Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Abdulaziz Mohamed Abood

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Morogoro Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwanza kwa kunipa nafasi hii kuchangia Hotuba ya Waziri Mkuu. Kwanza nichukue fursa hii ya kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu na timu yake yote kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya kuwatumikia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi nimesikia wakizungumzia kuhusu kilimo na ajira. Tatizo kubwa ambalo lipo sasa hivi ni vijana wengi kukosa ajira, lakini njia fupi na njia nyepesi duniani kote kuondoa uhaba wa ajira ni kilimo na hasa kilimo cha umwagiliaji. Tanzania tuna kila aina ya uwezo wa kufanya kilimo cha umwagiliaji. Tuna maziwa, tuna mito, tunaweza tukajenga mabwawa makubwa ya kuweza kukinga maji ya mvua na kufanya kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nijikite kwenye kilimo kimoja tu cha mpunga. Kilimo cha mpunga Tanzania tunaweza kuwa wazalishaji wakubwa Kusini mwa Afrika na Bara zima, kama tutaweza kutumia ardhi yetu vizuri katika kilimo hiki cha mpunga na hasa kilimo cha umwagiliaji. Kwa mfano, Morogoro tuna eneo linalofaa kwa umwagiliaji hekta 1,510,339 wakati eneo hilo sasa hivi linatumika hekta 40,558. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali tujaribu sana kujikita upande huo na ajira kubwa itatoka kwa vijana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nirudi Jimboni. Morogoro tuna tatizo kubwa la maji, tunao mradi wa maji wa AFD wa Shilingi Bilioni 180 lakini mpaka leo hii bado ni hadithi tu, kila siku tunasaini, tunatangaza, tunafanya hivi, tunafanya hivi. Ninaiomba Serikali itusaidie ili mradi huu uweze kutekelezwa usaidie Manispaa ya Morogoro na Morogoro unajua ni sehemu ya uwekezaji mkubwa unahitaji maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wawekezaji wanakuja kitu cha kwanza wanauliza maji yapo? na sisi tuna upungufu mkubwa sana wa maji na hasa katika Mji wa Morogoro maeneo mengi sana yamepata miradi midogomidogo ambayo Serikali imetoa pesa zake lakini imetoa pesa kutengeneza tenki, kupeleka mabomba lakini mabomba ya kusambaza kwa wananchi haikutoa pesa. Kwa hiyo, ninaomba Serikali itufikirie katika Bajeti hii 2022/2023 kutupatia pesa katika miradi hii ili iweze kupunguza kero ya maji katika Manispaa ya Morogoro, kusambamba mabomba kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kero ingine katika Halmashauri ya Morogoro tuna stendi mpya ambayo kijiografia ya Manispaa ya Morogoro iko mbali na wananchi. Kwa hiyo, wananchi wana safari ndefu ya kwenda kupanda basi kule wa mabasi ya daladala haya. Tuna stendi ya zamani iko Mjini Manispaa ya Morogoro, lakini nashangaa stendi ile haitumiki lakini imeamuliwa yale mabasi yapaki barabarani palepale karibu na stendi wakati Halmashauri inapoteza Shilingi Milioni 32 kwa mwezi. Tungeruhusu yale mabasi yaingie pale ingeweza kulipa hata deni ya stendi mpya. Kwa hiyo, mimi ninaiomba Serikali irudishe stendi ya zamani ili iendelee kutumika, wananchi wa Morogoro wapate huduma kwa sababu eneo kubwa la Morogoro linatumika ni stendi ya Morogoro Manispaa ya Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika sekta ya Afya tuna Hospitali ya Wilaya. Hii hospitali ya Wilaya tumepewa Shilingi Milioni 500 tu ambazo zimefika kujenga OPD na Maabara, hakuna maeneo ya kulaza wagonjwa. Kwa hiyo, tunaomba Serikali Mradi huu tuumalize kwa sababu huu mradi una miaka saba sasa, tunaomba Serikali itumalizie mradi huu ili tupate na wodi za wagonjwa katika Hospitali hii ya Wilaya ya Morogoro. Katika bajeti tulitengewa Milioni 500 hazitoshi, tunaomba tuzidishiwe ili tumalize, kwa sababu Hospitali ya Mkoa wa Morogoro imeelemewa. Kwa hiyo, tunaomba na Hospitali ya Mkoa wa Morogoro nayo iweze kupata upanuzi wa majengo yake ili nayo iweze kupokea wagonjwa wengi zaidi, kwa sababu Morogoro ni katikati ya Miji yote, wagonjwa ni wengi, ajali zinatokea nyingi zinahitaji Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ya Rufaa ipanuliwe iwekwe majengo mengine yaongezwe ili iweze kutoka huduma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kutoa ushauri kwa Serikali kwa sababu sisi Wabunge tuna wasaidizi. Wasaidizi wenyewe katika Majimbo yetu ni Madiwani, Madiwani wasaidi wao ni Wenyeviti. Kwa hiyo, mimi ninaishauri Serikali hali ya Madiwani na Wenyeviti na hasa Madiwani hali zao katika kipato ni kidogo sana. Kwa hiyo, ninaishauri Serikali tuwaongezee kidogo ili wafanye kazi vizuri, hata sisi Wabunge tunapokwenda kwenye Kata zao tunakuta kidogo kumechangamka na wameweza kuzungukia Kata zao. Kwa hiyo, maslahi yao tuyaboresha kidogo Madiwani na Wenyeviti wa Mitaa, tuwape posho za kuweza kujikimu katika kutumikia wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja mkono. (Makofi)