Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Dr. Charles Stephen Kimei

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nashukuru sana kwa fursa hii. Natumaini nami utanipa dakika 15. Kwanza nianze kwa kusema kwamba nampongeza sana Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Tunaona jinsi ambavyo wanakimbizana kutafuta wawekezaji kutoka nje, na zaidi kutafuta resources, fedha kutoka kwenye Mataifa rafiki na kutoka kwenye mashirika ya Kimataifa ili waweze kuongezea kile tulichonacho na kuweza kusukuma na kutekeleza mipango ambayo tulikuwa nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri kwamba wote tunaelewa kwamba lengo kuu la mipango tunayotunga hapa na bajeti ni ukuaji wa pato la Taifa ili wananchi waweze kuinua maisha yao kwa kujipatia kipato cha juu na kuweza kuboresha huduma wanazopata. Kwa hiyo, ndiyo lengo kuu. Kama tukishindwa kufikia hilo, basi hatujakamilisha kazi yetu kama tunavyostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naamini kwamba tumefeli kidogo. Kwa sababu gani? Katika lengo la mwaka huu kubwa kwenye bajeti ya mwaka uliopita na mpango wa mwaka huu ambao tunautekeleza pia, ni kwamba tuweze kufufua uchumi wetu. Sasa kufufua uchumi wetu siyo kupata 4.8% ambayo ilijitokeza baada ya madhara ya Uviko. Kufufua uchumi wetu maana yake ni kurudisha kasi ya ongezeko la pato letu kwenye 7% au zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Profesa Muhongo amesema sawa kwamba hatuwezi; na miaka hiyo ya nyuma kabla, tulipokuwa kwenye 7%, nia ilikuwa kwamba lazima tuongeze ile kasi ifike asilimia 8, 9 hata 10 ambayo ndiyo inaweza kupelekea kusema kwamba sasa tumejiondoa kwenye umasikini na kufika katika vurugu ya nchi ambazo zipo kwenye kipato cha kati na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama hatujaweza kufufua, tumebakia na asilimia 4.9; na ninashangaa kwenye huu mpango tulionao sasa hivi, tunasema kwamba hata mwaka unaokuja 2023 pato letu litakuwa kwa asilimia 5.3. Hata maoteo yanayofanyika kwenye mpango wetu huu hatujaweza kuwa courageous tukasema turudi kule tulipokuwa ndani ya kipindi cha miaka mingine miwili. Bado tuko chini ya 7% pengine mpaka mwaka 2025, ndiyo maoteo yaliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nafikiria kuna tatizo moja hapa, kama siyo kwenye takwimu, ni kwenye maandishi mengine. Ukweli ni kwamba haiwezekani nchi nyingine kama Botswana, Kenya na Rwanda; Rwanda imeongeza uchumi wake na kasi ya ukuaji wa pato lake ni asilimia 9.5 na Kenya ni asilimia 7.2. Sasa tunapoanza kusema kwamba aah, ni mvurugano wa logistic industry kwenye dunia, ni vita vya Ukraine, tusing’ang’anie huko. Tujaribu kuangalia ni kitu gani tunaweza tukafanya, tukarudisha uchumi wetu kwenye ukuaji wa 7% au zaidi ya 7%. La sivyo, hatutafika popote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati mkubwa ambao nashauri utumike kuweza kufufua uchumi wetu kwa haraka ni ule wa kushirikisha sekta binafsi. Inavyooneka sekta binafsi yetu haichangamkii fursa. Haioni fursa. Tunatengeneza miundombinu mizuri, kila kitu kinafanyika sawa sawa kwenye upande