Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Igalula
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia mpango uliowasilishwa na Waziri wa Fedha. Nami niungane na Wabunge wenzangu waliotangulia kuchangia, kwanza kwa kuipongeza Serikali yetu, Serikali ya Rais wetu, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhangaika huku na kule kuhakikisha Watanzania na sisi kama wawakilishi wa wananchi tunatekeleza yale aliyokuwa amedhamiria kwa kipindi chake cha miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tunazungumzia mpango wa Serikali ambao utatusababisha kutengeneza Bajeti Kuu ya mwaka 2023/2024; lakini pia tumekuwa na mpango wa miaka mitano. Waziri wa Fedha alishawasilisha mpango wa miaka mitano, nini Serikali itafanya kwa kipindi cha miaka mitano, kwa hiyo ndiyo maana tunaivunja hii mipango tunaiweka kwa mwaka mmoja mmoja ili iweze kutekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wamezungumza hapa kuhusu Serikali kuwa na mipango mingi bila utekelezaji, lakini tumekuwa na mipango ya muda mfupi. Tunatengeneza mpango wa miaka mitano, lakini baada ya miaka mitano ule mradi unakuwa hauna tija tena kwa jamii. Ndicho alichokuwa anakisema Mheshimiwa Shabiby. Tulitengeneza mpango wa kutengeneza ICD nje ya Dar es Salaam kilometa 40 ya Kwala pale, lakini sasa hivi ile ICD inaonesha haiwezi kuwa msaada kwa Watanzania ilhali wataalamu wetu walisema itakuwa msaada, na tayari shilingi bilioni 30 imeshakwenda pale. Kwa hiyo tunapokuja kujadili mipango basi iwe yenye tija na inakuwa msaada kwa muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge walishasema, tunapo-design miradi basi tuwe tunaangalia na muda wa mradi utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mingapi. Hauwezi kwenda ku-design mradi wa trilioni za fedha halafu life span yake inaishia miaka 10; hiyo tunakuwa tunakuwa tunamaliza fedha za wananchi na walipa kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishashauri hapa tukasema na kama Mbunge mmoja alisema hapa kama tungechora vizuri mradi wa Ziwa Victoria, tukatengeneza design ya kuleta maji safi na maji ambayo yatakuja kutumika kwenye kilimo nchi hii leo ingefungua fursa ya kilimo; lakini wataalamu wetu hawakulifikiria hilo wakafikiria kwenda kuwatibu wananchi halafu wakasahau wananchi wanahitaji kula. Na ndiyo maana wanasema kula ni lazima kuoga hiyari, hawakuliangalia hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kuwa tumeshakosea, tunashauri tena. Tuna mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda kuelekea Tanga, lakini linapotoka Uganda linapita nchini ketu kwa asilimia zaidi ya 70. Nchi yetu itakuwa inanufaika kwa kiasi kikubwa. Tulishauri hapa kwa kuwa, wenzetu wa Uganda wanapitisha bomba hilo la kupeleka mafuta ghafi kwenye Bandari ya Tanga, tukasema kupitia mradi huohuo na fidia hizohizo tutumie tena mradi huo tutengeneze bomba kwa upande mwingine ambalo litarudisha mafuta safi, ili tutakapokuwa tunalilinda kwa gharama zilezile za kulilinda kwa kupeleka mafuta ghafi na ndizo hizohizo gharama tutatumia kurudisha mafuta safi. Ambapo tungejenga matenki makubwa kwa ukanda wa Tabora pale Bukene, tungeweka matenki pale watu wa Mwanza, watu wa Shinyanga, Tabora, Kigoma na Katavi wangeweza kunywa mafuta pale na; malori yote yanayokwenda Dar-es-Salaam leo tusingeyaona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tungeenda kuweka huko kwa wajomba zangu huko Bukoba matenki mengine, yangeweza kulisha ukanda ule wote, yangeweza kutusaidia. Hata hao waganda wangeweza kupitisha mafuta safi kurudisha katika nchi yao, tungeweza kuokoa fedha nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda mji wa Dar es Salaam mpaka wanaweka limit ya malori kuingia mjini kwa sababu bidhaa, kila kitu tumeweka Dar-es-Salaam. Leo ile barabara ya Morogoro – Dar-es-Salaam siku ikija kupata majanga ya kufungwa barabara kwa siku tano na barabara ya Arusha, huku Kanda ya Ziwa kote mawasiliano yanakatika, hususan nishati ya mafuta. Kwa hiyo tulikuwa tunashauri jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo tunashauri hapa; wataalamu wa uchumi wamesema sekta ya kilimo inachangia Pato la Taifa kwa zaidi ya asilimia 30, na Serikali yetu ya Awamu ya Sita imejikita kwenye kuwasaidia wakulima wetu; kwa sababu wanafahamu unaweza kuzunguka popote lakini jioni lazima ukumbuke chakula. Hata kama ukisema uende siku mbili, siku tatu, lakini ya nne lazima ule na chakula chetu lazima tukizalishe nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumepitisha hapa bajeti ya Serikali zaidi ya bilioni 900 ambayo inakwenda kwenye sekta ya kilimo. Ni katika historia hatujawahi kupitisha bajeti ya namna hii, lakini sasa wataalamu wetu bado wako nyuma. Tunaona kila mwaka