Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami nitajikita katika maeneo yafuatayo: Awali ya yote pamoja na kutoa pole kwa Watanzania wenzetu, lakini inanirudisha kwenye Mpango wa suala zima la usimamizi wa maafa. Kuna kifungu cha 35 cha Sheria ya Bajeti Sura ya 439, kuanzishwa kwa Mfuko wa Dharura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuamini kwamba wenzetu katika suala zima la mipango ni kweli mengine yanakuja kwa mapenzi ya Mungu na vitu vingine vya namna hiyo. Hata hivyo ni vizuri tukajua kwamba maafa yapo na kwa misingi hiyo kama nchi tusipotengeneza mazingira maana yake inapofika sehemu Mtanzania anapoteza maisha kwa sababu tu hakuna gari ya kunyanyua kitu kizito anapata tabu. Kwa hiyo naendelea kuomba eneo hilo la usimamizi wa maafa tufike sehemu kama nchi mipango yetu tujielekeze huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa uchambuzi wa Kamati. Kamati imesema kwamba sekta zote zilizokua kwa kiasi kikubwa zimetokana na Serikali kuwekeza zaidi katika sekta hizo. Kwa mfano; Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Viwanda, Utalii na Uvuvi wa Bahari Kuu, lakini natamani kuongeza na madini. Hata hivyo, tumeambiwa Mfumuko wa bei, kupanda kwa bidhaa, mafuta ya kula, mbolea na petrol, UVIKO-19, Vita vya Urusi na Ukraine vimesababisha hilo. Hata hivyo, bado Kamati imetukumbusha kwamba haya tuyatumie kama fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napitia mtaalam mmoja wa Singapore, alikuwa anaeleza mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtaalam huyu alikuwa anasema nchi yao ya Singapore ni ndogo lakini wamewekeza katika size ya ngumi wakiutaja ubongo. Sehemu kubwa ya bajetii yao wameipeleka kwenye elimu kuhakikisha watu wanasoma. Baada ya kusoma kwa watu wao, wanaamini kwamba kwanza nchi ni ndogo, hawana eneo la kilimo, natural resources ni haba na kwa sura hiyo wameamua kuwekeza kwenye elimu ili sayansi na teknolojia yawe ni matunda na wamefika mahali ambapo umaskini wa nchi yao umegeuka kuwa ni utajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najiuliza nini? Kwa nchi kubwa kama Tanzania, hivi siku zote tunazungumza hapa na hata mimi nilishawahi kusema hapa, nchi kubwa kama hii mipango yetu hata tu uwepo wetu hapa tulipo, kijiografia, hivi mipango hiyo haituelekezi tuitumie kama ni fursa? Nchi zote zinazotuzunguka watu wanatutamani hapa tulipo, lakini niseme tu hata katika ardhi, yote yanayozungumzwa whether ni njaa ama ni nini bila matumizi bora ya ardhi hatutoacha kushuhudia ugomvi wa wakulima, wafugaji na watu wengine. Mipango yetu inasemaje katika maeneo hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kurudia kama siku nyingine unavyoniambia Mr. Kapufi declare wewe ni nani? Mimi ni mchimbaji mdogo wa madini. Naomba nijikite katika eneo hilo la uchimbaji mdogo wa madini. Amezungumza Mheshimiwa mmoja hapa akitaja nchi kwa upana wake na idadi ya madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda sijui tunapata tabu, mtu mmoja aliniambia ukienda sehemu halafu ukamwagiwa vitu vingi, kwa wakati mmoja unashindwa kujua uchukue hiki au hiki au hiki. Sasa nchi nzuri Tanzania madini yapo ya kutosha na tumeambiwa idadi hiyo nyingine, nataka nijikite tu kwenye madini ya dhahabu. Leo mipango yetu niseme angalau kwenye kilimo Serikali inatoa ruzuku, vipi kwa wachimbaji hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie hivi, amini usiamini dhahabu pekee inaweza ikafanya vitu vingine vikasubiri kwenye nchi hii. Pia achilia madini hayo mengine, nina mfano hai, kama kweli tumewawezesha vizuri watu wa GST, kwa maana ya tafiti zao, mtu unajua kabisa kwamba mashapo yaliyopo hapa, kwa maana kwamba, katika ekari moja pale chini ya ardhi labda huyu mtu ana kilo tatu, nne, tano au sita za dhahabu. Sasa utafiti utuelekeze tunaitoaje dhahabu hapo chini ili igeuke kuwa fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sura hiyo hatutawafanya wachimbaji waonekana wanashiriki ushirikina, kwa sababu tafiti zinaonyesha kwamba hapa chini kuna madini kiasi hicho na labda ni three grams per ton or five grams per ton, tengeneza mazingira tani kadhaa ziweze kuzalisha kiasi kadhaa cha kilo za dhahabu. Kwa sura hiyo, kwa kufanya kisayansi kama hivyo, tunaitoa nchi hii na itafika mbali. Pia niendelee kusema, bado naamini hatujafanya vya kutosha na wenzetu wa fedha mipango yetu iende huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingine zao lao ni moja uvuvi tu na wako mbali. Sasa Tanzania ukija kwenye uvuvi tuko vizuri, kwenye madini tuko vizuri na leo sioni sababu ya nchi kulalamika kuhusu kilimo. Niliwahi kusema hapa na Mheshimiwa Kingu akaniunga mkono, nilisema je, tuna mpango wa mtandao wa maji wa nchi hii? Leo ukitengeneza mtandao wa maji hauzungumzii njaa, hauzungumzii sijui shida ya maji. Je, hatujikiti huko jamani? Nilizungumza ndani ya Bunge hili, nchi kubwa kama China unaunganishwa kwa mtandao wa maji kwa vyanzo vyao tu, labda kutoka kaskazini kwenda kusini, kutoka mashariki kwenda magharibi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la maji tu, mipango ikijielekeza na kwa kutumia vyanzo vyetu tulivyonavyo, tuiweke kwenye mipango, hapa naomba pia twende mbali zaidi. Nimeona tumeambiwa kuhusu ununuzi wa vifaa vya kuchimba mabwawa na kuchimba visima. Bado Serikali wasiache kwenda kwenye tafiti. Sehemu nyingine duniani baadhi ya miji imeanza kuzama kutokana na uchimbaji wa maji haya ya visima. Kwa hiyo ningeweza kuishauri nchi yangu, sikatai, visima tuchimbe lakini tusisahau tafiti ili kuepuka hilo. Hata hivyo sehemu kubwa ya kuweza kupata maji ni kukinga maji ya mvua yanayopotea kwenda baharini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwa maana ya kufungamanisha fursa, leo unaweza ukakinga maji hayo na ukafanya shughuli zifuatazo: Utalima, kwa maana ya kumwagilia; Utafuga kwa maana ya samaki hapo; na Utafanya utalii kwa sababu ndani ya maji hayo hayo, watu wanaweza kufanya utalii ikiwemo man-made lakes and whatever, watu wanafanya mpaka utalii. Kwa hiyo tuyaangalie hayo…

