Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii ya Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu Mpango wa Maendeleo lakini pia Mpango wa Bajeti 2023/2024.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita kwenye miradi ambayo ninafikiri ni ya kimkakati na nianze na Reli ya Kati - SGR. Reli hii inakusudiwa kuunganisha Tanzania na nchi jirani, ibebe mizigo ya nchi jirani ili tupate uchumi kwa nchi yetu lakini lazima reli hii ikamilike. Mimi nimeona mpango unavyoendelea kwamba Reli hii ya Kati itajengwa na tayari sehemu ya kwanza ile ya Dar es Salaam - Morogoro imekamilika na Morogoro - Makutopora iko asilimia Fulani lakini ninaomba Serikali iweke nia sana. Hatuwezi kuwa na mpango wa ujenzi wa reli ambayo hatujui itakamilika lini. Tungependa kujiwekea mpango kwamba reli hii itaisha lini ili ilete faida nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo ningependa kuongelea ni ukamilishaji na ununuzi wa ndege Tano, ni wazo zuri sana kuiongezea uwezo ATCL na hasa ile ndege ya mizigo ambayo itabeba mizigo yetu kupeleka nje ya nchi moja kwa moja. Sasa hivi tunapata taabu ya kupeleka mizigo yetu kupitia nchi za Jirani, ni wazo zuri lakini Serikali isimame na tuipongeze iweze kukamilisha mradi huu wa ATCL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa kufua umeme kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere kule Rufiji, napata kidogo matatizo, kila siku ng’ombe wanakamatwa kwenye vyanzo vya maji na ule mradi unatumia maji, maji yasipopatikana ya kutosha kujaza Bwawa lile kule kwa sababu yoyote ile, mradi ule utakuwa ‘White Elephant’. Yapo Mabwawa ya namna hiyo yalijengwa katika nchi zetu za Afrika mfano kule Ghana na lile Bwawa halina maji mpaka leo. Mimi sitaki kuona uchungu wa tunavyojibana kuitafuta hela ya kujengea Bwawa hilo halafu watu wanakwenda kwenye vyanzo vya maji yanayokwenda Rufiji wanaharibu! Iko haja ya Serikali kujikita kindakindaki kuzuia kabisa uharibifu wa vyanzo vya maji yanayokwenda Bwawa la Mwalimu Nyerere. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi wa REA, mradi huu utafanya kazi vizuri sana kama Bwawa wa Mwalimu Nyerere litazalisha umeme wa kutosha lasivyo vijini umeme hautatosha. Tulionao sasa hivi hautoshi kuendesha vijiji vyote Tanzania nzima. Chanzo cha Mwalimu Nyerere ni muhimu sana kutunzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niwambie tu Waheshimiwa Wabunge, umeme vijijini huleta maendeleo makubwa sana. Badala ya watu kulala mapema na kuogopa giza, sasa kuna vituo wanaangalia centers nyingi za television, vile vile umeme wanachomeleaji grill wanazalisha kutokana na umemea ambao umewekwa vijijini. Kwa hiyo mradi huu ambao unaanza kusuasua tena, sehemu yangu katika vijiji vingi Wakandarasi wamedolora. Iko haja ya kuwasimamia ili ahadi ya Serikali kama ilivyo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwamba vijiji vyote vitapata umeme mwishoni mwa mwaka huu au mwanzoni mwa mwaka ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashuhudia pia mpango huu unaelezea ujenzi wa barabara na madaraja makubwa ambayo yataleta mhemuko wa kukua kwa uchumi kwa kusafirisha mizigo na watu. Madaraja mengine yanaunga nchi jirani na kadhalika. Kwa hiyo Serikali ikazane kumalizia madaraja na meli ambazo zinajengwa sasa hivi kwenye maziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kilimo, kila mtu anajua kwamba kulima kama biashara au kulima kama shughuli unagusa asilimia 