadai kwa Serikali takribani Trilioni 1.5;

KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali iwasilishe Bungeni mpango wa malipo ya mikopo ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (Loan Repayment Schedule) kwa madeni yote ambayo mifuko inaidai Serikali. Mpango huo wa malipo uwasilishwe Bungeni kabla ya kukamilika kwa mwaka wa fedha 2022/2023. (Makofi)

(xi) Kuhusu mapungufu katika uzingatiaji wa Sheria za Manunuzi ya Umma na Kanuni zake.

KWA KUWA, taarifa za CAG zimebainisha kuwa baadhi ya Taasisi za Umma zimekiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma na Kanuni zake hivyo kusababisha upotevu wa fedha za umma;

KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) ifanye ukaguzi wa kiuchunguzi katika manunuzi yenye dosari yaliyobainishwa na Kamati katika taasisi za TANESCO, Fungu Na. 57 Wizara ya Ulinzi, na kisha kuchukua hatua stahiki kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi. Aidha, TAKUKURU ianzishe uchunguzi wa wahusika waliofanya manunuzi bila kuzingatia sheria katika taasisi hizo na kuchukua hatua stahiki.

(xii) Kuhusu mapungufu katika mifumo ya udhibiti wa ndani.

KWA KUWA, taarifa ya CAG katika Mafungu mbalimbali zimebainisha mapungufu katika mifumo ya udhibiti wa ndani, hivyo kupelekea upotevu wa fedha za umma;

KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia;

(a) Serikali ichukue hatua za kisheria kwa watendaji na kampuni zilizohusika na ununuzi na usimikaji wa mifumo ambayo imeshindwa kufanya kazi kwa ufanisi katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA). Aidha, Kampuni hizo zifungiwe na Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi Serikalini (PPRA) kujihusisha na shughuli za usimikaji wa mifumo hapa nchini.

(b) Bodi ya SUMA JKT, ichukue hatua za kinidhamu na kisheria kwa Watendaji waliokuwa wakisimamia mradi wa mauzo ya matrekta kwa kuruhusu uuzaji wa matrekta bila mikataba ya mauzo.

(xiii) Kuhusu taarifa ya ukaguzi wa ufanisi.

KWA KUWA, taarifa Nne za ukaguzi wa ufanisi zimebainisha masuala kadhaa katika taasisi za Serikali yanayohusu dosari katika usimamizi wa fedha za umma;

KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi wa kina (Comprehensive Audit) katika mchakato mzima wa ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Aidha katika kipindi cha kila Miezi Mitatu Serikali ihakikishe inawasilisha Bungeni taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi wa ufanisi yaliyotolewa na CAG kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Tume ya Madini, TANROADS na BRELA.

(xiv) Usimamizi usioridhisha wa taarifa na huduma katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

KWA KUWA, taarifa ya CAG imebainisha dosari katika usimamizi na udhibiti wa taarifa muhimu za wanufaika wa huduma za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya na gharama za matibabu ambapo pamoja na mambo mengine ilibaini utolewaji wa huduma za uzazi kwa upasuaji wa wanaume 731. Aidha ukaguzi ulibaini kuwa NHIF kukataa kulipa malipo ya Shilingi Bilioni 3.18 kwa hospitali za Serikali zilizotoa huduma kutokana na kuwa na mfumo wenye mapungufu, utambuzi na usimamizi wa taarifa;

KWA HIYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali ifanye uchunguzi wa Idara ya Usimamizi na Udhibiti wa Huduma katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili kubaini iwapo inatekeleza majukumu yake ipasavyo. Aidha uchunguzi ufanyike kubaini watoa huduma ambao wamekuwa wakiuhujumu Mfuko kwa kuongeza gharama za matibabu kwa njia ya udanganyifu na kisha kuchukua hatua stahiki kwa wote watakaobainika.

Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kwa namna ya pekee kukushukuru wewe kwa namna ulivyosimamia mjadala wa taarifa za Kamati zinazotokana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao yenye tija na kujenga, ambayo imesaidia sana kuboresha mapendekezo ya maazimio ambayo yamewasilishwa hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, naafiki.