Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Handeni Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili na mimi niweze kuchangia Mapendekezo ya Mpango 2023/2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 08 Aprili, 2021 Waziri wa Fedha aliwasilisha hapa Mpango mkubwa wa nchi wa Miaka Mitano. Mpango huu wa miaka mitano ndio ambao umesababisha leo tunajadili mpango wa mwaka mmoja mmoja; na mpaka sasa tumekwisha jadili mipango miwili na sasa tuko kwenye mapendekezo ya mpango huu wa tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mpango ule mkubwa wa miaka mitano ambao ulikuwa wa 2021/2022- 2025/2026 uliandaliwa kwa kutumia rejea ya vitabu kadhaa, nitavitaja harakaharaka; Dira ya Taifa ya Maendeleo, Ilani ya Uchaguzi ya CCM, hii niliyoishika na watu waione, kitabu makini kabisa; Mpango Elekezi wa Muda Mrefu, matokeo ya tathmini, sera na mikakati mbalimbali ya kisekta, Dira ya Afrika Mashariki 2050, Dira ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Agenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hivi vitabu vyote nilivyovitaja hiki kimoja ndicho ambacho tulikwenda nacho kwa wananchi, ndicho ambacho tulikinadi, ndicho ambacho wananchi waliamua kwamba watakichagua hiki na wakaichagua Serikali ya CCM ili iweze kuleta maendeleo. Kwa hiyo mipango yote tunayoipanga lazima ilete tafsiri ya hiki kitabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye huu mpango mkubwa kulikuwa na shabaha za mpango ambazo ziko tano. Na mimi leo nataka tuzipitie vizuri tukirejea mapendekezo haya ya mpango yaliyopo mbele yetu tuone kama yanaleta tafsiri ya hiki ambacho kipo kwenye mpango wetu mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shabaha ya kwanza ya mpango ule mkubwa wa miaka mitano inasema, “ukuaji wa uchumi kuongezeka kutoka asilimia sita mwaka 2021 hadi kufikia 58% mwaka 2026.” Ilani yetu ya Uchaguzi ukurasa wa 13 (b)(1) inasema, “kuweka sera madhubuti za uchumi jumla ili kukuza uchumi kwa wastani usiopungua asilimia nane kwa mwaka.” Hiki ndicho ambacho tumewaahidi Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyongea kwa Januari mpaka Machi, 2022, uchumi wetu umeripotiwa kukua kwa asilimia 5.4. Hii ndiyo kusema tuko chini na nje ya mpango wetu ambao tumeuweka sisi wenyewe. Kwa hiyo, Serikali wanayo kazi ya kwenda kufanya kuhakikisha kwamba kitabu hiki wanakitafsiri na wanakitekeleza kwa namna ambavyo kinaelekeza. Kinataka ukuaji wa uchumi kwa asilimia nane, lakini Serikali imeripoti ukuaji wa uchumi wa asilimia 5.4.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shabaha ya pili ilikuwa ni mapato ya ndani ukijumuisha mapato ya halmashauri kuongezeka kutoka asilimia 15 ya pato la Taifa hadi kufikia asilimia 16. Hivi tunavyozungumza ukisoma haya mapendekezo ya mpango yaliyoletwa mbele yetu, sura ya 3 (3), (2)(i) inasema, mapato ya kodi; kwenye mpango wanatarajia yafikie asilimia 12 ya pato la Taifa. Yaani mpango huu wa mwaka mmoja uko nje kabisa ya mpango mkubwa ambao ndiyo tumekubaliana kuufanya. Wao wanaongelea mapato ya kodi kufikia asilimia 12 ya pato la Taifa ilhali mpango mkubwa unataka tufikie kuanzia asilima 15.9 mpaka 16.8.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa na mipango ya hivi. Mipango hii midogo ya mwaka mmoja mmoja inatakiwa itafsiri mpango ule mkubwa tuliojiwekea na ambao tumeupeleka kwa wananchi kuunadi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shabaha ya tatu ya ule mpango mkubwa inasema, “mfumuko wa bei kuendelea kuwa wa tarakimu moja, wastani wa 3% mpaka 5%.” Naipongeza Serikali kidogo hapa kwa sababu wamejitahidi sana kuweka mfumuko wa bei kwenye single digit. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikilizeni niwaambie jambo muhimu unapoongelea mfumuko wa bei na hasa kwa Watanzania. Jambo la muhimu kabisa tunapoongelea mfumuko wa bei kwa Watanzania wa kawaida na wananchi walio wengi tunaongelea mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi. Hicho ndicho kinachogusa Watanzania. Taarifa hii ya mpango mpaka kufikia Agosti, 2022, mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji baridi uko asilimia 7.8; it is above 3% to 5%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ya mfumuko wa bei ya chakula, nitumie hii nafasi niiombe sana Serikali, kama kuna vyakula kwenye maghala sasa hivi, waruhusu viende kwa wananchi. Hali ni mbaya sana. Hivi sasa Handeni Mjini… (Makofi)
