Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nami awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kwa kuiruzuku nchi yetu kuwa hapo ilipo kwa maana ya jiografia. Nalisema hilo makusudi, kwani leo hii tukizungumzia habari ya ardhi, iwe ni ardhi nzuri; watu wanazungumzia habari ya kilimo, habari ya maziwa na vitu vingine vyote, mimi narudi kumpelekea shukrani Mwenyezi Mungu kwa kuturuzuku hayo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, point yangu moja ya msingi, kuna bahati moja mbaya unapokuwa na kila kitu, unaweza ukafika sehemu ukashindwa kujua uanze na kipi. Ndiyo maana nataka kuleta point ya kwamba pamoja na haya yote mengi mazuri, ni lazima tuwe na vipaumbele. Hatuwezi tukafanya kila kitu, lazima tuwe na vipaumbele. Nami niseme, kwa mfano, tukizungumzia habari hii niliyosema ya ardhi nzuri; ardhi nzuri ni jambo moja na matumizi bora ya ardhi ni jambo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama tutafika sehemu tukijua tu tuna ardhi, ardhi, ardhi, tukaachana na matumizi bora ya ardhi, hautaacha kuona nchi hii ikiendelea kuwa kwenye migogoro ya ardhi, hautaacha kuona nchi hii ikiwa kwenye uzalisha duni. Kwa hiyo, naendelea kushauri na kusisitiza matumizi bora ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, najua kwa ruzuku hiyo hiyo, tunazungumzia habari ya uwekezaji katika maziwa. Ni jambo jema, lina afya. Nami ukizungumzia kule kwangu Katavi, ndiyo maana tuna uwekezaji mkubwa wa Bandari ya Karema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, point ni nini? Leo hii tukifanya vizuri katika eneo hilo, changamoto tunazokutana nazo za kuhakikisha labda mizigo yetu inapita kupitia nchi nyingine, tutakwepa hilo. Tukiwekeza vizuri katika hizo bandari, nakuhakikishia tutakuwa na uchumi mkubwa. Kwa wale waliobahatika kufika DRC, uchumi wa maeneo yale ni mkubwa. Sasa tunafanyaje ili kuweza ku-take uchumi huo? Ni pamoja na uwekezaji huu katika Ziwa Tanganyika na maziwa mengineyo. Naomba nitoke hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilifurahishwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu kuhusu Sera za Mapato na Matumizi; lakini eneo hili kwa ujumla wake, kama kila kitu kikifanyika vile ilivyotakiwa, basi kelele zingekuwa ni chache. Nalisema hilo kwa sababu gani? Pale tunaambiwa kwa maana ya Sera za Mapato na Matumizi, tumeelekezwa kwamba usimamizi madhubuti wa fedha za Umma, lakini yawepo maeneo yenye tija bila kusahau ajira na uchumi wa mtu mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiyasema hayo, tafsiri yake ni nini? Leo hii tunazungumzia habari ya uwezekaji na kwa maana nzima ya uwekezaji kuvutia wawekezaji. Pale tumeambiwa, kwa kuvutia uwekezaji, tunaweza tukazalisha ajira takribani 62,301. Nasema kuvutia wawekezaji, ni jambo moja, lakini tunasemaji kuhusu Watanzania hawa?

Mheshimiwa Spika, niseme jambo moja, tukifurahi kuona wawekezaji wanakuja, nami hapa naomba ni-declare interest, mimi ni mchimbaji mdogo wa madini. Katika eneo hilo la uwekezaji nimeshiriki kwa kina na mafao nayapata katika eneo hilo. Kwa hiyo, hata mimi naweza nikatoa darasa kwa wenzangu.

Mheshimiwa Spika, kama nchi, wakati tunazungumzia habari ya uwekezaji, tunafanyaje kwa maana ya kumsaidia Mtanzania? Je, kama nchi, tumetengeneza mazingira ya kumwandaa Mtanzania na mikataba ya Kimataifa? Maana kuna wakati mtu anaingia kichwa kichwa katika masuala hayo. Tutafika mahali Watanzania wenzangu watabaki kuwa watazamaji. Kwa sababu wanakuja watu ambao kwanza wana-financial muscles. Wana msuli wa kifedha, wanamkuta Mtanzania ambaye kwa sababu hajaandaliwa kwa maana ya elimu ya mikataba na vitu vingine, unaweza ukamkuta yeye na ardhi yake ambayo Mwenyezi Mungu amemruzuku, akaona kama haina thamani, akafikiri thamani ni kwa huyu tu anayekuja. Kumbe yeye huyu mtu ni tajiri, lakini hajatengenezewa mazingira ya kujua kwamba ana utajiri wa kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kwa eneo la uchimbaji. Bahati nzuri niseme mikakati mizuri inayoendelea katika nchi yetu, mtu mmoja anaweza akafika sehemu akaingia mkataba, kwakuwa mtu mmoja ana mashine, ana fedha, na kadhalika, yeye kama hajatengenezewa mazingira ya kujua, kuelimishwa zaidi na kupewa elimu ya mikataba, ana ardhi yake ambayo labda kama ingekuwa imethaminishwa, kwamba bwana wewe hapa tulipo mashapo ya eneo lako ni kiasi hiki na hiki na hiki. Kwa hiyo, unapokwenda kwenye meza, nenda ukiwa kifua mbele, ukijua na wewe ni kama alivyo yeye. Haya yote, naiomba nchi yangu na Serikali iendelee kufanya jambo hilo jema la kuhakikisha tunawasaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoke hapo kwenye eneo la elimu ya uwekezaji, kuna suala lingine la mwingiliano wa majukumu, taasisi za udhibiti na masuala mazima ya tozo. Kama hatutafika sehemu tukajaribu kuendelea kuona namna ambavyo kila taasisi inavyoingiliana na taasisi nyingine, masuala hayo ya tozo na vitu vingine vya namna hiyo, tunaweza tukakuta wakati mwingine tunarejesha nyuma ari ya watu kujituma katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la UVIKO na athari za UVIKO. Nafarijika kuona miradi mbalimbali ambayo imetengenezwa, lakini kama nchi, tumebaki na darasa lipi? Point yangu ya msingi ni hiyo. UVIKO kwa ujumla wake, angalia jinsi dunia ilivyosambaratika, angalia kila mtu alivyotamani kubaki kwake. Sasa katika mazingira haya ya kubaki kwetu, iwe ni somo. Kwa maana gani?

Mheshimiwa Spika, katika mazingira ambayo mtu wetu alikuwa anatakiwa labda akatibiwe India, Marekani au Uingereza, kwa somo lile la UVIKO unafika mahali unaona kumbe kama nchi, tuna kila sababu ya kuendeleza miundombinu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana naishukuru sana Serikali. Leo hii ukiichukulia Jakaya Kikwete pale, hata ukija tu Benjamin, shughuli zinazofanyika pale, uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali, hata kama ilikuwa UVIKO imetufikisha mahali ambapo tumefungiwa milango, kumbe unaweza ukafungiwa milango, lakini ukawa katika position ya baadhi ya mambo kujihudumia internally. Nilikuwa nasema, tukifurahia mambo mengine kwamba tumejenga madarasa, well and good; vituo vya afya, well and good, lakini somo pana tunalolipata ni lipi? Maana yake, tuendelee kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. (Makofi)