Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Hawa Subira Mwaifunga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mpango huu wa mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wowote wa uchumi katika nchi yoyote unategemea mipango thabiti ambayo mmejiwekea kama Taifa. Siku za nyuma kidogo kulikuwa na filamu ya Royal Tour. Tumeona ni kwa namna gani mafanikio makubwa ya filamu ya Royal Tour yanakuja katika nchi yetu, lakini kama Taifa tumejiandaa namna gani kukabiliana na wimbi la wageni ambalo litakuja katika nchi yetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango au katika mpango huu sijaona sehemu yoyote ikisisitiza kwamba kama Taifa tunategemea kuongeza mapato yetu kupitia utalii. Utalii kwa Tanzania unakua kwa kasi ya hali ya juu, lakini mpaka sasa kama Taifa tunategemea kupata mapato ya asilimia 17 tu kutoka katika suala zima la utalii. Tuna uwezekano mkubwa sana wa kuongeza mapato yetu kupitia sekta hii ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vitu vingi sana, tuna vivutio vingi sana, tuna mambo mengi sana katika nchi hii ambayo tukiyatangaza tukiyaweka vizuri katika Taifa letu haki ya Mungu utalii utakuwa unaongoza kwa zaidi ya asilimia Thelathini katika mapato ya Taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na hifadhi 16, leo tunapozungumza Tanzania tuna hifadhi 22. Hifadhi hizi 22 bado kama Taifa hatujaona umuhimu wa kutengeneza mpango madhubuti wa kuhakikisha hifadhi zote hizi angalau hata nusu ya hifadhi hizi zinaingiza kipato cha kutosha. Leo ninapozungumza na Bunge hili ni kwamba, bado watalii wanapokuja kwenye nchi yetu, wanatamani kwenda Serengeti na Zanzibar, lakini tunahifadhi na vivutio vingi kweli kweli ambavyo watalii hawa ama wananchi wa Tanzania ambao wanapenda kwenda kutalii wakitangaziwa nchi hii itakuwa inaongoza kwa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wizara haitakuwa na mpango madhubuti wa kuhakikisha kwamba inaongeza bajeti kwenye sekta hii ya utalii tutaendelea kupiga mark time na badada ya hii asilimia 17 tutashuka asilimia 15 mpaka asilimia 10 kwa sababu hatuko serious kwenye jambo hili la utalii. Shida yetu ni kwamba tunagusa kila kitu hatuangalii zile sekta muhimu ambazo zinaweza zikifufua uchumi wetu na uchumi ukapaa ukawa mkubwa kuliko ilivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo hifadhi ya TANAPA ambayo inasimamia hizi hifadhi 22, lakini bajeti waliyonayo tangu wanasimamia hifadhi 16 mpaka leo ni ileile Bilioni 1.5 wanaendelea kuwa nayo mpaka leo. Hivi kutoka hifadhi 16 mpaka leo 22, bajeti ni ileile hivi kweli tuko serious, tunataka utalii wa nchi hii ukue? Ningeomba sana katika mpango huu ambao tunakwenda kwa ajili ya kuandaa bajeti, hebu watuletee bajeti ya maana katika Wizara hii ya Maliasili ili tuweze kukuza utalii wetu. Tunahitaji kuwa na asilimia za kutosha katika sekta hii ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusiana na suala la Bandari Kavu. Mimi ninatokea Mkoa wa Tabora, Mkoa wa Tabora ni eneo ambalo reli ya SGR inapita. Kama ulivyoona hata katika sensa Tabora ni moja kati ya Mikoa mikubwa sana na ina maeneo makubwa sana, mimi ningeomba Serikali iache kigugumizi wapeleke Bandari Kavu katika Mkoa wa Tabora. Watakapopeleka Bandari Kavu katika Mkoa wa Tabora sisi tutafanya biashara na nchi za Maziwa Makuu kwa urahisi zaidi. Ukitoka Tabora kwenda Katavi, Mpanda na Kigoma ni rahisi kuliko maeneo mengine yoyote na tutaweza kufanya biashara na nchi Mbili mpaka Tatu kwa pamoja, kuliko ambavyo sasa hivi kumekuwa na kigugumizi tunataka huku tunataka huku. Serikali ifanye maamuzi katika Mpango mnaokuja nao, tengeni fedha ya kuhakikisha kwamba tunakwenda kujenga Bandari Kavu katika Mkoa wa Tabora na kama kuna nia thabiti ya kuinua Mikoa ya pembezoni basi fanyeni hili. (Makofi)

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti,taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kumpa taarifa mchangiaji Mheshimiwa Hawa Mwaifunga Dada yangu kuwa Serikali ya Mkoa wa Tabora chini ya Mkuu wetu wa Mkoa Mheshimiwa Batilda Burian umeshatenga eneo kwa ajili ya kujenga Bandari Kavu hii ambapo Serikali ikiwa tayari basi watapatiwa eneo. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hawa.

MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru kwa taarifa yake maana kutenga ni jambo moja lakini utekelezaji ni jambo lingine. Kwa hiyo, hapa tunachofanya ni kuhakikisha kwamba tunasisitiza kwa sababu tayari kumeshakuwa na mvutano, Mkoa wa Tabora tayari umeshatoa heka zaidi ya 1,000 bila fidia yoyote. Kwa hiyo, mimi ninaomba sana Mheshimiwa Waziri tusaidieni hii Mikoa ya pembezoni inahitaji kuendelea, ili tuweze kuendelea na wananchi wetu waweze kuwa na mafanikio katika uchumi wao tunaomba sana mtusaidie, hii Bandari kavu itakapokuja pale Tabora itasaidia sana wananchi wetu pia itasaidia kukuza uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie upande wa Kilimo, ni ukweli usiopingika kwamba Mikoa mingi inalima mazao ya biashara lakini sisi ambao tunatoka Mkoa wa Tabora zao kubwa la biashara ambalo tulikuwa tunalitegemea wakati wote ni zao la Tumbaku. Tabora ni Mkoa ambao umeonekana kwamba unao uwezo wa kulima mazao mengi ya biashara na yakastawi vizuri. Tabora tunalima alizeti, korosho, tumbaku, mahindi, maharagwe na kadhalika. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo kwa kazi kubwa ambayo anaifanya nasi tunamuahidi kumpa ushirikiano wa kutosha ili kuhakikisha kwamba nchi yetu tunakwenda kuingia kwenye kilimo cha kisasa badala ya kutegemea zaidi mvua na jembe la mkono.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono suala zima la block farming, lakini ninaiomba Serikali iliangalie hili jambo kwa jicho la tatu, iwe ni lazima kwenye kila Mkoa na Wilaya kutengwe maeneo kwa ajili ya hizi block farming ili wananchi wetu waweze kunufaika na kilimo kwenye suala zima la block farming. Kama Tabora tunao uwezo wa kulima korosho, lakini wanapotokea wateule wakasema kwamba hatuwezi kulima korosho kwa sababu yataharibu zao la asali. Mimi nimezaliwa Tabora nimekua Tabora, lakini sijawahi kuona tajiri wa asali zaidi ya watu wanaovuna asali hela wanayopata ni kwa ajili ya watoto kusoma, chakula na mambo mengine madogo madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kwenda mbali zaidi ili kuweza kuwasaidia wananchi wetu wawe na tija. Kwa mfano, likija zao la korosho baada ya miaka mitano au kumi watu wakaanza kuvuna korosho, Mkoa ule utabadilika na mwisho wa siku watu wetu wakawa matajiri na kufanya kazi kubwa. Kwa hiyo, ninaomba sana kupitia mipango hii kwenye suala zima la kilimo tusaidiane kuhakikisha kwamba angalau hawa wateule, kila mteule ajue kwamba katika Mikoa hii tuweke hizi block farming na katika Wilaya hizi ambazo tunaweza kuweka basi iweze kufanyika hivyo, ikiwepo Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tena nizungumzie suala zima la afya. Wakati nikipitia mpango nimeona kwamba wanazungumzia suala zima la kupunguza vifo vya watoto na mama wajawazito, lakini hizi takwimu zinasema sahihi? Je, hizi takwimu si ni zile ambazo zinakuwa recorded vipi kuhusu zile takwimu ambazo haziko recorded? Wanawake wengi sana wanajifungulia nyumbani na barabarani. Je, hawa nao takwimu zao tayari zinakuwa zimeshaorodheshwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza kwamba vifo viumepungua kwa asilimia hizi lazima tuwe na uhakika wa kuona hata kwenye yale maeneo ambayo wanawake wengi wanajifungulia majumbani na barabarani taarifa zake zinakuwa recorded na zinapelekwa na zinakuwa taarifa sahihi ili tuweze kujiridhisha na kuona kwamba ni ukweli kama Taifa tumepunguza vifo vya mama na mtoto, kuliko hivi sasa tunazungumza vitu kinadharia na vitu vile ambavyo tunaviona viko pale lakini kiuhalisia siyo sahihi. Kwa sababu sisi tunaotoka kwenye maeneo ya vijijini ambayo ni mbali na hospitali tumeshakutana na kadhia hizo nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta Mama ameshajifungua, wameshamfanyia kila kitu pale kamaliza biashara, lakini saa zingine unaweza kuta mtoto amepata athari au amekufa ama mama amekufa taarifa hizo hazitoki. Kwa hiyo, mimi niombe sana kama Wizara katika mpango wenu muangalie na muone namna gani ambavyo mnaweza kujua kwamba wanawake wangapi kwa mwaka wanakufa katika nchi hii kwa ajili ya uzazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)