Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu katika mapendekezo ya
mpango wa 2023/2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima nzima ni uchumi shirikishi na shindani. Nami nilikuwa namsikiliza jirani yangu hapa Mheshimiwa Engineer Magessa aki-analyze data za kuonesha namna gani uchumi wa nchi yetu unaonekana kwamba kukua kwake ni kwa asilimia 0.1 na amelinganisha sana na nchi nyingine. Nami nakubaliana naye kabisa, lakini mimi naona kabisa sababu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza inatakiwa tu interogate statistics zetu kama zinasema ukweli na ziko halisia kwa sababu kwa kuangalia tu wenzetu walikotoka na walikokwenda, inaonesha kabisa kwamba sisi tuna tatizo. Pia kuna tatizo zaidi katika uchumi wetu, kwa maana ya kwamba bado productive sectors hatujaweza ku- implement kimkakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakwenda kwa mifano katika moja ya mapendekezo yangu na nitachangia zaidi kwenye sekta ya kilimo ambayo naielewa zaidi kwa sasa. Tukianza na zao la chai kwa mfano, sisi kama Tanzania bado tupo chini sana kwenye uzalishaji wa chai, na kwa kweli chai inaweza ikatupa faida na ajira kubwa. Zao la chai hata kama hupati kodi kubwa sana, lakini ni zao ambalo linaongeza sana ajira kwa wananchi wetu wa kawaida, na kwa hiyo, linaongeza sana multiplier effect kwa wananchi wetu. Kwa hiyo, ni lazima tuhakikishe tunaendeleza kwa kiasi kikubwa zao la chai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea sasa, pamoja na mipango mizuri ya Wizara ya Kilimo, tunatakiwa tujue tunashindana kwenye zao hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu Kenya tayari wanazalisha karibu tani 570,000. Sisi bado tupo kwenye tani 30,000, lakini tuna wakulima wa chai ambao wanalima chai katika mazigira magumu. Naongelea wakulima wa chai wa Njombe, Tarafa ya Egweminyu kuna wakulima karibu 2,189, hao ni wakulima wa kawaida kabisa, smallholder farmers, siyo watu wakubwa. Hawa uzalishaji wao wa chai ni kilogramu milioni 3.6, lakini katika miaka mitano watakwenda kuzalisha kilogramu milioni 7.2, lakini ili waweze kufanya hilo wanahitaji kuwa na miundombinu wezeshi, sasa mpango wetu unaongelea vizuri sana kwamba kutakuwa na miundombinu wezeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhalisia ni kwamba wakulima hawa ukiangalia bajeti yao ya barabara za vijijini inaangaliwa kama bajeti ya TARURA. Ukienda kwenye TARURA wanapogawa bajeti wanasema, tutatoa Shilingi bilioni moja kwa kila Jimbo. Ukweli ni kwamba hatufanyi kazi kimkakati, tunataka wakulima hawa wafike kwenye huo uzalishaji wa chai, lakini ikifika kwenye barabara, hatuwapi fedha za kuwasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtandao wa barabara wa Njombe nzima ni kama kilometa kama 890. Katika 890, hizi za wakulima wa chai hazihesabiwi. Peke yao, mtandao wao mzima wa chai hawa watu 2,100 ni kama kilometa 400. Kilometa 400 hizi hazina huduma, hazina msaada, hivi tutawezaje kuzalisha chai? Tunawezaje kusema kwamba tunaweza tuka-compete na Kenya, tunawezaje kuwawezesha watu wetu wakawa washindani kwenye ukulima wa chai? Kwa hiyo, hatufanyi mambo kimkakati ingawa tuna nia nzuri ya kufanya haya mambo kimkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye zao la parachichi (avocado). Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, amekwenda China akaweza kufungua Soko la China kwa maana ya kuanzisha. Hii imetengeneza matumaini makubwa sana kwa Watanzania na wakulima wa avocado. Hata hivyo bado kazi ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema, tunapoongelea kilimo shindanishi na uchumi shindanishi katika mazao haya ya kupeleka nje, hapa ndipo ambapo kwa kweli Serikali na mapendekezo ya bajeti lazima yaangalie kwa umakini sana ni namna gani matumaini ya Watanzania ambao wanalima avocado kwa kiasi kikubwa sana wamechangamkia zao hili, wataweza kufanikisha ndoto zao kwa kuhakikisha kwamba wanapeleka kwenye masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufungua soko ni jambo moja, lakini kuna mambo mengine mawili. Kwanza ni ubora, na pili, ni gharama. Kwenye gharama ndiyo hapo pa kuja kwenye mpango. Kwenye gharama za export na hasa mazao ya horticulture Bandari yetu ya Dar es Salaam ndiyo moyo wa export na ndiyo moyo wa uchumi shindanishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia na tukilinganisha, kwenye zai la avocado unachogombania ni bei nzuri, lakini unachogombania, uwe na zao zuri. Moja ya kitu ambachoni ni cha muhimu sana kukiangalia tunaita shelf life. Kwa kweli watu wa THA wanatakiwa watusaidie sana kuongeza shelf life ya avocado yetu