Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Chambani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mchana huu. Aidha, ninakushukuru na wewe kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, wachangiaji wa leo ni wakali sana, kule kwetu tunasema moto umepata magogo sijui kwenye chanja utawaka! Wapemba wana methali inasema; “ukilima patosha utavuna pashakwisha” na ukilima usipo palilia ukivuna utalia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru mchangiaji aliyemaliza amemuonyesha chanzo kimoja cha mapato ambacho Mheshimiwa Waziri akikitumia anaweza kuongeza pato katika Wizara yake. Sasa na mimi nataka nimuonyeshe chanzo ambacho kama atakitumia basi Jeshi letu litakuwa ni chanzo kikubwa cha mapato hata pengine kuliko utalii au vyanzo vingine vya mapato katika nchi yetu kwenye Pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, Jeshi letu limesifiwa sana na linasifiwa sana na ndiyo ukweli kwa utendaji kazi na weledi na nidhamu ya hali ya juu ndani ya nchi yetu na nje ya nchi yetu, ni ukweli kwamba Jeshi letu linashiriki katika UN - Mission nyingi. Tunaomba leo, Mheshimiwa Waziri utakapo kuja hapa utuambie Jeshi letu linashiriki katika mission nyingi za UN; je, ni kiasi gani cha fedha tunazopata kutoka katika mission hizo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Mission hizo kuna dry lease ambazo tunapeleka wanajeshi na logistic nyingine zinafanywa na UN, lakini wet lease ambazo tunapeleka wanajeshi na vifaa, kila kifaa kinalipiwa kwa dola. Kwa mfano gari moja tu linalipiwa kati ya dola 500 hadi dola 800, na inalipwa katika vipindi vya miezi mitatu, mitatu. Tumeshiriki katika UN Mission nyingi, utuambie Mheshimiwa Waziri ni kiasi gani cha fedha za kigeni ambazo Jeshi letu linapata katika mission hizo au pato letu sisi ni yale majeneza tu yanayokuja na maiti hapa tunazika? (Makofo)
Mheshimiwa Spika, hapa lazima tujipange, dunia ya leo, missions hizi za UN ni mtaji. Nchi kama Bagladesh, India, South Africa, Ukraine, wamewekeza sana katika UN Missions majeshi yao na silaha, kwa sababu zinaingiza pato kubwa katika Jeshi la Wananchi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri tunaiomba Serikali sasa, nilisema wakati nachangia Wizara ya Kilimo hapa kwamba Serikali haina vision, tunaiomba Serikali sasa ikae, ipange hapa ili Jeshi letu lisiwe linaenda kule kupigana vita tu, lakini liwe linaenda kule linapigana vita kwa faida ya wao wenyewe, lakini na kwa faida ya nchi yetu na Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali lazima ipange tujuwe ni vifaa gani vinatakiwa vinunuliwe viwepo pale na katika ubora wake ili lile pato katika nchi yetu liwe ni pato kubwa na tusiwe tunapeleka askari wetu na kupoteza maisha tu kule! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kweli inasikitisha, Serikali hii ya CCM kwamba hata jeshi mnalipatia asilimia ndogo ya bajeti ambayo inapitishwa. Jeshi ambalo linalinda mipaka ya nchi yetu, Jeshi ambalo limekomboa nchi zote hizi za Kusini, Jeshi ambalo ni waaminifu, ni waadilifu, ni wasikivu.
Mheshimiwa Spika, Jeshi ambalo linafanya kazi katika mazingira magumu, yakitokea maafa sasa hivi hapa daraja limekatika ni wao huko, mvua, jua huko, leo katika bajeti yao wanaambiwa kwamba wanapata asilimia 18 katika bajeti ya maendeleo, hivi jamani kweli!
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika naendelea, kama kuna Mbunge hajaridhika anione kwa wakati wake nimsomeshe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapopeleka Wanajeshi wetu katika mission hizi kuna Chapter Seven kuna Chapter Six, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie namna gani askari wetu wanalipwa wanapoenda katika Chapter Seven na wanapoenda katika Chapter Six. Atuambie ni namna gani wanalipwa. Kwa sababu Chapter Seven ni ulinzi wa amani, lakini Chapter Six ni vita kamili. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri utupe ufafanuzi.
Mheshimiwa Spika, lakini pia utuambie Mheshimiwa Waziri kwa mfano, kama hawa waliokwenda DRC hivi karibuni tu, tumepoteza askari wawili muhumu sana! Luteni Rajabu na Meja Mshindo ni askari ambao ni muhimu sana katika jeshi letu, wamepotea katika kuisambaratisha M23 wamefanikiwa; je, waliporudi askari wale ambao walirudi na roho zao, Serikali imewathamini vipi? Wale ambao wamepoteza maisha katika vita ile ya kuisambaratisha M23 hadi leo ni vita ya kawaida tu pale na wao familia zao zitaenziwa vipi?
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iwaangalie askari wetu hawa angalau wawe na bima ya afya, wawe na bima ya ajali, wawe wana bima ya kazi hatarishi zile wanazo zifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni aibu leo kusikia askari mstaafu tena pengine alikuwa na cheo kikubwa anamaliza jeshi anakuwa fundi baiskeli au mziba pancha mtaani au mlinzi, ni vitu vya kusikitisha kwa kweli! Kwa hiyo, angalau basi wapatiwe hizi bima za afya askari wote wawe na bima za afya, wawe na uhakika angalau na maisha yao.
Mheshimiwa Spika, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa, katika ukurasa wa 24 wa hotuba yake amesema miongoni mwa kazi walizozifanya ni kutoa mafunzo katika jeshi, lakini pia na Jeshi la Akiba. Kwa hiyo atuambie hilo Jeshi la Akiba ambao wamepata mafunzo ni askari wangapi na mafunzo ya aina gani ili tuweze kujua hawa askari wetu wa akiba wamepata mafunzo ya aina gani.
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema kama hatutowathamini wanajeshi wetu na kama tutaendelea na usanii huu wa kwamba tunapitisha bajeti hapa katika Bunge, halafu bajeti zile haziendi hata kwa Jeshi, tunajipalia makaa wenyewe! Tunajipalia makaa sisi wenyewe pamoja na uaminifu na uadilifu waliyonao, lakini hawa ni wanadamu kama wanadamu wengine. Kwa nini bajeti ya Bunge ikamilike, kwa nini bajeti ya Serikali, Mawaziri na Maafisa wengine wapewe kwa ukamilifu, lakini bajeti ya Jeshi iende robo, kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata hawa wanaofanya kazi hizi tunashindwa kuwakamilishia bajeti! Ninaiomba Serikali sasa, tumepita katika Awamu Nne tumebabaisha sana, hii Awamu ya Tano ya hapa kazi tu na mmesema kwamba Awamu ya Tano hii ni nzuri sana, sisi tuna imani hiyo kwamba inaweza ikawa nzuri, basi mkae kama Serikali, mpange ili tuone Serikali inaendeshwaje.
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana.