Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Justin Lazaro Nyamoga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafsi ili na mimi niweze kuchangia mapendekezo ya mpango. Nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali kwenye majimbo yetu ikiwemo jimbo la Kilolo. Pia niishukuru Serikali kwa wasilisho la mpango ambao mmeuwasilisha. Huu ni wakati wetu ili sisi tuweze kutoa maoni na mapendekezo ambayo yatasaidia katika kuboresha mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nianze kwa kuzungumzia mashirika ya umma na namna ambavyo yanafanya kazi zake na jinsi ambavyo tunaweza tuyakaboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ina zaidi ya mashirika ya umma 200, sina idadi yake kamili, lakini sina hakika kama mashirika haya yote yana ufanisi na tija ambazo tunazihitaji. Ninaona kwamba kuna haja huu mpango wa Serikali ukaja na tathimini ya mashirika ya umma ili kujua kama yote yanahitajika na kama kweli yote hayafanyi vitu vinavyojirudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano; nimesoma kwenye taarifa nikaona kuna mashirkia mawili na nikaangalia kazi yalizozifanya kwa mwaka uliopita. Shirika la kwanza linaitwa CAMARTEC. Kwenye taarifa yake wametaja vitu walivyovifanya mwaka jana. Kwanza, wametengeneza tella moja, lKINI sijajua ni tella la nini? Pili, wametengeneza mashine mbili za kubangua korosho, kingine walichotengeneza ni mikokoteni 10 ya kuvutwa na Wanyama, pia wametengeneza mashine nne za kupura mtama. Naomba niishie hapo, na kuna vingine pia wamefanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mawazo yangu nafikiria, hivi vitu ndivyo vinavyoweza kufanywa na SIDO na Mashirika mengine. Sijajua kama hii ni taasisi ya ubunifu au ni taasisi ya uzalishaji? Kama ingekuwa ni ya ubunifu mashine moja ya kupura mtama ingetosha ku-display ili wengine nao watengeneze. Pia kama ni ya uzalishaji kwa nini wazalishe nne? Kwa hiyo kwa kifupi ni kwamba zipo baadhi ya taasisi hazihitajiki au kama zinahitajika kuna namna ya kujirudia katika utekelezaji wake. Kwa hiyo ni muhimu kufanyia tathimini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaenda kwenye shirika lingine la umma linaitwa TEMDO, nikasoma. Kitu kilichofanyika ni kukamilisha kwa majokofu mawili ya kuhifadhia maiti. Sasa haisemwi baada ya hayo majokofu mawili tunafanyaje labda ni kwa ajili ya kuwaonesha wengine ili watengeneze mengi au hayo hayo ndiyo wameyauza au ni kitu gani kimefanyika? Sasa tukienda hivi maana yake ni kwamba tuna allocate fedha kwenye makampuni ambayo tija yake ni ndogo halafu hatu-allocate fedha kwenye sehemu ambazo tija ni kubwa na matokeo yake ni kwamba kuna upotevu wa rasilimali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kule kuna taasisi hizo zina wafanyakazi, zina namna nyingi, tahthimini ingeweza kusaidia kuona umuhimu wa kuendelea kuwepo au kutokuwepo. Hivyo basi mimi nafikiri ni muhimu sana hilo tukaliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunazungumza hivyo, kuna shirika hili la Kibaha, hiki kiwanda cha viuadudu ambacho tumekuwa tukikizungumzia hapa kila wakati, kimekwishatumia shilingi bilioni 83 na bado hakifanyi kazi. Sasa kama tungekuwa tayari tumesha-restructure hizi kampuni zikawa chche maana yake tungeweza kuwa na rasilimali nyingi kuwekeza kwenye hii ya viuadudu ambayo sote tunajua kwamba ingeweza kuokoa fedha nyingi kutokana na uwekezaji ambao tungeweza kuufanya kwenye dawa za kuulia wadudu. Hata changamoto ya Malaria ingeweza kupungua na zile fedha ambazo tunatumia kwenye mambo ya malaria zingeweza