wa Serikali na utaona kwamba sekta zilizokuwa kwa kasi zaidi ya 8% ni zile ambazo zinapata uwekezaji wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya maji imekua kwa asilimia 11.9, huduma za jamii, ni asilimia 8.5, habari 8%, fedha na bima asilimia 10, madini na kadhalika. Ukienda hizi sekta nyingine ambazo tunashirikisha sekta binafsi, uchukuzi na uhifadhi imekua kwa asilimia 1.7 tu na ndiyo huko wenzetu tuko tunakimbizana. Ukienda kwenye kilimo 4%, pesa yote inaenda huko kwenye bajeti ya kilimo lakini ina-grow kwa 4% licha ya kazi kubwa inayofanywa na Mheshimiwa Bashe. Viwanda imekua kwa asilimia 6.3, biashara asilimia 4.4, ujenzi asilimia 5.3, upangishaji na majengo asilimia nne na nukta. Sasa hizo ndiyo sekta hasa za wajasiriamali, lakini hazikui. Hawajaweza kuchangamkia fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri njia ya kuweza kulazimisha watu wajiingize kwenye uchumi huu pengine, badala ya kutupa fedha za kupeleka kwenye barabara za TARURA kwa sababu tumeshapeleka kiasi kidogo na barabara zimeanza kuwa nzuri, tupe hiyo Shilingi milioni 500 kila Mbunge achangamkie mradi wake kwenye jimbo lake, aajiri watu, ahakikishe wajasiriamali 500 mpaka 1,000 wanaingia kwenye mradi huo, waanze kuzalisha, na hiyo iwe ni mbegu itakayozalishwa mwaka hadi mwaka. Pia tutakuwa tunashirikisha wajasiriamali wetu kwa nguvu zaidi kuliko kusubiri ile mikopo ya 4,4,2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini tukiweza kufanya vile itatusaidia. Lazima ile miradi inayoletwa ionekane kwamba itatekelezeka na Wabunge wasimamie na wajitolee katika kusimamia kweli.

Mhshimiwa Mwenyekiti, inavyoonekana, sekta hii haiwezi kupata fedha kutoka kwenye vyombo vya fedha. Kwa nini? Kama alivyosema Mheshimiwa Profesa Muhongo, riba ziko asilimia 16. Bbado asilimia 16, haijapungua! Toka mimi niingie huku Bungeni miaka ya nyuma riba ni asilimia 16. Sasa hii issue ni kwamba mtu mwingine anaogopa kuchukua mkopo wa riba asilimia 16. Watu wengi wanaogopa kwa sababu hakuna faida ya haraka namna hiyo, lakini tukitumia huu mpango wa sasa hivi wa fiscal stimulus, tuache hii monthly stimulus ambayo imeshindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, monthly stimulus imeshindwa kwa sababu ukweli ni kwamba inflation iliyopo na kadhalika, siyo a man management type ni supply oriented. Kwa hiyo, ni lazima tutumie mbinu nyingine ya kufanya fiscal stimulus; tutapeleka fedha namna gani kwenye uchumi wetu vijana waweze kuchakarika tuanze kuona mabadiliko yanatokea kwenye zile sekta ambazo naamini Mheshimiwa Prof. Muhongo amezitaja vizuri. Kama hilo likifanyika naamini tutakuwa na kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imezungumzwa issue ya inflation, mimi naamini bado tuko vizuri. Asilimia 4.6 ni nzuri, lakini naamini pia kuna suppressed inflation hapa. Watu wanaona bei zinakua sana, lakini tukienda kwenye karatasi tunaambiwa ni asilimia 4.6. Haiwezekani iwe 4.6 wakati Ulaya ambako inflation yao kwa kawaida ni 2% mpaka 3% iko asilimia 10. Ukienda UK ni asilimia 10, EU huko kwa wastani ni asilimia 10, na ni plus!

