Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika mpango ulioko mbele yetu. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wetu wa Fedha na Mipango kwa namna ambavyo amejitahidi sana kuwasilisha mpango wake kama maandalizi ya bajeti ya mwaka kesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuzungumzia hali halisi katika mazingira ya kawaida ya wananchi. Maana mimi nafika mahali najiuliza, yawezekana ni mimi tu kule Musoma au ni nchi nzima ndivyo ilivyo? Hali halisi ya maisha sasa hivi ni ngumu, kwa sababu vitu vimepanda sana bei. Nimeona hapa katika mpango Mheshimiwa Waziri anasema mfumuko wa bei siyo mkubwa, nikashindwa kuelewa kwamba yawezekana vigezo tunavyoviangalia siyo vigezo vinavyogusa hali halisi ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu mfano hai; leo ukiangalia bei ya chakula, nakumbuka mwaka 2021 mwezi Julai, mchele kwa pale Musoma ulikuwa unauzwa shilingi 1,100; lakini leo hivi tunavyozungumza, bei ya mchele ni shilingi 2,500. Hali hii ikiendelea kuja kufika mwezi Desemba, ni ukweli usiopingika kwamba utakuwa unauzwa siyo chini ya shilingi 3,000. Sasa kama bei ya chakula kama mchele ambao ni wa lazima, unaweza ukapanda mara tatu, halafu unawezaje kusema kwamba mfumuko wa bei siyo mkubwa! Unapozungumza habari ya mahindi Musoma mwaka 2021, tulikuwa tunanunua shilingi 50,000, leo hivi tunavyozungumza gunia moja la mahindi ni shilingi 120,000. Bei imepanda zaidi ya mara mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa namna yoyote ile, ni vizuri tuangalie kwamba hali halisi ya uchumi wa watu wetu wanapolia, wana haki ya kulia, kwa sababu kwanza fedha zenyewe hazipatikani, lakini bei yake ndiyo hiyo tu kwamba maisha yameendelea kuwa magumu kulingana na mfumuko wa bei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, kwanza naishukuru Serikali kwa maana ya Waziri wa Kilimo, wiki hii nimwomba chakula na ametupatia kiasi cha kutosha ambacho kiko njiani kinaenda Musoma kwa ajili ya kwenda kupunguza yale makali ya bei ya vyakula. Ombi langu ni kwamba basi wajitahidi hicho chakula kiendelee kwenda mara kwa mara, kwa sababu tofauti na hapo, naamini yawezekana chakula kitauzwa mpaka shilingi 150,000 kwa gunia na ukilinganisha na kipato cha watu wetu, hali ya maisha itaendelea kuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu sasa hivi tunachangia mpango kwamba nini kifanyike katika kuhakikisha kwamba angalau kwenye bajeti ya mwaka kesho tunaendelea kuboresha; kati ya maeneo ambayo tunadhani tunahitaji kuwekeza fedha sana, moja ni eneo la kilimo. Tunashukuru kwamba Serikali imeongeza kwenye bajeti iliyopita, lakini iendelee kuongeza zaidi. Kwa sababu tukiongeza fedha kwenye kilimo, kwanza tafasiri yake ni kwamba itawafanya wale watu wetu kule kwa maana ya Serikali iendelee kutengeneza miundombinu ya umwagiliaji. Maana hata kama tungeweka fedha kwenye kilimo halafu tukajikuta kwamba hatutengenezi miundombinu ya umwagiliaji na hali ya ukame ambayo inalisumbua Taifa letu, wakati mwingine tutajikuta kwamba fedha zimeongezeka, watu wamelima na matokeo yake bado shida inabaki pale pale kwa sababu ya ukosefu wa mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, itoshe tu kusema, katika nchi yetu kwa namna ilivyokaa, imezungukwa na nchi nyingi ambazo vile vile zinaitegemea Tanzania ili iweze kuilisha. Sasa tunadhani nini kifanyike katika mpango ujao? Hebu tujaribu kuwa na aina mbili za mazao; mazao ya chakula na mazao ya biashara. Kwa sababu leo ninavyojua, kama sisi watu wa Mara kwa mfano, mchele wetu mwingi unaliwa na watu wa Kenya na Uganda ambapo kwa kusema kweli wanatusaidia katika kutupatia fedha, lakini sasa, hata kama tunauza kule chakula, lazima tuwe na akiba yetu ya kutufanya tuendelee ku-survive.