Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kupata nafasi ya kuchangia mjadala huu muhimu sana kwa mstakabali wa Wizara ya Elimu na Taifa letu kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, na mimi nataka nielekee moja kwa moja kwenye hadidu ya rejea iliyotokana na maelekezo yako ndani ya Bunge lako hili Tukufu.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba maelekezo yaliyokuja kwenye Kamati yalikuwa ni kuona na kusikiliza Wizara pamoja Bodi ya Mikopo kama kuna pingamizi, kuna resistance au kuna kupingwa kwa maelekezo ya Wizara. Hata hivyo, kabla sijaendelea nataka kulithibitishia Bunge lako, mimi ni msema kweli na nitasema kweli daima, hakuna chembe chembe za kuzuia au kutokutekelezwa kwa maelekezo ya Wizara kwenye Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waziri alipofika mbele ya Kamati alieleza kwa uwazi kwamba yeye hana shida na Bodi ya Mikopo. Na maelezo yake alithibitisha kwa kuonesha kwamba yeye ndiyo mwenye mamlaka ya kuiwajibisha Bodi, na kwamba kama kungekuwa na namna yoyote ya kupingwa na Bodi angechukua hatua kwa sababu ipo kwenye mamlaka yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini alikwenda mbali zaidi, akasema maelekezo aliyoyatoa yote yalitekelezwa na Bodi, kwa hiyo hakuna suala la resistance. Hii inakinzana na maelezo ambayo yalitolewa mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Bodi ya Mikopo walithibitisha kwamba siku ambayo Wizara iliitembelea Bodi, ilikuwa ni mwaliko wa Bodi ya Mikopo kwa ajili ya kwenda kuzindua utaratibu mpya wa utolewaji wa mikopo kwa mwaka 2022/2023. Wakati Wizara imefika kwenye Bodi, ilienda pamoja na Wajumbe wa Kamati ambao Mheshimiwa Waziri aliwateua na Waziri alitoa maelekezo. Kwamba analeta Kamati husika ambayo aliitambulisha katika mkutano huo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa mambo kadhaa, lakini hapakuwa na maandishi.
Mheshimiwa Spika, government works on paper, hapakuwa na maelekezo ya kimaandishi kutoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara kwenda kwenye Bodi kuelekeza namna gani timu hiyo itakwenda kufanya kazi na hadidu za rejea ni zipi. Jambo hilo lilisababisha kuchelewa kutekelezwa kwa maelekezo hayo. Mpaka ilipoandikwa barua, Bodi haikuleta resistance, ilitekeleza. Kwa kuthibitisha hayo Bodi iliongeza hadidu za rejea katika hadidu za rejea mbili zilizopelekwa kwenye Bodi na Katibu Mkuu wa Wizara. Hii inatuonesha kwamba Bodi ilikuwa tayari kufanya kazi na Kamati iliyoundwa na Waziri.
Mheshimiwa Spika, lakini mbali zaidi, Bodi imegharimia gharama za Wajumbe wa Timu ya Uchunguzi kwenye Bodi ya Mikopo, Bodi ndiyo imegharamia. Hii inathibitisha pia kwamba hapakuwa na shida yoyote ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri kwenye Bodi.
Mheshimiwa Spika, shida ambayo tumeiona kubwa ni mawasiliano na mahusiano. Mbele ya Kamati tumethibitishiwa hilo, lakini namna ambavyo taarifa zimekuja pia imeonekana kuna namna fulani ama kuna hofu ndani ya Wizara au kuna hofu inatengenezwa kwenye Bodi, jambo ambalo linakwamisha utekelezaji wa majukumu katika maeneo hayo mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Ushauri Wangu; Mheshimiwa Kitila Mkumbo ameeleza vizuri, kwamba kama Waziri angetoa tamko hata kwenye vyombo vya habari, ingekuwa ni ngumu kutekelezwa na Bodi kama hapakwenda maandishi mahsusi kwa ajili ya tamko la Waziri. Na kwa kuwa machinery ya Waziri ipo; kuna Katibu Mkuu, kuna Katibu wa Waziri wao wangeweza kushusha yale maelekezo kwa maandishi kwa Bodi ingerahisha utekelezaji wa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri na hizi resistance ambazo zinazungumziwa leo zisingekuwepo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kikubwa ambacho naishauri Serikali ni kuimarisha mifumo ya mawasiliano. Kiongozi anapotoa maelekezo kwenye taasisi, wanaohusika kushusha hayo maelekezo kwa maandishi wafanye jambo hilo kwa wakati ili kuondoa hii mikanganyiko ambayo inaweza kutokea na kupoteza muda kama inavyotokea sasa.
Mheshimiwa Spika, utulivu ulio sasa kwenye Bodi ya Mikopo, mtakumbuka takribani miaka sita sasa inatengenezwa na namna ambavyo machinery ya Bodi inafanya kazi yake vizuri. Twende mbali zaidi, tusije tukahukumu mtu badala ya mfumo. Mfumo uliopo, Bodi ya Mikopo inatekeleza, inatoa mikopo kwa idadi ya wanafunzi kulingana na kiasi cha bajeti iliyopelekewa. Hapa tunaweza kuizungumzia Bodi kama wameshindwa kuwalipa hao watoto kwa wakati, lakini kama watoto wamelipwa kwa wakati hata kama wangelipwa watoto watatu kulingana na bajeti iliyopelekwa, hilo sio jambo la bodi ni jambo la Serikali kukaa chini, kuangalia namna nzuri ya kuongeza wanufaika wa Bodi kwa maana ya kupanua bajeti ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kuleta tija zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana naunga mkono hoja ya Kamati. (Makofi)