Mheshimiwa Mwenyekiti, East Africa, nchi za wenzetu hawa, wao inflation ni 9%. Wastani wa block yetu ni asilimia 9.5. Ukisema sisi ni asilimia 4.6, nasema na sisi tuko kwenye kisiwa fulani ambacho Mungu ametubariki. Kwa hiyo, naamini pengine siyo rahisi sana kufikia lengo hilo ambalo tumejiwekea sasa hivi ni 3% mpaka 5%, tutajiminya sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ina maana lazima tuache ile monthly accommodation kwamba mikopo itolewe kwa sababu kinacho-drive inflation ni mikopo ambayo inaongeza ujazo wa fedha, kufukuzana na supply ndogo. Kwa hiyo, lazima mikopo itolewe ili tufungue mwanya huo ili tuweze kusaidia sekta zile ambazo zinahitaji mikopo ili ziweze kuongeza uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kubana kiasi hicho, lazima tufuate monthly accommodation kukubali kwamba tuongeze kidogo inflation lakini kwa sababu ni muda mfupi, pengine ugavi (supply) itajifungua, halafu inflation itaanza kushuka tena.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upande wa kilimo naona matatizo. Ukweli ni kwamba tumejitahidi, lakini gharama za kilimo zimeongezeka sana. Kwenye korosho kwa mfano, wametumia gharama kubwa, wanasema kwamba bei za chakula duniani zinapanda kila mahali, lakini yule mtu aliyetumia gharama kubwa sana za kuvuna korosho yake this time anaambiwa bei zimeshuka. Hii dunia inatuonea namna gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani jitihada tunazoona Mheshimiwa Rais wetu anafanya kutafuta masoko, specific masoko kwa Marekani, ndiyo jitihada tunazohitaji kwa mazao mengine ili tuwe na a captive market ambayo tunajua kabisa kwamba kwa bei za kule tutapata kiasi hiki, lakini sasa hatuwezi kumwambia mtu aliyetumia gharama sijui mara ngapi, halafu unamwambia eti bei ya kuuzia korosho sasa imeshuka. Wanalia! Mimi nimesikia wanalia, lakini siyo kwa korosho tu, ni kila zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo ilivyo kwenye kilimo, wale wenzetu wanatusubiri, wanatupiga. Wewe unatumia gharama kubwa, unaenda step mbili forward unarudi nne nyuma kwa sababu bei inashuka unakuta income yako ni ile ile, gharama hujai-recover. Ni ngumu sana. Kwa hiyo, naona tuangalie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kuna tatizo lingine kwa upande wa mabwawa, ni mojawapo ya kufanya decision. Ni kwamba pale unapoona kwamba kuna mwanya wa mfanya maamuzi ili kupendelea, the only way ni kumfanya afanye kitu kwa haki. Kila mtu apate kwa usawa, basi unaamua kuweka rules au vigezo ambazo zita-guide ile decision. Ukiwa na rule, ni lazima kama yule mtu anagawa kwa mfano cake ya Taifa wanagawa hapa, ile bajeti ya kilimo inagawanywa, kungekuwa na rooms zinazosema kwamba ili upeleke bwawa mahali fulani, ni lazima kigezo hiki na hiki kifikiwe. Siyo unaenda kufikiria tu mwenyewe, unaamua peke yako, unaweka bwawa kubwa hakuna hata mtu, yaani mwaka mzima upepo ni mkubwa hata kitu hakioti, wewe unaenda kuweka mabwawa kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuweke vigezo ili kuhakikisha kwamba decisions zinafanyika kwa uhakika na kwa njia ambayo ni objective na sahihi. Kwa sababu fedha hizi za kwetu kwenye bajeti na kwenye mpango zinapotea wapi? Kwenye matumizi. Wewe utatafuta hela nyingi utapata, lakini kwenye matumizi ukitumia ovyo ovyo tu, ukatupatupa hutapata tija. It is not efficiently invested and you don’t get anything.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani naomba, hata tusipoongeza ile bajeti, lakini tukatumia kwa namna ambayo itatumika na itasimamiwa vizuri na miongozo ikatolewa sahihi na watu tuione; tutaiona hapa Bungeni, lakini miongozo itolewe, watu watumie kwa haki na wawe waadilifu na hatua zichukuliwe. Niliona Wabunge walikuwa wakali sana kwenye CAG report. Kwa hiyo itumike, naamini tutafika mahali penyewe na hakuna haja ya kuongeza kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, tunasema uchumi ukue lakini kwenye mazingira tulivu, natural economic stability. Sasa issue inajitokeza ni hivi, niliangalia bajeti kwa mfano ya wenzetu, majirani zetu, mwaka jana wao hawakutangaza new measures za revenue, walisema revenue measures za mwaka jana zitaendelea ku-hold, unaona lakini tutaongeza ufanisi kwenye ukusanyaji na kuziba mapengo kwenye ukusanyaji wa kodi. Kwa hiyo sasa maana yake nini? Ile kalenda ya kodi ikawa izingatiwe kwa hiyo tunamuomba pia Waziri, anapoenda kufikiria hili aione kama…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)