Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii nami nichangie katika hotuba hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nami nichukue fursa hii kuipongeza Serikali ya Chama change, Chama cha Mapinduzi, hususan Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anafanya hasa sisi Wabunge ambao tunatoka Majimbo ya vijijini. Ametupa heshima kubwa sana, kwa fedha nyingi ambazo zimeelekezwa katika shule zetu, hasa shule chipukizi. Mimi ni miongoni mwa jimbo ambalo ni Halmashauri na limenufaika sana kwa fedha za Mheshimiwa Rais hizi alizoenda kututafutia huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama kiranja wa Serikali. Amefanya kazi iliyotukuka na anakisaidia sana Chama chetu, Chama cha Mapinduzi kutekeleza Ilani yetu ya mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa spika, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, wanashughulika na vijana ambao ndio waathirika wakubwa sana wa ajira za nchi hii. Tunategemea vijana hawa waajiriwe katika Sekta ya Kilimo. Ofisi hii ya Waziri Mkuu imekuwa inashughulika pia na vitalunyumba, wakitoa mafunzo kwa vijana ili waweze kujiajiri katika kilimo hiki cha umwagiliaji wa njia ya matone kupitia vitalunyumba.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo ambalo naomba niishauri Serikali kupitia Ofisi hii ya Waziri Mkuu. Vitalunyumba hivi vinauzwa ghali sana. Vifaa peke yake inafikia takribani shilingi milioni 14 kujenga kitalunyumba ambacho ni cha kawaida. Kwa wananchi wetu masikini na hasa wa vijijini ambao wamekosa ajira; na vijana hawa wamepata elimu lakini ajira hakuna, wana nia ya kujiajiri.

Mheshimiwa Spika, naishauri Ofisi ya Waziri Mkuu itenge fedha kiasi kuweka ruzuku katika vitalunyumba ili vishuke bei na wananchi, wale vijana wanaopata mafunzo; ambapo wanatoa mafunzo kwa vijana 100 kwa kitalu nyumba kimoja ambacho kinajengwa katika Halmashauri moja. Sasa kitalunyumba kimoja kinaweza kuendeshwa na vijana watatu mpaka watano. Sasa wale vijana wanaobaki 97 wanakuwa wamepata elimu, lakini hakuna cha kufanya. Naishauri Serikali iweke ruzuku katika vitalunyumba, kwani itaongeza wigo wa ajira katika sekta hii ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, tumeona juzi Mheshimiwa Rais akitoa vitendea kazi zikiwemo pikipiki kwa Maafisa Ugani wetu, lakini tunashuhudia kuona nia ya kuongeza bajeti ya kilimo.

