Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hotuba iliyopo mbele yetu. Awali ya yote nipende kumshukuru Mwenyezi Mungu, nikushukuru wewe pia kwa kunipa nafasi. Nipende kwa kuanza kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho lake zuri, na mchango wangu wa kwanza nitapenda kuanza kuangazia deni la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba zote mbili zilizowasilishwa katika Bunge lako tukufu, ile ya Kamati ya Bajeti pamoja na ya Mheshimiwa Waziri zinatuambia kwamba deni la Taifa limekuwa likiendelea kukua ama likiongezeka hadi kufikia trilioni 71.56 kutoka ile 64.50. Hili ni sawa na ongezeko la asilimia 11.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tunaambiwa deni hili ni himilivu kwa viwango vya Kimataifa, ni vema sasa tuka-focus na tukapigia jicho zaidi kwenye miradi ya kimaendeleo na miradi ya kimkakati. Lengo ni kufanya miradi hii iweze kurudisha return ya haraka kwa mkopo huu wa shilingi trilioni 71.56.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii mikubwa ni miradi itakayosaidia kusimamisha uchumi wa nchi. Kwa hiyo, tukiacha sababu zile ambazo ziko dhahiri shahiri zinaonekana, lakini tuondokane na sababu za hapa na pale zinazopelekea kuchelewesha miradi hii ama sababu zinazopelekea miradi hii kwenda kuongezeka thamani ya fedha ukilinganisha na hile thamani ya mwanzo tuliyongia katika mikataba hii pale awali. Kwa kufanya hivyo tutaweza kukuza uchumi, tutaweza kukuza pato la Taifa na pia tutaweza kukuza ajira na fedha za kigeni. Haya yote kwa pamoja yatafanya uchumi wetu uweze kuwa stable zaidi, jambo ambalo litatusaidia sasa kupanga na kubajeti masuala mazima ya elimu, afya pamoja na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa pili upo katika eneo la mfumuko wa bei. Ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wake wa nne, ameelezea kwa namna gani mfumuko wa bei umekuwa ukiongezeka hususan kwenye bei za bidhaa ya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na ongezeko kubwa, tena kubwa sana, kutokea asilimia 3.6 mpaka asilimia 7.8; kilo ya mchele imeongezeka, kilo ya unga na mahindi imeongezeka; hivyo ni vyema sasa tukajikita kwenye mpango huu tunavyopanga mpango huu wa maendeleo, tukaangazia zaidi eneo hili kwani ndiyo eneo linalowagusa Watanzania wengi. Mtanzania wa leo anahitaji unga, maharage na mchele, lakini ndiyo sehemu ambayo bei imekuwa ikiongezeka kwa kasi. Kwa maana hiyo, hapa Mheshimiwa Waziri ni lazima afuate ushauri uliotolewa na Kamati juu ya suala zima la kuanza kutumia gesi asilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine namwomba Mheshimiwa Waziri, hebu atusaidie na alisaidie Taifa, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, kila mwezi anatoa ruzuku ya Shilingi bilioni 100 ili kwenda kuongezea kwenye bidhaa za nishati pamoja na fuel. Jambo la kusikitisha hapa, na kimsingi ni kwamba uongezwaji huu wa hii Shilingi bilioni 100 kila mwezi, ili iende ikapunguze usafirishaji pamoja na uzalishaji, jambo ambalo litasaidia bidhaa sokoni angalau zishuke bei. Cha ajabu bei ndiyo zimekuwa ziki-shoot kwa hali ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri akija atuambie nini faida ya hii Shilingi bilion 100 anayoitoa Mheshimiwa Rais kila mwisho wa mwezi kwa ajili ya kwenda kupunguza makali kwenye nishati na kwenye fuel ilhali bei za bidhaa ya chakula inapanda kila leo? Kwa hiyo, atakapokuja hapa, naomba anipatie hayo majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni kuhusiana na mikopo ya sekta binafsi. Tunakubaliana sote hapa kwamba sekta binafsi ni kichocheo kikubwa na kichocheo kizuri cha uchumi wa nchi yetu. Tunashukuru kuona kwamba mikopo kwenye sekta binafsi imekuwa ikiendelea kukua kutoka Shilingi trilioni 20 mpaka Shilingi trilioni 24. Ila ukija kwa upande wa riba, riba tunashukuru inapungua, lakini inapungua kwa kiasi kidogo, asilimia 0.19. Sasa kwa mipango na maendeleo tunayotaka kupanga ya nchi yetu, kwa upunguaji huu wa riba tutasababisha kukosa wawekezaji wa kutosha na wakopaji wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tulikuwa tunaiomba Benki Kuu na mabenki kukaa na kuangazia tena namna bora ya kuendelea kupunguza kiwango cha riba ili tupate wakopaji na wawekezaji wengi. Nia na madhumuni ni ku- boost uchumi wa nchi yetu, ajira zipatikane kwa wingi, kuingiza fedha za kigeni na katika yote tuweze kulisaidia Taifa hili kuweza kuwa na uchumi stable katika kupanga maendeleo endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kuhusu Bandari ya Bagamoyo. Sote tunafahamu kwamba bandarai ndio lango kubwa la uchumi na upanuzi unaofanywa kwenye Bandari ya Dar es Salaam imeishafika mahali, wanasema point of no return. Kwamba mbadala wa Bandari ya Dar es Salaam ni Bandari ya Bagamoyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa SGR unaoendelea unahitaji Bandari ya Bagamoyo. Uchimbaji wa Makaa ya Liganga na Mchuchuma utahitaji Bandari ya Bagamoyo, ukuaji wa uchumi wa nchi yetu unahitaji Bandari ya Bagamoyo, yaani ni Bandari ya Bagamoyo, Bandari ya Bagamoyo. Tukilala Bandari ya Bagamoyo, tukiamka Bandari ya Bagamoyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuomba Mheshimiwa Waziri, nimepitia Mpango nimeona tu nyota nyota. Nataka uje uniambie Mpango unasemaje kuhusiana na masuala mazima ya Bandari ya Bagamoyo? Vilevile nataka uje uniambie kuhusiana na kulipa fidia ya watu wa Bagamoyo ili tukawekeze kwenye Bandari ya Bagamoyo. Naomba unipe majibu, kwa sababu mradi huu wa Bandari ya Bagamoyo tayari kulishakuwa timu, tayari kulishakuwa na kikosi kazi na makubaliano, nitapenda uje uliambie Taifa, ile timu ya negotiation iliishia wapi? Tunataka tupate maelezo ya kina kuhusiana na Mradi wa Bandari hii Bagamoyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Bagamoyo utaenda uta-boost uchumi wa hii nchi, utateka masoko ya Jirani na utafungua ajira pamoja na kufanya tupate fedha za kigeni za kutosha. Tukiimarika hapo, hatutakuwa tunajenga madarasa halafu tunashindwa kuwaboreshea walimu stahiki zao. Ili tuweze kuwa na elimu bora, tunapaswa tujenge madarasa, mishahara ya walimu tuiboreshe, ndivyo tutakapoweza kupata elimu bora. Suluhisho ni huu mradi wa Bagamoyo utakaotuletea uchumi kukua kwa kasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaenda na vyote; tunajenga zahanati, tunapata vifaa tiba na at the same time stahiki za watumishi zinaboreshwa, lakini tukiwa tunafanya mipango yetu, eti tunajenga tu zahanati halafu vifaa tiba hatuna, work done is equal to zero. Tukiwa tunafanya mipango yetu, tunajenga madarasa halafu walimu hakuna, work done is equal to zero. Kwa hiyo, lazima mipango hii iende sambamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia napenda sana kuipongeza Serikali na kuiomba ipokee ushauri huu ambao tunaweza kuipatia ili kuweza kusongesha maendeleo ya Taifa letu mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushuru, ahsante sana. (Makofi)