Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hoja hii ya Waziri Mkuu. Kwanza napenda kukupa taarifa pia, mimi humu ndani najuiliakana kama Chifu Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Kalenga. Sasa nimeshangaa kwamba sijachangia, lakini umejua nimechangia, lakini nafiri ni error kidogo. Yupo Kiswaga mwingine, lakini humu ninajulikana kama Chifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza nimshukuru sana Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, hata Jimbo langu limefaidika sana katika kipindi cha mwaka mmoja ambapo Rais huyu ameingia madarakani. Pongezi hizo zinakwenda kwanza kwa kuwa nimeweza kupokea fedha, na kulikuwa kuna kilio kikubwa katika Kata ya Ifunda kwenda Lumuli, watu walikuwa wanashindwa kuvuka wakati wa mvua, lakini kwa fedha za dharura nimepokea kama shilingi milioni 900, tumeshaweza kutengeneza daraja pamoja na kivuko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru kwa sababu nimeweza kupokea shilingi milioni 500, tunajenga Kituo cha Afya pale Kiwele; pia nimepokea shilingi milioni 446, tumeunganisha Kijiji cha Mlanda pamoja na Magulilo ambapo ilikuwa ni shida sana kuvuka. Vile vile nimepokea shilingi milioni 470 kwa ajili ya kujenga Shule ya Sekondari pale Luhota. Pia nimepokea kiasi cha shilingi bilioni moja kutoka kwenye Mfuko wa UVIKO kwa ajili ya madarasa. Kwenye UVIKO pia nimepokea shilingi milioni 500 ambazo zinakwenda kwenye maji pale Magulilo Kijiji cha Nega ‘B’. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengi yametekelezeka, kwa hiyo, nimeona nami niweze kumpongeza. Nilikuwa najaribu kuangalia mambo haya mengi yamefanyika kwa muda mfupi Rais huyu akiwa mwanamama, nasi akina baba tulikuwepo, hatukuweza kufanya haraka haraka namna hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia dunia kwa ujumla wake, nikaona kwamba wanawake huwa hawapati nafasi sana za kiutawala. Nikiangalia katika mataifa makubwa, kwa mfano, Uingereza, tangu mwaka 1801 kumekuwa na Mawaziri Wakuu 55, lakini kumekuwa na wanawake wawili tu; alikuwepo Margaret Thatcher na baadaye akaja Theresa May. Huyu mama, Margaret Thatcher ambaye alikuwa mwanamke wa chuma, alifanya kazi kubwa sana za kuinua uchumi katika Taifa lile; na ndiye Waziri Mkuu peke yake aliyetawala muda mrefu na tunaamimi na Mama huyu atatawala muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilikwenda pale Ujerumani nikaona kumekuwa kuna ma-chancellor 33 tangu mwaka 1867, lakini ni mwanamke mmoja tu anaitwa Chancellor Angela Merkel, ametawala kwa miaka 16, kwa muda mrefu baada ya Chancellor yule mwanzilishi ambaye alikuwa Otto Von Bismarck. Kwa hiyo, wanawake wanafanya kazi kubwa katika dunia hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikija kwenye hoja baada ya kutoa hiyo shukrani, ni kwamba katika Hotuba ya Waziri Mkuu imekuwa ikieleza mambo mengi; inaeleza mipango ya maendeleo katika maeneo mbalimbali na inagusa miundombinu na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nikielekea kule kwangu, Jimbo la Kalenga na Mkoa wa Iringa kwa ujumla tuna mambo ambayo tulikuwa tukitamani Serikali iweze kufanya. Kwa mfano, kwenye upande wa miundombinu, tuna barabara mbili muhimu sana na nyingine za kiuchumi. Ukiangalia ile barabara inayotoka Iringa kupita Kalenga ikaenda kule Ruaha National Park kwa ndugu yangu Mheshimiwa Lukuvi, na ile barabara inayotoka Iringa, inapita Jimboni kwangu inaenda kule Kilolo, barabara hizi tumezizungumza mara nyingi, lakini tunaendelea kusisitiza kwa sababu zina umuhimu mkubwa sana katika uchumi wa Mkoa wa Iringa na kwa Taifa kwa ujumla kwa sababu zinakwenda katika maeneo yenye Utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru nimefanya vikao na Afisa Mtendaji Mkuu wa TANROADS, amenipa matumaini. Ameniambia hii barabara ya kutoka Iringa kwenda Kilolo tutaanza pengine mwezi wa Saba kwenye bajeti ya RISE; tunaomba hilo litekelezeke. Pia amenipa taarifa kwamba barabara ya kwenda Ruaha National Park, mazungumzo yanaendelea na World Bank, pengine tunaweza tukasaini mkataba mwezi wa sita na ujenzi ukaendelea. Kwa hiyo, tunaomba haya mambo yatekelezeke ili Mkoa wa Iringa uweze kufunguka na uchumi uweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana TARURA kwa kazi kubwa ambazo wanaendelea kuzifanya. Bajeti tumeongezewa kwenye Jimbo langu na kwenye maeneo mengine ya Taifa. Changamoto kubwa tulizonazo katika kutengeneza miundombinu ya barabara za vijijini, tumekuwa hatutengi bajeti vizuri kwa ajili ya mifereji pamoja na makalati. Hilo limekuwa ni tatizo kubwa sana. