Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kumpongeza Rais wangu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuiongoza nchi kwa weledi mkubwa, na pia kuijaza jimbo langu fedha nyingi katika sekta zote. Leo hii tunajenga Vituo vya Afya, Gumanga pamoja na tunajenga Ilunda. vilevile leo hii tunajenga shule ya thamani ya milioni mia nne sabini katika Kata ya Ilunda, tumepata fedha za barabara na tunaunganisha kata zetu; yote haya yanatokana na Uongozi wake mzuri, nampongeza sana kwa hili.
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, niiombe Serikali iunganishe haya mazuri kwa kutupatia kilomita arobaini na mbili za lami kutoka makao makuu ya wilaya kwenda makao makuu ya mkoa, ili wananchi wafaidi matunda hayo kwa kwenda vizuri katika mkoa wao na makao makuu ya wilaya yao.
Mheshimiwa Spika, niende sasa kwenye mchango wangu. Mimi ningependa kuongelea nia njema ya Serikali katika kulitizama upya suala la kilimo katika nchi hii. Nimeona nia njema ya Serikali sasa ya kupeleka fedha nyingi, na ushahidi tu ni juzi, Rais wetu amekabidhi takribani pikipiki 9,000 na vifaa vya kupima udongo kwa lengo la kuinua kilimo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo ninapata hofu kama nia hii njema itafanikiwa vizuri kutokana na kitendo cha kuzingunisha Idara zetu mbili katika Halmashauri, Idara ya Kilimo na Idara ya Mifugo kuwa Idara moja. Hizi Idara ni kubwa sana. Sote tunatambua umuhimu na ukubwa wa Idara ya Mifugo katika kuchangia pato la nchi hii na pia tunafahamu Idara ya Kilimo ilivyo muhimu. Kama ambavyo zipo Wizara mbili tofauti, Wizara ya Mifugo na Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Spika, sijui ni busara gani imetumika katika kuunganisaha Idara hizi katika ngazi ya Halmashauri kuwa Idara moja. Tunafahamu Mkuu wa Idara atakuwa mmoja na kwa vyovyote lazima atabobea aidha, kwenye kilimo au kwenye mifugo; na kwa vyovyote utendaji wake utaendana zaidi na ubobezi wake. Sasa jambo hili la kuunganisha Idara hii kuwa moja wakati Mawaziri ni wawili na Idara zenyewe ni kubwa na zinapelekewa fedha sasa kwenda kuinua uchumi wa nchi, naona kama ni jambo ambalo tume-overlook kama Serikali.
Mheshimiwa Spika, mimi ningependa kuishauri Serikali, kwamba idara hizi zibaki kuwa idara mbili tofuati ili fedha nyingi hizi zinazopelekwa kwenye kilimo na kwenye mifugo ziweze kusimamiwa vizuri na wataalam katika kuleta tija katika nchi yetu. Kama kweli lengo ilikuwa ni kubana matumizi, sidhani, kwa sababu kwa kuunganisha idara hizi bado tumeongeza idara nyingine. Zilikuwa kama 19, sasa hivi ukiangalia idara na vitengo zinakaribia 23. Kwa hiyo mimi ningeomba niishauri Serikali yangu iliangalie upya suala hili la kufanya Idara hizi zisiwe moja ziwe Idara mbili tofauti kama ambavyo Wizara zipo tofauti, ili lengo jema hili hili la kuinua kilimo na mifugo iweze kufanikiwa vizuri katika Idara zetu.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, ningependa kuishauri Serikali yangu kuhusiana na suala la mipaka ya kiutawala katika nchi yetu. Mipaka ya mikoa, wilaya, kata, vijiji mpaka vitogoji ina migogoro mikubwa sana katika nchi yetu. Jambo hili linasababisha wananchi wetu wanagombana mpaka sehemu nyingine wanapoteza maisha; lakini vilevile maendeleo ya nchi yanarudi nyuma kwa sababu ya suala hili. Ipo mikoa imeanza hivi karibu kwa mfano, Mkoa wangu wa Singida ulikuwepo kabla ya Manyara. Manyara ilipoanzishwa, leo hii ukichukua GN ya Singida, ukichukua GN ya Manyara katika maeneo yanayopakana kila Mkoa unatambua eneo tofauti. Hivyo hivyo ukienda kwenye wilaya n ahata kwenye kata zetu.
Mheshimiwa Spika, sasa mimi ningeshauri Serikali ifanye program maalum ya kuhuisha na kuangalia mipaka yote ya kiutawala katika nchi hii, ili kuleta utulivu wa nchi, kuleta maendeleo ya nchi na wananchi wetu wafanye kazi zao wakiwa katika hali yenye utulivu. Kwa hiyo ningependa kuishauri Serikali yangu…
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Mtinga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Festo Sanga.
T A A R I F A
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, alolizungumza Mheshimiwa Mbunge ni sahihi kabisa. Hata kule Njombe na Mkoa wa Mbeya kuna changamoto kubwa ya mipaka ambayo imesababisha hata hili zoezi la uwekaji wa anuani za makazi kwenye nchi hii imekuwa changamoto sana maeneo ya mipakani. Kwa hiyo ni kweli anachokizungumza Mheshimiwa Mbunge, nilikuwa nataka kumpa taarifa kuhusu hilo.
SPIKA: Mheshimiwa Mtinga unaipokea taarifa hiyo.
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa hii kwa mikono miwili, na ninaamini hapa hata Wabunge wote wangepata nafasi wangekubaliana na jambo hili, ni tatizo kubwa, kwa hivyo niiombe Serikali ichukulie jambo hili kwa muhimu sana kwa sababu wananchi wetu wanapata tabu sana kwa kugombania mipaka. Tunashindwa kufanya nyingi kwa kusuluhisha migogoro hii. Kwa hivyo Serikali ilichukulie jambo hili ihuishe tu mipaka wananchi waelezwe, sisi Viongozi tuelezwe, mpaka unapita hapa, unapita pale ili kazi za nchi hii ziweze kuendelea vizuri.
Mheshimiwa Spika, mimi leo nilipenda nijikite katika maeneo hayo kwa sababu sipendi sana kupigiwa kengele. Lakini nikupongeze sana kwa jinsi ambavyo unaliongoza Bunge letu vizuri. Nilikuwa Mkoa wa Mbeya katika Halmashauri yako pale ya Manispaa hauna double road hata moja. Niombe Wizara ya Ujenzi pale panatia aibu, mji umebanana sana ule angalau iwepo double road pale katikati ili Mji wa Spika wetu ufanane na Jiji la Mbeya, ahsante sana. (Makofi)