Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Issa Ally Mchungahela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kunipa nafasi hii ya kupumua. Nakushukuru wewe pia kwa kunipa nafasi ya kuchangia mchango wa mapendekezo na bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kuwa, pato la Tanzania kwa maana ya pato la nchi limekuwa likiongezeka kwa wastani wa asilimia 4.9, wastani ambao ni pungufu kwa 1% ya wastani ule tuliokuwa tumeukusudia. Ongezeko hili limechangiwa na sekta mbalimbali. Sekta zilizosaidia kuchangia ongezeko hili ni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Sanaa na Burudani imechangia kwa asilimia 19.4; Sekta ya Umeme imechangia asilimia10; Sekta ya Madini imechangia asilimia 9.6; halikadhalika Sekta ya Habari na Mawasiliano imechangia kwa asilimia 9.1. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mchango huo mzuri kwenye hizo sekta, bado kuna sekta muhimu sana za kiuchumi ambazo zenyewe zinategemewa kuwa ndiyo nyenzo za kufanya pato la Mtanzania au pato la nchi likue kwa haraka, lakini sekta hizi hazikukua katika kiwango kinachoridhisa. Sekta hizi zimechangia mchango kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Elimu ni asilimia 5.1; Sekta ya Viwanda imechangia kwa asilimia 4.8; halikadhalika Sekta ya Kilimo imechangia kwa asilimia 3.9; Sekta ya Biashara kwa asilimia 3.5; na Sekta ya Fedha na Bima imechangia kwa asilimia 4.9. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hizi ni muhimu sana kama nilivyosema kwa ajili ya ukuaji wa pato la Taifa. Kama kungekuwa na jitihada za kuhakikisha kwamba sekta hizi nilizozitaja hapo ambazo ni muhimu katika ukuaji wa pato la Taifa zingeangaliwa au kupewa attention ya kutosha, bila shaka hali ya uchumi ingekuwa imekua zaidi ya hali iliyoko sasa.

Mheshimiwa Spika, ili tuendelee tunahitaji sekta hizi zikue zaidi kiasi cha kuwezesha wastani mzima wa pato la Taifa kukua kwa angalau 8% na kuendelea. Hivyo ndiyo hali halisi ilivyojitokeza katika nchi nyingi sana zilizoendelea au zinazoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufanikiwa au kutokufanikiwa kunatokana na sababu, na sababu hii ni jinsi tafsiri iliyopatikana kwenye sekta hizi nilizozitaja kwenye mpango ule: Je, mpango ule umetafsiri nini katika sekta hizi? Kwamba inajua kitu gani kuhusiana na hizi sekta? Kwa mfano, ukuaji wa elimu, tafsiri sahihi ya ukuaji wa elimu, lazima iwe kama ifuatavyo: Kwamba nchi yenye ukuaji wa elimu basi itakuwa na rasilimali watu bora ya kutosha kwa ajili ya uzalishaji; pia itakuwa na watu wenye fikra pevu; na halikadhalika ina watu wastaarabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri ya ukuaji wa viwanda ni nini hasa? Soko la uzalishaji linaonekana hapo katika tafsiri ya ukuaji wa viwanda. Ukuaji wa viwanda pia unatafsiriwa na ukuaji wa vitu vilivyozalishwa kama vile madini, mazao ya kilimo, mazao ya misitu, mazao ya uchumi, mazao ya uchumi wa bluu na mazao ya mifugo. Pia sekta hii ukuaji wake unatafsiri kodi iliyokuwa rafiki kwa maana kama kodi ni rafiki, inaweza ikaonekana waziwazi katika ukuaji wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa biashara pia unachangia sana katika kuenenda, yaani kuonesha jinsi gani uchumi unatakiwa uwe. Tafsiri sahihi ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa biashara pia unachangia sana katika kuenenda, yaani kuonesha jinsi gani uchumi unatakiwa uwe. Hapa tafsiri sahihi ni nini? Tafsiri inaonyesha kwamba, kama biashara imekuwa hapa kuna suala la ukuaji wa uwekezaji. Hali kadhalika, kuna ukuaji wa pato la