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
T A A R I F A
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nimefurahishwa sana na mchango wa kaka yangu, Mheshimiwa Mbunge ninayemheshimu sana, lakini napenda kumpa taarifa kwamba analolizungumza, tayari Serikali ya CCM wameshaliona. Leo ninavyozungumza, Ikungi tumepokea Tani 100 za mahindi kuwauzia wananchi kwa bei ambayo itapunguza tension. Kwa hiyo, kwa kweli Serikali na Wizara ya Kilimo tunaIshukuru sana. Naomba nimpe taarifa hiyo. Sasa itakuwa ni vyema na kule kwake wapeleke. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Reuben.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawazungumzia wananchi wa Handeni ambao mpaka leo asubuhi wamenunua kilo ya sembe kwa shilingi 2000. Sasa kama Mheshimiwa Mbunge, mahindi yamefika kwake Ikungi, hilo ni jambo la kuishukuru Serikali ya CCM. Ninachosema hapa ni kwamba Mpango huu uwe wa Kitaifa na siyo wa Ikungi peke yake. Kwa hiyo, ni muhimu sana tukazingatia kilichopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Kwa hiyo, hili la chakula narudia tena, naomba Serikali kama ina chakula kwenye maghala, i- offload ili mahindi yawafikie wananchi kwa bei ambayo itakuwa ni elekezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shabaha namba nne ambayo mpango mkubwa umeuweka inasema, akiba ya fedha za kigeni kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa. Hili nalo naipongeza Serikali. Mpaka sasa wamejitahidi sana ku-mantain akiba ya fedha za Kigeni around 5.1 billion US Dollars ambazo zina uwezo wa kuagiza vitu kutoka nje monthly kwa asilimia 4.6. Kwa hiyo, hili nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kwenye ule mpango mkubwa, ni sekta binafsi kuzalisha ajira zipatazo 8,000,000, ndicho tulichokubaliana na ndicho ambacho tumekipeleka kwa wananchi. Ukifungua Ilani ya Uchaguzi ukurasa wa nane kipengele cha f(1) hadi (4) inasema, “kutengeneza ajira zisizopungua 8,000,000 katika sekta rasmi na isiyo rasmi kwa ajili ya vijana.” Wamesema, hayo yanaweza yakafikiwa endapo tutawekeza kwenye kilimo, mifugo, uvuvi, madini, maliasili, sekta za huduma na utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ajira 8,000,000, mwaka wa kwanza wa mpango umepita, na mwaka wa pili wa mpango umepita. Tafsiri yake ni nini? Ni kwamba mpaka sasa Serikali ilitakiwa iwe imezalisha ajira milioni 3,200,000. Namtaka Waziri mwenye dhamana ya huu mpango atakaposimama hapa atuambie wamezalisha ajira ngapi? Kwa sababu kama ni 8,000,000, maana yake kila mwaka ni 1,600,000. Kwa hiyo, kwa miaka miwili ambayo tayari tumeshaimaliza, ilitakiwa tuwe tumeshatengeneza ajira 3,200,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili nisiishie tu kukosoa, niwashauri pia kwamba hatuwezi kuzalisha hizi ajira ikiwa hatukufanya uwekezaji. Siongelei ule uwekezaji ambao ninyi mna mtazamo nao Serikalini; siongelei ule uwekezaji wa mtu anatoka nje na fedha anakuja kufanya jambo hapa. Naongelea uwekezaji wa kuwawezesha Watanzania kuzalisha. Tunaongelea habari ya kilimo, tunataka Serikali yetu iwawezeshe Watanzania kwenye kilimo, tuwe na millionaires na billionaires kwenye kilimo ambao ni Watanzania. Ukiongelea mifugo, tunataka tumwone tajiri mmoja Mtanzania ambaye Serikali hii imemtengeneza. Tunataka tumwone mvuvi mmoja, vivyo hivyo na kwenye madini. Kwa hiyo, lazima tuwe na uwekezaji ambao ni very strategic. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikilizeni niwaambie; ukanda wote huu wa Bahari kuanzia Dar es Salaam, shuka Tanga nyumbani pale, mpaka Mtwara na Lindi, ni aibu kwamba hatuna hata kiwanda kimoja kikubwa cha ku-process Samaki. Ni aibu! Sasa tunaongelea uchumi gani kama hilo hatuwezi kufanya? Uwekezaji ninaousema ni ule unaojikita kwenye big production chains. Mfano mzuri, tazama Kiwanda cha Cement kilivyo pale, uone chain ambayo iko involved kwenye kiwanda. Vivyo hivyo ndiyo itakuwa kwenye Kiwanda cha Samaki na maeneo mengine. Kwa hiyo, tujikite kwenye maeneo hayo.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)