Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalambo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi ili na mimi niwe miongoni mwa wachangiaji jioni ya leo. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, kwa hiyo mchango uliotolewa na kamati mimi ni miongoni mwa waliochangia. Hata hivyo kwa jioni ya leo nitaomba nichangie maeneo machache kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitapenda kujikita zaidi katika eneo linalohusu gharama za usafirishaji na jinsi ambavyo zinaongeza gharama kubwa katika ufanyaji wa biashara katika nchi yetu. Kipindi cha mwaka jana tukiwa hapa Bungeni sisi Waheshimiwa Wabunge tulipata fursa ya kugawiwa kitabu ambacho kimeandikwa na Mtanzania mwenzetu, Ndugu Erastus Mtui chenye jina la “Poverty Within Not on The Skin”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wabunge tupate fursa ya kukipitia kitabu hiki, kina elimu ya kutosha na hasa kwa watunga sera ni kitabu cha lazima cha kukisoma. Nilikuta katika ambao wame-recommend kitabu hiki kisomwe ni pamoja na Prof. Kitila Mkumbo. Hakika kitabu hiki kinatoa elimu ya kutosha na kinatufaa Watanzania. Tanzania tuna watu wazuri ambao ni vizuri tukaunga mkono kazi nzuri wanazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma katika ibara ya sita ya kitabu hiki unakutana na maongezi kati ya bilionea Aliko Dangote pamoja na Mo Ibrahim wakiwa wanaeleza jinsi ambavyo gharama ilivyokuwa kubwa kuchukua mzigo kutoka mpaka mmoja ndani ya Afrika kwenda upande wa pili wa Afrika. Ni wakati muafaka mpango wetu ujielekeze ni namna gani tunaenda kuboresha ufanyaji biashara. Maana ni ukweli usiopingika, ukishaweka gharama kubwa katika usafirishaji tafsiri yake ni kwamba gharama za mlaji lazima ziongezeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ambayo napenda niongelee kwa kirefu zaidi ni kuhusiana na mpaka wetu wa Tunduma. Wako Wabunge waliotangulia kuchangia, wanaeleza jinsi ambavyo kuna ugumu wa mpaka ule kufanya kazi vile ambavyo inatakiwa. Ni ukweli usiopingika inafika kipindi ambapo malori yanakaa mpaka siku nne mpaka siku tano bila kuvusha mzigo. Tafsiri yake ni kwamba tunaharibu uchumi wa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kipekee niipongeze Serikali imefanya kazi kubwa sana katika ujenzi wa barabara. Ni wakati muafaka sasa tufungue corridor ya kupitia Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mwenye lori anataka kusafiri kutoka Mwanza kwa kwenda mpaka Tunduma anaenda kilometa 1,400, mpaka kwenda kufika mpaka wa Tunduma na Nakonde; lakini huyohuyo aliyekuwa na mzigo kutoka Mwanza akipita Tabora – Sikonge – Mpanda mpaka kufika Sumbawanga na kufika Kalambo, Kasesha Border, ni kilometa 1,000 tu; maana yake anaokoa zaidi ya kilometa 400, kiuchumi tunaharibu uchumi kwa kupita umbali mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama kuna mtu ambaye anasafirisha mzigo kutoka mpakani mwa Tanzania na Uganda kwa maana ya Mutukula mpaka kwenda kufika Tunduma ni kilometa 1,700; lakini akapita short cut, akapita Tabora – Mpanda – Sumbawanga na mpaka kufika Kalambo ni kilometa 1,080 tofauti ya kilometa 620. Kama hiyo haitoshi, gari limefika hapo likiwa na shehena ya mzigo, aidha inaenda upande wa pili au inakuja upande wa kwetu sisi, lori likikaa siku zaidi ya tatu mpaka siku nne ni gharama kubwa kwa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali, katika mipango ya kuhakikisha kwamba, tunaboresha ufanyaji biashara na kupunguza gharama katika ufanyaji biashara ni kazi ndogo tu, mawasiliano kati ya Serikali yetu ya Tanzania ambayo naamini tuna mahusiano mazuri na Serikali upande wa pili wa Zambia, kufanya mpaka wa Kasesha ufanye kazi saa 24 kama ilivyo Tunduma. Tafsiri yake ni kwamba, badala ya malori kukaa muda mrefu Tunduma yataka mengine yataenda kupita Kasesha, na hivyo kufanya mzunguko wa kibiashara kuwa mkubwa. Ni kama ambavyo mwanzo kulikuwa na hofu kwamba kukiwa na Kasimuro Border ikiwa inafanya kazi itapunguza biashara Tunduma, lakini ukweli ni kwamba, frequency za kusafiri zitakuwa nyingi na kibiashara hakika uchumi utachehemka na itasaidia Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, itakuwa haina maana kujenga barabara za lami kwenda Tabora, Sikonge, kama barabara hizi zitakuwa unasubiri malori, ulione lori moja baada ya wiki. Na kimsingi naomba nipongeze wanaoenda Kigoma na Burundi wameanza kutumia hii route. Sasa ni wakati muafaka kwa Serikali kutoa hamasa; na hii itapunguza hata uharibu wa barabara ya kwenda Tunduma kwa hiyo, hata hiyo itakayokuwa inajengwa itakaa muda mrefu, tutahudumia magari mengi, shehena itakuwa kubwa na gharama ya ufanyaji biashara itakuwa ndogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inaonesha kwamba, usafirishaji wa mizigo kwa nchi za Afrika Mashariki ni asilimia 30 gharama zaidi ukilinganisha na nchi za Kusini mwa Asia. Ukilinganisha na Marekani gharama zetu ziko kubwa zaidi kwa asilimia 60 mpaka 70. Sasa kwa vyovyote vile mlaji wa mwisho ndiye anaumia. Ni wakati muafaka mpango huu ukatafsiri kwa vitendo maana hakuna uwekezaji mkubwa ambao unahitajika, ni suala la kuhakikisha tu kwamba tunafungua hiyo corridor na inaanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya mchango huu nakushukuru kwa nafasi. (Makofi)