kuokolewa. Kwa hiyo ningependekeza kwamba, hizi kampuni zaidi ya 200, Serikali kwenye mpango wake iyafanyie tathimini ione kama zote zina tija. Kama kuna ambazo hazina tija ziondolewe ili tusiendelee kuwekeza kwenye sehemu ambayo hakuna tija yoyote katika kuwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii mifano miwili inaweza ikatoa picha halisi ya mengine mengi ambayo unaweza ukakuta kile kinachofanyika hakiwezi kuwa na tija. Huwezi ukawa na tija ya tella moja, huwezi ukawa na tija ya mkokoteni ambao hata watu wengine huko wanatengeneza. Hatuhitaji kampuni ya kiserikali kuanza kutengeneza mikokoteni ya kuvutwa na ng’ombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niizungumzie pia benki ya kilimo (TADB). Kwanza niipongeze Serikali imewekeza shilingi bilioni 60 ni jambo zuri. Pia mtaji wake sasa umekwishafikia shilingi bilioni 268, ni hatua kubwa. Hata hivyo hii benki ni invisible, haionekani. Hata hapa Dodoma nikiwauliza Waheshimiwa Wabunge hii benki iko wapi hata hapa Dodoma Makao Makuu Hawajui. Mimi nilifanya kazi ya kuitafuta, iko nane nane ndani kwenye fence. Sasa benki zote ziko hapa mjinii, hii iko nane nane tena kwenye fence na wakati huo wakulima wako vijijini. Tufanye tathimini ya hii benki ili kila mkulima aweze kuielewa vizuri hii benki na aweze kuelewa namna anavyoweza kui-access ili wakati tunapokuwa tunafanya block farming ziweze kuunganishwa na hii benki ili uwekezaji huo uweze kuwa na tija. Nani atajua kuna benki ya kilimo iko pale nane nane ilhali hata kibao hakipo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo kwenye mikoa yetu tunayotoka, wengi wetu hapa tumesema, mimi Iringa sijaiona, wala Kilolo sijawahi kuiona na kama Mimi Mbunge mwenyewe sijawahi kuiona na hata wakulima wenyewe pia hawajawahi kuiona na hawaielewi. Kwa hiyo, kwa sababu ndiyo benki pekee inayowekeza kwenye kilimo, ukisema benki sio mfuko. Mfuko unaweza ukawa na ofisi mahali lakini benki sisi Watanzania tunaelewa benki utaiona popote pale. Sasa benki gani haionekani? Hii ni changamoto, ipo ina mtaji basi sasa ionekane ili wananchi waweze kufanya uwekezaji. Hilo litakuwa ni jambo la muhimu sana kwa sababu linaweza kusaidia katika kuboresha kilimo katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie jambo la mwisho katika mchango wangu ambalo linahusu mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Kwanza nipongeze kwa hatua iliyofikiwa. na mimi ninahakika kwamba mradi huu utafanya kazi vizuri tu. Lakini, ili mradi ule uweze kufanya kazi, raw material yake ni maji na haya maji yanatoka kwenye vyanzo na Kilolo ni mojawapo ya vyanzo. Sasa kama wewe unajenga Bwawa lakini huwekezi kwenye kulinda vyanzo vya maji au kuwa na miradi itakayovifanya vyanzo hivyo vya maji viendelee kuwa endelevu maana yake ni kwamba raw material rasilimali ya ule mradi haipo. Sisi tunajua sasa hivi kwa mfano kilimo cha miti kinatakiwa kiwe na tija, sasa kama hakutawekwa ruzuku kwenye kilimo cha miti ili wakulima wa miti kwenye milima ya udzungwa waendelee kulima miti, mti mmoja uuzwe shilingi 2000 wataikata, watalima mazao mengine na hayo maji hayatakuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati huu tunapozungumzia mabadiliko ya tabia ya nchi ni ushauri wangu kwa Serikali, maeneo yote yenye vyanzo vya maji yanayolisha Bwawa la Mtera, Bwawa la Mwalimu Nyerere, Bwawa la Kidatu na Mahali mengine ikiwemo maeneo kama Kilolo, Makete na maeneo mengine yafanyiwe tathimini ya kupewa ruzuku kwenye kilimo cha miti kitakacholinda vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.