Tanzania. Tukilinganisha na Kenya, nitatoa statistic kidogo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uki-export avocado kutoka Kenya, kwanza unapofikisha mzigo ambao uko kwenye kontena refrigerated, inachukua siku hiyo hiyo mzigo unaingia kwenye dock, unaondika kwenye meli. Ukichelewa sana ni ndani ya masaa 24. Hapa kwetu ukipeleka mzigo kwenye bandari utakaa kwa siku kumi kabla haujaondoka; kati ya tano mpaka siku kumi. Hiyo yote inakupunguzia shelf life ya product yako na matokeo yake ni kwamba wenzetu kwenye uchumi shindanishi wanaweza wakafikisha avocado kwenye soko zikiwa na shelf life ya siku kumi na tano. Sisi tunafikisha parachichi kwenye masoko zikiwa na Shelf Life ndogo sana ya siku tano mpaka siku nane. Kwa hiyo, matokeo yake itakuwa ni ngumu sana sisi kushindana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye mpango, jambo hili limeelezewa vizuri kwamba tutaangalia miundombinu wezeshi, tutaangalia bandari zetu, lakini mara nyingi tunaongea mambo haya kwa ujumla sana, hatuendi kuangalia ni ni hasa kifanyike ili kusaidia wakulima wengi ambao wanahitaji kufikisha haya mazao na kuondoa umasikini wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuangalia hilo, kuna gharama. Kwa miaka mingi tutaendelea kutumia Bandari ya Mombasa tupende tusipende. Pia tuna uwezo mkubwa wa kutumia bandari yetu kuondoa kontena la avocado kutoka Njombe, kutoka southern highlands, au eneo lolote lile, unatakiwa ulipe zaidi ya mtu anayetoa kutoa kontena kutoka maeneo mengine kama ya Nairobi hata maeneo mbalimbali ya Kenya. Sisi tunatakiwa tulipe Dola 4,000 mpaka 5,000 kwa kontena kuliondoa huku na kulifikisha bandarini. Maana yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, inatakiwa THA itusaidie kwa kuhakisha kwamba moja, ipunguze angalau zile gharama za pale kwenye bandari, lakini ya pili angalau tuwe na dedicated birth, najua inaongelewa siku zote, lakini naomba kwenye bajeti hii Mheshimiwa Waziri tuje na mipango kabambe, ioneshe wazi kabisa plan yetu ni nini? Inakwisha lini? Lini itaanza kuwa implemented?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke shippers hawana mahusiano na mtu yeyote anayezalisha. Wao wanaangalia biashara yao ya ku-ship, wanaangalia risk ambayo ikoinvolved kwenye ku-ship products zetu, wao wataangalia lini walete meli hapa, na kama kuna mzigo wa kutosha, na kama hakuna risk yoyote ya hayo mazao kuharibika kabla hawajayachukua. Kwa hiyo, hayo mambo yanafanyika yote kwa pamoja na tuyaangalie kwa makini sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana utaona sisi tunaongelea kwamba uchumi wetu kama vile unakua pole pole, lakini ni kama uchumi umeshikwa, umefungwa, tuna bandari, wengine wameongelea SGR hapa, inataengenezwa lakini bado kule hatuangalii itafika wapi? Itatoa wapi mzigo? Haya ndiyo mambo ambayo yanafanya tuseme kwamba uchumi wetu ni mkubwa, mnasema uko stable, microeconomics ziko vizuri, lakini ni kama uchumi umekamatwa, umeshikwa, haupanuki na hauchechemki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuongelea kidogo tu sekta ya madini. Nilikuwa naangalia hapa kwenye Mpango. Ukiangalia kwenye kilimo, tunaongelea utafiti kwamba utafiti ufanyike kwenye mbegu, masoko na miundombinu, lakini ukija kwenye madini, bado suala la utafiti haliongewi hata kidogo, na ile ni moyo na uhai wa sekta ya madini yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuseme wazi kabisa kwamba tuna options mbili kwenye utafiti, au Serikali i-invest kiasi kikubwa kwenye makampuni yetu makubwa ya utafiti ya Kitanzani kama STAMICO, lakini tunachokiona, na nimesoma ripoti ya CAG; katika moja ya kampuni au mashirika ya kimkakati ambayo yana ukwasi ni pamoja na Shirika la STAMICO. Hawana fedha zozote za kutosha kufanya utafiti. Utafiti unataka fedha nyingi sana. Kwa hiyo, option iliyobaki ni kuwa na sekta binafsi iweze kuingia kwa kiasi kikubwa kwenye utafiti. Ila sekta binafsi haina urafiki na mtu, yenyewe inaangalia kwamba inaweza ikafanya hii kazi kwa faida huko mbele ya safari?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sheria zetu kwa ujumla pamoja na improvement yote kwenye production, lakini bado kwenye eneo la utafiti sheria zetu hazivutii utafiti katika sekta ya madini. Kwa hiyo, mpango huu kama Waziri atakubali, wajaribu kuangalia ni kwa kiasi gani tunaweza tuka-incentivize zaidi sekta ya utafiti ili tuweze kuchimba madini mbalimbali. Mungu ametujalia madini ya kila aina katika nchi hii, kila kona unakoenda kuna madini.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimwa Mwanyika kwa mchango mzuri.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.