Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami kuchangia ajenda ambayo Kamati imeleta. Kimsingi nami naiunga mkono.
Mheshimiwa Spika, kuna haja sasa baada ya haya kutokea, kuona umuhimu wa Mawaziri na Makatibu Wakuu kufanya wajibu wao kitaasisi. Nafikiri Mheshimiwa Waziri alipokwenda kuitambulisha ile timu aliyoichagua kwa bodi, kimsingi tu Katibu ilikuwa achukue jukumu la kuendelea kufanya shughuli za kiofisi na kuandika barua, ndivyo ninavyoona mimi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninalo swalli dogo tu kwamba, kwa nini hii bodi iliamua kuilipa fedha Kamati hiyo? Kwa sababu kama timu imechaguliwa kuja kukuchunguza, halafu unaenda kuilipa fedha, hakuna kitu ambacho kama unashawishi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najaribu tu kujiuliza kwa sauti labda kama sijaielewa Kamati. Kwa sababu wewe unaenda kuchunguzwa, halafu wewe bodi unatoa fedha kwenye hiyo timu; huoni kama kuna tatizo hapo? Kwa hiyo, hilo tu peke yake nilikuwa nalifikiria...(Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Sophia Mwakagenda kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Neema Mwandabila.
T A A R I F A
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nilitaka nimpe taarifa dada yangu Mheshimiwa Sophia kwamba, nia ya Waziri ilikuwa ni kuboresha mfumo wa utoaji mikopo na siyo kufanya uchunguzi kwa bodi na ndiyo maana unakuta hata hadidu za rejea hizo mbili walizokuwa wamezitanguliza, wakajadiliana, na bodi ikashauri kwamba ziongezwe hadidu za rejea nyingine. Ingekuwa ni uchunguzi, nadhani bodi isingepata nafasi ya kuongeza hadidu za rejea kwa ajili ya hiyo kazi ya maboresho ya mfumo wa utoaji mikopo. Ahsante.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kimsingi najua Waziri amefanya kazi yake kama Waziri, na hapo mwanzo nimesema Makatibu na Wasaidizi wa Mawaziri kazi yao kubwa ni kuwasaidia Mawaziri kutimiza makusudi na kazi zao wanazozifanya. Nimesema bodi yenyewe ambayo inafanya kazi na Waziri, hatujasema imegombana na Waziri, lakini kama umepewa jukumu la kufanya kazi hiyo ya kuisaidia bodi kwa Watanzania na hasa wanafunzi wetu, kwa nini utoe fedha? Basi kama ni hivyo, basi kanuni zibadilishwe kama inawezekana. Mimi nafikiri hivyo, unless kama sijaielewa Kamati.
Mheshimiwa Spika, naomba, kukosea kupo, lakini hata kama wanasema amelidanganya Bunge, mimi sijaona kama amelidanganya Bunge, vinginevyo wewe usingetoa nafasi ya kufanya. Aliomba msaada wa kusaidiwa kuweza kuhakikisha Taifa letu linafanya kazi vizuri. Mimi sijaona kama ameshitaki, alifanya wajibu wake kama Waziri. Sijaona kama ni kitu kibaya, wala tusikichukulie hivyo, ndiyo maana wewe ukaona usimame kama mhimili kuhakikisha kazi hii inatendeka vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tupo hapa kwa ajili ya kujenga, kutengeneza na ndiyo maana sisi hapa tunaitwa Wapinzani, tunaotoa mawazo mbadala pale ambapo Serikali imekosea. (Makofi)
Kwa hiyo, ninaamini Mheshimiwa Waziri alikuwa sahihi, bodi iko sahihi na kuanzia sasa bodi itakuwa very sensitive, kwa sababu tayari imeshaona kumbe ukikosea kidogo unaweza ukaitwa, unaweza ukaenda kufanywa kitu fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja ya Kamati, naipongeza na maoni yao yazingatiwe, na Wabunge wenzangu tuyawekee mfumo mzuri na tuyakubali maoni yao. Ninampongeza Waziri na ninaipogeza bodi vile vile maana tunataka kusonga mbele, hatutaki kurudi nyuma. Ahsante. (Makofi)