Mheshimiwa Spika, tunapokwenda kuongeza bajeti ya kilimo, tuhakikishe basi kunakuwepo na matrekta na pembejeo nyingine zikiwemo power tiller, plau za kukokotwa na ng’ombe, lakini mbolea. Serikali inatumia fursa hii kuweka ruzuku. Juzi tumeona baadhi ya Wabunge wakichangia na kulalamika, matrekta yaliyoletwa yanakatika kwa sababu hayana ubora. Huko nyuma Serikali yetu ilikuwa na sera mbalimbali za kilimo ikiwemo siasa ni kilimo, hapa tulimsikia Mheshimiwa hapa mwandishi wa vitabu Shigongo akisema. Pia kulikuwa na kilimo cha kufa na kupona na mwisho hapa juzi juzi tulikuwa na kilimo kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule nyuma tulikuwa na matrekta bora sana. Yalikuwepo matrekta ya Ford, Massey Ferguson, John Deere lakini kuanzia kilimo kwanza tumeanza kuleta matrekta ya ajabu. Kulikuwa na matrekta ya Farm Truck mtu anakopeshwa trekta kabla hajalipa deni, trekta limeshaharibika na ndio maana umeona taasisi ile ambayo ilikuwa inakopesha matrekta SUMA JKT walipotea hapa. Kwa sababu, hasara ile ilikuwa huwezi kuikamata, trekta imeshakuwa scraper na mtu bado ana deni. Baadhi ya vijiji vingi na wakulima wengi waliathirika, lakini hii Ursus ambayo imeletwa miaka hii ya karibuni ni ya hatari kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini tusirudi tukaleta matrekta ambayo yanafaa kwa kilimo cha ardhi ya Tanzania? Matrekta ya Ford, Massey Ferguson, John Deere, matrekta imara ambayo mtu alinunua akiwa kijana na mpaka anafikia miaka 60 kama mimi anaweza kulitumia. Leo trekta zinauzwa mpaka shilingi milioni 50, shilingi milioni 60. Kama tunataka kwenda kufanya kilimo kama ilivyo kilimo ni uti wa mgongo basi tuhakikishe Serikali inaweka nguvu kubwa katika kuleta trekta, ambazo ni imara lakini ruzuku ya Serikali iwepo ili ziuzwe kwa bei ambayo mwananchi anaona anaweza kununua. Mwananchi mmoja akinunua trekta watakaolima ni zaidi ya familia 10, kwa sababu akishamaliza kulima shamba lake atamkodisha mwingine, akimaliza atamkodisha mwingine. Hii maana yake ni nini? Tunaongeza kilimo katika fursa ambayo tunaitarajia kwamba iajiri wananchi walio wengi katika Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini Serikali kwa ujumla imeifanya Mkoa wa Singida, Mkoa wa Dodoma na Mkoa wa Simiyu kuwa mikoa ya kielelezo, katika kuhakikisha kupunguza deficit hii ya mafutam ambayo tunaagiza mafuta ghafi kule nje ili yaje yachakatwe hapa ili tutengeneze mafuta ambayo hayana cholesterol yanayotokana na mbegu za alizeti. Serikali ilifanya jitihada sana za kusambaza mbegu japo hazikuwa bora. Dhamira yetu ni kuona sasa basi Serikali inaingia katika kusambaza mbegu bora kabisa za Hysun za alizeti ambazo zitakuwa na tija kubwa katika kuzalisha mazao ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naendelea kuishauri Serikali iongeze na iendelee katika kilimo cha umwagiliaji. Kilimo ambacho kitatoa ajira na ambacho kina uhakika sana na uvunaji, ukiacha kilimo cha mvua ni kilimo cha umwagiliaji. Tuna namna nyingi ambazo baadhi ya mito inapotea, inakwenda kumwaga maji katika bahari na maziwa, tungeitumia ile kukinga mabwawa ya kutosha ili tuweze kupata kilimo cha umwagiliaji. Pia maji ya chini ya ardhi yakitumika yatatusaidia sana kuongeza kilimo, kama njia mojawapo ya kusaidia kilimo cha nchi hii.

Mheshimiwa Spika, ninalo jambo lingine ambalo naishauri Serikali, irudishe Tume ya Mipango ili ibuni vyanzo vingi vya mapato. Tumezoea kujikita katika vyanzo ambavyo ni vile vile miaka nenda, miaka rudi. Kama tusipoirudisha Tume ya Mipango, isaidie kuchakata namna bora ya vyanzo vipya vya mapato, tutaendelea kubaki hapa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sidhani tunapokwenda tunaongeza shilingi trilioni tatu kwa kila mwaka au shilingi trilioni mbili kutoka 36 kuja 39 bila vyanzo vipya vya mapato, tutaendelea kuikaba sekta ya mafuta ya petroli, ndio chanzo chetu kikubwa cha mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kuna jambo hili ambalo limeanza mchakato siku nyingi, naiomba sana Serikali yangu, iikubali na imalize mchakato wa kuchakata LNG, gesi yetu ije katika kimiminika iweze kutumika kama mbadala wa mafuta. Magari mengi madogo yaweze kutumia LNG ili tutoke katika utegemezi wa kuagiza mafuta. Tumeshuhudia mafuta yalivyopanda kutokana na vita ya nchi jirani zinazosakamana na kusukumana za Ukraine na Urusi. Leo dunia inahamanika kwa sababu hii. Kama tungekuwa tumeanza kuichakata gesi yetu na ikatumika kama kimiminika, leo baadhi ya magari mengi yangeanza kutumia LNG na tungetokana na tungepunguza kiasi kikubwa cha utegemezi wa mafuta ya petroli katika uendeshaji magari na mitambo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na ahsante sana kwa nafasi. (Makofi)