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ungeniuliza ushauri wangu ningesema, kila mkoa uandae mazao yao ya chakula na mazao ya biashara. Kwenye yale mazao ya chakula hebu tujaribu kuwa strict tusiyauze nje. Mfano, kwa pale Mara, leo tukianzisha mfano, kilimo cha mihogo ambacho mpaka leo tunalima mihogo na tukawa strict kwamba mihogo tusii-export nje na Serikali ikaweka nguvu pale katika kusaidia wale wakulima wa mihogo kama ambavyo inasaidia kwenye maeneo mengineā¦
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Fedha, umesikia mihogo! (Kicheko/Makofi)
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafasiri yake ni kwamba sisi Mara tutajua kabisa kwamba zao letu la chakula, tunalima mihogo na mtama; ambapo ukichanganya mhogo na mtama ni chakula safi kabisa kuliko hata mahindi. Kwa hiyo, kwa sababu wenzetu wa Kenya wanahitaji mahindi, sisi Mara tutalima mahindi, tutawasafirishia, tutalima mpunga kwa maana ya mchele tutawasafirishia. Kwa hiyo, tutamaliza sasa katika kuondoa tatizo. Kumbe sasa tukishakuwa na huo utaratibu wa zao la chakula na zao la biashara, basi itatusaidia sana kuhakikisha kwamba tunaendelea ku- survive na mfumuko wa bei unaendelea kushuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine lililopo ambalo ni kubwa sana ni tatizo la ajira. Yaani ukiangalia kadri vijana wanaozalishwa kuingia kwenye soko la ajira, lakini wakati huo hakuna ajira, siyo mjini, wala vijijini. Hata zile ajira za mjini kwa sisi watu wa mjini ni zile biashara ndogo ndogo. Ukizungumza biashara ndogo ndogo tunafika mahali tunasema Wamachinga watengewe maeneo. Kumbuka kwamba wale ni watu wenye mitaji midogo, lakini tunawatenga mbali na soko, mbali na watu. Matokeo yake ni kwamba tunapofanya hivyo, ndiyo maana kila leo wanalazimisha kurudi mjini. Kwa hiyo, wanakukwa ni kama wakimbizi katika nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani katika mpango huu ni vizuri vile vile tukaangalia katika yale maeneo ambayo yana mikusanyiko ya watu, hata kama kuna taasisi ya Kiserikali pale tuone namna ya wao kupata eneo ili waweze kufanya biashara. Tofauti na hapo, maana yake ni kwamba maisha yanaendelea kuwa magumu na Wamachinga hawawezi kufanya biashara, lakini hata kule kijijini ambako wangeweza kwenda, bado nako hawataweza kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo lingine ambalo naishukuru kwamba Serikali imeanza kuliona, lakini hebu iongeze bidii ni kwenye eneo la uvuvi. Tunakubali kwamba angalau kwa sasa hivi, Serikali imeweka mpango wa kukopesha wale wavuvi wadogo wadogo. Tunadhani watu wengi suala la elimu bado linawasumbua sana na vile vile namna ya kuweza kuipata mikopo. Kwa hiyo, ombi langu, tuweke katika mpango namna ya kuendelea kuelimisha wananchi wetu ili waone namna bora zaidi ya kuweza kupata mikopo. Pia baadhi ya maeneo Serikali inapaswa iwekeze. Mfano, leo unapozungumza pale kwangu mjini, eneo kama la Makoko, ni eneo ambalo ni zuri sana kwa biashara ya dagaa, utawakuta akina mama wamebeba mabeseni wanaenda kuanika halafu wanauza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbe Serikali ikiwekeza pale, wale akina mama wakaweza kuwa wanakaushiwa dagaa zao vizuri, tafsiri yake ni kwamba wale wavuvi watawekeza kwenye vifaa vizuri vya kuvulia. Hata akina mama ambao wanahangaika na mabeseni kichwani, wataweza kukausha dagaa zao pale pale na hatimaye watauza katika maeneo yote ambayo tunadhani yanahitaji hao dagaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakushukuru sana kwa nafasi hii.