Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia Mpango wa Taifa. Nitaanza kuipongeza Wizara kwanza jinsi inavyofanya kazi yake na jinsi inavyorejesha mrejesho kwa wananchi na tunaona matunda yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo ambayo Serikali ikiyachukua na kuyafanyia kazi, naamini tutakuwa na pato kubwa la Taifa kwenye nchi yetu. Tunayo Bandari ya Dar-es-Salaam, Bandari ya Dar-es-Saalam imezidiwa na mzigo, lakini tunayo Bandari Kavu ya Kwala, wakichukua Mpango Mahususi wa haraka kwenda kuipunguzia Bandari ya Dar-es-Saalam tukaiboreshe ile Bandari Kavu ya Kwala, naamini pato letu litaongezeka kwa kasi sana kulingana na mizigo mingi inayopita hivi sasa. Nasema hivi kwa sababu mizigo inayopita pale ya transit kwa maana ya DRC-Congo, Zambia, Malawi, Uganda pamoja na Rwanda. Kwa hiyo utaona kwamba Bandari ya Dar es Salaam ime-stuck na meli nyingi ukitazama zimesimama zile ni fedha na ndiyo mipango tunayoijadili hapa. Kwa maana hiyo tukitumia ile Bandari Kavu kwa muda mfupi na kwa haraka zaidi naamini pato letu litaongezeka na mahitaji tutakuwa tunayapata kwa haraka zaidi kulingana na vyanzo tulivyonavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Serikali basi iangalie umuhimu wa kuangalia uwekezaji katika maeneo mbalimbali. Tunayo port ya Kigoma lakini na Ziwa Tanganyika, naamini maeneo haya Serikali ikiyachukua na kuanza kuyafanyia kazi, tutapata mapato ya kutosha. Vilevile uwekezaji wetu na mipango yetu tunayoipanga inategemea na mali tunayoingiza kutoka katika maeneo mbalimbali, lakini tofauti za kibiashara ukiangalia kwa Ruvuma tunayo makaa ya mawe, tukiiboresha Bandari ya Mtwara, ina maana katika uchumi, kibiashara zaidi tutavutia wawekezaji wengi wa kutosha na vilevile Bandari ya Mtwara itabeba mzigo wa kutosha kwa maana makaa ya mawe ukiangalia na changamoto iliyopo sasa hivi tutajikuta pato letu linaongezeka kwa kasi kubwa sana. Pamoja na hayo na mipango tunayoendelea kuifanya, tunayo mipango sasa hivi tunakuja na Bima ya Afya, maana yake nini? Mipango na fedha zote tunazozitafuta hizi, tukiboresha mazingira haya yote tunayoyapanga, Watanzania watatibiwa bure kwa sababu tayari watakuwa na mchango ndani ya Taifa lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile juzi Jumamosi wakati tunapitisha hoja za CAG, tulikuwa tunaangalia mapato na matumizi yasiyo rasmi na vitu vingine. Ushauri tu kwenye Mpango wa Taifa kupitia Waziri wa Fedha, basi angeenda kuangalia namna gani ataelekeza fedha zingine, mfano, kwenye halmashauri zetu tunatoza asilimia moja ya mapato ya ndani ambayo wakulima ndiyo wanayazalisha wao na tunatoa asilimia mia moja. Asilimia arobaini inaenda kwenye maendeleo na asilimia sitini inabaki kwa matumizi ya ndani. Kwa nini asilimia ishirini isitolewe ikaelekezwa kwenye sehemu ya Bima ya Afya kwa wananchi ambao wako kwenye mazingira magumu huko vijijini ambayo ukiitengenezea mpango itasaidia kwa Taifa letu kwa sababu wananchi ndiyo hao hao wanaozalisha na ndiyo hao hao tunaowatoza kodi, kwa nini wasibaki na asilimia arobaini ya matumizi na asilimia ishirini ikaenda kwa wananchi na asilimia ishirini ikaenda kwenye maendeleo ambayo tunayatarajia kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, mipango tunayoiweka hii basi tuweke na mipango ya kudhibiti wizi unaoendelea kwenye nchi yetu hii, kwa sababu bila ya kuwa na mpango wa kudhibiti nako ni sehemu ya tatizo. Ukisikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge, lakini na hali iliyopo kule vijijini kwa wananchi na mabilioni tunayoyataja hapa utaona bado hatujafanya kazi ya kudhibiti fedha. Bado tunafanya kazi ya kukusanya mapato mengi lakini matumizi yake yanaenda nje ya utaratibu. Hii ni hatari na wananchi hawawezi kutuelewa, lakini kwa vile Serikali ipo na inasikia ni vyema sana kila ngazi inayohusika ikahakikisha inadhibiti kile ambacho tunakipata ili kiende kufanya kazi inayotarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo naamini kabisa Taifa letu ni tajiri na lina mipango mizuri na kazi zinazoendelea vizuri kwa sababu tunaendelea kupata fedha kutoka nje lakini na sisi humu ndani tuna fedha, ni vyema sana tukatumia tulichonacho pamoja na za nje zikasaidia Taifa letu lakini kwa mipango tunayoiweka halafu fedha hizo zinaenda nje ya utaratibu, kwa kweli hii ni hatari na wananchi hawawezi kutuelewa. Hivyo, ni vyema sana tukajikita kwenye sehemu ambayo tunaweza tukafanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tukienda sehemu ya uzalishashaji. Wenzangu wamechangia vizuri kwamba tunayo maeneo muhimu sana ambayo nchi kama nchi inaweza ikayagawanya. Watawala wa mwanzo Hayati Mwalimu aligawanya majukumu Mtwara akaweka korosho, Lindi akaweka mbao, Rukwa akaweka kilimo yaani kila maeneo aliweka utaratibu. Sasa ni vizuri mipango tunayoipanga tukaangalia nini kwenye nchi yetu ambacho kinahitajika kwa uharaka zaidi? Eneo fulani tukaliwekea utaratibu, tukaanza kutengeneza uzalishaji. Tukiweka katika mazingira hayo, naamini kabisa tutafanya mambo makubwa na kelele zitakuwa zimepungua, lakini vilevile wananchi wataelewa tunafanya nini kwenye Serikali yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya haya machache, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)