Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kuweza kunipa nafasi ili na mimi nichangie katika bajeti iliyopo mbele yetu. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa wasilisho lake la jana kwa bajeti ambayo kwa kweli inatupeleka tunapotaka.
Mheshimiwa Spika, ninaishukuru sana Serikali kwa kuongeza kiwango cha bajeti, na kwa hivyo nitazungumzia katika masuala mazima ya kuzuia maambukizi ya UKIMWI. Kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 Serikali imetenga zaidi ya bilioni 1.8 kwa ajili ya kutekeleza afua za kupambana na maambukizi ya UKIMWI. Hata hivyo nitoe masikitiko yangu kwa bajeti hii ambayo inakwenda kumalizika mwezi wa sita, Serikali ilitenga kutoa Shilingi bilioni moja kwa afua za kupambana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa fedha za maendeleo zinazotokana na mfuko wa ndani.
Mheshimiwa Spika, wafadhili au fedha za nje zilikuwa jumla ya milioni mia tatu themanini na kitu, na wafadhili wametoa fedha kwa asilimia mia moja. Hata hivyo, lakini kwa masikitiko makubwa fedha za ndani ambayo ni milioni moja ilitengwa mpaka Machi haikutoka hata Shilingi moja. Sasa nikifikiria juhudi ambazo tunazo kama nchi na malengo ya Dunia ya kudhibiti maambukizi mapya virusi vya UKIMWI; na Tanzania tukiwa katika mstari wa mbele kuhakikisha kwamba maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI, yanapungua. Sasa kama bajeti ya Serikali, vyanzo vya ndani fedha hazitoki, ikitokea wafadhili wameacha kutoa fedha itakuwaje? Napata mashaka sana napata uchungu sana.
Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba kuna mkakati wa kufikisha asilimia 95 ya watu wote ambao wanapimwa virusi vya UKIMWI kujua afya zao, asilimia 95 kwa wale ambao wamegundulika na virusi vya UKIMWI kuhakikisha kwamba wanakuwa katika matibabu; na asilimia 95 ya wale ambao wapo kwenye matibabu kuhakikisha kwamba wanapima kujua wingi wa virusi. Sasa kwa trend hii ya utoaji fedha, napata mashaka.
Mheshimiwa Spika, suala la maambukizi ya UKIMWI naona bado ni tatizo kubwa, hasa kwa vijana wenye umri kati ya miaka 15 mpaka 24. Vile vile kwa wananchi ambao wapo pembezoni; wako kwenye mialo, maeneo ya migodi, hasa sasa hivi kumekuwa kukizuka migodi mingi. Mfano Mkoa wa Shinyanga, maeneo ya Kahama, Mwakitolio kuna migodi mingi ambayo inaibuka. Sasa hali ya kiafya, hali ya kuzuia maambukizi ya virusi vya UKIMWI imekaaje.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Takwimu ya Tanzania HIV Impact Survey iliyofanyika mwaka 2016/2017 inaonesha kwamba idadi ya vijana wengi wenye umri wa miaka 15 mpaka 24 wameshajiingiza katika vitendo vya kujamiiana. Katika idadi hiyo ya kundi hilo hilo la hao vijana wa miaka 20 hadi 24, kati yao wasichana wameambukizwa zaidi kwa asilimia 3.4 ukilinganisha na wavulana ambao wameathirika, wameambukizwa kwa asilimia 1.9. Hii inaashirika nini? Ni kwamba vijana wetu wengi wameshaingia katika hili janga la maambuziki ya virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Spika, fedha ambazo zinatolewa na Serikali, fedha za ndani hazitolewi kwa wakati. Tunategemea kwa asilimia kubwa wafadhili. Je, tutawalinda hawa vijana ambao kwa kweli wapo kwenye risk kubwa? Je, tutawafikia wale watu ambao wapo kwenye mialo? Kwa tabia za wavuvi, wanaondoka majumbani kwao usiku kwenda kutega, wanarudi alfajiri wamechoka. Inabidi sisi watoa huduma za afya ndio tufanye juhudi binafsi kuwafuata kuwafikia.