Serikali kupitia vyanzo vya kodi ikiwa ni pamoja na leseni pamoja na tozo. Vilevile pato la mtu mmoja mmoja linakuwa linajionyesha hapa, hii ndio tafsiri inayopatikana katika ukuaji wa biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna uwezo wa mtu mmoja mmoja katika kufanya manunuzi yaani purchasing power, inaonekana hapa. Halikadhalika, ongezeko la bidhaa bora, ambazo zenye kuweza kuleta ushindani, mnunuzi ana uwezo wa kuchagua bidhaa anayojisikia. Haya yote yanatokana na ukuaji uliokuwa bora wa biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa fedha na bima tafsiri yake ni nini pia? Tafsiri yake ni kwamba, kuna ongezeko kubwa la mtaji, lakini kuna kuimarika kwa biashara pia na uwekezaji. Vilevile inaonesha hapa kuna mikopo shindani ambapo benki zinashindana kuweka riba ya chini kabisa ya mkopo, kiasi kwamba mlaji au mtumiaji wa mkopo ule anachagua wapi aende akachukue. Hali hii inaleta athari kubwa katika pale ambapo yeye atawekeza, halikadhalika ni kuwezesha uchumi wote wa nchi hii kwa ujumla au nchi husika kukua kwa kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa kilimo na wenyewe una athari zake ambazo una tafsiri sahihi, ambazo tafsiri hizi zinatakiwa pia zionekane wakati tunatengeneza plan au tuna-plan bajeti. Ongezeko la uzalishaji linaonekana pale, pia bei nzuri ya bidhaa zile zilizozalishwa. Pia kuna kinga ya bidhaa na bei, hapa kinga ni nini? Maana yake kwamba kile kilichozalishwa, kama kunatokea changamoto ya uzalishaji, kwa mfano, mvua, maana yake changamoto hii inaweza ikafidiwa kwa ile kinga iliyowekwa pale kwa maana ya bima. Vile vile hata kama bei itashuka, pia bei ile itafidiwa na bima ile, kwa maana hiyo kinga hii itakuwa imesaidia. Hizi ndio tafsiri za msingi kabisa ambazo zinatakiwa zi-reflect katika mipango yetu. Kama mpango wowote ule hauwezi ku- reflect tafsiri ya mambo haya basi ni kiasi kidogo sana tutaona kuna ukuaji wa pato la mtu mmoja mmoja, lakini na pato la Taifa ukuaji wake utakuwa mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojaribu kuanza kusema kule mwanzo, tafsiri hizi lazima zionekane katika mpango na mpango ambao utazalisha bajeti. Kwa sababu hiyo Mpango lazima uzungumze waziwazi products zote zile zinazotengenezwa soko lake liko wapi. Kama mpango hauonyeshi soko basi ni kama vile mpango huu umefeli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta mbalimbali za habari na mawasiliano ambazo zimeonyeshwa pale katika zile sekta zilizochangia maendeleo au ukuaji wa pato la Taifa, zilionyesha kama kwamba zimekua kwa kiasi kikubwa. Pamoja na ukuaji ule kwa sababu Sekta hii ya Habari na Mawasiliano ni sekta unganishi tu, ni sekta ambayo haiwezi kutoa athari yake moja kwa moja katika pato, kwa maana vile vyanzo ambavyo ni muhimu nilivyovitaja vinaunganishwa na sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumeonekana pia ongezeko la madini, lakini athari ya madini haiwezi kujionyesha moja kwa moja kutokana na hali ya sasa ya uchumi ulivyo, kwa sababu madini haya tunauza ghafi. Kama tungekuwa tumeyauza yakishakuwa processed bila shaka hali ya uchumi wa sasa hivi au ongezeko la pato la Taifa ingekuwa ni kubwa kuliko hali ilivyo sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojaribu kuzungumza pale, mpango huu wa sasa hivi kwa mfano, umeonesha changamoto nyingi. Changamoto mojawapo ni kutokuonesha masoko ya product ambazo zinatokana na uzalishaji. Mfano ni uzalishaji wa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, kengele ya pili.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)