Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kondoa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. ALLY J. MAKOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami kuweza kuchangia huu mchango. Awali ya yote mimi nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukamilisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, kwa sababu zoezi hili litatufanya sasa sisi Wasaidizi wake na Viongozi kuweza kutumia vizuri takwimu za watu katika kuhakikisha tunapanga maendeleo ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye maeneo matatu. Kwanza kwenye sekta ya ardhi. Kutokana na ukuaji wa idadi ya watu kama tulivyoona kwenye taarifa ya sensa, tunagundua kwamba tumeweza kuongezeka kutoka miaka 10 iliyopita kwa asilimia Tatu. Watu wameongezeka kwa idadi ya zaidi Milioni 16.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama watu wameongezeka kwa kiasi hiki ni lazima Taifa tuweze kuweka mpango mzuri wa kuhakikisha kwamba mipango ya ardhi inawekwa sawa kwa ajili ya matumizi ya leo na kesho. Kama hatukuweka mipango mizuri ya matumizi ya ardhi leo, huko tunapokwenda kutakuwa na vurugu na migogoro mingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango huu, ninashauri kwamba mpango ujikite sana katika kuiwezesha Wizara ya Ardhi hasa kule kwenye Tume ya Mipango ili iweze kuongeza kasi ya ukuaji wa upimaji wa viwanja na maeneo ili kuweza kupanga Watanzania na kuondoa migogoro. Leo migogoro mingi inasababishwa na eneo kubwa la nchi yetu kutokupimwa na kupangwa. Kwa hiyo, napendekeza mpango uweke nguvu kubwa katika Wizara ya Ardhi hasa kule kwenye Tume ya Mipango ya Ardhi ili tuweze kufanya kazi kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kwenye sekta ya maliasili. Leo utaona wananchi wengi na Waheshimiwa Wabunge, wakilalamika kuhusiana na migogoro baina ya wanyama na wanadamu. Sasa kutokana na hilo, iko haja sasa mpango wetu ukajikita sana katika kuhakikisha wanaiwezesha Wizara ya Maliasili katika kuhakikisha kwamba wanakabiliana na majanga kama hayo. Tunapaswa kupanga mipango na tunapaswa kuiwezesha Wizara, kiwango kile ambacho kinaweza kunufaisha Taifa. Mfano, leo Wizara ya Maliasili inachangia asilimia 17 kwenye Pato la Taifa, lakini kiuhalisia ukiangalia vyanzo vya utalii vilivyomo katika nchi haviendani na kiwango cha mchango wa Pato la Taifa la asilimia 17. Hivyo tunataka tuone kwamba tunaweka mipango thabiti kuhakikisha kipato kinachochangiwa na sekta hii ya utalii kinaongezeka kulingana na ukubwa wa vyanzo vyetu vya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaliwezaje hili? Ni pale Serikali itakapokuwa tayari sasa kuhakikisha wanaweka nguvu kwenye sekta hii. Serikali imefanya vizuri sana katika kuiwezesha Wizara ya Maliasili. Mfano, wamegaiwa magari ya kuweka miundombinu katika mbuga zetu na hifadhi mbalimbali. Je, baada ya mradi ule kuisha, yale magari tunaweza kuyaendesha vizuri yakaendelea kukaa muda mrefu katika maeneo yetu ama kwa ukosefu wa bajeti inawezekana magari yale yakaharibika muda mrefu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, TANAPA mwanzo ilikuwa inasimamia hifadhi 16, bajeti yao ilikuwa ni Shilingi Bilioni 100. Miaka kadhaa baadae ikaongezewa hifadhi nyingine kufikia hifadhi 22, lakini bajeti ilibaki vilevile. Zoezi la kusimamia hifadhi hizi kwa vyovyote lazima litakuwa ni gumu kwa sababu wameongezewa idadi ya maeneo. Mfano, mwanzo walikuwa na kilometa za mraba 57,333, wameongezewa kilometa za mraba 47,471 lakini bajeti katika kipindi cha miaka mitatu imebaki hiyo hiyo Bilioni 100. Kwa hiyo, ili tuweze kuwasaidia watu hawa wa maliasili waweze kukabiliana na tembo na wanyama waharibifu lazima tuone uwezekano wa kuisaidia Wizara hii ili kuondoa migogoro baina ya wanyama pamoja na wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia migogoro ya ardhi baina ya hifadhi na vijiji. Mheshimiwa Rais ametuma Kamati ya Mawaziri Nane katika kuhakikisha wanatatua migogoro. Sasa sijajua huko maeneo mengine lakini juzi mimi nilihudhuria kwenye kikao kimoja cha utatuzi, nilichokigundua, kama Mawaziri Nane hawajachukua lile jukumu lao kikamilifu, wakawaachia watu wa ngazi za Wilaya, migogoro hii haitaisha na itaendelea kuwa mikubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hawatasimamia wenyewe wakawaachia kule Wilayani, tutajikuta kwamba migogoro hii haitaisha. Mfano, nimepokea taarifa ya Halmashauri mbili, Halmashauri ya Chemba na Halmashauri ya Kondoa na Halmashauri ya Mji, mapendekezo yaliyotoka Wilayani yana-double standard. Mfano wanatoa kaya 411 zote zitoke halafu hazielekezwi kaya hizo zenye watu zaidi ya 1,700 waende wapi. Taarifa inasema waende kwenye Kijiji Mama. Ukienda kwenye Kijiji Mama unakuta kila mmoja ana eneo lake. Sasa kaya hizi kwa taarifa nyepesi nyepesi kama hizi itakuwa hatusaidii badala ya kutatua mgogoro, tutazalisha migogoro mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo bado ninatoa rai kwa Serikali iweze kulisimamia hili vizuri ili kuhakikisha inatatuliwa kwa sababu migogoro pia inakwamisha mipango ya Serikali hasa kwa mtu mmoja mmoja na uchumi wa nchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye sekta ya uchukuzi. Nilizungumza Bunge lililopita hapa. Barabara hii ya Handeni ambayo nimeikuta pia hapa kwenye mpango huu. Kwa sababu Ilani ya CCM ilitaja barabara hii lazima ifike Kondoa halafu utekelezaji inapitia Chemba. Kwa sababu mipango yote, mpango wa miaka mitano na mpango huu ulielezea barabara hii ipitie kule, basi Serikali ikumbuke jambo hili. Mpango ule wa awali na Ilani inavyosema barabara hii ipitie Kondoa, halafu hii barabara mpya waliyoichonga waiingize kwenye Mpango huu ili na yenyewe iwe inatekelezwa kwa mujibu wa Mpango na Ilani ya CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyaseama hayo, ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)