Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami niungane na Wabunge wenzangu kuchangia Wizara hii ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu na wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika kwa kuchaguliwa kuwa Spika wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kitila Mkumbo na Mheshimiwa Gambo wamejaribu kuliongea vizuri suala hili la kupanda vitu, lakini mimi bado nina wazo. Sisi Waislamu tumeambiwa tukatafute elimu mpaka China ila tusije tukachukua dini ya Wachina. Pia Biblia imesema, “watu wangu wataangamia kwa kukosa maarifa.” Mwenyezi Mungu hakusema wataangamia kwa kutojua kusoma na kuandika, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakisema ukachukue elimu mpaka China, walichomaanisha ni kwamba tukachukue mawazo ya Wachina na siyo maandishi ya Wachina; ila kama una wasiwasi utasahau, unaweza ukajifunza Kichina kidogo ukaandika ili uje ukumbuke huku. Wataalam wetu, wasomi wetu wa Tanzania asilimia 90 wanajua kusoma na kuandika siyo maarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi niko kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara. Hapa tunapolia mabati, Serikali inakataa mabati kuanzia gauge 33 mpaka gauge 40, kwa nini? Je, imepiga marufuku nyumba za nyasi? Imepiga marufuku nyumba za tembe? Sasa wewe una shida nyumbani kwako, huna hela ya kuweza kula ugali mweupe, si unasaga dona? Si ndiyo maana yake? Sasa wakati huu wa shida, wewe unakataa watu wasiezekee mabati ya gauge 40 wakati hujatukataza sisi kutumia nyasi. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Spika, hii elimu ya kwenu ndiyo iliyotutoa sisi kwenye nyasi ikatupeleka kwenye bati. Ninyi mlikuja mkatuambia kwamba nyumba za nyasi ni mbaya, anzeni kutumia mabati. Leo mabati yamepanda, mnatuwekea sheria tena tusitumie ya gauge 40, kwa sababu gani? Tunamwomba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara atoe hiyo dharura maana bati la gauge 40 ni shilingi 8,000/=, unamkatazaje mwananchi? Leo nyasi hazipo na hawa new generation hawawezi kuezeka nyumba ya nyasi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia viwanda vya cement kwenye Kamati vime-confirm vinayo cement ya shingili 5,000. Mheshimiwa Waziri anakataa, anasema wataalam wamemwambia kwamba maghorofa yataanguka. Wananchi wanajenga maghorofa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nimesema kwamba wataalam wetu asilimia 90 wanajua kusoma na kuandika, hawana maarifa. Wananchi kule vijijini wanatulalamikia mno kwamba hivi nyie kweli, ndiyo mmesoma, unanikataza mimi, lakini juu nimeweka turubai navujiwa; umenikatalia bati la gauge 40, inakuja kweli kwenye akili? Haiwezekani! Hata kama mnasema tukaiambie Serikari ipunguze, itapunguzaje sasa? Itafanyaje kupunguza? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo tulipewa hela hapa za Mheshimiwa Mama Samia shilingi trilioni moja na kitu, zote tumempa Dangote, mmekataa matofali ya kuchoma. Hela si wangebakiza kwa wananchi? Shule za matofali ya kuchoma leo zina miaka 150 na Makanisa yapo. Sasa Dangote kachukua hela, ALAF wamechukua hela ambao ni Wachina, sisi ndiyo tutalipa deni. Kwanini hela nyingine isingeenda kwenye matofali ya kuchoma, wananchi wetu wakapata hela na ndiyo walipaji wa lile deni? kwa hiyo, najaribu kuleta hili wazo ambalo wenzetu wataalam lazima tukubaliane kwamba tuna watu wa hali ya chini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, juzi hapa kama sikosei, ni miezi miwili au mitatu kuna gazeti la Busara lilitoa mwelekeo kwamba taasisi inayoongoza kwa kufanya vizuri sasa hivi, ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania ikifuatiwa na wananchi wale wenye mila za kienyeji. Sisi Bunge ni taasisi ya saba kwa kuwa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa ombi langu, sisi kule Kanda ya Ziwa asilimia 75 ya watu wetu wana dini za mila. Kwa nini Serikali isiruhusu wafundishe na wao dini yao mle kwenye shule? Serikari ipitie vile vitabu vyao, linapokuja somo la dini wanapofundishwa Wakristo na Waislamu, na wao wafundishe. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu, hawa watu wako asilimia 75, lakini dini yao ni nzuri mno. Wao wanachofundisha ni kusalimia umepiga magoti kwa mtu mzima, siku ya harusi wanafanyia harusi kwenye mti, wala hamna kadi wala hamna nini; kwenye mazishi mnaleta chakula toka kwa jirani. Je, ni kosa utaratibu huo ukifundishwa; ili siku wakija kufika sasa wenye dini, wakute watu hao ni wastaarabu. Ila sasa hivi, mnachofanya nyie, mnawapelekea kamari na disco. Sasa ipi bora? Wafundishwe utaratibu wao waishi vizuri kwa utaratibu ili siku nyie mkifika na dini zenu, basi wanaweza wakaungana, kuliko sasa hivi tukiwaacha hivyo hivyo na kila mtu anawasakama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Utamaduni alifikirie, maana yake Mheshimiwa Rais sasa hivi mnafahamu ndiyo Kiongozi wa Machifu, sasa Machifu gani kama hawatakuwa na kitabu cha kufundishia wale watu wao?(Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia tu, ni suala hili la mtihani. Siku ya mtihani wanakuja polisi, kuna kuwa na vurugu pale shuleni, najaribu kujiuliza hivi kweli mtu toka darasa la kwanza huwa anakuwa wa kwanza mpaka darasa la saba mpaka form one, wewe hofu yako nini mpaka unaleta polisi siku hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini kama matokeo yatakuja tofauti wewe unayemtilia shaka ni yule ambaye huwa wa mwisho, kama wa mwisho amefaulu si uangalie kwenye notice zake tu za kila siku toka darasa la kwanza, kwa nini we leo umefaulu. Kwani akili ya binadamu ni bando kwamba wewe uliweka bando leo siku ya mtihani.(Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, sioni sababu maana wale watoto wanakuwa na hofu, wanaona polisi, kunakuwa na hekaheka, ni ya nini, toka darasa la kwanza rekodi zote zipo, kama atafaulu ambaye hafaulu basi, ni kwa nini unafuta mtihani wa shule nzima. Kwa nini usichukue tu wale ambao unaona huwa hawana akili leo wamefaulu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo najaribu tu kuona kwamba wataalam wetu wajaribu kufikiria maisha ya wananchi, wasiwe rigid, kuna mabati ya asbestos, yalipigwa marufuku hapa miaka 40 iliyopita, sababu ilisemwa ni kansa, tunamuuliza Mheshimiwa Waziri miaka 40 iliyopita sababu hizo zipo, wataalam tunao kwa nini wasifanye research tena, maana yake bati la asbestos linatengenezwa kwa mkono, leo nani angelia mabati na unatumia katani na cement linakuwa bati mbona sie tunaezekea matope na nyasi? Ndio tunataka elimu iwe hivyo hatutaki elimu ya kiingereza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunataka elimu ikawasaidie wananchi hasa wakati huu wa matatizo, hata wakisema tumbane Mheshimiwa Rais, wataweza kupunguza bei ya vitu duniani, kwa nini wanakataa tusirudi huko ambako kuna solution ya dakika moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaomba Waziri atangaze kwamba kuanzia kesho kwa dharura hii tumeruhusu sasa hivi unaweza kutumia mabati ya gauge 40.
Mheshimiwa Spika, baada ya mchango huo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)