Mheshimiwa Spika, kwa trend ya fedha ambazo zinatengwa na Serikali tunapitisha hapa Bungeni, lakini hazitoki kwenda kuwahudumia au kuwafikia kule. Kwa kweli bado ninaona suala zima la vita dhidi ya maambukizi mapya ya UKIMWI itakuwa ni changamoto kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, ukiangalia hata katika hii tafiti ya vijana iliyofanyika, wanaopima wengi ni wasichana; wavulana hawapimi. Kwa nini? Kwa sababu baba zao wenyewe hawapimi; na ukizingatia kwamba malezi yanaanzia nyumbani. Baba hana interest ya kupima, anasubiria mke wake awe mjamzito, aende akapime kliniki, akishagundulika kwamba yupo salama, basi naye anajiaminisha kwamba yupo salama. Hakumbuki kwamba kuna maambukizi ambayo mwenza mmoja anaweza akawa na maambukizi na mwingine asiwe na maambukizi, unaona.
Mheshimiwa Spika, kama baba hana utamaduni wa kwenda kupima, huyu kijana wa kiume atakuwa na courage ya kwenda kupima? Jibu ni hapana. Niwasihi sana wanaume, mjitokeze kwenda kupima, kwa sababu ninyi ndio mnaowafuata hata hao wasichana wadogo wenye miaka 20 mpaka 24, ambao wako Vyuo Vikuu, kwenda kuwarubuni, kuwapa vichipsi mayai, kuwanunulia vi-IST, ili mwarubuni wapate UKIMWI ambao tayari wanao. (Makofi)
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
T A A R I F A
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba anachokizungumza kwamba wanaume hatuna tabia za kupima, siyo kweli. Wanaume tuna tabia za kupima; na hata Wabunge wanaume hapa ndani tupo tayari kwenda kupima afya zetu hapo nje. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Spika, siIkubali hiyo taarifa kwa sababu utafiti ndivyo unavyoonesha. Ameshasema kabisa kwamba leo nje pale atakwenda kupima, kwa maana hiyo, hajapima mpaka sasa hivi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba wanaume wengi hawapimi na wana tabia ya kufuata watoto wa shule ambao wana miaka 20 mpaka 24, lakini hata sasa hivi na sisi wanawake kuna wimbi ambalo limetokea, wanawake wengi hasa wenye uwezo wa kipato kuwarubuni watoto wetu wa kiume na kwenda kuwaambukiza virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe shime kwa Serikali yetu chini ya Wizara yetu inashughulikia masuala ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwamba tunahitaji nguvu ya ziada kuhakikisha kwamba tunaelimisha watoto wetu, vijana wetu ambao wapo shule za sekondari na vyuo vikuu kwamba UKIMWI bado upo, ni janga kubwa sana la kitaifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongelee suala la maambukizi mapya ya UKIMWI. Tumekuwa kwenye ziara Kanda ya Ziwa. Kwa kweli maambukizi ya virusi vya UKIMWI bado yapo juu, hasa katika Mkoa wa Mwanza. Kwa survey iliyofanyika mwaka 2016/2017, maambukizi ya UKIMWI yametoka kutoka kwenye asilimia 4.7 kwenda 7.2 ambapo ukilinganisha na ya kitaifa ambayo ni 4.7 unaona kabisa bado kuna maambukizi mapya yanayokuja kwa kasi kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa. Hii ni kwa sababu kuna highways, kuna mipaka, kuna migodi mingi, kuna wavuvi na mialo. Kwa hiyo, kuna mazingira hatarishi ambayo yanapelekea wananchi wetu kupata virusi vya UKIMWI.
Mheshimiwa Spika, hiyo, naomba basi, kwa bajeti hii ambayo tunakwenda kuipitisha, kwenye masuala mazima ya kupambana na virusi vya UKIMWI, kama Serikali imetenga shilingi bilioni 1.8 kwa fedha za maendeleo za ndani tunaomba izitoe hizo fedha ili afua ambazo zinatolewa ziweze kutekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda kusema kwamba UKIMWI upo, UKIMWI unaoua. Pamoja na kwamba sasa hivi tunajielekeza kwenye magonjwa yasiyoambukiza, kweli yapo na yanatusumbua wengi, hasa Wabunge kwa sababu muda mwingi tunakaa, wengine hatutaki kufanya mazoezi, tunakula vizuri; naomba kabisa kwamba juhudi ziongezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, magonjwa yasiyoambukiza ni hatari kushinda UKIMWI, kwa sababu ukiugua Kisukari hapa, ukiugua Hypertension na masharti ya vyakula yanabadilika, lakini UKIMWI utakula kila kitu. Kwa hiyo, magonjwa yote yanayoambukiza na yasiyoambukiza ni lazima tupambane nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)