Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na mimi kupata nafasi ya kuweza kuchangia katika mpango, lengo langu si kuyarudia yale ambayo yametoka kusemwa na wenzangu lakini mengi yameshagusiwa kuhusiana na maeneo ya kimkakati ambayo Bunge linashauri Serikali iende kuyaangalia ambayo yatasaidia kukuza uchumi wetu sambamba na hilo litakwenda kuzalisha ajira mpya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mfumuko wa bei nalo limegusiwa ni jambo ambalo linawaathiri wananchi wengi, ukizingatia kwamba sasa hivi tuna tatizo la ukame bei ya vyakula itaenda kupanda mara dufu, mimi siyo mchumi lakini naiona hii hali ambayo tunakwenda nayo tusipoweka mikakati thabiti ni jambo ambalo litatuletea shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijielekeza nirudi tena katika mpango. Nimesikiliza sana michango ya Waheshimiwa Wabunge wengi, kuna mambo ambayo na mimi nayaona kuna changamoto. Jambo la kwanza katika mipango hii ambayo tunaileta Bungeni kila mwaka, kunakosekana muunganiko mpango wa mwaka jana hakuna muunganiko na mpango wa mwaka huu na mpango ambao tunaumaliza sasa hivi hauna muunganiko na ule ambao tumepita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunaona kwamba hakuna mwendelezo. Vilevile jambo la tatu ambalo naliona ni kwamba tunatengeza mpango ambao siyo shirikishi na ukiangalia mikakati ya sekta mbalimbali ukija ukiangalia hapa katika mpango huu huwezi kuuona huo muunganiko. Kwa hiyo, inaonekana kwamba Wizara ya Fedha ipo kivyake, Wizara nyingine ambazo za kisekta nazo ziko kivyake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka nitoe ushauri na mchango wangu utakuwa mfupi sana. Jambo la kwanza ambalo naliona nataka kuishauri Serikali ni kuirudisha Tume ya Mipango. Wizara ya Fedha ibaki kuwa Wizara ya Fedha isimamie Sera ya Fedha, isimamie ukusanyaji wa fedha, isimamie matumizi ya fedha. Sasa hivi ukiingalia ile iliyokuwa Tume ya Mipango imemezwa ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango na majukumu yake yamefinywafinywa sana huioni kujitokeza. Kwa hiyo, nashauri ile Tume ya Mipango irudi iwe chini ya Ofisi ya Mheshimiwa Rais na kazi iwe sasa kufanya yale ambayo nimeyaainisha kwamba itusaidie kukaa na kuangalia mpango mzima wa maendeleo wa muda mfupi, wa muda wa kati na muda mrefu, kutengeneza mwelekeo, kutengeneza mwendelezo vilevile na kuainisha vipaumbele ambavyo sasa tutakuwa tunakaa tunaviongelea ambavyo vitakuwa na tija katika maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ushauri wangu wa pili. Tulianza lakini hapo katikati tukaivunja kitu kinaitwa Presidential Delivery Bureau ama Presidential Delivery Unity tunahitaji hiki chombo. Sababu ambazo nazisema kwa nini tunakihitaji hiki chombo ni kwa sababu hiki kitatusaidia katika masuala ya uratibu ambayo ni changamoto tunaiona. Kwa sababu ukiangalia sasa hivi kila sekta inaonekana kama ina-operate kivyake vyake, sasa tukiwa na chombo kama hiki, kitatusaidia katika hii miradi ya kimkakati kuwa na uratibu mzuri, itafanya tathmini na ufuatiliaji wa hii miradi mikubwa ambayo tunaitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauiri wangu wa mwisho. Hii inatuhusu sisi kama Wabunge, Kamati yetu ya Bajeti inafanya kazi nzuri sana, lakini inaitwa Kamati ya Bajeti. Mimi nilitaka tu na Mheshimiwa Spika yupo hapa ninaomba na kushauri tupanue wigo wa Kamati hii tuuite Kamati ya Fedha Mipango na Ufuatiliaji, ili hii sasa ikae kuangalia ule mtiriko mzima tangia tunaweka mipango, fedha gani tunazibajeti? zinakuwa disbursed kwa kiasi gani? Na hii ndiyo changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatengeneza bajeti hapa lakini fedha ambayo inaenda kutolewa mwisho wa siku hailingani na kile ambacho tulikuwa tumekibajeti. Sasa tukiwa na Kamati ya Bunge ambayo itakuwa inafanya ufuatiliaji pamoja na zile Kamati zetu za kisekta itatusaidia sana. Kwa hiyo mimi ushauri wangu ni kuwa, hii Kamati yetu ya Bunge ya Bajeti iwe ni Kamati ya Fedha, Mipango na Ufuatiliaji, tukienda kwa staili hii itatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho nimalizie kuhusu Dar-es-Salaam. Ukiangalia ina asilimia Nane ya wakazi wa Tanzania nzima, lakini uchimi wa Tanzania hii asilimia zaidi ya themanini unatoka Dar-es-Salaam. Sambamba na hilo ukiangalia wingi wa magari yako Dar- es-Salaam, ukiangalia miundombinu ya Dar-es-Salaam hailingani na uwekezaji uliopo pale. Vilevile ukiangalia Dar es Salaam tunafanya uwekezaji mkubwa wa reli ya SGR, tunafanya upanuzi wa Bandari hivyo unaendelea, tunaanza kufikiria vilevile kuwa na Bandari ya Bagamoyo, lakini ili uweze kufika Bagamoyo lazima upite Dar-es- Salaam ili uweze kufikia reli ya SGR lazima ufike Dar-es- salaam. Kwa hiyo, pamoja na hili Waziri Mwigulu Nchemba analijua, sisi kwetu wana Dar-es-Salaam wa DMDP ni mradi wa kimkakati na ni mradi muhimu sana kwa hiyo pamoja na zile barabara walizokuwa wanazisema lakini sisi kama Dar-es-Salaam tunazihitaji hizo barabara. Tunazihitaji hizo barabara jana, tulikuwa tunazihitaji leo na tunahitaji tufike kesho katika msingi wa kupata hizo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.