67, kwa sababu kila mtu hapa anakula, na tunamalizia mkutano hapa tukale, kwa hiyo kilimo ni jambo muhimu sana. Serikali katika mpango wake huu imekuja na wazo zuri sana la kutoa ruzuku kwa ajili ya wakulima wote na kusajili wakulima wako wangapi; na sasa tumeshapata wakulima 2,118,911 mwanzo. Hata hivyo mbolea ya ruzuku imeshaagizwa ya kutosha na inagawiwa. Jambo hili litakuza uchumi na litakuza tija ya mazao shambani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo kadhaa ambayo mengine yameelezwa katika mpango huu hasa maji. Maji ni kikwazo kikubwa sana cha maisha vijijini. Hata hivyo mpango unaelekezea kukuza mpango wa maji mpaka asilimia 74.5, vile vile asilimia 86.5 mijini. Jambo hili si dogo ni jambo kubwa sana. Tunaishukuru pia Serikali imejiandaa kununua mitambo kwa ajili ya kuchimba malambo, Mabwawa na vile vile kuchimba visima. Jambo hili linastahili pongezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, mpango unaelezea kuendelea kupata elimu msingi bure, vile vile pamoja na elimu msingi hii tumejenga madarasa, tumejaribu kujenga maabara katika sekondari zetu. Kwa hiyo mpango uko vizuri kwa njia hiyo na elimu ndio ufunguo wa Maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchumi wa bluu yako mambo mengi ambayo yameelezwa kwenye uchumi wa bluu. Hapa Tanzania bara kulikuwa na shirika kubwa sana linaitwa TAFICO, lilikuwa shirika ambalo linajiendesha vizuri na ambalo lilikuwa ndilo chanzo cha mlango wa boiashara ya uchumi wa bluu. TAFICO ikauzwa, baadaye ikarudhishwa sasa hivi inajikongoja, hamna chchote. Naomba Serikali katika mpango wake isisahau uchumi wa bluu ili tuweze kuvua samaki. Pia tutumie mpango huo kwa ajili ya kupata fedha na kupata maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi huko Lindi. Hivi karibuni tulipata meli kubwa ya kwetu, kibiashara tumeipeperusha bendera ya Tanzania. Ile meli haiwezi kuteremsha Samaki hapa Tanzania, na tulikuwa na mgao wa Samaki karibia tani 300, sasa inaenda kuteremsha Samaki seashells zitiwe kwenye kontena ndio zije hapa Dar es salaam. Jambo hili linawashangaza hata tuliowapa hiyo meli, kwamba hatuna pakuteremshia Samaki wala hatuna bandari. Kwa hiyo katika mpango huo wa maendeleo nimeona tuna mpango wa kuendeleza ile Bandari ya Uvuvi Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulikuwa na mpango wa kununua meli nane; lakini siuoni ule mpango na kulikuwa na meli moja kwa ajili ya TAFICO, meli nne ilitakiwa ziende Zanzibar na meli nne zibaki Tanzania Bara kwa ajili ya kukuza uchumi wa bluu, lakini sizioni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la mradi wa gesi asilia. Mimi sitaki mambo ya kujifikirisha Mwenyewe kwamba tutapata. Tunataka kujenga LNG pale Lindi, mimi nilikwenda kutembelea mradi wa LNG ughaibuni kule, na jana tulikuwa na wenzetu wa Mozambique hapa tukawauliza wenzetu vipi LNG? Majibu niliyoyapata kule nje yalikuwa ni kwamba wananchi hawanufaiki na LNG. Kama ambavyo watu walivyochimba malori na malori ya dhahabu hapa hatukupata hata senti tano mpaka tulipobadilisha sheria. Naogopa Mradi wa LNG huu, kama hatutakuwa na sheria ambazo zitatulinda, watu watachimba gesi na kuzipeleka nje. Kama vilivyo vitalu vya gesi huko high seas hatufaidiki sisi. Naogopa sana kuutia mpango wa LNG kwenye mpango wa Serikali bila kuwa na uhakika kwamba utatuingizia hela au la.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kengele ya mwisho hiyo naunga mkono hoja.