Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUSSA R. SIMA K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kukushukuru sana kwa kuendelea kuruhusu mjadala huu ambao una tija kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge sita pamoja na Mheshimiwa Waziri kwanza wamekubaliana na kazi ya Kamati, tunawashukuru sana kwa niaba ya Mwenyekiti na Wanakamati wote, kwa kukubali kazi ambayo tumeifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, umekuwa ukielekeza mara kwa mara na hoja ya msingi hapa ni kwamba Bodi inamkwamisha Waziri kufanya kazi yake na Waziri amesema na Hansard zipo. Sasa ame-declare ina maana hili alilolisema sasa angelisema awali usingeitisha Kamati kufanya kazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sitaki kurejea sana ndani, kwa kuwa Waziri amesema kwamba hakusema, hakuwa anamaanisha resistance ya Bodi kwenye kufanya kazi yake na ameomba Hansard, nataka hii niiachie meza yako au kiti chako kifanyie kazi hilo, lakini sisi tumetekeleza wajibu wa maelekezo uliotupatia na hayo ndio yalikuwa majibu yetu.
Mheshimiwa Spika, jambo ambalo naweza kulitolea maelezo la Mheshimiwa Mwakagenda alizungumza kuhusiana na Bodi kulipa fedha. Bodi fedha zote zile ni za Wizara ya Elimu isipokuwa kulikuwa na Mradi wa HEET. HEET maana yake ni Higher Education Economic Transformation ambayo ina mchanganyiko wa miradi mingi ndani.
Mheshimiwa Spika, moja ya fedha iliyoko pale ni ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Sasa ile Bodi zaidi ya nadhani shilingi milioni 79 ilikuwa imetengwa kwa ajili ya kulipa hiyo Kamati ambayo Mheshimiwa Waziri aliiunda na hizo fedha hawezi kuidhinisha Mkurugenzi wa Bodi au Mwenyekiti, ni lazima uandike barua kwa Katibu Mkuu wa Wizara, Katibu Mkuu ndio awape ruhusa ya kulipa hizo fedha. Kwa hiyo kwa ujumla ni fedha za Wizara.
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine nikushukuru sana na nishukuru Bunge lako tukufu kwa hatua hii ambayo tumefikia. Ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla hujatoka hapo mbele, tusaidie kwa sababu hujaja na ile taarifa yako, lakini katika yale maoni na mapendekezo kulikuwa na mapendekezo matatu; (a); (b) na (c). Lile la tatu linasema msingi wa malalamiko ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu yaliyosababisha hoja ya...; mimi naona hili kwa sababu halikuwa sehemu ya ile hadidu ya rejea, sijui kama hii huwa ina umoja na wingi, lakini kwenye hadidu za rejea hili halikuwepo, kwa hivyo wakati nawahoji Wabunge ili tuwe tumeongozana vizuri, tusaidie aidha, uliondoe hili lisiwepo ili wanapohojiwa wahojiwe kwenye haya mawili ambayo Kamati mmependekeza au kuna namna yoyote ambayo ungetamani hili liwepo, lakini sasa liendane na ile hoja ambayo ililetwa mbele ya Kamati.
MHE. MUSSA R. SIMA K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII: Mheshimiwa Spika, kwa ujumla nikushukuru, tutaondoa neno msingi wa hoja hiyo, lakini hiyo ni miongoni mwa mambo ambayo yamepelekea mjadala uliopelekea hoja hiyo kutuagiza Kamati kuifanyia kazi. Tutaondoa hilo neno kwamba sio msingi wa hiyo hoja.
SPIKA: Sawa. Sasa hapa mwisho inasema; Kamati inasisitiza Serikali itekeleze maagizo ya Bunge ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaostahili mikopo wanapata mikopo yao, yaani ndio mwendelezo wa hii hadidu ya rejea na hiyo siku tulishapitisha sisi azimio, yaani Bunge lilishapitisha azimio kuhusu jambo hili.
MHE. MUSSA R. SIMA K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII: Mheshimiwa Spika, nakubaliana na wewe sasa tunaweza kuondoa hicho kipengele (c) kwa sababu tulishapitisha azimio hapa. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana.
Waheshimiwa Wabunge, sasa nitawahoji kwa hoja hii ikiwa na hayo mapendekezo mawili ambayo ili sote tuwe kwenye picha moja nitayasoma. Kamati inapendekeza kama ifuatavyo: -
Mosi; mawasiliano ndani ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yaboreshwe ili maelekezo ya viongozi wa sera na wasimamizi wa utekelezaji wa maelekezo ya kisera yaratibiwe kwa ufanisi na tija.
La pili, ni Kamati iliyoundwa na Waziri iendelee kufanya kazi yake ambayo imeonekana kuwa na tija. Ufanisi wake utategemea ushirikiano itakayopata kutoka Bodi na Wizara pamoja na miongozo na mawasiliano bora baina na Bodi na Wizara kwa upande mmoja na Kamati hiyo kwa upande mwingine. Kwa hiyo mmesikia haya ambayo Bunge linaazimia.
Waheshimiwa Wabunge, baada ya kusema hayo, Mheshimiwa Sima uko sehemu gani? Ilibidi utoe hoja tena, eeh kwa hiyo rudi utoe hoja, halafu tuone inaungwa mkono ama haiungwi mkono. Kama haiungwi mkono hatutalihoji Bunge, ikiungwa mkono ndio tunalihoji Bunge.
MHE. MUSSA R. SIMA K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII: Mheshimiwa Spika, nashukuru naomba sasa kutoa hoja juu ya wasilisho la Kamati ambalo nimelisoma hivi karibuni. (Makofi)
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, naafiki.