Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili kuwa mmoja wa wachangiaji katika hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Awali ya yote, nianze kwa kuipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa inayoendelea kuifanya katika maeneo yetu na katika majimbo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata fedha nyingi ambazo kila jimbo, kila kata na kila kijiji kuna miradi inayoendelea chini ya Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi. Katika Jimbo langu la Igalula juzi tu nimepokea fedha za kwenda kujenga Vituo vya Afya vya Tula na Kata ya Loya ambavyo wananchi hawa hawakuwa kabisa kwenye mafikirio ya kupata huduma bora ya afya, kwa hiyo sina budi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Igalula kufikisha salamu zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakwenda kujadili hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ameiwasilisha hapa yenye mambo mengi ambayo yatakwenda kusaidia wananchi wetu katika majimbo yetu. Kazi yetu sisi Wabunge ni kuishauri na kuisimamia Serikali pindi inapofanya vizuri lazima tuipongeze lakini pindi ambapo wanaenda ndivyo sivyo lazima tuwape ushauri ili waweze kwenda kwenye mstari. Jukumu la kuleta maendeleo ni la sisi sote wala siyo Serikali peke yake na ndiyo maana kuna miradi ambayo wananchi wao wenyewe wanaanza kwa kujenga na baadaye Serikali inaiunga mkono. Kwa hiyo Serikali ina jukumu la kuwaletea maendeleo lakini na sisi wenyewe kama wananchi tuna jukumu la kusaidiana na Serikali kuleta maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nishauri kwenye mambo machache. Jambo la kwanza tumekuwa na miradi mingi sana ambayo ipo katika maeneo hasa miradi ya maji, tunaiomba Serikali sasa ifike mwisho miradi hii iwe inafika mwisho kuliko kuwa tunaenda vipande vipande na baadaye haileti tija. Kwa mfano, mimi nina mradi wa tangu mwaka 2019 wa kutanua maji ya Ziwa Victoria ambao umeanza kuongelewa toka mwaka 2019 katika Kata za Goweko, Igagula, Nsololo na Kigwa, lakini mpaka leo mradi huu unakwenda taratibu. Kwa hiyo, naiomba Serikali kupitia bajeti hii basi tutenge fedha ambayo tutakwenda kumaliza mradi huu ambao tumekadiria wananchi zaidi ya 150,000 watanufaika na vijiji zaidi ya ishirini watanufaika na upatikanaji wa maji haya. Kwa hiyo, niiombe Serikali twende tukamalize changamoto hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, wote ni mashahidi tulipokea fedha ambazo Mheshimiwa Rais alikwenda kuzitafuta kule na zikaenda kila mkoa, kila jimbo. Fedha hizo zimeenda kutekeleza miradi mbalimbali, lakini kuna baadhi ya maeneo ambayo fedha hiyo ipo lakini bado haijaanza kutelekeza miradi hiyo. Kwa mfano, katika jimbo langu tulipewa bilioni moja na milioni mia tano kwenda kutekeleza barabara tatu katika kata tatu tofauti tofauti; kuna barabara ya kutoka Izumba kupitia Idekamizo mpaka Simbojigulu mkandarasi amesaini mkataba lakini mpaka leo hajaanza kazi. Vilevile kuna barabara zingine wakandarasi wapo site lakini hawafanyi kazi kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa jukumu la kuleta maendeleo ni letu sote ni kuikumbusha Serikali iweze kuongeza speed governor ya kuwasimamia vizuri wakandarasi hawa basi wamalize kazi na makusudio ya Mheshimiwa Rais kuwasaidia wananchi kufungua mitandao ya barabara yaweze kutimia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo lakini wananchi wa Jimbo la Igalula walinituma; wana changamoto kubwa Serikali ilitoa maelekezo ya upandaji wa uunganishaji wa nishati ya umeme, wakasema zaidi kwamba kutoka shilingi 27,000 mpaka shilingi 320,000; Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwa wewe ndiye baba wa Wizara zote niiombe kupitia Wizara ya Nishati iweze kuangalia kuna maeneo mengine wameyapandisha kimakosa wananchi sasa wameshindwa hata kuendeleza kupata huduma ambayo Serikali ilikusudia kuwafikishia hasa katika Kata ya Goweko Kijiji cha Goweko wamekipandisha hadhi ya kutoka shilingi 27,000 kwenda shilingi 320,000. Kata ya Kigwa, Kijiji cha Kigwa wamekipandisha hadhi kutoka shilingi 27,000 mpaka shilingi 320,000; vilevile Kata ya Igalula na kwingineko katika Jimbo la Igalula.
Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali, kama mnaona hii miji imekuwa kwa sababu wananchi wanapenda maendeleo na sisi Serikali kazi yetu ni kuwasaidia wananchi yale maendeleo yao yasiweze kuwaponyoka katika mikono yao, tusiende kuwavuna sana. Niiombe Serikali iweze kuangalia ni namna gani ya kuwasaidia angalau kushusha kufikia hata nusu au robo ya gharama hizo ilimradi wananchi wengi wapate huduma na sababu Serikali kusudio lake si kufanya biashara ni kufikisha huduma kwa wananchi niiombe Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizo sasa nirudi kwenye michango na mijadala ambayo ipo katika nchi yetu kwa sasa. Kila Mbunge humu nadhani kama alifanya mikutano wiki mbili au tatu zilizopita, wamekutana na maswali mengi kwa wananchi wao hasa mfumuko wa upandaji wa bei. Bado Serikali ina haja ya kuliangalia hili suala kwa umakini mfumuko huu wa bei watu wamechukua advantage kwa sababu wamekwisha ona na sisi watu wa Serikali tumeanza kulalamika kuwa kuna hiki kimesababisha mfumuko wa bei, lakini kuna bidhaa ambazo hazihitaji kabisa kupandishwa bei, lakini wananchi au wafanyabiashara wameona wapitie humo humo kwa sababu na sisi kama Serikali tumeanza kulalamika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, leo tuna bidhaa ambazo tunazizalisha humu, zimepanda mara mbili kwa kile ambacho tulichokuwa tunakizania. Kwa hiyo kuna haja kama Serikali kuangalia huu mfumuko wa bei, tusiruhusu sasa wafanyabiashara wakaanza kupitisha mambo yao ambayo yanakwenda kuwaumiza wananchi ninyi wote ni mashahidi wakati tumeingiza fedha za UVIKO ziliingia katika majimbo yetu, miradi mingi ikaenda kutekelezwa kule tulikuwa tuna janga la COVID-19 ilikuwa ikiendelea katika nchi yetu, lakini mfahamu baada ya fedha kupatikana wafanyabiashara walichukua fursa hiyo ya fedha nyingi zimeletwa na Mheshimiwa Rais wakapandisha vifaa vya ujenzi mara mbili tofauti na awali walivyokuwa wanauza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ilipanda cement kutoka shilingi 19,000 mpaka tukaenda shilingi 24,000 mpaka shilingi 26,000 katika baadhi ya maeneo, lakini leo ninavyokuambia cement imeshuka na vita ya Ukraine inaendelea, imeshuka mpaka shilingi 18,500. sasa najiuliza kwa nini wakati ule fedha zilizopatikana walipandisha saizi wameshusha kitu gani kilichosababisha kushusha wakati nchi sasa hivi tunasema tupo kwenye janga kubwa la vita ya wenzetu kule Ukraine na Urusi, lakini bidhaa hii imeshuka. Vilevile Waziri wa Viwanda na Biashara yupo, hakuna majibu ambayo tuliyatoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaishauri Serikali, iangalie huu mfumuko wa bei umetokana na nini? Mfumuko wa bei ni halali kweli bei kupanda maana sasa hivi bajaji au bodaboda tulikuwa tunaenda kwa sh.1,000 imekuwa Sh.3,000 imepanda kwa asilimia 200. Je, yale mahitaji yamepanda kwa asilimia hizo? Nauli za mabasi sehemu ya Sh.15,000 imekwenda mpaka Sh.25,000 au Sh.30,000, uhalisia wa upandaji wa gharama za uendeshaji na uhalisia wa upandaji ambao wanatozwa wananchi wetu hauendani. Kama Serikali tuone ni namna gani ya kuboresha katika suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ipo mijadala ambayo inaendelea na nataka nigusie na Serikali itusaidie, tunapoleta humu changamoto tunahitaji tuweze kutengeneza…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naomba niunge mkono hoja. (Makofi)