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba hata nchi zinazoendelea wanatumia maji ya bahari, wanaya-purify na wanayarudisha kuyatumia. Kwa hiyo hata nchi yetu ianze kufikiri namna ambavyo tunaweza kwenda kwenye utaratibu wa kutumia maji ya bahari kwa sababu hata kina cha bahari kinaongezeka.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat wana-purify au wanafanya desalination?

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mimi ni Mswahili, naomba nitumie Kiswahili, wanayaondoa chumvi, wanayasafisha, wanayaondoa chumvi, yanatumika.

MWENYEKITI: Kwa hiyo ni desalination. Haya Mheshimiwa Kapufi.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea taarifa, lakini nimsaidie tu dada yangu hatujafika mahali pa kutumia maji ya bahari kwa vyanzo tulivyonavyo nchi hii. Maziwa yote tuliyonayo nenda Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria, ziwa Nyasa, mito mikubwa mpaka tukaikute Bahari ya Hindi ni baadaye sana. Kwa hiyo sasa hivi nchi ijielekeze kwenye vyanzo vyote vikubwa tulivyonavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, nafahamu kila mmoja anasema kilimo ni uti wa mgongo. Siamini sana kwa watu wengi kushiriki kilimo halafu ni kilimo kisicho na tija. Bora wachache wakafanye kilimo walishe wengine, wengine wakavue, wengine wakachimbe na kadhalika. Nchi za wenzetu percent kidogo ya watu wanaoshiriki kilimo wanalisha the rest of the world. Sasa sisi asilimia kubwa lakini hatujilishi hata wenyewe, kuna kitu cha kufanya hapo, lazima turudi tupaangalie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sio muumini wa nchi nzima kulima korosho au kulima sijui kama nini, mimi huko sipo. Tugawe kanda za kilimo, haiwezekani wote tukawe wakulima wa parachichi au korosho. Kwa hiyo mipango yetu nayo ijielekeze huko isije ikawa Mtwara walipata bei nzuri ya korosho, basi nchi nzima tunataka tulime korosho. Ikawa sijui Rungwe walipata bei nzuri ya parachichi, wote tunataka, hapana. Tugawane Kanda za kilimo, lakini kila watu wafanye kwa tafiti na mambo mengine ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado narudia kusema, kwa kupitia madini peke yake, mipango ijielekeze huko na kama leo kwa mfano tunatoa ruzuku za kilimo, wachimbaji hawa wadogo wapewe ruzuku. Naamini kwa kufanya hivyo, Marehemu Rais John Magufuli alituita wachimbaji wote, akasema nataka mniambie mnafanyaje kuitoa nchi hapa ilipo kwa kupitia madini? Hata hivyo, watu waliuza mawazo yake, kwa hiyo hata kwa mipango yetu hebu tuwashirikishe hawa, kwa sababu kuna wakati ukisikia kuna gold rush, mfumuko wa dhahabu somewhere, ni kazi ya wachimbaji wadogo. Sasa kama mchimbaji mdogo ndiye anaweza kugundua dhahabu shambani, anagundua akiwa anachimba kisima, watafiti wetu wako wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende mbali zaidi, kwa kupitia taarifa zile, kwa mfano kama ni GST wangefanya vizuri, taarifa ya kitafiti isimame, ni fedha. Leo kuna watu wengine kwa kuuza tu taarifa za kitafiti wanasababisha watu wengine wawe matajiri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.