Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mkinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia kwenye Hotuba ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kumshuruku Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema ambaye ameturuzuku uhai na pumzi hii tuliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichukue fursa hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanyika katika nchi yetu. Tumeona kazi kubwa inayofanyika kwenye Sekta ya Afya, tumeona kazi kubwa inayofanyika kwenye Sekta ya Elimu, tunaona kazi kubwa inayofanyika kwenye barabara za vijijini, hongera sana kwa Serikali. Tunaomba kazi hii iendelee ili tuweze kuwaondolea wananchi matatizo yanayowakabili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii vilevile kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa ziara ambayo aliifanya kwenye Jimbo langu la Mkinga, ziara ambayo imeleta chachu ya maendeleo katika Wilaya yetu. Hapa nitazungumzia kiujumla. Kuna kazi kubwa inafanyika kwenye vituo vyetu vya mipakani kwa facilitate biashara na kuingiza mapato kwenye nchi yetu. Kwa kipindi kirefu, border yetu ya Horohoro ilikuwa haifanyi vizuri, lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja, amefanya kazi kubwa, na leo hii tunasimama kifua mbele, border ile inaingiza mapato mengi sana kwa nchi yetu. Tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati naipongeza, yapo mambo ambayo tunayaona Mkinga na tunahisi vilevile kwenye maeneo mengine ya mipakani yapo. Pamoja na kazi kubwa iliyofanyika hii ya kukusanya mapato, lakini kituo chetu kile kina matatizo ya miundombinu ya usafiri. Kuna matatizo makubwa ya vifaa vya usafiri na vile vile kuna tatizo la huduma ya zimamoto. Vituo hivi vinakuwa na shehena kubwa ya mizigo. Naiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwezesha kupata fire equipment katika maeneo ya mipakani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mkinga inapakana na nchi ya Kenya na mpaka wetu kule ni porous, kwa hiyo, tunahitajika kufanya ulinzi wa mara kwa mara; kufanya doria ya mara kwa mara. Tatizo tunaloliona, watu wetu wa vyombo vya usalama wana matatizo makubwa ya vyombo vya usafiri. Sasa naomba Serikali iangalie hili kwa jicho la pekee kwa Mkinga. Ninaposema hivi Serikali mnaelewa, position ya Mkinga tunahitaji kufanya doria ya nguvu, mambo ya uhamiaji haramu mnayajua, tusaidieni watu wetu wa Polisi wapate gari waweze kufanya shughuli zao vizuri.
Mhehsimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja kwenye ziara yake alitoa maagizo baada ya kusikia wananchi wana matatizo ya ardhi. Naishukuru Serikali inalifanyia kazi jambo hili kupitia kikosi kazi cha timu ya Mawaziri. Rai yangu, kikosi kazi hiki kinapofanya kazi nchi nzima, lazima kioanishe na ahadi walizotoa viongozi wetu. Kikosi kazi hiki kikienda kufanya shughuli kikasahau kutekeleza ahadi za viongozi wetu, tutakuwa tumewadhalilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja Mkinga, alisikia kilio cha wananchi wa Mkinga, pale Maramba hawana ardhi, akaagiza kazi ifanyike ya tathmini ya tatizo lile mwezi wa Pili mwaka 2020. Miezi sita baadaye Waziri Mkuu aliporudi Tanga, akatoa tamko akiwa Lushoto kwamba wanaenda kumega ardhi ya Shamba la Mwele ili wananchi wapate ardhi. Alipokuja Mkinga wiki moja baadaye akatoa agizo kwamba Serikali inaenda kumega sehemu ya shamba ili wananchi wale waweze kupatiwa ardhi. Tunaposema hapa ni kwa sababu ya tatizo kubwa la ardhi kwenye vijiji vile vya Maramba A na Maramba B.
Mheshimiwa Naibu Spika, Maramba A yenye kaya 1,747 umiliki wa ardhi kwa kila mwananchi mmoja, ni asilimia 0.36 ya hekta; Maramba B yenye kaya 725, umiliki wa ardhi ni asilimia 0.6. Huu ni umasikini mkubwa kwa wananchi hawa. Tunampongeza Waziri Mkuu, aliliona hili. Tunaiomba Serikali, ahadi hizi za viongozi wetu wa wakuu ziweze kufanyiwa kazi. Hili linaenda sambamba na kazi kubwa iliyokuwa imefanyika tangu mwaka 2016 na kikosi kazi kilichoundwa na Serikali, kikafanya kazi kubwa ya kuzunguka vijiji vyote vinavyohusisha Pori Tengefu kwenye Wilaya ya Muheza, Wilaya ya Korogwe na Wilaya ya Mkinga. Maagizo yale tuliyokubaliana, tunaomba yahusishwe kwenye shughuli hii inayoendelea sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwenye Huduma ya Afya imetupatia Hospitali ya Wilaya. Naomba sasa hospitali hizi zijengewe wodi ili wananchi waweze kupata huduma za uhakika. Tumeahidiwa kwa kuda mrefu bandari ya Moa, ambazo ni bandari bubu, kwamba sasa inaenda kuwekewa miundombinu ili biashara kati ya Mkinga na Zanzibar, Mkinga na Pemba iweze kuwa facilitated. Tunaomba ahadi hiyo iweze kutekelezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali kwa jitihada za reli zinazofanyika; maendeleo kwenye sekta ya reli, lakini tunachokiona ni kwamba ujenzi wa reli ule hauendi sambamba na reli nyingine. Reli ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha imesahaulika, kazi inayofanyika sivyo kama tulivyokuwa tumeahidiwa mwanzoni. Tunaomba na reli ile iweze kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)