Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. George Mcheche Masaju

Sex

Male

Party

Ex-Officio

Constituent

None

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa hii. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri ambayo imejaa mipango na mikakati na hatua ambazo Serikali inachukua katika sekta hii ya afya na nichukue fursa hii pia kumshukuru Waziri Kivuli wa Afya kwa hotuba yake nzuri ambayo imeeleza ushauri mzuri kuhusiana na mikakati ambayo Serikali inachukua katika kutekeleza wajibu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kufafanua mambo machache ya Kisheria na Kikatiba. Nikianza na hili linalozungumzwa juu ya Ibara ya 46(1)(g) ya Katiba inayodaiwa kueleza kwamba, wanawake wana haki ya kupata huduma za afya (women with right to health).
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisme tu kwamba, Serikali inatambua kuwa, wanawake wanastahili na wana haki ya kupata huduma za afya na imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa huduma hii inapatikana kama ilivyoelezwa na Waziri katika hotuba yake. Hata hivyo, ni vizuri kuweka kumbukumbu sahihi kuwa Ibara ya 46(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haiweki masharti kuhusu haki ya wanawake kupata huduma za afya kama ilivyoelezwa na Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 46 ya Katiba inaweka masharti kuhusu kinga aliyonayo Rais dhidi ya mashtaka ya madai au jinai. Masharti kuhusu haki ya wanawake kupata huduma ya afya yalivyotajwa na Mheshimiwa Mbunge yako katika Ibara ya 57(1) ya rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na iliyokuwa Tume ya Marekebisho ya Katiba. Hata hivyo, haki hiyo iliboreshwa na Bunge Maalum la Katiba na kuwekwa katika Ibara ya 57(f) ya Katiba inayopendekezwa ambayo inaelezwa kwamba, kila mwanamke ana haki ya kupata huduma bora ya afya ikiwemo afya ya uzazi salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba hii inayopendekezwa inatoa haki mbalimbali ikiwemo haki ya kupata maji salama na safi. Hata hivyo, Katiba hii inayopendekezwa sasa haina nguvu za kisheria kwa sababu haijapigiwa kura na kuanza kutumika. Hilo niliona nilitoe kama ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ambayo naomba kuifafanua ni kwamba, imedaiwa kuwa, kuna manyanyaso, ukatili na hakuna haki ya watoto walioko magerezani au wenye kesi za kwamba, wananyimwa haki kuanzia kwenye usikilizwaji wa kesi mpaka kwenye mazingira wanayoishi ndani ya gereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kushauri kwamba pamoja na changamoto zilizoelezwa na Waheshimiwa Wabunge kuhusu usikilizwaji na uendeshwaji wa kesi za jinai dhidi ya mtoto. Napenda kulifahamisha Bunge hili kuwa Serikali imeweka mfumo wa kitaasisi na kisheria kuhusu namna ya kushughulikia masuala yanayohusu watoto ikiwemo kesi za jinai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali pamoja na kuridhia mikataba inayohusu haki za watoto (The United Nation Conventions for the Rights of the Child and African Charter on the Rights and Welfare of the Child), imetunga Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo imeweka masharti yaliyomo katika mikataba hiyo. Hii sheria inaweka masharti kuhusu haki ya mtoto ambayo anakabiliwa na kosa la jinai na kuweka masharti kuhusu kukamatwa kwake, kuwekwa mahabusu, uendeshaji wa kesi yake na adhabu na baadhi ya masharti hayo ni kama ifuatavyo:-
Moja, imeweka Mahakama ya Watoto, ambayo itafahamika kama Mahakama ya Watoto kwa madhumuni ya kusikiliza na kuamua masuala yanayohusiana na watoto.
Pia, Mahakama ya Watoto itakuwa na uwezo wa kusikiliza na kuamua mashauri yote ya jinai dhidi ya mtoto na kwenye Kifungu cha 99 inawekwa utaratibu wa kuendesha mashauri katika Mahakama ya Mtoto katika masuala yote kulingana na Kanuni zitakazokuwa zimetungwa na Jaji Mkuu, kwa namna yoyote zitakuwa ni kulingana na masharti yafutayo:-
(i) Kwanza, Mahakama ya Watoto itakaa mara nyingi kama itakavyolazimu;
(ii) Mashauri yataendeshwa kwa faragha;
(iii) Kadri inavyowezekana mashauri yataendeshwa kwa njia isiyo rasmi na yataendeshwa kwa kuulizwa maswali bila kuwekwa mtoto katika utaratibu wa advisory, atahudhuria pia Afisa wa Ustawi wa Jamii;
(iv) Mzazi, mlezi au mtu anayemwakilisha mtoto atakuwa na haki ya kuhudhuria;
(v) Mtoto atakuwa na haki ya kuwa na nguvu na kuwakilishwa na Wakili, kuwa na ndugu;
(vi) Haki ya kukata rufaa itawekwa bayana kwa mtoto; na
(vii) Mtoto atakuwa na haki ya kujieleza na kutoa maoni yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wakati wa…..
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa AG, ahsante.