maji yanapotea, kila mwaka tunasema mito imejaa wakati wa masika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa naomba Wizara ya Kilimo, hakuna njia bora ambayo tunaweza kuwaokoa Watanzania kama tukiwekeza kwenye kilimo. Leo ukija pale katika Mkoa wa Tabora; huu ni Mkoa ambao uko kimkakati wa kulisha chakula mikoa ya Kanda ya ziwa, Kanda ya kati na Mkoa wa Dar es Salaam, pale chakula kingi kinatoka. Kule tuna mbuga nyingi nzuri ambazo zinatoa mchele mzuri, lakini leo mimi nashangaa hata kwenye Wizara yetu hatuna block farm hata moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo ielekeze Mkoa wa Tabora kutenga maeneo ambayo yatakwenda kusaidia kutengeneza block farm ambayo tuzalisha chakula ambacho kitalisha mikoa hiyo niliyoitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale katika Jimbo langu la Igalula kuna maji mengi ikifika wakati wa masika yanaleta maafa katika Kata ya Loya na Miswati. Yale maji tukiyawekea mtiririko mzuri, tukaweka kilimo cha umwagiliaji, basi hata yale maafa ambayo huwa yanatokea kila mwaka katika Kata za Loya na Miswati hatutayaona. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ilete mipango ya muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la tatu. Tumetengeneza SGR, SGR hii ni kwaajili ya kwenda kufungua fursa ya kiuchumi katika nchi yetu, lakini tumeweka lot zaidi ya tano ambazo zinaendelea sasahivi katika ujenzi wa reli. Sasa, kuchelewa kwa miradi hii ambayo tunaweka fedha nyingi basi ndiyo tujue tunasababisha wananchi wetu kuchelewa kupata maendeleo kwa sababu wananchi wamefunga mikanda kusubiria miradi yao iweze kukamilika. Leo tunasema mradi wa SGR kutoka Dar-es-Salaam kuja Morogoro na kutoka Morogoro mpaka Dodoma umechelewa kwa zaidi ya miezi 12 na zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukija kuangalia mradi ambao tumesaini wa kutoka Makutupora kwenda Tabora na Makutupora kwenda Kigoma ambao tunategemea utakamilika 2024 kwa delay hii ambayo tumeiona tunapata mashaka, kwamba kama tusipojipanga vizuri kama Serikali hata hiyo miradi haitakamilika kwa wakati. Mimi niiombe Serikali kwenye hii miradi, ambapo tumeamua kufungua nchi, lazima tuwe serious ili tuweze kufikia malengo. Watanzania wana imani kubwa na Serikali yao, lakini watakuwa na imani kubwa kama hii miradi tukiifikisha na ikianza kuleta tija kwa wananchi wetu. Kwa hiyo lazima tuangalie jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ambalo tunatakiwa tuliangalie, lazima tutengeneze viwanda vyetu vya ndani viweze kufanya kazi. Sasa, hatuwezi kutengeneza viwanda kama hatuna umeme wa kutosha. Leo tunapeleka umeme kila Kijiji, bado hatujaunganisha umeme kila Kijiji, lakini kuna tatizo kubwa la umeme katika nchi yetu kiasi kwamba sijawahi kuona. Vijiji vyenyewe mnasema tupeleke kule, bado hatujapeleka resources nzuri za kutosha ambazo zitakwenda kudhibiti upatikanaji wa umeme wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi jiiombe Serikali kuna umuhimu wa kuhakikisha tunaharakisha bwawa letu la Mwalimu Nyerere ili likamilike haraka ili liweze kwenda kufungua nchi. Leo viwanda vinaendeshwa kwa gharama kubwa kwa sababu ya ukosefu wa umeme, lakini kama tukitengeneza umeme wetu wa uhakika na ukatufikisha katika vijiji vyetu, leo tunapeleka umeme kule angalao bora tungewaacha na solar zao zina uhakika zaidi kuliko umeme huu wa TANESCO ambao tunaupeleka. Dakika 10 umekatika, dakika mbili umerudi, taabu tupu inaendelea huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niiombe Serikali, pamoja na nia njema ya kupeleka umeme kwa kila Kijiji lazima na sisi tujipange. Kule tunapeleka umeme watu wa Mwamabondo kule ambako hawajawahi kufikiwa na umeme wakiona shoti watafute solution kwa kutumia njia gani? Maana tunaweza kupeleka umeme kule, hakuna wafanyakazi, hakuna vifaa vya kuwawezesha TANESCO kufika kutatua na matatizo kule; tunakuwa tumepeleka matatizo kwa wananchi wetu. Kwa hiyo mimi nilitaka nichangie katika mpango huu ambao tunaenda kuujadili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la mwisho ni kuhusu sekta ya ufugaji ambayo inasemekana inachangia baadhi ya pato katika mfuko mkuu wa Serikali. Hata hivyo wafugaji wetu tumewarundikia mrundikano wa tozo nyingi sana. Mimi nimuombe Mheshimiwa Waziri, hebu pitieni hizi tozo. Kila siku, mara chanjo ya mapele, inakuja heleni, heleni yenyewe ambayo tunaiweka unaweza kuitengeneza hata kwa kupitia Wizara yako kwa shilingi 200, lakini mmempa mzabuni anaenda kuwatoza wafugaji shilingi 1,700. Bora hata ingekuwa inaingia kwenye Serikali wananchi wajue wanaisaidia Serikali kuingiza mapato yataenda kuwaletea maendeleo, lakini inakuwa fedha hii inaingia mfukoni mwa watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)