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali na TARURA kwa ujumla, tunapokwenda kuweka hizi bajeti, tuzingatie sana makalavati pamoja na madaraja madogo madogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru pia CEO wa TARURA, ndugu yangu Seif, nimefanya naye vikao kadha wa kadha na amenihakikishia kwamba mwaka huu katika Mradi wa RISE vijijini, tutakwenda kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka pale Uwenda, ikatokeze Mgama kilometa 19. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba hilo litekelezwe kama tulivyoongea ili sasa tuweze kuomba mahitaji mengine. Kwa mfano, barabara inayotoka Kalenga kwenda Mafinga kupita Wasa, kupita Maboga, ni barabara muhimu sana ambayo kama mkoa tunaweza kuitumia kama njia mbadala.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa kuna changamoto kubwa sana kwenye nchi yetu, maeneo mengi hayana barabara mbadala. Kwa hiyo, ikitoka kama jam au ajali njiani, unakuta kwamba kunakuwa na ucheleweshaji mkubwa. Kwa hiyo, kama tukitengeneza hii barabara ya Kalenga, ikaingia Uwasa, ikatokea Mafinga itakuwa ni njia mbadala ya Mkoa ili hata ikitokea tatizo, tunaweza kuitumia. Yale mazungumzo nimeshaanza kufanya na TANROAD na TARURA, tumekubaliana kwamba tutaitembelea. Naomba hii iingie kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge ili ije itekelezwe baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, Serikali imekuwa ikifanya kazi nzuri sana kwenye miundombinu ya elimu na madarasa mengi tumejenga lakini changamoto kubwa ambayo tunayo ni upungufu wa walimu na mabweni. Tunatamani sana sasa Serikali ijielekeze kwanza kukarabati shule kongwe. Tuna shule kongwe nyingi ambazo zimejengwa tangu miaka 1970 na kuendelea, ambazo zimechakaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna upungufu wa walimu. Kwa mfano, weekend nilikuwa Jimboni, nimekuwa vijiji vya Nega ‘B’ na vijiji vya Mlanda. Kijiji cha Nega ‘B’ Shule ya Msingi ina walimu watano. Mfano tu natolea, Mlanda Shule ya Msingi ina walimu saba. Kwa hiyo, naomba Serikali sasa iweke nguvu katika kupeleka walimu kwenye shule zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ujenzi wa vyoo; ukiangalia tumepewa fedha kwenye vituo shikizi. Hivi vituo shikizi vimekuja bila fedha ya choo. Kwa hiyo, hilo nalo tuliangalie kwenye bajeti zetu, maana kuna Halmashauri nyingi ambazo hazina uwezo. Hilo tuliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tukija kwenye Afya, sera yetu inasema kwamba tutakuwa na zahanati kila Kijiji, na nguvu za wananchi zimekuwa zikitumika maeneo mbalimbali, na tuna vijiji vingi ambavyo tayari vimeshakamilisha maboma. Kwa mfano, nilikuwa Ndiwili Jumamosi, wameshakamilisha boma, lakini bado hawajaezeka. Sasa Serikali lazima iwaunge mkono mara moja ili sasa nao waweze kufurahia ile kazi yao ambayo wanaifanya na Serikali kuwaunga mkono kwa haraka. Hata pale Nega ‘B’ tayari wameshakamilisha boma lakini bado hatujaweza kuwakamilishia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kwa upande wa vituo vya afya, ni kweli tunayo sera ambayo inasema tuwe na vituo vya afya kila kata. Sasa kazi kubwa imefanyika. Kwa mfano, Jimbo la Kalenga lina vituo vitatu ambavyo vimekamilika. Kwa mfano, kituo cha Nzihi ni cha siku nyingi lakini hakina wards. Kwa hiyo, hiyo ni changamoto kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile ukienda kwa mfano Kituo cha Mgama; pale Mgama wananchi wameshaweka msingi kwenye kujenga wodi kwa ajili ya akina baba na akina mama, lakini miaka karibu minne hakijamalizika. Kwa hiyo, naomba Serikali kwenye bajeti zake sasa ikamilishe hivi vituo vya zamani ukiacha hivi vipya ambavyo tunavileta ili sasa na wananchi waweze kuifurahia Serikali yao kwa kazi kubwa ambayo inafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambazo nilipenda pia kuzungumzia ni kwenye upande wa umeme. Serikali imeagiza kwamba ifikapo mwezi wa 12 tuwe tumemaliza umeme kwenye vitongoji vyetu vyote, lakini nikiangalia kasi tunayokwendanayo sasa, bado tupo nyuma sana.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja, mengine nitaandika kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)