Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buchosa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhana Wataallah kunipa nafasi ya kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu, nimshukuru sana Jehova kwa upendeleo alionipa kuwa mmoja wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana wewe kunipa nafasi ya kusimama lakini niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Buchosa kwa kunituma hapa Bungeni kuwawakilisha, nataka niendelee kuwaahidi ya kwamba nitakuwa mwakilishi bora nitakaye wawakilisha wao hapa Bungeni na sitajiwakilisha mwenyewe hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda mbele sana naomba kwanza niunge mkono hoja, lakini niongee mambo matatu au manne hivi kabla sijazungumza hasa jambo nataka kuchangia.
Mheshimiwa Spika, kwanza; nataka nizungumze suala la uwezeshaji wa wazawa kiuchumi, nimezungumza hili suala mara kadhaa nataka nilizungumze tena leo. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 8 (1)(b) jukumu kubwa la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa ni kusimamia ustawi wa watu wake. Mwaka 2004 tukatunga sheria katika Bunge hili ya kuwawezesha wazawa wa nchi hii kushikilia uchumi wa nchi yao baada ya kuona kwamba uchumi ulikuwa mikononi mwa wageni, sheria hiyo ilisainiwa na Rais Mkapa Marehemu mwaka 2005 na ikaunda Baraza la Uwezeshaji wa Wazawa Kiuchumi ambalo lipo mpaka leo.
Mheshimiwa Spika, naomba sana bajeti tunayopitisha mwaka huu ya zaidi ya shilingi trilioni 40 hivi naomba iweze ku-consider sana wazawa wa nchi hii. Wazawa wa nchi hii wamechoka kuona sehemu ya bajeti kubwa kama hiyo inaishia kwenda nje na wao wanabaki na umaskini. Kwa hiyo, naomba hilo lizingatiwe kabla sijaenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la pili; nchi hii ina vijana wengi sana wabunifu. Nchi hii ina watu wengi sana wenye uwezo mkubwa wa kubuni solutions mbalimbali, lakini wengi wanaenda nazo kaburini kwa sababu ya ukosefu wa uwezo wa kuzalisha bidhaa au kuendelea mbele na ubunifu wao. Naiomba sana bajeti hii izingatie suala zima la kuanzisha National Innovation Fund, Mfuko wa kuwawezesha vijana wabunifu wa nchi hii waweze kwenda mbele na ubunifu wao na kutengeneza bidhaa. Hii ninaongea ni kama mara ya tatu ya nne hapa Bungeni kwa sababu wapo watu wengi sana wana ubunifu upo ndani ya kabati lakini hawana mtaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huko duniani kuna kitu kinaitwa Global Innovation Fund ambayo huwa inatoa fedha nyingi sana kwa mataifa mbalimbali kusaidia wabunifu wao. Ethiopia mwaka jana wamepewa Euro Milioni Sita na hizi zinakuja siyo mkopo zinatolewa kama grant kwa wabunifu wetu wanaotoka vyuo vikuu ambao hawana mtaji na hawakopesheki na benki zetu.
Mheshimiwa Spika, ninawaomba watalaam wetu, PhD ambazo tunazo katika nchi hii ziandike maandiko ili tuweze kupata sehemu ya fedha hizo ziwasaidie watu wetu.
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu; nataka kukumbusha kabla sijaenda mbele ni suala zima la kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mkataba au makubaliano ambayo iliingia na nchi za Uarabuni kuhusu mafuta. Waliingia makubaliano ya kwamba nchi za Uarabuni zitakuja hapa zitawekeza kwenye mafuta zitaweka matenki makubwa ili mafuta yawe yanawekwa hapa Tanzania igeuke kama Dubai au Gulf ya Afrika Mashariki na Kati. Naomba Serikali yangu itekeleza jambo hili mapema hizi deal na urasimu huu uondolewe ili jambo hili lingekuwa limeshafanyika mapema hakika tusingekuwa pengine tunapata changamoto tunayoipata leo. Kwa hiyo, naomba hilo lifanyike mapema sana.
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho na ninaomba niungane na Profesa Kitila Mkumbo ya kwamba ex-ordinary times require ex-ordinary decisions. Nchi yetu inapita kwenye wakati mgumu sana hivi sasa na siyo Tanzania peke yake ni dunia nzima inapita kwenye wakati usiokuwa wa kawaida, ninaiomba Serikali yangu Tukufu ifanye maamuzi magumu kwenye kipindi hiki.
