Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kawe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami nichangie katika hoja hii iliyopo mbele yetu. Kwanza ninakushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii lakini kwa maksudi ya kuokoa wakati, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa bidii yake anayoifanya kutusimamia Watanzania na kuhakikisha ndoto ya Watanzania inatimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nichukue nafasi hii kuwashukuru vijana wa kutoka Jimbo la Kawe, Kata ya Mabwepande ambao vijana hawa walitembea kwa mguu kutokea Dar es Salaam mpaka Bukoba kwa kusudi la kum- support Mheshimiwa Rais katika juhudi zake. Shukurani zangu ni kubwa sana kwao kwa sababu wametembea kilometa 1,382 kwa siku 35. Wakati wana wa Israel walipokuwa wanatoka katika nchi ya Misri, walisafiri kilometa 405 kwa miaka 40, lakini hawa vijana wamesafiri kilometa 1,382 kwa siku 35, hawa ndiyo mashajaa wa Jimbo la Kawe. Vijana hao ni Abiudi Maugo, Alinda Albert, Saidi Apollo, Idrissa Rajabu, Mossi Fikiri, Kassim Kidole na Bura William, nawashukuru sana hawa vijana wa Jimbo la Kawe.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuchangia hoja iliyo mbele yetu. Nitachangia mchango huu tena na tena mpaka Yesu Kristo atakaporudi tena kama haijafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka ieleweke kwamba, Friction au msuguano ni sehemu mojawapo ya ujenzi, na tujue kwamba msuguano au friction ndio ulileta ufumbuzi wa kwanza wa moto. Kutofautiana kimawazo ni jambo la kawaida kama lengo lenu ni kujenga nyumba moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaza kwamba pamoja na mpango mzuri ambao Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango aliuwasilisha lakini tunahitaji Mpango wa muda mrefu. Nataka nikubaliane na Mheshimiwa Shabiby aliyechangia jana, kwamba hakuna nchi duniani, narudia tena there is no country on global ambayo imeweza kuwavusha watu wake au kuleta maendeleo kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote ambazo zimevusha watu wao zilikuwa na mipango ya muda mrefu na zikaisimamia. Kwa mfano tunakumbuka baada ya vita vya kwanza vya dunia, nchi za Ulaya zote zilifilisika; ni kwa sababu tu Marekeni haikupigana vita hivyo katika nchi yake; lakini zaidi ya nchi 16 Ulaya zilifilisika na zilikuwa zimekwisha kabisa kiuchumi. Kipindi kile alikuwepo Rais wa Marekani anaitwa Truman na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje George Marshall akaweka mpango wa kuziokoa nchi
16 za Ulaya kiuchumi na zikapewa fedha. Na katika mpango wake zikaambiwa kwanza ziandae Mpango wa Maendeleo wa muda mrefu. Nchi zile zikaanda Mpango wa Maendeleo wa muda mrefu katika nchi 16 za Ulaya, ikiwemo Ujerumani na Swaziland.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maandalizi yake ya Mpango wa muda mrefu na fedha zilizopata kutokea Marekani wakavusha nchi zao mpaka leo ni nchi za ulimwengu wa tatu, zilikuwa zimefilisika kabisa. Ukimwona mwenzako anatumia farasi fulani wa kumkimbiza kwenda kwenye hatma na wewe ukimtumia farasi huyo huyo atakufikisha kwenye hatma hiyo hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashangaa kwa nini sisi pamoja na mipango mizuri ya mwaka mmoja, miaka mitano tunashindwa nini kuwa na mipango ya muda mrefu miaka 60 ya maendeleo ya Tanzania au miaka 70 ya maendeleo ya Tanzania na hii mipango ikavunjwa kwenye vipande vidogovidogo kwa malengo ya kuitimiza. Kwa mfano tumejenga SGR ni jambo zuri na ni safi kabisa. Lengo la SGR ni kwamba tubebe mzigo wa kutosha ili tuiongezee nchi yetu kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mzigo unatokea wapi? Mzigo unatokea bandarini. Kwa hiyo lakini bandari haijapanuliwa bado; tumeanza na SGR na bandari bado ile ile. Kwa hiyo kama tungekuwa na mipango tungekuwa tumeanza kupanua bandari kwanza ili kusudi hii bandari SGR itakapokamilika tuweze kubeba mzigo mkubwa tuupeleke mpaka Kigoma na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa unaona ukweli wenyewe kwamba SGR inaelekea Kigoma, Bandari ya Dar es Salaam ni hiyo hiyo, tumehamia tena Bandari ya Bagamoyo mahala ambapo SGR haipo. Kitakacholazimisha kufanyika tena itabidi tujenge kipande kingine cha kutokea Bagamoyo kwenda kuunga kwenye SGR ili tuwe na uwezo wa kubeba mizigo mikubwa na kuiongezea uchumi nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili lisingekuwepo kama tuna mipango. Wakati huo huo hii mizigo mingi ambayo tunataka tubebe inaelekea wapi? tunakwenda mpaka Kigoma tuivushe kwenda Congo. Je, tumeshajiandaa kuivusha mizigo hiyo kutokea Kigoma ama kwa njia ya Ziwa Tanganyika kwenda Congo? Hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ya muda mrefu ya nchi ndiyo njia peke yake ambazo nchi zilizoendelea zilitumia kuzitoa nchi zao zilipokuwa na kuzipeleka mahala ambapo nchi hizi zilikwenda. Nitoe mfano mwingine, ya kukufanya Mheshimiwa Mwenyekiti na Wabunge wenzangu kuwafikirisha, kwa mfano tumejenga Stigler’s Gorge mahala ambapo tutazalisha umeme mwingi ni jambo zuri kwa sababu power ndiyo njia pekee ya kuifanya nchi ijenge viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mpango wa kujenga Stigler’s Gorge hatukupanga ule umeme tutautoaje hapo Stigler’s Gorge kuingia kwenye gridi ya Taifa. Mtu yeyote ambaye ni genuine nimuulize, je, wakati mnapanga ujenzi wa Stigler’s Gorge je, kuna bajeti ya kutoa umeme pale Stigler’s kuingiza kwenye gridi ya Taifa mpango haukuwepo. Hii ni kuonesha kwamba, nasema sisi simlaumu mtu, ni kuonesha kwamba matatizo yetu yanatokana na kukosa mipango ya muda mrefu. Tunapopanga mipango ya muda mfupi there is no country on the global will ever develop kwa kuwa na mipango ya muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja ambalo linaweza likamgusa mtu lakini sio kwa ubaya. Ili nchi iendelee haihitaji tu natural resources, hapana, nchi kwa mfano Sweden, Denmark, Sweden wanatengeneza scania hawahimbi chuma kama cha kwetu. Japan ndio supplier wa magari, iron ya Japan ilikwisha muda mrefu wanaagiza chuma kutoka Australia. Ni mipango tu wanayofanya. Lakini sisi tuna natural resources za kutosha ila ile akili ya kugeuza natural resources kuwa maisha ya wananchi ndiyo hiyo tunapungukiwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri, namwita Mheshimiwa Festo Sanga ajiandae Mheshimiwa Asha…
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)