Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia mada iliyoko mbele yetu. Awali ya yote naomba nichukue fursa hii kukubaliana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa mapendekezo haya ya mpango. Mapendekezo haya akizingatia ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, hao ambao nimewasikiliza utakuwa mpango mzuri, tutatoka na mpango mzuri ambao tukijituma, na tutajituma na kuutekeleza tutaweza kutimiza malengo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea na mchango wangu, nichukue fursa hii kutoa pole kwa Watanzania na wananchi wa Kagera kutokana na ajali ya ndege ya Shirika la Precision Air, Sina zaidi nianze kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajadili Mpango wa Tatu katika mipango Mitano ya mwaka mmoja mmoja, inayokamilisha Mpango wa Tatu wa miaka Mitano na huu ndiyo mpango wa tatu wa miaka mitano unaomalizia mipango mitatu ya miaka mitano mitano tukiwa tunafikia Dira ya Taifa ya 2025. Kumbe huu mpango wa tatu ndiyo dira yenyewe ya 2025. Ninapochangia nitajaribu kurejea dhima ya mpango wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya mpango wa tatu wa miaka mitano ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. Uchumi shindani ni upi? Uchumi shindani ni ule ambao shughuli zake zinatawaliwa na tija kubwa, shughuli zote zinatawaliwa na tija kubwa. Uchumi shindani ni ule ambao una ujumuishi, umma umejumuishwa, lakini shughuli ya ushindani na ujumuishi inakuwa endelevu. Pamoja na uchumi shindani tunajenga viwanda kwa maendeleo ya watu. Hili la maendeleo ya watu niliseme kidogo, watu wengine huwa na kigugumizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya watu kuna vigezo vingi lakini kuna hili la afya, tunalisema sana, kuna hili la elimu tunalisema sana, lakini kuna lile la kipato. Unasikia watu wengine wanazungumza sasa tunapojipima lazima tujipime kwa vigezo vyote. Baada ya kueleza hayo, mimi nitajikita zaidi kwa sababu natambua mchango wa walionitangulia hususani Prof. Muhongo, nizungumzie utatuzi wa changamoto za kibajeti na mipango au mikakati ya kukabiliana na changamoto na vihatarishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetengeneza mapendekezo ya mpango tutakuja na mpango lakini huenda tusifikie mpango. Ni kitu gani Wachumi wanaita ceteris paribus yaani unaweka assumption ambazo kama zisipokudhuru unaweza kutekeleza mpango wako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nizungumzie namna ya kukabili vihatarishi. Mojawapo ya vihatarishi Waheshimiwa Wabunge, wengine wamevisema ni suala la mazingira na hali ya hewa. Tumeona nguvu za kidunia mojawapo ikiwa vurugu ya vita ya Ukraine na kupanda kwa bei ya mafuta. Napenda nishauri kwamba Serikali yetu pamoja na kutoa ruzuku lazima tuongeze kasi ya kutumia gesi asilia. Moja, tutumie gesi asilia sana, lakini pamoja na agizo la Mheshimiwa Rais alilolitoa la kutumia gesi kwenye taasisi za Kiserikali, tutumie gesi asilia kwenye taasisi za Kiserikali. Hii itatupunguzia mzigo wa ku-import products hali ambayo itaongeza import bill. Kwa hiyo gesi asilia ni rahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kilimanjaro Hotel Dar es Salaam wanabeba mitungi kutoka kwenye kituo mama (mother station) ya natural gas, wanaleta ile mitungi, wanakuja kutumia wanairudisha. Ni mtungi mkubwa, tunaweza kufanya hivyo kwa radius ya kufika mpaka Dodoma, tukaweza kufanya hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ni hili la mazingira na tabianchi. Kuna suala moja, kuna presha za mazingira zinazotoka nje ya nchi lakini kuna presha za mazingira zinazotoka hapa nchini. Ulilidokeza jana, kuna matatizo yanayotupata sasa kwa sababu tumeharibu mazingira. Katika mapendekezo ya mpango huu, vidokezo vilivyotolewa na Serikali haviwezi kutatua tatizo hili. Mojawapo ya eneo nataka kupendekeza, lazima tuje na sera na sheria ya kuiondoa Tanzania katika utaratibu wa uchungaji wa mifugo, tuende kwenye ufugaji ni suala gumu lakini lazima tulizungumzie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ninalotaka kuzungumzia ni suala la mikakati ya kuongeza mapato. Kuongeza mapato ni muhimu na suala mojawapo la kuongeza mapato ni ku-invest kwenye re-export. Tuna VISA re-export kutoka Tanzania, lakini tuwekeze kwenye viwanda. Ujenzi wa uchumi shindani na viwanda. Viwanda tunavyovilenga ni viwanda vya Kitanzania, siyo viwanda vya Tanzania, viwanda vya Kitanzania. Mheshimiwa Kakosa alisema jana kwamba tutengeneze mamilionea wa Kitanzania – ndiyo! Tutengeneze viwanda vya Kitanzania kwa sababu hawa wawekezaji wanaotoka nje ni watoto wa kufikia, watarudi kwao wakati ukifika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la kusimamia matumizi yetu. Kuna haja ya kuimarisha Idara za Kiukaguzi. Hii idara ya kiukaguzi ipewe uhuru zaidi, rasilimali, itungiwe sheria kusudi Mkaguzi awe na nguvu za kumsimamia yule anayemsimamia. Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri hawezi kusema juu ya Mkurugenzi wake. Hata yule wa Mkoani hawezi, hata Mkaguzi wa Wizarani hawezi kusema kwa Katibu Mkuu. Lazima hii taasisi tuitengenezee sheria, sera na mamlaka na tu-train watu wetu kwenye ukaguzi wa leo, waweze kukagua mifumo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakaguzi wetu wamesomea kukagua makaratasi, hard papers, wafundishwe zaidi kukagua mifumo hii. Kenya wanao Wataalam wa namna hii karibu 1,800,000 sisi tunao Wataalam kama 200. Kwa hiyo lazima tuende kwa teknolojia, ndiko hali inakokwenda. Fedha nyingi zinakuja, zinakusanywa lakini namna ya kusimamia hayo matumizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni Tume ya Mipango. Tunahitaji Tume ya Mipango, moja ni kwamba tunamahitaji mengi lakini tunahitaji kwenda kwa kasi kubwa. Baada ya hayo, naunga mkono hoja naona mapendekezo haya ni mazuri. (Makofi)