Mheshimiwa Spika, mwaka 1979 baada ya vita ya Uganda nakumbuka Rais wetu Hayati Baba wa Taifa alisema tufunge mkanda kwa miezi 18, watanzania tunatakiwa kufunga mkanda kipindi hiki kwa sababu ni wakati mgumu kabisa na yafanyike maamuzi ambayo yatasaidia wananchi wawe na unafuu wa maisha. Huko vijijini kwa watu wa chini kabisa achana na sisi huku juu, ukienda watu wana malalamiko makubwa sana. Kila kitu kimepanda bei, mafuta ya kupikia, mafuta ya petrol, kila kitu kipo juu na wananchi wanashindwa hata ku-afford Maisha. Kwa hiyo, tufanye maamuzi ambayo yatakuwa na maslahi kwa Taifa.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nizungumzie suala la umaskini wa Taifa hili. Mwaka jana tumesherehekea uhuru wa nchi yetu mwezi wa 12, ni kweli Taifa hili limepiga hatua kubwa sana na mimi nakubali, lakini umaskini bado upo na umaskini unawasumbua sana watu wa nchi hii. Sisi wote hapa tunatoka vijijini na wengi wetu hapa tunatoka katika familia maskini tunaelewa madhara ya umaskini.
Mheshimiwa Spika, Taifa hili umaskini mkubwa unawakabili wakulima wa nchi yetu. Nchi hii wakulima wanapata shida na ndiyo mafukara namba moja, kilimo kimeajiri asilimia 65 ya watu. Naomba nizungumzie suala la kilimo kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, ili nchi hii iondoke kwenye umaskini unaotukabili ni lazima tuwekeze sana kwenye kilimo chetu, hatuwekezi vya kutosha kwenye kilimo. Nchi hii wakulima wanazidi kuwa maskini kila siku, tumeshakuja na mipango mingi sana, siasa ni kilimo, kilimo cha kufa na kupona, kilimo kwanza, mambo mengi tuna-fail wakati umefika tujiulize ni kwa nini tuna-fail. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Taifa hili lina ardhi kubwa sana square kilometer Laki Tisa hivi, na ardhi ambayo inaweza kulimwa ni kama square kilometer za miraba Laki Nne hivi. Lakini nchi ya Malawi ni ndogo, ardhi yao ambayo inaweza ikalimwa ni square kilometer kama 50,000 hivi, lakini wanazalisha soya bean tani 230 kwa mwaka sisi tunazalisha tani 6,000 mpaka 20,000 kwa mwaka na ukubwa wa hekta tunao na mchango wa kilimo kwenye pato la Taifa ni asilimia 26% lakini Malawi ina 42 % what is wrong with us. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka tujiulize kama Taifa nini shida yetu katika kilimo? Naomba uwekezaji kwenye kilimo ufanyike kwa nguvu kubwa sana kuwasaidia wakulima wanchi hii. Mazao ya nchi hii wakulima wetu wanalima lakini mwisho wa siku mazao yanaishia kuharibika, post-harvest loss kwenye Taifa hili ni asilimia 40, tafsiri yake ni kwamba unalima mazao lakini asilimia 40 yanaharibika.
Mheshimiwa Spika, miwa katika Taifa hili tunavuna tani Milioni Nane kwa mwaka, lakini tunatumia tani Milioni Nne peke yake na tani Milioni Nne zinaharibika. Naambiwa na wataalam wa kilimo kwamba tani Milioni Nne zinazoharibika zingeweza kuchakatwa kuwa sukari tusingeagiza sukari, hivyo, forex yetu tungeweza kuiokoa! Kwa nini hatuwekezi kwenye utengenezaji wa mitambo ya kuchakata sukari? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, TEMDO taasisi yetu ya Tanzania Engineering Manufacturing Development Organization wanatengeneza mitambo, wametengeneza mitambo, mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara wametengeneza mtambo wa kuchakata sukari ambao unaweza kusaidia wakulima wadogo wadogo wakikopeshwa na SIDO, SIDO kuna kitu wanaita NEDF wanakopeshwa wakawa wanatengeneza sukari hii miwa tutaiokoa. Kwa nini hatuwekezi sasa kwenye TEMDO?
Mheshimiwa Spika, kazi ya Mheshimiwa Bashe ni kulima, kazi ya Mheshimiwa Bashe siyo kuuza, kazi ya kuuza ni ya Mheshimiwa Dada yangu Dkt. Ashatu Kijaji, Wizara ya Viwanda na Biashara. Sasa najiuliza tunaweka bajeti kubwa kwenye kilimo lakini kwa nini hatuweki bajeti humu ya kutafuta masoko?
Mheshimiwa Spika, mimi ni Mwenyekiti ninakuambia TANTRADE hawana pesa watatafutaje masoko? Mheshimiwa Bashe atalima atauza wapi? Matokeo yake tutalima lakini mazao yataoza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sana tubadilishe mtazamo wetu kwenye kilimo, ni kilimo peke yake kitaitoa nchi hii hapa ilipo kwenda mbele.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja tena. Ahsante. (Makofi)